Baada ya mjadala wa mlipuko kutokana na maneno ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kuhusu masuala ya glovu na malipo ya mama mjamzito, ambaye aliomba tujikite kwanza katika mkutano wa kimataifa uliokuwa ukifanyika hapa nchini, naona mkutano huo umekwisha, na ni muhimu kurudia mjadala huu.
Kwanza, katika kufafanua, mkuu huyuhuyu, ambaye aliwataka akina mama wasiyomudu gharama za glovu wakajifungulie nyumbani, alidai kwamba yeye amekuwa mwalimu, hivyo anajua jinsi ya kutumia mifano kushibisha hoja yake.
Labda mama huyu aliyeambiwa arudi nyumbani, yeye na mume wake, atafute mkasi wa kumzalisha baada ya kushindwa kununua glovu, kama inavyotakiwa hospitalini, ilikuwa ni stori tu. Bora kama kweli ilikuwa hivyo. Lakini kama mwalimu mwenzake, kwa nini atumie stori ya kikatili hivyo, stori ya kukatisha tamaa ya kuumiza, kujenga hoja yake?
Kweli, hata katika hadithi, mkubwa wa Serikali anaweza kutumia mfano wa kiongozi kumwambia mama mjamzito alie tu, aumie tu, ahatarishe maisha yake tu? Haiyumkiniki.
Na hapo ninawashangaa sana wanaharakati wa haki za binadamu na jinsia walivyoamua kukaa kimya.
Nafahamu shirika moja tu limetoa tamko la kushutumu udhalilishaji huo. Wengine wako wapi? Ama kweli, nikilinganisha na miaka 20 iliyopita mambo yamebadilika kabisa.
Lakini pili, hata katika stori, kwa nini mama huyu alimpigia mkuu wa mkoa? Alimpigia kutokana na sera kwamba akina mama wajawazito na wanaonyonyesha, pamoja na watoto wadogo, na hata sisi wazee, wanatibiwa bure. Ndiyo sera ambayo imeimbwa miaka mingi kama vile ni kiitikio cha wimbo wa kanisa!
SOMA ZAIDI: Uchambuzi Bajeti Wizara ya Afya Kwa Mwaka 2024/25
Manesi na madaktari wengine wameshutumiwa na kuhukumiwa kwa kudai vivyohivyo mama mjamzito anapofika kwenye zahanati yao bila glovu na zahanati yenyewe haina glovu. Wameenda kinyume cha sera.
Hapo kuna mawili. Kweli hakuna glovu, ambayo maana yake kuna kasoro katika utekelezaji? Iwapo ni sera wahudumiwe bure, ndiyo sera, nani anaihujumu sera hii kwa kutopeleka vifaa vinavyohitajika ili sera itekelezwe? Watekelezaji wamekuwa watelekezaji?
Au, kama ninavyotonywa, glovu mara nyingine zipo lakini ni mbinu ya wahudumu – au wahujumu? – kujiongezea kipato kwa kuwalazimisha akina mama wajawazito kununua glovu katika duka lao la dawa na vifaa tiba nje ya geti ya zahanati. Hawa nao wamekuwa watelekezaji. Lakini kuna ufuatiliaji? Iwapo wahudumu wamegeuka wahujumu, kwa nini wanaachwa kuendelea?
Lakini, kwa vyovyote, hali halisi ni kwamba sera inasema hivi lakini utekelezaji unasema vingine. Na utetezi wa mkuu wetu wa mkoa ni kwamba vitu hivi ni gharama. Duh! Haloooo! Ndiyo tunajua hivyo leo? Kumbe hii ina maana kwamba si tu sera haitekelezwi, ni kwamba haitekelezeki. Pesa zinazohitajika kutekeleza sera hazipo, hivyo sera haitekelezeki basi.
Tunadanganywa
Kwa hiyo, wanaoimba sera kama kiitikio cha wimbo wa kanisa wanatudanganya. Wanatoa ahadi tamutamu bila kujali kwamba ahadi ni deni. Ndiyo maana ahadi imekuwa duni. Na watu wanaumia. Akina mama wengine wamekufa, au watoto wao watarajiwa wamekufa, au wote wawili.
Na wengine wamepata athari za kudumu. Waingereza wanasema sheria, au sera, isiyotekelezeka ni sheria, au sera, mbovu maana inajenga matarajio bila mafanikio.
Kwa hiyo, tusemeje hapa? Msemo wa shirika langu la zamani, TAMASHA, ni
If you want it, Budget. Ndiyo, ukitaka kitu, kiwekee bajeti ya kukifanikisha.
SOMA ZAIDI: Vituo vya Afya vya Tozo za Miamala Vyashindwa Kuwahudumia Wananchi Mbeya, Songwe
Je, vipaumbele vikoje? Maisha ya fahari ya walionacho, au huduma za msingi kwa wananchi wa kawaida? Iwapo bajeti ya magari ya fahari kwa viongozi inazidi bajeti za wizara nyingine nzimanzima, vipaumbele vyetu ni sahihi? Kwa bei ya gari moja la gharama tungeweza kununua delivery kit ngapi?
Na mamilioni ya posho ya makalio ya wakubwa wa mashirika, hata wa afya, na waheshimiwa wa sponji huko Dodoma, na posho za kujikimu zilizogeuka kuwa posho za kujikirimu, na kadhalika. Anasa za walionacho zimetunasa vibaya sana.
Misaada ya Marekani
Ndipo hapo, napenda kugusia yaliyotokea juzi kwa mropokaji mwingine, tena mbaya zaidi. Katika mipango yake ya kufyeka, anayejiona bosi wa dunia alisimamisha msaada wote kwa nchi za nje. Wacha watu washikwe na mchecheto, hasa wale waliokuwa wanajikimu kwa pesa za Marekani.
Lakini mbaya zaidi, afya ya mamilioni duniani, na hapa petu pia, ilitishiwa kwa kukosa msaada wa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI. Kwa bahati nzuri mpango wake umesitishwa, lakini imeibua maswali mengi.
Tutaendelea kutegemea watu wengine kujali afya za wananchi, huku wenye maamuzi hujali magari yao zaidi? Kuna mipango mingapi ya afya – na elimu, na kadhalika – itakufa siku ambayo wafadhili na mafedhuli wataamua kukata mirija ya msaada?
Nimewahi kutumia mfano wa wilaya fulani ambapo kulikuwa na mpango bora sana wa ulinzi wa watoto na wanawake dhidi ya unyanyasaji. Tatizo lilikuwa kwamba wakati watu wa nchi za nje wamegharamia milioni mia moja ishirini, halmashauri husika iligharamia milioni tano tu.
SOMA ZAIDI: Walazimika Kujifungulia Nyumbani Baada ya Kituo cha Afya Kukosa Wahudumu
Kwa nini tunafikiri kwamba ni haki yetu kuwakabidhi watu wa nje jambo muhimu kama afya na usalama wa watoto na wanawake wetu? Kiserikali, kumbe kuna msemo mwingine: We want it, but let others budget. Naam, tunataka vitu, lakini wacha wengine wabebe gharama ili na sisi tuendelee na maisha yetu ya anasa na kujikirimu!
Pesa hazitoshi?
Lakini inawezekana pia kwamba pamoja na kupunguza matumizi na matanuzi ya walionacho kwa pesa zetu za kodi na kadhalika, bado pesa hazitoshi. Alivyosema mkuu wetu wa mkoa katika stori yake, vitu hivi ni ghali. Tunaweza kumudu?
Na kama hatuwezi kumudu, tutaendelea kudanganya wananchi hadi lini? Kama haitekelezeki, tujitokeze na kusema, “Ee jamani, samahani, imeshindikana mpaka hapo baadaye. Kwa hiyo, mjiandae wenyewe kabla ya kwenda kujifungua.”
Nimetonywa pia kwamba katika hali halisi ndivyo ilivyo. Wazazi wanapohudhuria kliniki huelekezwa kuandaa pesa na mahitaji ya wakati wa kujifungua, maarufu kama delivery pack inayokuwa na kila kitu kinachohitajika kwa mama na mtoto wakati wa kujifungua. Mkinzano huo.
Na mheshimiwa mdogo wa afya alichangia bila kujijua kwa kudai kwamba mtu anachangia milioni moja katika harusi, lakini anashindwa kulipa elfu hamsini kwa ajili ya mke wake kujifungua. Kwanza, huu mfano ni sawa na stori ya mkuu wa mkoa.
Mwenye kutoa milioni moja kwenye harusi atapeleka mke wake hospitali binafsi na kulipia gharama zote. Wanaolia ni wale ambao hata kadi za harusi hawazitaki maana hawana pesa hizo. Lakini hapo pia mheshimiwa mdogo wa afya amekubali kumbe tunatakiwa kulipa hizi elfu hamsini. Tukubali sera imekuwa ni sura tu. Tunadanganyana kitu gani?
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ni Muhimu Kufungamanisha Bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii?
Labda kazi yetu ni bima tu. Lakini bado tutahitaji kuwa na uhakika wa vifaa kuwepo. Yaonekana mheshimiwa wetu wa mkoa ametumia mfano mbovu kutuambia ukweli.
Kama amesema uongo tena wa kikatili, awajibishwe.
Kama ameumbua uongo wa ahadi, si ajabu atawajibishwa kwa kuumbua; na kama ametangaza hadharani sera mpya, basi tushukuru. Sasa twajua!
Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.