The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Maarifa 6 ya Jamii Ambayo Mtoto Anaweza Kujifunza Wakati Huu wa Likizo

Ili watoto waweze kuwa na mahusiano bora na marafiki zao pamoja na watu wanaowazunguka na kuwa watu wazima, wenye wajibu na busara, basi sisi kama wazazi inatupasa kuwafundisha maarifa mema yaliyopo katika jamii.

subscribe to our newsletter!

Shule zimefungwa na watoto wamerudi nyumbani. Huu ni muda muafaka wa kukaa karibu na watoto wetu na kuwafundisha vitu mbali mbali ikiwemo maarifa ya jamii yatakayowaongoza katika maisha ya kila siku. 

Kiuhalisia, watu wazima huwa tuna tabia zinazoendesha maisha yetu ya kila siku. Tunasalimia wafanyakazi wenzetu, majirani, wapita njia, ndugu pamoja na kuwajulia hali na kuwauliza kazi na biashara zao zinaendeleje. 

Wakati mwingine huwa tunaingia kwenye mitafaruku na kuombana radhi. Yote haya huibua hisia tofauti ambazo tunaweza kukabiliana nazo kwa namna inayokubalika na jamii kwakuwa ndivyo busara za utu uzima zinatutaka kuwa hivyo.

SOMA ZAIDI: Mahusiano Mazuri ya Wazazi ni Muhimu Katika Malezi ya Watoto

Watoto pia hupitia michakato kama hii, ila tofauti ni kwamba, wao hawajawa na uwezo wa kukabiliana na hisia hizi kwa kila jambo na watu wanaokutana nao. 

Hata hivyo, ili watoto waweze kuwa na mahusiano bora na marafiki zao pamoja na watu wanaowazunguka na kuwa watu wazima, wenye wajibu na busara, basi sisi kama wazazi inatupasa kuwafundisha maarifa mema yaliyopo katika jamii. 

Kwanza tuwafundishe kufuata maelekezo. Hili ni jambo muhimu sana kwa watoto kujifunza haswa wakiwa katika umri mdogo. 

Mzazi unaweza kuanza kwa kuwaelekeza kufanya majukumu madogo madogo kama vile kuhifadhi vitu vyao vya kuchezea mahali pamoja baada ya kumaliza kucheza, kuhifadhi viatu, mabegi yao ya shule sehemu maalumu pamoja na vitu vingine vya nyumbani kama vile visu, chumvi sukari, rimoti nk. 

Wasistize mara kwa mara kwamba mtu akiwaelekeza jambo wanatakiwa kumtazama usoni na kumsikiliza kwa umakini. Hii siyo tu ishara ya ukarimu bali pia huwasaidia kuelewa maelekezo.

SOMA ZAIDI: Msimu Huu wa Sikukuu, Tukumbashane Umuhimu wa Kuimarisha Ulinzi wa Watoto

Pili, tuwafundishe watoto namna ya kujikita katika kazi au jukumu moja. Kujikita katika kufanya jambo moja huwa siyo rahisi kwa wengi wetu, hivyo ni muhimu kuwafundisha watoto wetu kuwa na ujuzi huu. 

Weka muda wa kutosha wa yeye kufanya kitu kimoja na mfundishe kuweka kando mambo yote yanayoweza kuingilia umakini wake. Kwa mfano; ataruhusiwa kuangalia TV baada tu ya kukamilisha jambo fulani.

Jambo lingine ni kumfundisha mtoto ni kukukubali jibu la “Hapana”.  Huwa inakera kumwambia mtu hapana asikuelewe au akakukasirikia. Hivyo, ni vizuri watoto kufahamu kwamba mambo hayawezi kwenda wanavyotaka kila wakati. 

Watoto wasiojifunza kukubali jibu la “hapana” hukua wakidhani kuwa wasemalo wao ndilo na jamii itakubaliana nao kwa kila jambo. Kitu ambacho si kweli.

SOMA ZAIDI: Msimu Huu wa Sikukuu, Tukumbuke Vitu vya Kuzingatia Tunaposafiri na Watoto

Kitu cha nne ambacho tunaweza kuwafundisha watoto wetu wakati huu wa likizo ni kutokukubaliana kwa busara. Katika umri mdogo kabisa mtoto anapaswa kufahamu kuwa watu huwa na mitazamo tofauti juu ya mambo mbalimbali.

Uzoefu wao wa kwanza wa kutokukubaliana au kukataa jambo kutaanzia kwako au kwa ndugu zao, kwa hiyo ni vyema ukawajuza kuwa kila mtu ana haki ya kuwa na maoni tofauti.  

Kama mtoto hakubaliani na jambo fulani, hakuna haja ya yeye kupayuka, kuwaita wenzake majina yasiyofaa au kufoka, badala yake anapaswa kusikiliza na kuelewa mawazo ya mtu mwingine na kwanini wanawaza vile.

SOMA ZAIDI: Tunavyoweza Kuwafundisha Watoto Kuwa Salama Wakati Wanacheza

Cha tano ni kuonyesha shukrani. Tuwafundishe watoto kuwa shukrani ni zawadi nzuri anayoweza kumpatia mtu aliyemtendea wema na kwamba kuonyesha shukrani ni kuwafanya watu wengine wajiskie wanathaminiwa. 

Wasisitizie kusema ahsante kwa zawadi, ahsante kwa chakula, kwa dada anayewahudumia, kwa rafiki yao anayewapa zawadi au hata mtu anayewavusha barabara.

Jambo la mwisho ni kuomba radhi. Kukosea ni sehemu ya ubinadamu wetu, hivyo kujua kuomba msamaha ni kitu cha muhimu sana kwa mtoto kujifunza akiwa nyumbani, shuleni na hata katika maisha yake ya kila siku. Mfundishe kuomba msamaha kutoka moyoni, kwa kumaanisha na siyo kutafuta sababu ya kuthibitisha matendo yake.

Tabia huuundwa, tujitahidi kutumia muda huu wa likizo kuwajengea watoto wetu tabia nzuri na maadili mema.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *