The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Bei Duni, Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Vilio Vikubwa vya Wakulima wa Mwani Z’bar

Mtaalamu abainisha hatua Serikali inapaswa kuchukua kuufanya mwani kuwa na tija zaidi kwa wakulima na nchi kwa ujumla.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Wakulima wa mwani visiwani hapa wamesikitikia athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi ambayo, ukijumlisha na bei isiyoridhisha, yanafanya kilimo hicho cha zao hilo la biashara kushindwa kuwawezesha kukabiliana na ugumu wa maisha unaowakabili.

Wakulima hao, wengi wao wakiwa ni wanawake, wameieleza The Chanzo kwamba kinachowasukuma kuendelea na shughuli hiyo ni mazoea ya kulima zao hilo linalochangia upatikanaji wa fedha za kigeni Zanzibar yakichangiwa na kukosa shughuli nyingine m’badala za kiuchumi.

Wakati kuna namna mbalimbali ambapo athari za mabadiliko ya tabianchi zinajidhihirisha kwenye kilimo cha mwani, wanawake hawa wanaelezea kuumizwa zaidi na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari, hali inayowalazimu kufanya kilimo chao hicho kwenye kina kirefu cha maji.

Athari nyingine kubwa inayotokana na mabadiliko ya tabianchi inayolalamikiwa na wakulima hawa ni kuongezeka kwa hali ya joto, hali ambayo imepelekea mwani kuoza na hivyo kufanya malengo yao kutotimia kwani mwani huo unakuwa hauuziki tena.

Nadra Mohamed Said, mkaazi wa kijiji cha Mfumbwi huko Jambiani, wilaya ya Kusini, mkoa wa Kusini Unguja, ameimbia The Chanzo ilipomtembelea kwenye shamba lake la mwani hivi karibuni kwamba amekuwa akijihusisha na kilimo hicho kwa miaka kumi sasa na athari hizo za tabianchi zimezidi kuathiri ustawi wake kama mkulima.

SOMA ZAIDI: Wanawake Wajitosa Kwenye Sekta ya Madini Licha ya Changamoto Wanazopitia

“Zamani bei ilikuwa ndogo lakini mwani ulikuwa mwingi,” Nadra, 38, anasema. “Tulikuwa tunavuna gunia mpaka 50 kwa wiki. Lakini sasa hivi unaweza kupata gunia kumi kwa wiki.” 

Mama huyo wa watoto watano anasema hali hiyo imemuathiri sana katika jitihada zake za kumsaidia mumewe kukidhi haja za familia yao.

“Joto ni kubwa na mwani unaoza,” Nadra, niliyemkuta akiwa katika upandaji wa miche, aliendelea kusema. “Mwani una kazi sana. Kama unavyoona, kwa kweli tunahangaika na mpaka miguu imechanika na kucha zimeharibika. Lakini kilio chetu kikubwa ni bei maana hadi sasa tunaambiwa kilo ni Shilingi 800 badala ya Shilingi 1,000.”

Hali siyo mbaya?

Kilio chake ni kilio cha wanawake wenzake walio wengi wanaojihusisha na kilimo cha mwani ambao tathmini yao ya kilimo hicho inatofautiana sana na ile ya Serikali ambayo imeiambia The Chanzo kwamba hali siyo mbaya sana sasa ukilinganisha na zamani kama wakulima hao wanavyojaribu kudokeza.

Serikali inataja kuongezeka kwa bei ya zao hilo ndani ya kipindi cha miaka kumi kutoka Shilingi 375 mwaka 2013 mpaka Shilingi 1,000 mwaka 2023 kama moja ya kielelezo cha ukuaji wa kilimo cha mwani visiwani Zanzibar na maslahi yanayoambatana nacho kwa wakulima.

Serikali pia inasema ni jitihada hizi za kuongezeka kwa bei ya mwani ndizo zilizopelekea uzalishaji wa zao hilo la biashara kuongezeka ndani ya miaka kumi iliyopita kutoka tani 11,044 zilizozalishwa mwaka 2013 mpaka tani 16,653 mwaka 2023.

“Tuliona uzalishaji umepungua, hivyo Serikali ilichukua juhudi za kuweka  kiasi cha Shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kuwawezesha wakulima wa mwani Unguja na Pemba,” Dk Salim Soud Hemed, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Bahari, alisema kwenye mahojiano na The Chanzo hivi karibuni.

Lakini utafiti mdogo uliofanywa na The Chanzo umebaini kwamba licha ya jitihada hizi za Serikali wakulima wengi wa zao hili la mwani hawaridhishwi na mwenendo wa uzalishaji wake, huku baadhi yao wakiacha kabisa kujishughulisha na kilimo hicho.

