The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Msimu Huu wa Sikukuu, Tukumbashane Umuhimu wa Kuimarisha Ulinzi wa Watoto

Hatupaswi kusubiri maafa yatokee ndipo tuone umuhimu wa kuchukua tahadhari kwani kinga ni bora kuliko tiba!

subscribe to our newsletter!

Msimu wa sikukuu huambatana na furaha zisizo na kifani, furaha ambayo huwapunguzia wazazi uchovu unaotokana na mihangaiko ya kutafuta mkate wa kila siku, furaha ambayo huiweka sawa miili na akili za watoto, hususan mara baada ya kutoka masomoni. 

Vilevile, hii ni furaha ambayo hujumuishwa na utolewaji na upokeaji wa zawadi kedekede miongoni mwa wazazi na watoto ndani na nje ya familia.

Katika kipindi hiki cha sikukuu, wakati furaha zibubujikapo miongoni wa wazazi na watoto, kamwe hatupaswi kuziacha zipitilize na mwishowe zikakengeusha ukweli kuhusu maisha, zikaharibu misingi na utu, ama kuacha kovu la kudumu, katika maisha ya watoto. 

Ingawa ‘furaha ya mzazi ni mtoto kufurahia,’ tusisahau pia kuwa ‘majuto ni mjukuu.’ Tuelewe kwamba watoto wanapaswa kulindwa wakati wote. 

Tumepata kushuhudia, ama kusikia, vitendo vingi vya kikatili vinavyofanywa dhidi ya watoto na idadi kubwa miongoni mwao wakipitia unyanyasaji wa hali ya juu. Tumesisikia ajali za barabarani ambazo zingekwepeka. 

SOMA ZAIDI: Msimu Huu wa Sikukuu, Tukumbuke Vitu vya Kuzingatia Tunaposafiri na Watoto

Pia, tumesikia habari za watoto kupotea na purupushani kadha wa kadha zifikapo nyakati za sikukuu. Kwa mantiki hiyo, kuimarisha ulinzi dhidi yao ni jambo la msingi sana.

Hatushangai Jeshi la Polisi nchini kutoa angalizo, nukuu na maonyo kadhaa dhidi yetu wazazi juu ya mwenendo na mapokeo yaliyozoeleka ya kuwaacha watoto watembee peke yao, wakimbie huku na kule, kucheza pembezoni mwa fukwe za bahari, barabarani, maeneo ya wazi yenye michezo ya watoto na hata kumbi za starehe. 

Hii ni kwa sababu mida kama hii ya shamrashamra za likizo matukio ya kihalifu huongezeka.

Aidha, wazazi wengi, hususan wanaomiliki simu janja, hutupia picha na video mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonesha wakiwa na watoto wao katika ‘viwanja’ tofauti vya kujivinjari. 

Ila, tuwe makini kwani kusambaa kwa picha na video hizo huenda kukawa ni chanzo kimoja wapo cha unyanyasaji mpya wa watoto mtandaoni endapo maudhui yake yatapata kutafsirika vibaya miongoni mwa wanajamii humo mtandaoni.

SOMA ZAIDI: Je, Ni Ipi Aina Yako Ya Malezi?

Hivyo basi, tujitahidi kuhakikisha kuwa mazingira watakapocheza, au kufurahia, watoto sikukuu hii ni salama na yako chini ya uangalizi wa watu wazima. 

Tuwaelezee watoto sheria za msingi za usalama wao, kama vile kutokutoka nje bila idhini na kutokujaribu vitu vya hatari. Tujitahidi kufuatilia matumizi yao ya vifaa vya kielektroniki na teknolojia ili kuhakikisha wanavitumia kwa usalama. 

Pia, tuweke mawasiliano ya dharura na kuwaonyesha wanapoweza kupata msaada iwapo kutatokea shida ya aina yoyote. Hii itatusaidia kujenga mazingira salama na yenye furaha kwa watoto wakati wa kusherehekea sikukuu.

Hatupaswi kusubiri maafa yatokee ndipo tuone umuhimu wa kuchukua tahadhari kwani kinga ni bora kuliko tiba! Tunapaswa kutambua kuwa watoto wanahitaji uangalizi wa hali ya juu kwa kuwa miili na akili zao bado havijakomaa na wanatutegemea sisi wazazi na walezi.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *