Kila ninapofuatilia baadhi ya habari zinazochapishwa na vyombo vyetu vya habari siku hizi hapa nchini, swali moja huendelea kunijia akilini: Kwa nini tuna waandishi wa habari? Kwa mtazamo wangu, mwandishi wa habari ni zaidi ya mtu anayetuambia kilichotokea.
Ni daraja kati ya mwananchi na maeneo ambayo mwananchi wa kawaida hawezi kufika moja kwa moja. Mwananchi anayeishi Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga, Kigoma au kijijini hawezi kuwepo katika kila kikao cha Serikali, hawezi kuingia katika kila taasisi, hawezi kuzungumza na kila kiongozi wala kufuatilia kwa karibu kila mradi mkubwa wa Kitaifa.
Lakini maamuzi yanayofanyika katika maeneo hayo yanamhusu moja kwa moja. Bajeti inamhusu, uwekezaji wa umma unamhusu, miradi mikubwa ya miundombinu inamhusu, na hali ya elimu, afya, maji, nishati, kilimo, ajira na biashara inamhusu. Kwa hiyo, kwa sehemu kubwa, mwananchi huyu anategemea mwandishi wa habari kumpeleka kule ambako yeye hawezi kufika na kumrudishia taarifa ambayo itamsaidia kulielewa taifa lake.
Ndiyo maana napatwa na wasiwasi ninapoona sehemu ya habari zinazopaswa kumjengea mwananchi uelewa wa nchi yake zikisukumwa pembeni na habari ambazo, kwa maoni yangu, ni petty—habari ndogo na nyepesi ambazo mara nyingi hazimwachi msomaji, msikilizaji au mtazamaji na maarifa yoyote ya maana.
Leo unaweza kukutana na habari inayosema, “Tazama kiongozi fulani akitimua mbio”; kesho, “Waziri aendesha baiskeli”; na siku inayofuata, “Kiongozi ale chakula katika mgahawa wa kawaida.” Sina hoja kwamba habari kama hizo hazipaswi kuwepo kabisa. Vyombo vya habari vina nafasi ya kuburudisha, kuonyesha maisha ya kawaida ya viongozi, na hata kutupatia habari nyepesi zinazotupa nafasi ya kupumua katika mazingira yenye mambo mengi mazito.
Hoja yangu ni kuhusu uwiano. Pale ambapo habari hizi zinaanza kuchukua nafasi ya masuala yenye uzito zaidi, tunapaswa kujiuliza kama uandishi wetu wa habari bado unatimiza wajibu wake mkubwa kwa jamii.
Nini kinafuata?
Mwananchi akijua kwamba Waziri amekula chakula kwa Mama Ntilie, swali linalofuata ni: what next? Maarifa gani mapya amepata kuhusu nchi yake? Je, taarifa hiyo imemsaidia kuelewa kwa nini gharama za maisha zinapanda au kushuka? Imemsaidia kuelewa bajeti? Imefafanua sera fulani? Imemsaidia kujua hali ya elimu, ajira, uwekezaji au miradi mikubwa ya taifa?
Hapa ndipo ninapoona umuhimu wa kutofautisha kati ya habari inayovutia na habari yenye thamani ya muda mrefu kwa jamii. Habari inaweza kuwa maarufu sana kwa saa chache, ikasambazwa kwa wingi na ikapata maelfu ya maoni, lakini bado isimwongezee mwananchi uelewa wa jambo lolote muhimu kuhusu maisha yake au taifa lake.
Tunaishi katika zama ambazo habari hupimwa kwa views, likes, shares na comments. Mazingira haya yamebadilisha sana namna habari zinavyotengenezwa na kusambazwa. Mwandishi, au chombo cha habari, kinaweza kuanza kujiuliza: ni habari gani italeta traffic, ni kichwa gani kitawafanya watu wabofye, ni video gani itasambaa zaidi?
Hili lenyewe si kosa. Vyombo vya habari navyo vinaendesha taasisi zinazohitaji wasomaji, watazamaji na wasikilizaji. Lakini tatizo linaanza pale ambapo kile kinachovutia zaidi kinachukua nafasi ya kile ambacho ni muhimu zaidi. Tukifika mahali ambapo thamani ya habari inapimwa zaidi kwa idadi ya “likes” kuliko maarifa anayopata mwananchi, basi tunakuwa tumebadili maana ya habari.
SOMA ZAIDI: Ukiwa Mzembe, Vyombo vya Habari Vitakulisha ‘Matango Pori.’ Udadisi Utakusaidia Kulikwepa Hilo
Habari inaweza kupata “likes” 50,000 bila kumsaidia mwananchi kuelewa taifa lake, wakati habari nyingine yenye “likes” chache inaweza kumweleza mradi mkubwa umegharimu kiasi gani, fedha zimetoka wapi, nani anausimamia, changamoto zake ni zipi na wananchi watanufaikaje.
Wananchi wanataka?
Wapo watakaosema kwamba vyombo vya habari vinatoa habari hizi kwa sababu ndizo ambazo wananchi wanataka. Hoja hii ina ukweli fulani, lakini si ukweli wote. Watu pia hujifunza kupenda kile wanachopewa mara kwa mara.
Mtoto ambaye kila siku anapewa biskuti anaweza kuanza kuzitaka kila wakati, lakini hilo halimaanishi kwamba biskuti ndicho chakula bora zaidi kwake. Vivyo hivyo, tunapowazoesha wananchi habari nyepesi, matukio madogo, kauli za kusisimua na vipande vifupi vya burudani, taratibu tunawajengea utamaduni wa kutafuta maudhui ya aina hiyo.
Kwa hiyo, jukumu la chombo cha habari si kufuata tu kile hadhira inachotaka wakati huo; ni pia kusaidia kujenga kile hadhira inapaswa kutaka kukifahamu. Uandishi wa habari wa maana haupaswi kuwa kioo cha matakwa ya hadhira pekee, bali pia chombo cha kupanua upeo wa wananchi.
Chukua mfano wa miradi mikubwa ya Kitaifa. Watanzania wengi wanaweza kutaja SGR, Bwawa la Julius Nyerere na miradi mingine mikubwa. Lakini tukienda hatua moja zaidi na kuuliza: mradi umegharimu kiasi gani, fedha zimetoka wapi, utaleta faida gani, kwa muda gani, nani anausimamia, changamoto zake ni zipi, na mwananchi wa kawaida atanufaikaje?
Hapo ndipo tunaweza kugundua kuwa tunajua majina ya miradi, lakini hatuielewi miradi yenyewe. Hilo ni pengo kubwa la taarifa. Taifa halihitaji wananchi wanaoweza kutaja majina ya miradi pekee; linahitaji wananchi wanaoweza kuelewa kwa nini miradi hiyo inafanyika, ina maana gani kwa uchumi, inalipiwaje na inaathiri maisha yao kwa namna gani.
Kina, uwiano na kusudi
Hapo ndipo mwandishi wa habari anapaswa kuwa muhimu zaidi. Mwandishi anapaswa kwenda kule ambako mwananchi hawezi kufika, aulize maswali ambayo mwananchi hana nafasi ya kuyauliza, asome nyaraka ambazo wananchi wengi hawana muda wa kuzisoma, azungumze na wataalamu, achambue takwimu, afuatilie ahadi na, inapobidi, ahoji maamuzi ya wenye mamlaka.
Baada ya kufanya hayo, anapaswa kurudi kwa mwananchi na kusema kwa lugha rahisi: “Hiki ndicho kinachoendelea katika taifa lako, na hivi ndivyo kinavyokuhusu.” Hapo ndipo uandishi wa habari unapokuwa daraja la kweli kati ya wananchi na maisha ya taifa lao.
Sisemi kwamba habari nyepesi ziondolewe, wala sisemi kwamba kila habari iwe uchambuzi wa bajeti, sera au uchumi. Ninachosisitiza ni uwiano. Lazima kuwe na uwiano kati ya burudani na maarifa, kati ya habari nyepesi na habari nzito, na kati ya kile kinachovutia macho na kile kinachojenga uelewa.
Vyombo vya habari haviwezi kujaza sehemu kubwa ya maudhui kwa mambo madogo halafu vikategemea wananchi wawe na uelewa mkubwa wa mambo makubwa ya taifa. Kalamu ya mwandishi inaweza kumsaidia mwananchi kuelewa kodi, bajeti, sera, elimu, uchumi, uwekezaji na fursa zilizopo.
SOMA ZAIDI: Uvamizi Dhidi ya Tasnia ya Habari? Tuzungumze Matumizi Mabovu ya Kiswahili Yafanywao na Waandishi wa Habari
Lakini kalamu hiyo hiyo inaweza kutumika kutuambia kila siku nani amekula wapi, nani amevaa nini na nani ameendesha baiskeli. Uchaguzi huo una matokeo.
Mwisho wa yote, tunahitaji kurudisha kina, uwiano na kusudi katika uandishi wetu wa habari. Mwandishi wa habari si mtu anayeshikilia kamera, kipaza sauti au kalamu tu. Ni macho ya mwananchi kule ambako hawezi kuona, ni masikio yake kule ambako hawezi kusikia, na ni daraja linalopaswa kumsaidia kulielewa taifa lake.
Daraja hilo likifanya kazi vizuri, tunajenga wananchi wenye maarifa na uwezo mkubwa wa kushiriki katika maendeleo ya nchi yao. Lakini daraja hilo likigeuka kuwa njia ya kutuambia zaidi nani amekula wapi, nani ameendesha baiskeli, au nani ametimua mbio, basi tunapaswa kujiuliza kwa umakini: Je, uandishi wetu wa habari bado unatimiza kusudi lake?
Linden Mwampashe ni mtaalamu wa mawasiliano kwa umma anayefanya kazi na shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu, lakini haya ni maoni binafsi, siyo yale ya mwajiriwa wake. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia lindenmwampashe8@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.