The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tufuatilie Sakata la Man City kwa Makini Tukijitathmini

Sakata la Manchester City lina somo kubwa kwa soka la Tanzania, lakini kama tutalifuatilia kwa makini na kuangalia maeneo ambayo yanalingana na hali yetu kwa sasa

subscribe to our newsletter!

Kwa sasa dunia inafuatilia kwa makini na kusubiri kwa hamu mwenendo na uamuzi wa mashtaka 115 ya uvunjaji wa kanuni za kifedha unaotuhumiwa kufanywa na klabu ya Manchester City inayoshiriki Ligi Kuu ya soka ya England.

Kamisheni huru inayosikiliza shauri hilo ilianza kazi Jumatatu ya Septemba 16 baada ya Ligi Kuu ya England kuituhumu klabu hiyo kuwa ilikiuka kanuni za kifedha, maarufu kama Financial Fair Play (FFP), ambazo zinataka klabu kutumia fedha kulingana na mapato yake.

Ligi Kuu inadai kuwa mbali na kudanganya kuhusu mapato inayopata kutoka kwa mdhamini, Man City haikutoa ushirikiano wakati wachunguzi wa tuhuma hizo walipokuwa wakihitaji nyaraka kwa ajili ya kusaidia uchunguzi.

Iwapo mabingwa hao wa England watatiwa hatiani, adhabu inaweza kuwa ni kuondolewa katika mashindano yote, kupokonywa pointi au kushushwa daraja, uamuzi ambao utakuwa wa kihistoria katika ulimwengu wa soka, na hasa baada ya kanuni hizo kutungwa mwaka 2019 kuzilinda klabu na kuporomoka kwa uchumi wa dunia kulikosababishwa na ugonjwa wa UVIKO-19.

Kashfa hiyo iliibuliwa kwanza na raia wa Ureno, Rui Pinto, ambaye alifungua tovuti ya Football Leaks iliyochapisha nyaraka za siri kwa vyombo vya habari, yakiwemo mawasiliano ya ndani ya barua pepe ya Man City kuhusu udhamini na malipo.

SOMA ZAIDI: Sakata la Lawi, Kagoma ni Utapeli Katika Soka

Kama ilivyo kawaida kwa wafichua uovu, Pinto alishtakiwa kwa kosa la kupata nyaraka hizo isivyo halali na mahakama ya Ureno ikamuhukumu kifungo cha miaka mine, huku utekelezaji wa adhabu hiyo ukizuiwa kwanza.

Baadaye jarida  la Der Spiegel la Ujerumani likachapisha nyaraka za kashfa hiyo na kuibua mijadala mikubwa barani Ulaya.

Kutokana na umakini wa wenzetu kwa watu wanaoibua uovu na uhalifu, suala hilo halikuishia kwa hukumu ya Pinto na taarifa za Der Spiegel pekee, bali uchunguzi uliendelea na ulifanyika kwa miaka mine na sasa shauri la Ligi Kuu lililotokana na kazi ya Pinto, limewasilishwa mbele ya kamisheni hiyo huru na uamuzi wake unaweza kusababisha mabadiliko makubwa katika uendeshaji soka.

Sisi huku wa dunia ya tatu tunafuatilia suala hilo kama sinema kwamba linawezekana barani Ulaya tu, na si huku kwetu ambako ni vigumu kwa nyaraka kama hizo kudukuliwa na hata zikidukuliwa kutatafutwa kila mbinu kuzidogosha na kuonyesha kuwa aliyezidukua alikuwa na njaa zake na si kwamba alifanya hivyo kwa maslahi ya mchezo wenyewe au ya taifa kwa ujumla.

Mafunzo

Lakini kuna mambo mengi zaidi ya kujifunza katika suala hilo bila ya kujali hukumu dhidi ya Manchester City itakuwaje.

SOMA ZAIDI: Tumeanza Vibaya AFCON 2025 Lakini Hatujuti

Kanuni makini na nzuri kuhusu uungwana katika masuala ya kifedha ndio zilisababisha Pinto afanye kila jitihada kutafuta ukweli wa udhamini wa Manchester City na utoaji fedha wa mmiliki, ambaye ni familia tawala ya Abu Dhabi.

Kanuni hizo zina vipengele vingi vinavyodhibiti mtiririko wa fedha zisizotokana na mapato ya mpira wa miguu kwenda kwenye klabu. Hii husaidia pia kudhibiti utakatishaji fedha na ndio maana wakati fulani ilibidi mmiliki wa City alazimike kununua haki za jina la uwanja na kuuita Etihad baada ya kutuhumiwa kumimina fedha klabuni kinyume na kanuni hizo za FFP.

