The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

‘Howani Mwana Howani’: Malezi, Ndoa na Maisha Mengine ya Waswahili

Unaposoma ‘Howani Mwana Howani’ na kuambulia lolote ujue unajinasibisha na elimu-malezi ya kadiri ya mapokeo ya Waswahili.

subscribe to our newsletter!

Je, ni mambo gani muhimu katika malezi ya mtoto, haswa akiwa wa kike? Hili ndilo jambo lililomsukuma Zaynab Himid Mohammed kutuandikia tenzi mbili zinazoelezea makuzi ya mtoto wa kike hadi anapoolewa katika jamii ya Waswahili. Jina la kitabu linatokana na utenzi wa kwanza Howani Mwana Howani-Kitunguu na Ubani

Utenzi huu unaelezea maisha ya mtoto kuanzia kuzaliwa hadi kubalehe. Wa pili ni Utenzi wa Mwama Kukuwa unaosimulia maisha ya Mwanakukuwa (kwenye kitabu Kukuwa) baada ya unyago, kuposwa hadi mpaka sherehe za harusi. Tenzi hizi zimehaririwa na Saida Yahya-Othman na Abdulhakim S. Yahya. 

Japo uandishi wa tenzi huwa ni beti fupi za mistari minne tu, Bi. Zaynab H. Mohammed ameandika tenzi ndefu kiasi. Utenzi wa Howani ni jumla ya beti 398. Kukuwa ni beti 1,128. Ameenda mbali kote ili kututengenezea rejea sisi wazazi wa sasa. 

Naye anarejea yale aliyojifunza kutoka kwa mama yake kuhusu maisha ya zamani zaid ya Waswahili. Hivyo, unaposoma Howani Mwana Howani na kuambulia lolote ujue unajinasibisha na elimu-malezi ya kadiri ya mapokeo ya Waswahili. Binafsi nimejifunza mambo kadhaa ambayo napenda tuyajadili. 

Utamaduni

Malezi ya binadamu yana taratibu na matambiko mengi yanayoendana na kila hatua ya maisha. Kwenye Howani Mwana Howani tunaoneshwa mtoto wa Kiswahili akiwa mchanga, kwa mfano, hupakwa wanja na hutengenzwa kisogo.  

SOMA ZAIDI: Lulu za ‘Barua Ndefu Kama Hii’ na Maswali Muhimu ya Kutafakari Pamoja 

Akifika umri wa balehe msichana huchezwa ngoma. Akikaribia kuolewa somo huitwa tena kumfunda na kumuandaa na ndoa. Tenzi za Howani Mwana Howani zinatuonesha utamaduni wa Mswahili hutegemea matambiko ya kidini na kushiriki kwa ndugu na jamaa katika kila hatua ya ukuaji.  

Tunapouita ubeberu na ukoloni unyama maana yake ni kwamba hutunyima uwezo wa kuendelea kutengeneza mila zinazotokana na mazingira na imani zetu. Kwa kiasi fulani, bado tunafanya arobaini za watoto wachanga lakini kuwacheza ngoma wasichana inaonekana kama mila duni inayomkandamiza mwanamke. 

Ukiacha kijifunza mizungu na mambo ya mahusiano ya mke na mume ujuzi atakaouhitaji baadaye, ni kipi kibaya katika kumfundisha mtoto wa kike usafi, uchapa kazi, umaridadi? 

Kweli tunaweza tusifuate neno kwa neno kama Bi Zaynab H. Mohammed alivyoandika, lakini tutafakari tena unyago na hizo tunazoziita “mila kandamizi.” Je, kweli ni mila kandamizi au ni matokeo ya ukoloni kuziita tamaduni zetu “za kishenzi?”

Elimu

Zaynab H. Mohammed anatueleza kwamba elimu ya mtoto huanza pale anaponyonyeshwa. Yaani, mama anavyouona ulimwengu ndio mtoto atakavyouchukulia. 

SOMA ZAIDI: Kale ya Washairi wa Pemba: Wasotumia Akili Mnemba 

Kiimani (Kiislamu) anafundishwa kumjua na kumtegemea Mungu. Mungu huwapa binadamu mitihani, lakini pia husikia dua zao. Kwenye malezi, wazazi humuomba Mungu aendelee kumuongoza mtoto wao kwa sababu wanajua anaweza kukengeuka kama watoto wengine.  

Ndio maana Kukuwa anaambiwa akiona wengine wanakosea asiwacheke na kujiona ni bora (382). Wazazi wanamfundisha kuhusu historia na misingi ya Uislam ili imani isiwe tu nadharia bali kujua sababu za misimamo, taratibu na matambiko ya Kiislam. 

Kukuwa anafundishwa kufanya kazi za mikono kama ususi wa mikeka ili apate vitu vya kutumia mwenyewe, vitu vya kuuza na vya kutoa zawadi. Uchapa kazi unaelezwa kuwa ni kinga dhidi ya wizi na tamaa kwani unakuwa na kipato chako mwenyewe hutatamani cha mtu mwingine. 

Kuanzia Kukuwa anapovunja ungo mpaka anapoolewa mkufunzi wake ni somo. Mwali akiwa na sifa njema ni somo. Hivyo, somo anamfundisha Kukuwa jinsi ya kuishi na mume, wakwe na mahusiano mengine kama mashoga zake. Somo pia ni mueleishaji rika kwani anawatahadharisha wasichana dhidi ya ngono. 

Wakati wa kumkabidhi Kukuwa, anamwambia bwana harusi kumpiga mke ni mwiko labda kwa upane wa kanga. Somo pia anawataka wakwe kuahidi kumtunza Kukuwa. 

SOMA ZAIDI: ‘Kale ya Washairi wa Pemba’ na Ufundi wa Mshairi Mahiri Kamange

Kwa kifupi, Kukuwa chuoni anajifunza maadili na ucha Mungu, nyumbani anafundishwa kufanya kazi na kwa somo anajifunza jinsi ya kujenga mahusiano. Mimi sasa nimeingia kwenye rika la uzazi wa watoto wa miaka saba mpaka kumi na nne, umri wa mtoto wa shule ya msingi. 

Nawaza juu ya watoto wetu wanaoamka alfajiri kuwahi usafiri. Wanarudi nyumbani baada ya saa kumi. Muda tunaokaa nao jioni tunawasaidia kufanya homework. Wikendi na wakati mwingine likizo pia wanaenda shule kwa sababu ni “darasa la mitihani.” 

Katika ratiba hizi ndefu za shule ni kwa namna gani tutawafundisha watoto wetu kukabili mambo yaliyo nje ya uwezo wa binadamu (imani), kufanya kazi na mahusiano? 

‘Mume si Mbuzi Dume’

Kwa sababu Mume si Mbuzi Dume’ (129), mke anavyoendelea kufanya vitu vidogo vidogo ndivyo ndoa itavyostawi. Mwandishi anasema: 

270: Mambo ya ndoa ni kunga, 

Makuti kuunga unga, 

Wala sivyo kuifunga, 

Mwanangu mwana imani. 

Mwanamke anashauriwa siku hizi tunaita kujiongeza. Sio tu kupika na kupakua, akiweza hata chakula amlishe mumewe. Mama na Baba Kukuwa wanaonekana kuwa wenye mahusiano mazuri. 

SOMA ZAIDI: Funzo Kutoka Riwaya ya ‘Haini’ ya Adam Shafi: Mtu Yeyote, na Muda Wowote, Anaweza Kugeuzwa Mhaini

Mama Kukuwa anatuelezea jinsi mumewe akivaa nguo zinamkaa na akitembea anaonekana mwenye mvuto mpaka anaanza kuwa na wivu labda wanawake wengine watamuona uzuri wake. Mama Kukuwa ni mwepesi kutawaliwa na mawazo. 

Anakuwa na uoga mazungumzo ya posa yanapoanza na wanapoanza mipango ya harusi. Baba Kukuwa anajua maneno ya kumwambia mkewe mpaka akatulia kila mara. Hivyo, japo anayehusiwa ni mwanamke; wote wawili, mke na mume, hupaswa kuendela kupalilia penzi. 

Wambea na mahasidi

Kukuwa anaambiwa asiikaribishe husda. Mfano anaopewa ni kujiwekea mipaka na mashoga zake. Wasiyajue, wala kuyaingilia, ya ndani kwake. Japo wanacheka naye mmoja wao  anaweza kuwa anamuonea kijicho akaja kumharibia. Baada ya Kukuwa kuchezwa ngoma wambeya wanataka kwa sababu alikuwa hatoki ndani hovyo hovyo. 

Mara wanataka kujua posa inaendaje. Siku ya harusi wanataka kujua zawadi amepata zawadi gani. Harusi ikaisha vizuri, wakakosa la kusema. Baada ya fungate walimsubiri Kukuwa wamuone yukoje. 

Ndio maana jambo la mwisho kabla ya somo kumaliza anamsihi Kukuwa asije kuwa mmbeya. Japo wambea huwezi kuwaepuka walau unawapunguzia taarifa. Hivyo, familia ya Kukuwa walifanya mambo yao kimya kimya mpaka posa ilipotolewa. 

SOMA ZAIDI: Utenzi wa Mwanakupona na Jitihada za Kumpumbaza Mume Kudumisha Ndoa

Mazingira ya Kukuwa ni tofauti na sasa kwenye mitandao ya kijamii. Ni kweli mtu anaweza kupanga harusi nzima bila kujiposti au kupostiwa?     

Ndoa muhimu kuliko harusi

Baada ya kuchezwa, Kukuwa anakaa miaka miwili ndipo akaolewa. Kwa wakati wote huo, na hata baada ya kuposwa, baba yake anasema mara mbili mwanae hajachina. Hivyo, hakuna haja ya kuharakisha ndoa wala harusi. 

Hakika yeye si kama wale wazazi wa kusema “nimeshachangia sana watu, nawe uolewe nami nichangiwe.” Kwa sababu hiyo mipango ya ndoa inaenda taratibu pia. Inapofika muda wa kuanza maandalizi ya harusi wanafuata hatua tatu. 

Kwanza, ndugu wa karibu wanaahidi na kuleta zawadi za bibi harusi. Bibi yake Kukuwa anaona hakuna maana ya wao kuja wamependeza endapo bi harusi hana vyombo. (554). Pili, wanachangia gharama za harusi. Mwisho ndio waende kwenye harusi. 

Mamia ya watu wanaokuja kwenye harusi sio waliopewa kadi za mchango bila kumfahamu bi harusi. Ni ndugu, jamaa, majirani na wale walioko kwenye vyama vya ngoma. 

SOMA ZAIDI: Utendi wa Fumo Liyongo: Kama Watawala Hawataacha Kutengeneza Hila, Nasi Tuendelee Kubuni Mbinu za Ukombozi

Kwa jinsi familia ilivyoweka mbele ndoa na Kukuwa kuanza maisha imeniwazisha sana kuhusu ukubwa wa harusi. Labda harusi za siku hizi zingekuwa chache na za bajeti ndogo endapo kamati za maandalizi zingetakiwa kuwapa maharusi samani na vyombo.

Kitabu kimeandikwa kwa mtiririko wa moja kwa moja. Howani Mwana Howani inaanza  mtoto anapozaliwa kisha akiwa na miaka: sita, saba, kumi na mbili, kumi na nne. 

Kwenye Utenzi wa Mwanakukuwa, mwandishi anaeleza mchakato mzima kuanzia kuposa mpaka baada ya fungate. Wakati mwingine anaelezea vizuri mazingira unajenga taswira inakukaa kichwani.Kitabu kizima anaeleze marashi na vitu vya kunukia. 

Wageni wanapewa Hal-udi. Nguo zinafukiwa na bibi harusi huwa na kanga mahususi iliyofukizwa kwa udi. Wakati wa harusi mwali anasingwa wa mawaridi na asumini. Yaani marashi ni sehemu muhimu sana ya ustaarabu wa Waswahili. Unaweza kunyakua macho wakati unasoma ukaanza kuzitafuta harufu ya hal-udi, wallahi!

Zaynab H. Mohammed anatushirikisha malezi na ndoa za Kiswahili. Wakati huo huo anajihadhari kwa kujua kuna watu wanaweza wakapinga vikali mtizamo wake. Naona anajilinda kwa kusema haya ni mambo ya zamani. 

READ MORE: Utenzi wa Mwanakupona na Jitihada za Kumpumbaza Mume Kudumisha Ndoa 

Hata bibi yake Kupona anapoanza taratibu za harusi, ikiwemo kumuita somo na kufuatilia maandalizi ya zawadi anasema huku akiwa na shaka kama maneno yake hayatapuuzwa kwa sababu yeye ni mzee tu.  

Wewe ukisoma Howani Mwana Howani unaona nini kuhusu malezi na ndoa za Waswahili? Ni kweli ya kale ni dhahabu au tutupe jongoo na mti wake?

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×