The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali Ianze Kutoa Ruzuku kwa Vyama Teule vya Michezo

subscribe to our newsletter!

Nimemsikia Waziri wa Utamaduni, Michezo na Sanaa, Damas Ndumbaro, akiahidi kuwa Tanzania itatwaa medali kwenye michezo ijayo ya Olimpiki itakayofanyika Marekani mwaka 2028.

Ni ahadi nzuri na iliyotolewa kwa wakati muafaka. Kwamba leo, mwezi mmoja baada ya kumalizika kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris, angalau Serikali imeelekeza macho kwenye michezo ijayo itakayofanyika miaka mine ijayo.

Maana yake ni kwamba huenda kuna mkakati mkubwa wa kuanza maandalizi mapema ili ifikapo mwaka 2028 tuwe na wanamichezo wanaoweza kushindana na kushinda katika mashindano hayo makubwa duniani.

Na kwa kweli tumetoka kwenye aibu baada ya kutuma wanamichezo saba jijini Paris ambao wamerejea mikono mitupu. Kati ya wanamichezo saba, ni wanne tu waliofuzu kushiriki Olimpiki, yaani wanariadha wa marathoni ambao katika mashindano mbalimbali ya kimataifa waliweza kufikia muda uliowekwa wa kushiriki Olimpiki.

Lakini wale wa judo na kuogelea walipata tiketi ya upendeleo na hata hivyo hawakuweza kufanya maajabu yoyote.

Kuna mkakati?

Ahadi ya Ndumbaro ina mkakati wowote nyuma yake? Huenda ni kweli amethubutu kumuahidi Rais wa nchi kuwa tutaweza kutwaa medali kwa kuwa anajua ameweka mkakati gani. 

SOMA ZAIDI: Tufuatilie Sakata la Man City kwa Makini Tukijitathmini

Lakini hajauweka bayana. Lakini pia inawezekana ametoa ahadi hiyo kisiasa, kwamba hadi mwaka 2028 hatakuwa wizara husika, na hivyo hakuna ambaye atamuuliza imekuwaje iwapo hatutatwaa medali. 

Na hata kama akiulizwa, huenda jibu lake litakuwa rahisi tu kwamba hayupo wizara husika. Kama kweli kuna mkakati, basi sisi wadau tunachangia tu kuuboresha.

Jijini Paris tulipeleka timu za michezo mitatu: riadha, judo, na kuogelea. Lakini tuna michezo mingi inayoweza kutusaidia kutuma wanamichezo wengi zaidi iwapo vyama vitawezeshwa. 

Michezo kama mpira wa kikapu, wavu, ngumi za ridhaa, mikono, mpira wa magongo, wa meza na mbio za masafa ya kati na fupi imelala kutokana na ukosefu wa fedha, lakini inaweza kuwa kimbilio.

Mchezo mwingine ambao hauko kwenye Olimpiki ni mpira wa pete au netiboli. Huu ni mchezo ambao msichana wa Kitanzania anakutana nao mapema anapoanza kupata akili. 

Unaweza kuwa ni mchezo wa pili kwa ukubwa nchini Tanzania kutokana na urahisi wa kuucheza na unafuu wa vifaa vyake na miundombinu, kama ulivyo mpira wa miguu.

Ni muhimu kwa Serikali kuiangalia michezo hii kwa jicho kubwa zaidi. 

Fedha

Na hii itahusisha kukaa pamoja na vionghozi wa vyama hivyo na kujadili jinsi ya kuisisimua michezo hiyo na tatizo la ukosefu wa fedha ambalo ndilo kuu. Ukiacha mpira wa miguu unaoweza kuingiza mabilioni ya fedha, michezo mingine haiwezi kuingiza fedha za hata kulipia ada za uanachama kwa mashirikisho ya kimataifa.

SOMA ZAIDI: Sakata la Lawi, Kagoma ni Utapeli Katika Soka

Tumeona jinsi netiboli ilivyoshindwsa kutuma timu kwenye mashindano ya kanda ya Afrika kwa sababu tu haikuwa imelipia ada yake ya uanachama. Tumeona jinsi timu ya taifa ya mpira wa wavu ilivyolazimika kuondolewa mashindanoni jijini Kigali, Rwanda, kwa kutokuwa na fedha za kulipia malazi.

Haya yote ni matatizo ya kifedha ambayo yanafanya viongozi wa vyama hivi washindwe kuandaa mashindano ya kitaifa na kushindwa kutuma timu zao kwenye mashindano ya kanda kwa ajili ya kutafuta tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia.

Wazo langu ni kwamba Serikali, angalau kwa kipindi cha miaka mitano, inaweza kuamua kufufua michezo hii kwa kutenga fedha za ruzuku kusaidia vyama husika na itakavyoviteua kwa vigezo maalum. 

Yaani Shilingi bilioni moja kwa vyama kumi kwa mwaka, kila kimoja kikipata Shilingi milioni 100 itakuwa ni ruzuku tosha ya kuwezesha vyama hivi kufanya shughuli zake na kufufua michezo yao.

Najua kwamba wizara imekuwa ikitengewa fedha kidogo za maendeleo katika bajeti, isipokuwa mwaka huu ambao Serikali imeweka fedha nyingi kwa ajili ya maandalizi ya fainali za mpira wa miguu za Afrika zitakazofanyika mwaka 2027.

Lakini kutenga Shilingi bilioni moja kwa ajili ya kusisimua michezo iliyolala haitakuwa tatizo kubwa kwa Serikali. Na nchi nyingine hufanya hivyo.

Ndoto kuwa kweli

Kama Ndumbaro aliahidi medali kwa mkakati wake, basi ukiambatana na mpango wa kuvipa vyama ruzuku, kunaweza kuwa na ndoto ya kuongeza medali Olimpiki kwa kuwa hadi sasa tumeshawahi kutwaa medali mbili tu.

SOMA ZAIDI: Tumeanza Vibaya AFCON 2025 Lakini Hatujuti

Kama mchezo wa netiboli utawezeshwa, kuna uwezekano mkubwa wasichana wengi na wanawake watarudi kwenye mchezo wao ambao wanasiasa walikuwa wakiufuata kwa wingi pale Relwe Gerezani ulipokuwa maarufu.

Kama ngumi za ridhaa zitawezeshwa, kuna uwezekano mkubwa hata ngumi za kulipwa zitaongezeka ubora kwa kuwa mabondia wengi wa ngumi za kulipwa duniani huibukia kwenye Olimpiki. Na ruzuku itawezesha kurudisha zile enzi za mapambano pale DDC Kariakoo au Relwe Gerezani.

Hali kadhalika, mpira wa wavu uliinuka wakati kampuni ya Bonite Bottlers ikidhamini mashindano kule Moshi, au wakati Kampuni ya Bia Tanzania ikikidhamini Chama cha Mpira wa Wavu Dar es Salaam (DAREVA).

Maana yake fedha ndio ziliwezesha mashindano kuwa na msisimko. Kama vyama hivi havina fedha vitawezeshaje nchi kuwa na uwezo wa kutwaa medali?

Ni muhimu sasa, Serikali ifikirie kutoa ruzuku kwa vyama teule kwa angalau kipindi kifupi cha miaka mitano, ikiwa ni mkakati wa kufufua michezo na kuwa na ndoto thabiti za kutwaa medali kwenye mashindano makubwa duniani.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts