The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tafakuri Fupi Kuhusu Filamu ya Tanzania: The Royal Tour

Filamu ya Tanzania: The Royal Tour inaelekea kufanikiwa katika hatua hii ya pili baada ya uzalishaji. Lakini siku za usoni tusifanikiwe kwa kubahatisha. Ni muhimu kwa vyombo vyetu, hasa vile vya sanaa, kuwa na mipango mikakati ya kukuza sanaa Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Aprili 27, 2022, nilifanikiwa kukutana na Peter Greenberg, ambaye ni mtayarishaji wa kipindi cha televisheni cha The Royal Tour na nilipata fursa ya kuzungumza naye mambo mengi kuhusu kipindi hicho na uzoefu wake kama mwanahabari na mzalishaji wa vipindi vya televisheni vya utalii duniani kwa miaka mingi, akifanya kazi na shirika kubwa kabisa la CBS la nchini Marekani.

Ninamshukuru Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bwana Donald Wright aliyenialika nyumbani kwake kwa mapokezi mazuri na ukarimu wake, pamoja na wafanyakazi wa ubalozi. Nimepata nafasi ya kuongea na maafisa kadhaa kwenye dawati la utamaduni ubalozini hapo na kuweza kujifunza mengi.

Wakati wa mazungumzo yetu, Greenberg alitangulia kwa kusema kuwa anaiona Tanzania kama nchi nzuri sana yenye amani na la msingi, kwa maneno yake, Tanzania ni nchi inayoruhusu mazungumzo.

Watu kuzungumza, kwa mujibu wake, ni jambo la msingi na la kistaarabu. Wakati onyesho la filamu hiyo ya Tanzania: The Royal Tour uliofanyika nyumbani kwa balozi hapa Dar es Salaam tuliona vipande vipande vilivyochaguliwa na siyo sinema yote kwa sababu ya muda lakini pia kupisha mazungumzo baina ya waalikwa na mtayarishaji huyo.

Kwa msingi huo, siwezi kufanya uchambuzi wa kitaalam wa kimaudhui juu ya filamu hiyo.

Magufuli hakuvutiwa kushiriki

Greenberg alinieleza kwamba amekuwa akijaribu kutengeneza filamu hiyo nchini Tanzania kwa miaka mingi, kuanzia kipindi cha Rais Jakaya Kikwete, ambaye alikubali kushiriki ingawa wasaidizi wake hawakupenda wazo hilo.

Greenberg alibainisha kwamba alimjaribu Hayati Rais John Magufuli lakini Rais huyo wa awamu ya tano hakuvutiwa kushiriki kwenye filamu hiyo.

Kipindi cha The Royal Tour, alisema Greenberg, kilianza mnamo mwaka 2000 wakati Mfalme Abdullah II bin Al-Hussein wa Jordan alipokubali kushiriki kwenye filamu hiyo iliyopewa jina la Jordan: The Royal Tour.

Tanzania: The Royal Tour itaonyeshwa katika chaneli 350 duniani. Filamu hii imepata onyesho maalum la kwanza (premiered) huko nchini Marekani kisha kufuatiwa na streaming, halafu ikaonyeshwa jijini Arusha kabla haijakwenda Zanzibar na kumalizia jijini Dar es Salaam.

Mfululizo wa vipindi hivi utakuwepo kwenye mtandao kwa miaka mingi ijayo na kuangaliwa na watu wengi zaidi.

Greenberg amesema kuwa amekabidhi rekodi zote, zikiwamo zile ambazo hazikuingizwa kwenye vipindi, yaani raw footages, kwa Wizara ya Maliasili na Utalii ili waweze kuzitumia.

Mnamo Aprili 28, 2022, wakati akiwa jijini Arusha Rais Samia Suluhu Hassan amefafanua kwamba pesa zote zilizotumika katika utengenezaji na utayarishaji wa filamu ya Tanzania: The Royal Tour zimetokana na michango ya wafanyabiashara mbalimbali ndani ya sekta ya utalii na nje ya utalii.

Hii ni tofauti na baadhi yetu tulivyofikiri mwanzoni kuwa mashirika yetu kama vile Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yalichangia gharama hizo.

Fikra kwamba mashirika haya yamechangia utengenezaji wa filamu hii ilichangiwa na barua ya Aprili 18, 2022, iliyoandikwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyoyatambua mashirika haya yaliyopeleka wawakilishi huko kwenye uzinduzi nchini Marekani kama “wafadhili.”