SOMA ZAIDI: Simulizi za Wapiga Debe Wanawake Stendi ya Magufuli: ‘Sisi Siyo Mateja’

Huko Matemwe Kigomani, wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa Kaskazini, Unguja, kikundi cha wanawake 12 cha Hodari kimeacha kabisa kujishughulisha na ulimaji wa mwani kwa miaka mitatu sasa, wakitaja maslahi duni yanayotokana na kilimo hicho yasiyolingana na nguvu wanazowekeza.

Mwingiliano wa biashara

Kwenye mazungumzo yao na The Chanzo, wanawake hao walibainisha kwamba mbali na sababu zingine kama vile athari za mabadiliko ya tabianchi na bei duni, mwingiliano wa biashara ya utalii katika maeneo ambayo walikuwa wakilima mwani, yanayojumuisha kuvamiwa kwa maeneo hayo na waendesha mashua za kitalii, uliwasukuma kuacha kuendelea na kilimo hicho.

“Hili eneo hili ndilo tulikuwa tunalima mwani na kulikuwa hakuna haya mambo ya mashua,” Kesha Makungu, Katibu wa kikundi hicho, anasema huku akionesha shamba hilo. “Lakini sasa toka hii biashara kukuwa, hali imebadilika, na tumekuwa kwenye ugomvi na hawa wamiliki wa hizi mashua kwa siku nyingi.” 

Kesha, 52, kwa sasa anajishughulisha na biashara ya kukaanga samaki.

Dk Hemed aliiambia The Chanzo kwamba Serikali inatambua changamoto zinazowakabili wakulima wa mwani visiwani Zanzibar, akisema kwamba mikakati kadhaa inachukuliwa hivi sasa kutatua changamoto hizo na kuboresha ustawi wa wakulima hao.

SOMA ZAIDI: Wanawake Machinga Complex Dodoma Wafurahia Uwepo wa Vyumba vya Kunyonyeshea, Malezi: ‘Ni Ukombozi

Mikakati hii ni pamoja na kuwapatia mafunzo wakulima yatakayowawezesha kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kuwapatia wakulima hao, kupitia vikundi vyao, boti maalumu zinazowawezesha kufanya kilimo hicho kwenye kina kirefu cha maji.

Jumla ya boti 500 zimetolewa mpaka sasa kwa wakulima takriban 5,000 wa Unguja na Pemba ambazo Dk Hemed anaamini zitakuwa na msaada mkubwa katika kuchochea uzalishaji wa mwani na kuboresha ustawi wa wakulima wake.

Mkulima wa mwani akiwa amebeba mwani aliovuna. PICHA | NAJJAT OMAR

Abuubakar Hamad ni Afisa Uhusiano na Habari wa Kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO), kampuni ya Serikali iliyoanzishwa hivi karibuni kuutafutia soko mwani unaozalishwa visiwani humo, ameiambia The Chanzo kwamba bei hupanda au hushuka kulingana na hali ilivyo katika soko la dunia.

Kuongeza ubora

“Soko la dunia kwenye mwani ni soko la ushindani na siyo sisi peke yetu tunaozalisha mwani kwenye soko hilo, kuna nchi kama Malaysia, Indonesia na nyenginezo wanazalisha,” alisema Hamad. “Tunahitaji kuwekeza nguvu kwenye kuongeza ubora wa mwani tunaozalisha kwani hiyo inaweza kupelekea bei pia kupanda.”

The Chanzo ilimuuliza Dk Mary Mtumwa Hatibu, ambaye ni Msimamizi wa Kitengo cha Mazao ya Bahari, Mazingira na Maliasili kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) ni hatua gani zitapaswa kuchukuliwa kama Serikali itadhamiria kuongeza ubora wa mwani unaozalishwa Zanzibar?

SOMA ZAIDI: Dhuluma Baada ya Kuachika Inavyowasukuma Wanawake Zanzibar Kutaka Kumiliki Ardhi Kisheria

“Serikali kwanza ianze utekelezaji wa mpango wa matumizi sahihi ya bahari kwa kuona umuhimu wa kuangalia masuala ya utalii, mabadiliko ya tabianchi, uvuvi na shughuli salama za mataumizi ya bahari ili hizi tabia za makusudi za kuharibu uoto wa asili zisiendelee,” Dk Hatibu alieleza.

Mtaalamu huyo aliendelea kufafanua kwamba kilimo cha mwani kinashuka katika uvunaji wake kutokana na kuwepo kwa mbegu inayotumika hivi sasa ambayo anasema ni ya zamani sana, iliyoletwa Zanzibar mwaka 1980 na ambayo haijawahi kubadilishwa ili kuendana na mabadiliko ya tabianchi.

“Serikali ifanye utafiti kujua ni aina gani ya mbegu inaweza kuhimili hali ya hewa iliyopo sasa,” aliongeza mtaalamu huyo kwenye mahojiano yake na The Chanzo. “Pia, kuwapatia elimu wakulima wa mwani kujua namna ya kuuongezea thamani ili kuweza kuchakata na kuongeza mnyororo wa thamani.”

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts