Mnamo Machi 15, 2024, Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, zamani Twitter, ulitangaza msaada wake uliotoa kwa shule moja huko jijini Dodoma chini ya mpango wa ubalozi huo uitwao ‘Tuwalishe Pamoja.’
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, msaada huo unajumuisha “mchele ulioongezewa virutubisho” pamoja na maharage na mafuta ya alizeti ambavyo vyote ubalozi ulisema vinatoka kwa “wakulima wa Marekani.”
Taarifa hiyo, hata hivyo, imezua mjadala mpana na kuibua hisia nyingi miongoni mwa watumiaji wa mtandao huo wa kijamii, wengi wao wakionesha wasiwasi kuhusiana na mchele huo ulioongezewa virutubisho.
Baadhi ya wachangiaji wanadai kwamba mchele huo unaweza kuwa umetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni, au GMO.
Ni muhimu kufahamu kwamba teknolojia ya uhandisi jeni hutumika kuongeza, kunyamazisha, au kuhariri vinasaba vya viumbe kwa ajili ya faida au kutatua changamoto fulani. Matokeo ya mchakato huo ni kutengeneza genetically modified organisms, yaani viumbe hai vilivyofanyiwa uhandisi jeni.
SOMA ZAIDI: GMO: Suluhisho la Usalama wa Chakula Afrika?
Kwenye kilimo, teknolojia hii inaweza kutumika kutengeneza mimea na wanyama ambao wanaweza kuzalisha zaidi, kustahimili changamoto za kimazingira au kibaiolojia kama vile ukame na magonjwa na hata kuongeza virutubisho.
Mifano ipo mingi, kama vile mahindi yanayostahimili ukame na wadudu waharibifu na mchele wenye kirutubisho cha vitamini A.
Lakini je, chakula hiki cha msaada kutoka kwa Marekani ni GMO au siyo GMO? Kwanza, hakuna mahali kwenye taarifa iliyotolewa na ubalozi kunasema kwamba chakula hicho ni cha GMO.
Pia, ni vizuri kutambua kuwa kuna njia nyingi za kuongeza virutubisho kwa mazao ya chakula, bila kutumia teknolojia ya uhandisi jeni, wengi wanayoita GMO.
Mfano mzuri ni viazi lishe tunavyolima hapa nchini vilivyoongezewa virutubisho bila ya matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni (GM). Kuna sehemu ya nchi pia wanalima mahindi, maarufu kwa jina la yanga, haya siyo GMO, licha ya kuongezewa virutubisho.
SOMA ZAIDI: ‘Sioni Uhususiano Kati ya Majaribio ya Mbegu za GMO na Tanzania Kuwa Tegemezi Kwenye Mbegu’
Ukweli ni kwamba ni miaka ya hivi karibuni tu ndiyo matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni yameanza kutumika kuongeza virutubisho kwenye mazao.
Lakini kwa nini watu wana wasiwasi na GMO? Ni kwa sababu wanadhani kwamba kama teknolojia hiyo imetumika kwenye chakula fulani, chakula hicho hakitakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
Kwenye hili, tungependa kufafanua kwamba Serikali, kupitia taasisi na idara zake, husimamia viwango na usalama wa chakula kwa matumizi ya binadamu na wanyama bila kujali kama chakula hicho kinazalishwa hapa nchini ama kimeagizwa kutoka nje ya nchi.
Pia, Serikali hutumia viwango hivyo hivyo kwa chakula kinachoingizwa nchini kwa ajili ya biashara, viwanda na misaada. Kwenye hili, wale wenye wasiwasi na msaada uliotolewa basi wangehoji usalama wa chakula kwa mlaji badala ya kuhoji kama wakulima walitumia teknolojia ya uhandisi jeni (GM) au la.
Lakini tupende tu kusema na kuwahakikishia Watanzania kwamba chakula kilichozalishwa kwa njia ya GMO, na kuidhinishwa kuingia sokoni, usalama wake kwa mlaji ni sawa na kile kilichozalishwa kwa njia nyingine.
SOMA ZAIDI: ‘Mbegu za GMO ni Hatari kwa Mfumo wa Taifa wa Chakula’
Hapa Tanzania, sera, sheria na miongozo inaruhusu matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni kuanzia hatua ya utafiti, kuagiza, kuingiza, na kutumia bidhaa za GMO. Msisitizo umewekwa kwenye kufuata kanuni husika.
Hata hivyo, kumekuwepo uwekezaji mdogo sana kwenye teknolojia hii kutokana na ukweli kwamba kanuni zilizowekwa zimejikita zaidi kwenye udhibiti au kuzuia kuliko kuweka mazingira wezeshi ya matumizi salama ya teknolojia hii.
Pamoja na ugumu huo, mtu, kampuni au taasisi yoyote ikiridhia kufanya utafiti au biashara katika mazingira hayo, inaweza kuomba kibali ofisi ya Divisheni ya mazingira, Makamu wa Rais Muungano. Iwapo watapata kibali, basi wanaweza kuendelea na programu husika.
Tumalizie safu hii kwa kuuliza swali ambalo wachangiaji wengi pia waliliibua baada ya taarifa hiyo ya Ubalozi wa Marekani: je, ni kweli Tanzania imeshindwa kujilisha mpaka kufikia hatua ya kupatiwa msaada?
Pamoja na kua na ardhi yenye rutuba ya kutosha, maeneo yanayopata mvua za kutosha au maji ya kutosha kufanya umwagiliaji, wataalamu wa utafiti wa kilimo na asilimia kubwa ya wananchi wanaojihusha na kilimo, kwa nini bado kuna changamoto ya chakula nchini?
SOMA ZAIDI: Kilimo na Umasikini, Malaysia na Tanzania
Ni muhimu sana kuongelea masuala ya usalama wa chakula, hasa kinapokuja kutoka sehemu nyingine, lakini ni muhimu zaidi kujitafakari tunapokwama ili kuweza kufikia utoshelevu wa chakula hapa nchini kwetu.
Kuna msemo unasema mgonjwa hachagui dawa. Japo leo tunaongea sana kuhusu huu msaada, ila siku tatizo la njaa likiwa kali zaidi hatutakuwa na muda na nafasi ya kujadili usalama wake. Tuwekeze kwenye kujitosheleza kwa chakula kama taifa.
Philbert Nyinondi anafundisha mawasiliano ya sayansi katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), anapatikana kupitia pnyinondi@yahoo.com. Aneth David anafundisha Bioteknolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anapatikana kupitia anethdavid367@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.