Vyovyote vile iwavyo, nchi yetu imewekeza na ni mzalishaji (producer) wa filamu hiyo, hivyo asilimia fulani ya mapato yatokanayo na uuzwaji, fedha za leseni (licencing) ya filamu hii tunapaswa kufaidika nayo.

Swali nisiloweza kulijibu ni kuwa je, jambo hilo liko kimkataba?

Utalii wa utamaduni

Alipoulizwa swali kuhusu utalii wa utamaduni, Greenberg alisema hakuna utalii bila utalii wa utamaduni. Greenberg aliongeza kwa kubainisha kwamba wageni wengi wanaokuja kutalii Tanzania ni watu wenye akili zao na wakisha kuangalia vivutio hutaka kujua maisha ya watu na tamaduni zao.

Nilipomuuliza juu ya nini kifanyike ile Watanzania waanze kutengeneza filamu kwa kutumia vivutio vyetu ambavyo kwa sasa vinatumika na wageni na kuhusu soko la filamu hizo duniani, Greenberg alisema kitu cha msingi ni kueleza hadithi na mambo yenu, akaongeza kuwa soko lipo tena kubwa sana.

Greenberg anadhani ni muhimu kulidhibiti hilo soko, yaani kudhibiti idadi ya watalii ili kusiwe na uharibifu na utalii uwe wa kudumu.

Nilipomuuliza kuhusu suala la uzalishaji wa kazi bora za filamu, Greenberg alisema kwa kurudia: “Jengeni studio za uzalishaji zenye ubora.” Aliposema hivi niliikumbuka miundombinu ya filamu nchini, moyoni nilijisemea tu, “Hajui nchi nzima hii tuna majumba 11 tu ya filamu yanayofanya kazi.”

Kwenye eneo la ujuzi, Greenberg alisema kuwa Tanzania: The Royal Tour imeshirikisha Watanzania, yaani local crew, katika uzalishaji wake kwani watu tisa katika crew ya watu 43 walikuwa ni Watanzania. Hiyo si haba kwani ni takriban asilimia 30 ya crew nzima.

Siku za usoni ni muhimu jambo hili liwe la kisheria ili kuhakikisha ipo ‘kwota’ ya watu wetu katika kila uzalishaji wa filamu utakaofanyika nchini ili kupata ujuzi.

Wapi Bodi ya Filamu?

Kwa mtazamo wangu, toka zoezi hili la kutengeneza filamu hii lianze inaonekana wazi kuwa Bodi ya Filamu haikushirikishwa kikamilifu, na kama walishirikishwa basi kwa uhafifu sana.

Inasikitisha kuona hawaonekani kwenye hatua nyingi, ikiwemo kwenye uzinduzi wa kule nchini Marekani. Kama tuliwapeleka akina TANAPA, NCAA, TTB, TAWA na TFS basi tungewapeleka na Bodi ya Filamu pia. Hii naisema nikizingatia tulipeleka watu wengi huko. Ni muhimu siku za usoni washirikishwe ili kuwajengea uwezo.

Wakati vijana wetu hapa ndani wanabanwa na masharti haya, filamu hii ilipewa njia ya mwendokasi kwani haikuwasilisha andiko la muswada (script) wala raw footage kabla ya umaliziaji wake kama sheria inavyotaka.

Binafsi sizipendi sheria hizi kwani siyo rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje. Basi tuzirekebishe. Nafahamu Wizara ya Sanaa na Bodi ya Filamu wako katika zoezi la kuziandika kanuni zetu upya.

Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) pia hawakushirikishwa. Utengenezaji wa filamu una asilimia 80 ya taaluma kwenye sanaa za uoni (visual arts). Kama tunakubali kuwa utalii wa utamaduni ni sehemu nyeti ya utalii basi BASATA ina nafasi ya kipekee ya kushiriki.

Hivyo, nafasi ya BASATA ni ya msingi hasa katika kujifunza, kuweka kumbukumbu lakini pia kuingiza katika mipango. Tukumbuke BASATA ndiye msajili wa wasanii wote na hata Mama Rais Samia ajitayarishe kwenda kusajiliwa huko.

Kushirikisha vyombo hivi kikamilifu pia kunasaidia kuandikwa kwa ripoti mbalimbali ambazo zingesaidia kuongoza utafutaji masoko, utungaji sera, kanuni na sheria.

