The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Msimu Huu wa Sikukuu, Tukumbuke Vitu vya Kuzingatia Tunaposafiri na Watoto

Kusafiri na watoto kunaweza kuwa na changamoto za hapa na pale, lakini ukiwa na maandalizi mazuri na mipango sahihi, wewe na familia yako mnaweza kuwa na safari yenye amani na furaha.

subscribe to our newsletter!

Mwisho wa mwaka umewadia na likizo zimeanza. Huu ni wakati mzuri wa kujumuika na familia, kufurahi pamoja na kujenga kumbukumbu zitakazodumu. Wakati huu, wengi tunapenda kusafiri peke yetu au na watoto wetu. Kama una mpango wa kusafiri na watoto mwaka huu, basi ni vyema ukajua nini cha kuzingatia.

Kitu cha kwanza kabisa ni kupanga safari yako mapema: siku utakayo safiri, na aina ya usafiri utakaokufaa wewe na familia yako. Kama utatumia ndege, basi au treni hakikisha unakata tiketi mapema. 

Taratibu za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) zinasema, ukisafiri na mtoto mdogo mwenye umri chini ya kwenda shule, huyo halipiwi nauli. Lakini kama unasafiri naye katika mabasi makubwa ya kwenda safari ndefu, na atakalia kiti, basi utawajibika kumlipia nauli ya mtu mzima.

Ukishafanya hivyo, wajulishe watoto kuhusu safari, waelezee sehemu unayowapeleka. Kama ni kuwasalimia babu na bibi, au kutalii, basi ni vyema watoto wapate fursa ya kujiandaa kisaikolojia na kuchangia maoni yao. 

Hii itawawezesha kujisikia kama sehemu ya maandalizi na kuongeza shauku yao ya safari. Mnaweza kushirikiana kutengenza ratiba ya vitu ambavyo wangependa kufanya safarini na mtakapofikia.

SOMA ZAIDI: Je, Ni Ipi Aina Yako Ya Malezi?

Ukiwa unajiandaa kwa ajili ya safari, fahamu kuwa takwimu zinaonesha kwamba wasafiri wengi wa safari ndefu hulala wawapo safarini. Hivyo, iwapo unapanga kusafiri na watoto wako, jipe muda wa kutosha wa kulala na kupumzika kabla ya safari kuanza. 

Kutegemea umri wa watoto wako , wewe unapaswa kuwa macho muda wote wa safari. Hii ni kwa sababu watoto wana tabia ya kutaka kusimama na kucheza mkiwa safarini, na hufungua mikanda ya viti vyao ili wapate fursa hii. 

Iwapo utahisi usingizi, mpatie mtoto kitu cha kufanya wakati huo, inaweza kuwa kitabu cha kusoma au kuchora, video za vikatuni, nakadhalika.

Vipi kuhusu chakula njiani? Unapopanga mizigo ya safari usisahau chupa ya maji ya kunywa na vyakula vinavyobebeka kama mkate, korosho, keki, nakadhalika. Tofauti na watu wazima, watoto hula mara nyingi zaidi katika siku na ule utaratibu wa mabasi kuingia migahawani unaweza ukawachelewesha watoto mda wao wa kula na kuleta kadhia safarini.

Pia, katika kupanga vitu muhimu vya safari, tafadhali usisahau nguo za kusitiri baridi hata kama mnasafiri katika msimu wa joto. Kwani safarini lolote laweza kutokea na mkalala njiani. 

Chukua masweta, ikiwezekana hata shuka, na kama mtoto ni mdogo sana, beba kanga za kutosha. Beba pia tochi kwani unaweza kuihitaji wakati wa usiku. Hakikisha simu yako ina chaji ya kutosha pamoja na kihifadhi chaji, au power-bank ikiwezekana. Simu ni kifaa muhimu sana wakati wa dharura.

SOMA ZAIDI: Tunavyoweza Kuwafundisha Watoto Kuwa Salama Wakati Wanacheza

Mwisho, kumbuka kuzingatia usalama na afya ya watoto wako. Hakikisha una dawa za dharura, vitabu vya kumbukumbu za matibabu, na taarifa za mawasiliano za hospitali au vituo vya afya vinavyoweza kufikiwa kwa haraka iwapo kuna dharura sehemu mtakayofikia. 

Pia, usisahau kubeba vitakasa mikono, au sanitizer na vitambaa, au wipes kwa ajili ya kufutia mikono kama maji yatakosekana.

Kusafiri na watoto kunaweza kuwa na changamoto za hapa na pale, lakini ukiwa na maandalizi mazuri na mipango sahihi, wewe na familia yako mnaweza kuwa na safari yenye amani na furaha.

Kwa hayo machache, uwe na safari njema!
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *