The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tumejitahidi AFCON, Lakini Tunajipangaje Upya?

Tunaposema tutajipanga upya, tuseme kwa dhati kuwa tumeamua kurekebisha mambo tofauti na yalivyokuwa mwaka 2019 tulipofuzu kwa mara ya pili na mwaka 2023 tulipofanikiwa kupata pointi mbili za kwanza.

subscribe to our newsletter!

Kila tunapoondolewa mashindanoni, faraja yetu kubwa huwa “tumepambana lakini hatujafanikiwa, turudi tukajipange upya” na maisha huendelea hadi yanapokuja mashindano mengine.

Ndivyo inavyofanyika kwa timu zetu za taifa, na ndivyo inavyofanyika kwa klabu zetu; iwe zimeondolewa kwa kupata matokeo mabaya sana au kwa matokeo mazuri yanayotia moyo kuwa huenda tukijiandaa vizuri tunaweza kupata matokeo mengine mazuri zaidi.

Na ndiyo maneno yanayosemwa baada ya timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, kuondolewa katika hatua ya makundi ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) zinazoendelea nchini Ivory Coast.

Tanzania ilianza vibaya fainali hizo ilipofungwa mabao 3-0 na Morocco katika mchezo ambao Taifa Stars ilimaliza ikiwa na wachezaji 10 baada ya Novatus Miroshi kuonyeshwa kadi ya pili ya njano katikati ya kipindi cha pili na kuweka uwezekano wa timu yake kuruhusu mabao mengi zaidi.

Ilizinduka katika mechi ya pili ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 na Zambia, Tanzania ikitangulia kufunga kwa bao la Simon Msuva kabla ya Wazambia kusawazisha mwishoni mwa mchezo.

SOMA ZAIDI: Usajili Dirisha Dogo Ni Kwa Ajili ya Kuziba Mapengo Tu

Kwa hali hiyo, Stars ilihitaji ushindi wa aina yoyote katika mechi ya mwisho dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili ivuke hatua ya makundi kwa mara ya kwanza, ikiwa inashiriki fainali hizo kwa mara ya tatu. Lakini mchezo haukuwa rahisi na ukaisha kwa sare ya bila kufungana.

Angalau safari hii, Tanzania imeondoka mashindanoni ikiwa na mafanikio kidogo; imepata pointi zake za kwanza katika fainali hizo kutokana na sare mbili dhidi ya Zambia na Congo DR, mafanikio ambayo yameibua ile faraja ya “turudi tukajipange upya”.

Ni kweli tunarudi kujipanga upya au imekuwa ni kauli ya kuondokea mashindanoni na kujenga matumaini kuwa kuna kitu zaidi kitafanyika?

Natumaini baada ya miezi miwili ukimuuliza kiongozi tumeshaanza kujipanga upya, hatakuwa na jibu sahihi na badala yake anaweza kukutajia mlolongo wa mafanikio na mipango iliyopo mbele ya Shirikisho la Soka (TFF), bila ya kuihusisha na neno la faraja la “tukajipange upya.”

Mauritania

Lakini fainali hizi zimetuonyesha jinsi timu zinavyojipanga na zile zinazojipanga upya. Zimetuonyesha jinsi ya kushughulikia hali ya kutojituma na kuigeuza kuwa ya kujituma.

Mauritania ni moja ya nchi ambazo zilikubaliana na matokeo ya kufanya vibaya na kujipanga upya ili kupata matokeo mazuri zaidi katika mashindano yanayofuata. 

Miaka michache iliyopita usingeweza kuamini kuwa Mauritania, ambayo ina watu milioni tano tu, ingeweza kufuzu kucheza fainali za AFCON mara tatu mfululizo, lakini imeweza na safari hii ilienda na malengo makubwa zaidi.

SOMA ZAIDI: Waamuzi Zanzibar Wametia Doa Kombe la Mapinduzi 

“Tutajaribu kufanya vizuri zaidi ya ilivyokuwa katika mashindano yaliyopita,” alisema kocha Amir Abdou baada ya timu hiyo kuwasili Ivory Coast kwa ajili ya fainali za mwaka huu, akijua kuwa Mauritania haikuwahi kupata ushindi mara zote mbili za kwanza.

“Tutafanya kila liwezekanalo kushinda mechi yetu ya kwanza dhidi ya Burkina Faso,” aliongeza Abdou. “Hicho ndio kitakuwa kitu muhimu.” Hata hivyo, ushindi haukuwezekana baada ya Burkina Faso kushinda kwa mabao 2-0 katika klundi lililohusisha pia nchi za Angola na Algeria.

Alikuwa anazungumza kwa uhakika akijua uwezekano wa kupata matokeo ya kushangaza ulikuwa mkubwa baada ya kufanya hivyo akiwa na timu ya taifa ya nchi yake, Comoro, katika fainali za mwaka 2022 ilipoishangaza Afrika kwa kuishinda Ghana na kusonga mbele kwenda hatua ya mtoano ilikotolewa na Cameroon.

Mauritania ilimchukua Abdou kama moja ya hatua za kujipanga upya, ikijua kuwa aliweza kutumia kwa ufanisi rasilimali chache ambazo Comoro ilikuwa nazo. Alikusanya wachezaji waliokuwa na asili ya Comoro ambao walikuwa wakicheza barani Ulaya, hasa Ufaransa, na kujenga kikosi kilichoshangaza wengi kwenye fainali za 2022.