Biashara kwanza, siasa baadaye

Kwa nchi ya siasa-mbele kama Tanzania changamoto kubwa ni kuifanya Tanzania: The Royal Tour kuwa jambo lenye lengo la kibiashara na kiutalii badala ya jambo la kisiasa.

Tunaona kuwa kwa sasa baadhi ya vyombo vyetu vinaliuza jambo hili kama la kisiasa zaidi. Vyombo hivi huchukua muda mwingi kumsifia Rais Samia. Filamu ya Tanzania: The Royal Tour si maalum kwa ajili ya Samia bali inatangaza nini Tanzania ilichonacho na ambacho inaweza kuipatia dunia!

Nimeona viongozi wengi wakipita kwenye vyombo vya habari wakidai, “Tukae mkao wa kula kwani baada ya Royal Tour Tanzania itapata watalii wengi sana.” Hii siyo sahihi kwani bidii kubwa inahitajika kwenye maeneo mengi ili kuwavuta watalii.

Rais Samia amefanya kazi yake, sasa unapoongea na hadhira ya ndani kwa lengo la kukuza utalii wa ndani husemi “Mama kaupiga mwingi” bali unaoanisha bidhaa mbalimbali kama wanyama, uzuri wa maeneo, ngoma na maajabu yaliyopo katika nchi yetu kimkakati ili kuvutia Watanzania waende kuona maajabu hayo.

Kwa mujibu wa Greenberg, Serikali nyingi duniani hazifanyi vizuri katika kuvutia watalii. Kwa hiyo, Tanzania ina nafasi nzuri ya kufanya kazi hiyo.

Kwa mtazamo wangu, nafikiri hatutakiwi kutangaza jina ‘Royal Tour’ kwani royal tour ziko nyingi bali ‘Tanzania Royal Tour.’ Pia, ni muhimu kutambua kwamba filamu hii inalenga kuvutia watalii wa nje na siyo wale wa ndani.

Hivyo, nguvu ielekezwe huko. Balozi zetu na taasisi za utalii zinaweza kushiriki vyema.

Greenberg amekubali kuwa hakwenda kabisa kwenye eneo la Kusini mwa nchi yetu bali ameishia Kaskazini. Kwa maoni yangu, huku Kusini siyo tu kuna vivutio vizuri bali maeneo aliyoenda ya Kaskazini siyo mageni kwa watalii duniani, haya yameshatangazwa sana siku za nyuma.

Ingependeza kama angeenda pia kufukua tamaduni na maisha, mbuga, makabila ya Kusini kama Wamakua, Wangoni, Wamakonde, Wanyakyusa na wengineo na hili lingechangia kuleta jambo jipya katika senema hii.

Ni upi mkakati wa Tanzania kwenye utalii wa utamaduni?

Ni muhimu sasa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ikishirikiana na Wizara ya Utalii na wadau husika, ikakaa na kuona ni jinsi gani watatengeneza mpango wa kitaifa wa utalii wa kiutamaduni.

Muhimu pia kupitisha Sera ya Filamu, Sera ya Miliki Bunifu na kuandika sheria mpya ya filamu kwani iliyopo ni ya 1976 ambayo imepitwa na wakati. Baadhi ya wanaoshangilia ‘mama kuupiga mwingi’ ndiyo hao wamekuwa kikwazo katika kuboresha sekta ya filamu iliyojaa wizi tena wa waziwazi kabisa nchini.

Filamu ya Tanzania: The Royal Tour inaelekea kufanikiwa katika hatua hii ya pili baada ya uzalishaji. Lakini siku za usoni tusifanikiwe kwa kubahatisha. Kwa nini nasema hivi? Kwa sababu mpaka sasa vyombo vyetu, hasa vile vya sanaa, havina mipango mikakati.

Bodi ya Filamu, wizara husika, na BASATA hawana mipango ya kimkakati. Huko mbeleni tusisubiri “Peter” mwingine aje na mradi kisha nasi turuke naye tukishangilia kwa vigelegele.

Tutengeneze mpango mkakati wetu wa miaka mitano na pawepo mahala panapozungumzia uwekezaji kutoka nje katika filamu. Tunajua Serikali iko mbioni kuandika Sera ya Uwekezaji basi ni vyema ikumbuke kuandika yahusuyo katika filamu na sanaa kwa ujumla.

Robert Mwampembwa ni msanii, mwandishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mtandao wa Sekta Bunifu Tanzania (CINT). Kwa maoni, anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni ‎robert@ubunifu.co.tz. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 Responses

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *