The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Utalii wa Mashamba ya Viungo Zanzibar Fursa ya Ajira Kwa Vijana

Utalii wa viungo ulianza kuimarika Zanzibar mwaka 1995, sambamba na kuitangaza zaidi Zanzibar kama ‘the Spice Islands’

subscribe to our newsletter!

Zanzibar –  Harufu ya mdalasini, karafuu, pilipili na mchaichai inatawala mashamba ya viungo Zanzibar, huku watalii wakitembea katikati ya miti na mimea wakijifunza asili ya viungo wanavyovitumia majumbani mwao. 

Kwao, ziara hizo ni fursa ya kuona namna viungo vinavyolimwa na kuvunwa. Lakini kwa wenyeji, mashamba hayo yamegeuka kuwa zaidi ya maeneo ya uzalishaji wa mazao; ni chanzo cha ajira, kipato na matumaini ya maisha bora, hususan kwa vijana.

Akiwa na umri wa miaka 35, Hassan Hamad, mmiliki wa shamba la Zito Spice Tour lililopo Dole, Unguja, ni miongoni mwa wanaotumia fursa hiyo kuunganisha kilimo na utalii. Shamba hilo, alilorithi kutoka kwa wazazi wake, lina ukubwa wa zaidi ya hekta tano na limekuwa chanzo cha ajira kwa vijana zaidi ya 70.

Mkarafuu kwenye moja ya shamba la viungo | Picha na Najjat Omar

“Tumefanikiwa kuwashirikisha vijana zaidi ya 73 katika shughuli mbalimbali za shamba hili. Hii imewasaidia kupata ajira na kipato cha kujikimu kimaisha,” anasema Hassan.

Utalii wa viungo ulianza kuimarika Zanzibar mwaka 1995, sambamba na kuitangaza zaidi Zanzibar kama  ‘the Spice Islands’. Miongoni mwa mazao yanayolimwa ni karafuu, mdalasini, pilipili manga, tangawizi, iliki, binzari manjano, vanilla na mchaichai.

Kwa watalii, kuviona viungo hivyo katika mazingira yake ya asili ni sehemu inayofanya ziara hizo kuwa za kipekee. Kassim Malik Kassimu, Meneja wa Zito Spice Tour, anasema wageni wengi huvutiwa na fursa ya kuona, kunusa na kugusa mimea inayozalisha viungo wanavyovifahamu.

Kassim Malik Kassim, Meneja katika Shamba la Viungo la Zito akionesha jinsi mti wa Mfenesi | Picha/Najjat Omar

Anasema utalii huo unawapa wazawa nafasi kubwa ya ajira kwa sababu wana uelewa wa namna ya kupanda, kutunza na kutumia viungo hivyo.

Miongoni mwa wanaonufaika ni Abdallah Soud, mwenye umri wa miaka 22, anayefanya kazi katika Shamba la Viungo la Tangawizi, Dole, kwa miaka minne sasa. Mbali na kupata kipato, kazi hiyo imemwezesha kujifunza lugha za Kitaliano na Kifaransa kupitia mawasiliano na watalii.

“Kazi hii imenisaidia kupata kipato cha kukidhi mahitaji yangu ya kila siku. Pia nimeweza kukarabati nyumba ya mama yangu na kununua pikipiki yenye thamani ya shilingi milioni sita. Nikifanikiwa, mwakani nataka kununua kiwanja,” anasema Abdallah.

SOMA ZAIDI: Bajeti ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Inaakisi Umuhimu wa Sekta ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi?

Kwa upande mwingine, Mrisho Hassan, mwenye umri wa miaka 30 na baba wa watoto wawili, amekuwa akipata kipato kwa kukwea minazi na kuwaonesha watalii namna nazi zinavyovunwa, huku akiimba nyimbo za Kiswahili.

Mrisho Hassan, mkwezi wa minazi akichonga dafu kwa ajili ya wageni | Picha Najjat Omar

Mbali na kazi hiyo, huuza madafu kwa shilingi 800 kila moja. Kwa siku anaweza kuuza kati ya madafu 15 na 30, na kujipatia shilingi 12,000 hadi 24,000.

“Si lazima nitegemee kukwea minazi pekee. Wageni wanapokuja, napata pia fursa ya kuuza madafu na kuongeza kipato,” anasema.

Takwimu zinaonesha kuwa utalii wa viungo umeajiri moja kwa moja takribani watu 3,500 hadi 4,000, huku vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 wakichukua karibu asilimia 65 ya ajira hizo. Aidha, uzalishaji wa viungo Zanzibar uliongezeka kutoka tani 7,500 mwaka 2023 hadi tani 8,200 mwaka 2025, huku mauzo ya nje yakifikia dola milioni 60 mwaka 2025.

Petra Puchta mtalii kutoka Ujerumani akiwa kwenye Shamba ya Viungo la Zitto | Picha na Najjat Omar

Hata hivyo, pamoja na ongezeko la watalii, wamiliki wa mashamba bado wanakabiliwa na changamoto ya kunufaika moja kwa moja na mapato ya ziara hizo.

Hassan anasema wageni wengi hulipia ziara kupitia kampuni za utalii zinazojumuisha mashamba ya viungo katika vifurushi vya safari, hali inayopunguza mapato yanayowafikia wenye mashamba.

Changamoto nyingine ni ushiriki mdogo wa wanawake. Masoud Kassim, Mjumbe wa Sheha wa Shehia ya Dole, anasema mitazamo hasi ya baadhi ya wanajamii kuhusu shughuli za utalii huwafanya wanawake kusita kushiriki katika fursa hizo, licha ya kuwepo kwa nafasi za kujipatia kipato.

Alexandre Jean-Pierre, mtalii kutoka Ufaransa, akiwa ameambatana na mkewe pamoja na wazazi wake | Picha na Najjat Omar

Hata hivyo, Serikali inasema inaendelea kuweka mazingira bora ya kuendeleza sekta hiyo. Kupitia Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji, zaidi ya miche 250,000 ya viungo imesambazwa kwa wakulima, huku ushirikiano na mradi wa AGRI-CONNECT uliofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ukiwezesha usambazaji wa miche kati ya mwaka 2020 na 2024.

Bidhaa zitokanazo na viungo na mimea iliyopo shambani.Picha na Najjat Omar

Kwa upande wa utalii, Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kupitia Kamisheni ya Utalii imekuwa na majadiliano na wamiliki wa mashamba kuhusu kuanzisha mfumo wa kiingilio utakaowezesha mashamba kunufaika moja kwa moja na wageni wanaoyatembelea.

SOMA ZAIDI: Mikoko:Uhifadhi wa Bahari Unaoangamizwa na Shughuli za Kibinadamu Zanzibar

Hakim Ali Kimara, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Kamisheni ya Utalii, anasema utaratibu huo unaendelea kujadiliwa ili kuhakikisha mapato ya utalii wa viungo yanawanufaisha wadau wote.

Kwa Dkt. Aboud Suleiman Jumbe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, utalii wa viungo ni rasilimali muhimu inayounganisha urithi wa kihistoria wa Zanzibar na fursa za kiuchumi na kijamii.

“Katika Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tunaendelea kuimarisha utalii wa viungo kama sehemu ya urithi wetu wa kihistoria na fursa ya kiuchumi. Lengo ni kuhakikisha tunaitangaza Zanzibar kimataifa, tunavutia watalii wengi zaidi na wananchi, hususan wakulima wanufaike na fursa zinazotokana na utalii huu,” amesema Dkt. Aboud.

Dkt. Aboud amesisitiza kwamba, ili kuwepo kwa manufaa zaidi, ni vyema ushirikiano ukaendelea kati ya Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale na Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji, ili kuongeza uzalishaji wa viungo na kuibua fursa mbalimbali zinazotokana na mashamba hayo.

Najjat Omar ni mhariri na mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar, unaweza kuwasiliana nae kwa email –najjatomar@gmail.com.   

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×