Wakati Chama cha Soka cha Mauritania kikiendelea na mikakati yake ya maendeleo ya mchezo huo ambayo kwa kawaida huchukua muda, kiliona kocha Abdou ndiye angefaa kwa wakati huu katika kujipanga upya. 

SOMA ZAIDI: Kamati ya Hamasa Bila ya Mkakati wa TFF

Isingewezekana kwa mipango ya maendeleo iliyoanza mwaka 2011 wakati Ahmed Yahya anachukua urais wa soka, izalishe kikosi bora cha kupambana kikamilifu nchini Ivory Coast, au Misri na Cameroon kulikofanyika fainali zilizopita.

Kwa hiyo, Abdou mwenye jicho la kuona kipaji na uwezo wa wachezaji wenye asili ya Mauritania na ushawishi, ndiye alifaa kubeba matumaini mapya ya kuondoa mkosi wa kuishia hatua kundi la wachezaji wa ndani na nje wenye uwezo, wapambanaji na wafia nchi ambao hadi sasa wameshangaza mashabiki katika fainali za mwaka huu.

Hawa walijipanga upya na bila shaka watajijenga juu ya mafanikio ya mwaka huu na kuwa imara zaidi watakapofuzu kwa fainali zijazo, wakitarajia matokeo mazuri zaidi katika mipango yao ya maendeleo inayohusisha kuwekeza Dola za Kimarekani milioni 11 ilizopokea kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) kujenga upya ofisi za makao makuu, kukarabati uwanja wa Sheikh Buyidah ulioko Nouakchott, viwanja vya mazoezi na pia mradi wa mashindano ya shule yanayoandaliwa kila mara vijijini.

Namibia

Somo jingine ya kujipanga upya limeonekana kwa Namibia, ambayo pia inashiriki fainali hizi kwa mara yake ya tatu tangu nchi hiyo ipate uanachama wa FIFA mwaka 1990 na wa CAF mwaka 1992. Ilipata matokeo mazuri dhidi ya Tunisia na Mali, wakati ikakubali kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya jirani zao wa Afrika Kusini.

Haikuwahi kupata ushindi katika fainali hizo, lakini mwaka huu ilifanya maajabu. Ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tunisia na ikamaliza kwa sare ya bila kufungana na Mali na hivyo kutwaa moja ya nafasi sita za timu bora ya tatu.

SOMA ZAIDI: Simba Iongeze Muda wa Maoni Marekebisho ya Katiba

Mbali na miradi mingi ya maendeleo ya michezo inayohusisha ushirikiano na FIFA na Chama cha Soka cha Ujerumani, mashindano ya kila mwaka ya Chama cha Soka cha Nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA) ambayo huanzia vijana wenye umri chini ya miaka 17 hadi timu kubwa, yamesaidia kuijenga Namibia kisoka hadi ikawa na timu ambazo zinasumbua mashindano ya klabu.

Somo jingine ni la kujipanga upya katikati ya mashindano. Nyota wa zamani wa Cameroon, Samuel Eto’o, ameonyesha mfano wa kiongozi bora, alipoamua kwenda kuzungumza na wachezaji kwa hisia mara tu baada ya timu hiyo, inayoundwa na nyota wanaotamba duniani, kuanza vibaya fainali hizo.

Eto’o aliwaonyesha wachezaji jinsi wanavyoonekana kucheza kwa kukosa uzalendo, akiwaambia wengi wao wamezaliwa na kukulia Ulaya na hawajawahi hata kuchezea klabu za Cameroon na kwamba baada ya fainali hizo mambo yatabadilika.

Alitoa mfano wa enzi zake, akiwaomba radhi kwa kutumia mfano unaomuhusu na kuwataka wajitume. Hotuba yake inaonekana kubadili kila kitu ndani ya timu hadi ikafuzu kucheza 16 bora. 

Eto’o hakukaa jukwaani kujiona kuwa ndiye aliyesababisha matokeo kubadilika, bali alikimbilia uwanjani baada ya mechi kuwapongeza wachezaji, huku akionyesha dhahiri kuwa alifurahishwa kupita kiasi na mchezo wao wa mwisho dhidi ya Gambia.

SOMA ZAIDI: Kila la Heri Maandalizi ya Stars AFCON 2023

Eto’o alitoa aina ya hotuba zinazozindua akili ya mtu na kumfanya afikirie upya kile anachokipigania. Na hata kabla ya mechi ya mwisho, aliongea na wachezaji kuwaambia kuwa wanaweza na kwamba yeye aliweza kwa sababu aliamini kuwa ana uwezo.

Sijaiona hii kwa timu yetu zaidi ya viongozi wa kisiasa kuona umuhimu huo.

Leo tunaporudi kutoka Ivory Coast na ile faraja ya “kujipanga upya,” tumeshaanza kufikiria tutafanya nini? Tumeshafikiria tutajipanga upya katika maeneo gani? Nani ataongoza jahazi la kujipanga upya iwe ni uwanjani au nje ya uwanja? 

Na kwa nini awe yeye na si mwingine? Nini kitatuwezesha kujipima kama tunafanikiwa kujipanga upya? Nani tutashirikiana naye?

Tunaposema tutajipanga upya, tuseme kwa dhati kuwa tumeamua kurekebisha mambo tofauti na yalivyokuwa mwaka 2019 tulipofuzu kwa mara ya pili na mwaka 2023 tulipofanikiwa kupata pointi mbili za kwanza.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts