Shughuli za sera ya mambo ya nje ya Tanzania zimechangamka zaidi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, nchi ikipiga hatua katika kujenga upya uanuai na imani katika ushirikiano wa nje baada ya kipindi cha kujitenga chini ya mtangulizi wake.
Mapitio rasmi ya sera ya mambo ya nje ambayo yamekuwa yakiendelea tangu mwaka 2023 yanatoa fursa sasa ya kusimika uamsho huu na kuhakikisha kuwa mahusiano ya nje ya Tanzania yanatoa manufaa makubwa kwa wananchi wake, pasipo kukiuka miiko ya msingi.
Kati ya mwaka 2022 na 2024, taasisi ya sera za kimataifa Chatham House na ofisi ya Konrad-Adenauer-Stiftung (KAS) ya Tanzania wameshirikiana katika mradi wa utafiti kuchambua hali ya sera ya mambo ya nje ya Tanzania. Mradi huu umewaleta pamoja wataalamu wa mambo ya nje na watunga sera kujadili fursa zinazojitokeza katika mchakato wa mapitio.
Utafiti uliyochapishwa hivi karibuni, Reviving Tanzania’s Regional Leadership and Global Engagement: Priorities for an Effective Foreign Policy Reset, au kwa tafsiri isiyo rasmi sana, Kufufua Uongozi wa Kikanda na Ushiriki wa Kimataifa wa Tanzania: Vipaumbele vya Sera Mpya ya Mambo ya Nje, ni matokeo ya mchakato huu, na unatoa mapendekezo ya sera kwa wadau wa Tanzania na washirika wa kidiplomasia. Utafiti huu unaweza kusomwa kikamilifu hapa.
Utafiti huu unaweka wazi kwamba mwenendo wa polepole, au wa kusitasita, pekee hautatosha kuilinda nchi dhidi ya kurudi kwa sera umizi ya kujitenga ya kiongozi aliyepita. Mkakati mpya wa Tanzania lazima uweke msisitizo kwa kushirikiana kikamilifu na taasisi za kikanda na washirika wengine wa kimataifa.
Vipaumbele
Kukamilika kwa tathmini ya sasa ya sera ya mambo ya nje bila shaka kutatoa msukumo katika masuala mengi ya maudhui kuhusu mahusiano ya nje. Mengi ya haya ni rahisi na hayana utata: kwa mfano, mafanikio ya haraka yatapatikana kwa kuweka marejeleo ya ‘uchumi wa bluu’ au mabadiliko ya tabianchi kwa mara ya kwanza.
Bila shaka, masuala haya ni muhimu kabisa, lakini kuingizwa kwake kwa moja kwa moja kusisababishe, au hata kuwezesha, kubweteka.
SOMA ZAIDI: Mapinduzi ya Kijeshi Niger: Je, Mfumo ‘Amerafrique’ Kuchukua Nafasi ya ‘Francafrique?’
Kazi halisi katika mapitio haya ya sera ya mambo ya nje ya Tanzania ipo katika kuweka wazi maono thabiti ya kimkakati, kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa masuala ya kimataifa, na kufanya vyote hivi viendane na uratibu mzuri wa mifumo ya ndani.
Hii ya mwisho lazima iwe ni pamoja na kuipa sera ya mambo ya nje nafasi muhimu katika mkakati wa maendeleo – Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050–, na kuoanisha sera nyingine, kwa mfano zile zihusuzo mabadiliko ya tabianchi na madini muhimu, ili kuchangamkia kikamilifu fursa za kimataifa zilizopo.
Katika muktadha wa kikanda, mahusiano ya Tanzania na majirani zake, ikiwa ni pamoja na Kenya na Msumbiji, yameimarishwa zaidi chini ya uongozi wa Rais Samia. Sasa kuna jukwaa la wazi la kukuza uongozi wa taasisi kwa kuridhia mikakati mbalimbali kama vile Mkataba wa Biashara Huria, au Tripartite Free Trade Agreement (TFTA) kwa kimombo, kurejesha ushiriki wa kikamilifu katika masuala ya usuluhishi na kutatua migogoro, na kujiunga tena na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
Hatua kama hizo zitakuwa na uwiano na jukumu, au nafasi, ya kihistoria ya Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini na mwenendo wake wa kiuchumi unaotarajiwa.
Ramani ya maendeleo ya miundombinu ya kikanda ya Tanzania (Chanzo: Chatham House).
Hali ya biashara kati ya Tanzania na nchi zingine za EAC na SADC, 2018–23 (Chanzo: Takwimu za Benki ya Tanzania).
Katika jukwaa la kimataifa, kurejea kwa wazi kwa ushirikiano na washirika mbalimbali wa kimataifa tayari kunaleta uwanja mkubwa wa machaguzi na uthabiti zaidi katika fursa za kibiashara na uwekezaji wa kigeni.
Mifano ya suala hili iliyojadiliwa kwa undani zaidi katika utafiti ni jitihada za kujenga mahusiano imara na nchi kama vile Indonesia na Vietnam; kudumisha ushirikiano wa kimkakati unaoibuka, hususan na nchi za Ghuba za Kiarabu; na urekebishaji wa mahusiano yaliyoanzishwa na China, India, na washirika wa nchi za Magharibi.
SOMA ZAIDI: Jumuiya ya Madola Imepoteza Dira, Muelekeo. Hiyo Inaiathiri Vipi Afrika?
Uwekezaji wa nje katika miradi mikubwa ya miundombinu umeibuka kuwa mstari wa mbele katika diplomasia ya kiuchumi ya Tanzania, na una mchango wa moja kwa moja katika mahusiano na washirika wa kimkakati wa nchi.
Lakini kama utata kuhusu bandari ya Dar es Salaam unavyoonyesha, ukosefu wa uwazi na mawasiliano au taarifa za wazi kuhusu faida zinazotokana na mahusiano haya kumechochea dhana ya utengano kati ya dola, au Serikali, na maslahi ya umma.
Ufufuaji wa taratibu wa ushiriki na sauti ya Tanzania katika masuala ya kimataifa na ya pande nyingi pia unaendelea. Lakini ufufuaji huu bado haujatiwa msukumo na hatua madhubuti za kurejea katika makubaliano ambayo nchi ilijitoa wakati wa mwenendo wake chini ya Serikali iliyopita.
Fursa zaidi zipo zinazohitaji uongozi wa Tanzania katika kutatua changamoto na fursa mbalimbali za kimataifa, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, madini muhimu, na udumishaji wa amani.
Mwisho wa siku, kurudisha tu upya diplomasia ya kiuchumi isiyofungamana na upande wowote hakutaakisi kikamilifu kazi ya uhodari wa Tanzania ambayo tayari imefanywa kurejesha taswira ya kimataifa ya Tanzania, wala kazi ambayo bado inapaswa kufanywa.
Rais Samia amesema kwamba lengo la sera yake ya mambo ya nje ni kwa Tanzania kurudi ‘mahali pake sahihi’ pa uongozi wa kimataifa. Uhuishwaji wa sera ya mambo ya nje ambayo ni thabiti na inayoonyesha vipengele chanya vya mkakati usiyofungamana na upande wowote ingekuwa hatua muhimu kuelekea kufikia lengo hilo.
Kiwango cha uuzwaji wa nje wa Tanzania kwa uelekeo na kiwango cha manunuzi kwa chanzo, 2013–22 (Chanzo: Umoja wa Mataifa (2023) ‘UN Comtrade Database’, Idara ya Masuala ya Uchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa.
Mapendekezo ya kisera
Utafiti huo kutoka Chatham House na KAS unatoa mlolongo wa mapendekezo ya kina yaliyowalenga watunga sera wa Tanzania na washirika wa kimataifa wa Tanzania, ambapo yafuatayo ni muhtasari. Pamoja na mapendekezo maalum, utafiti unawataka watunga sera:
SOMA ZAIDI: Tafakuri Fupi Kuhusu Filamu ya Tanzania: The Royal Tour
Kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza muungano wa kiuchumi wa kikanda. Tanzania lazima ichukue fursa katika eneo la ukanda wa karibu, huku ikitarajia kuwa taifa lenye uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki na kusaidia kulinda uwezekano wa miradi mikubwa ya miundombinu inayovuka mipaka.
Simika nafasi ya Tanzania katika kutatua migogoro ya kikanda. Ili kuondoa dhana ya kuwa na maslahi yaliyogawanyika na kuendeleza rekodi ya kihistoria ya Tanzania katika juhudi za upatanishi wa migogoro, mapitio ya sera yanaweza kuimarisha jukumu la Arusha na Zanzibar katika kuwa wenyeji wa mazungumzo na kuonyesha uongozi katika masuala ya jumla ya usalama Afrika Mashariki na Kusini, ikiwa ni pamoja na katika eneo la bahari.
Rejesha uanachama katika jitihada za uongozi na kisheria za kimataifa. Tanzania inapaswa kurejesha uanachama wake katika mikataba na jitihada ambazo awali ilijiondoa, kama vile Open Government Partnership (OGP), na kuweka ulinzi wa kisheria wa kuzuia kuondoka tena siku za usoni.
Hakikisha mkakati mpya unasisitiza wazi lengo la kushirikiana na kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi nyingine za kipato cha kati. Hii inaweza kujumuisha kuimarisha zaidi uhusiano na washirika wanaochipukia kama vile Indonesia, Vietnam, na nchi za Kati na Mashariki mwa Ulaya.
Kukumbatia fursa za uongozi wa kimataifa ili kupigia chepuo misingi ya muhimu ya ushirikiano wa Kusini-Kusini. Tanzania inaweza kutoa ishara ya nia yake ya kutafuta uanachama usiokuwa wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006, ikionyesha umoja na michango yake ya sasa katika kulinda amani na kukuza ajenda yake ya mageuzi ya Umoja wa Mataifa kwa ujumla.
SOMA ZAIDI: Kauli ya Samia Kwamba Alitofautiana na Magufuli Kwenye Mambo Mengi Inatufundisha Nini?
Kuwa wazi kuhusu makubaliano ya uwekezaji wa kigeni na kuruhusu maoni yanayopinga sera ya mambo ya nje kutolewa kwa uhuru. Kushughulika kwa mabavu kwa ukosoaji – kama vile kuhusu uwekezaji wa miundombinu katika bandari unaofanywa na nchi za Ghuba – yanaweza kuzidisha mwelekeo wa kujitenga na hatimaye kukatisha tamaa ushiriki wa washirika wa kigeni katika miradi mikubwa muhimu.
Nenda mbali zaidi ya maneno matupu pale sera inapozungumza kuhusu mabadiliko ya tabianchi na masuala mengine ya mazingira. Mapitio lazima yasaidie katika kuunda hadidu za rejea kwa maafisa wa Tanzania wanaposhiriki katika mabaraza ya kimataifa wakati wakifuatilia miradi mikubwa ya mafuta na gesi. Maendeleo ya mkakati wa madini muhimu pia yanapaswa kulinganishwa na malengo ya nchi katika diplomasia ya kiuchumi.
Onyesha mbinu mpya na tofautisha mkakati mpya wa sera ya mambo ya nje na ule wa utawala uliopita kwa kutumia lugha mpya. Mkakati mpya lazima uonekane kama hatua ya mageuzi, na lazima ukatae desturi zilizojipenyeza za kutokuaminiana na kusuasua katika mahusiano ya nje.
Kubakiza mtazamo uleule wa kimkakati wa msingi wa diplomasia ya kiuchumi na kutokufangamana na upande wowote, huku vikiongezwa vipengele vipya, kunaweza kupeleka ujumbe wa utulivu zaidi kuliko maazimio ambayo Tanzania inastahili.
Fergus Kell ni meneja miradi na mchambuzi wa tafiti kutoka Chatham House, Programu ya Afrika. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia FKell@chathamhouse.org au katika mtandao wa X kama @FergusKell. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.