Hivi karibuni, klabu za Ligi Kuu zilikubaliana kuimarisha kanuni hizo kwa kuweka kifungu cha muamala kutoka mshirikishwaji, au kwa kifupi fedha kutoka kwa mdhamini, au third party, kwa kimombo. 

Kanuni hiyo inayoitwa Associated Party Transaction (APT) inataka fedha zinazotolewa na mdhamini zilingane na thamani ya soko na imeweka taratibu nyingi za utoaji wa fedha kutoka kwa mdhamini, ikiwa ni pamoja na kutoa tamko kwanza na kumpa nafasi msajili kuchunguza kama fedha hizo zinalingana na mahitaji.

Tunaweza kufikia

Ni mambo ya kiufundi sana ambayo mtu wa kawaida kutoka dunia yetu akiangalia anaweza kukata tamaa na kusema hatuwezi kufikia huko waliko wenzetu. 

SOMA ZAIDI: Ubashiri Hatma ya Samatta Stars Haukutakiwa Kuwepo

Lakini ukweli ni kwamba hata wao kuna sehemu walianzia katika kutaka kudhibiti uchumi wa klabu na kuulinda mpira wa miguu dhidi ya misukosuko ya kiuchumi na kufanya mambo kwa utashi wa mtu mmoja na hivyo kutokuwa na uhakika kama kesho ataendelea au ataamka vibaya na kuvuruga kila kitu.

Ni muhimu basi kwa mamlaka zetu za soka kufuatilia sakata la Manchester City kwa makini na kuangalia ni jinsi gani zinaweza kuanza kutengeneza kanuni za kuzilinda klabu zetu na misukosuko ya kiuchumi, utakatishaji fedha, kusaidia kampuni kukwepa kodi na hata kudhibiti matumizi yanayoweza kuathiri ushiriki wa timu katika mashindano.

Hadi sasa, Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) haina nguvu zozote za kudhibiti klabu kifedha. Matumizi yamekuwa ni makubwa, hasa katika kusajili wachezaji wa nje, kuliko uhalisia wa mapato yao na hivyo si ajabu ligi kuanza na msukosuko wa kutokamilisha taratibu za usajili kama ilivyokuwa kwa Tabora United msimu uliopita na huu, na pia Singida Fountain Gate.

Hakuna klabu inayowajibika kuwasilisha TPLB taarifa zake za fedha ili kujua uwezo wake wa kushiriki kikamilifu mechi zote za ligi na kulipa wachezaji na wafanyakazi wake wote kwa kadiri ya mikataba yao.

Kushtakiwa FIFA

Limekuwa ni jambo la kawaida kusikia klabu zinashtakiwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) kwa kushindwa kuwajibika kulipa haki za wachezaji zilioachana nao na siku zote klanbu hizo zinapatikana na hatia na kuilipishwa faini kubwa. Ni aibu kwa soka la Tanzania lakini pia si afya.

SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Iondoe Hisia Hasi za Udhamini

Kanuni zinataka klabu ziwe zinawasilisha taarifa za fedha na sheria ya nchi hali kadhalika. Lakini inaonekana kama si muhimu, hasa kwa kuwa kanuni hizo zimebakia kuwa na sentensi moja isiyo na utaratibu wa nini kifanyike na hatua gani zinaweza kuchukuliwa.

Bila ya kuanzia hapo, tunaweza kujikuta tumeachwa mbali na uovu wa wamiliki na wawekezaji utakapokithiri, mamlaka za Serikali zitalazimika kuingilia kati na hapo ndipo patakuwa mwanzo wa kusambaratika kwa baadhi ya klabu, na hata soka kwa ujumla.

Ni muhimu sana TPLB ianze kutafuta mbinu za jinsi ya kuwa na sauti katika mapato na matumizi ya klabu ili ile haki katika mpira ionekane na si klabu zitumie fedha ambazo hazitokani na shughuli zake za soka.

Hii pia itadhibiti utakatishaji fedha, lakini muhimu zaidi pia itaiwezesha TPLB kujua wamiliki na wawekezaji katika hizi klabu kwa sababu miamala kutoka kwao itakuwa inasomeka na inaeleweka imetolewa kwa sababu gani.

Sakata la Manchester City lina somo kubwa kwa soka la Tanzania, lakini kama tutalifuatilia kwa makini na kuangalia maeneo ambayo yanalingana na hali yetu kwa sasa.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *