Kampuni ya maziwa ya Asas Diaries imejikuta matatani hivi karibuni baada ya watumiaji waliowengi wa mtandao wa kijamii wa Twitter kupigia kampeni kampuni shindani ya Tanga Fresh kufuatia kitendo cha Mkurugenzi Mtendaji wa Asas Diaries, Ahmed Asas, kufanya kitu katika mtandao huo ambacho watumiaje wake wengi walikitafsiri kama siyo cha kiungwana.
Sakata hilo lililoanzia Jumanne, Aprili 6, 2021, na kuendelea kwa takribani siku tatu lilitokana na hatua ya Ahmed Asas kuvujisha mawasiliano binafsi kati yake na mtumiaji mmoja wa Twitter, Hassan Abui, yaliyohusisha kijana huyo kuomba kazi kutoka kwa bosi huyo wa Asas Diaries, jambo ambalo watu wengi hawakufurashishwa nalo.
Katika mawasiliano hayo yanayoonekana kufanyika mwaka 2020, kijana huyo alikuwa akiomba kazi ya kutangaza bidhaa za Asas Diaries katika mtandao huo wa Twitter na Instagram, akisema angefurahi kupata kazi hiyo kwani kwa kipindi hicho hakuwa na ajira yoyote nyengine inayoweza kumuingizia kipato. Hata hivyo, Ahmed Asas hakujibu ujumbe huo aliotumiwa na Abui kwa kutumia njia ya Direct Messaging, au DM, kama inavyojulikana kwa watumiaji wa Twitter.
Hata hivyo, Ahmed Asas alikuja kuyavujisha mawasiliano yake hayo na Abui, yaliyojumuisha namba ya simu ya Abui, baada ya Abui kusambaza katika mtandao huo wa Twitter andiko la zamani la Ahmed Asas linalomsifia hayati John Magufuli kwenye andiko ambalo Ahmed Asas anamsifia Rais Samia Suluhu Hassan, akimuuliza: “Huyu ni wewe?” Ndipo Ahmed Asas alipomjibu Abui kwa kumuuliza swali hilo hilo huku akiambatanisha screenshot ya mawasiliano baina yao, chapisho ambalo alilifuta baadaye.
Hatua hiyo haikuwafurahisha watumiaji wengi wa mtandao huo wa kijamii ambao walianza kumkosoa Ahmed Asas, wengine kwa njia za kistaarabu na wengine kwa namna walivyokuwa wanajisikia wenyewe. “Hata dini unayoifuata haikubaliana na aina hii ya kujikuza,” Geofrey Lea, mchambuzi maarufu wa mpira wa miguu nchini Tanzania, aliandika kufuatia uamuzi huo wa Ahmed Asas.
“Kuwa masikini, fukara au kuwa na shida za kifedha, hakukuzuii kuhoji, kuwa na hoja, mtazamo au msimamo,” mwanamuziki wa kizazi kipya Webiro Wasira maarufu Wakazi pia aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kufuatia hatua hiyo. “Thamani yako ipo kwenye tabia, utu na moyo wako kwenye kusaidia wengine. Fedha ni majaliwa na nyongeza.”
Carol Ndosi, mwanaharakati na mjasiriamali, aliandika haya kufuatia hatua hiyo: “Inasikitisha. Mungu atujalie moyo mkuu. Kwa bahati mbaya, hata ukiifuta [hiyo tweet] intaneti huwa haisahau kamwe. Huko mbeleni, ni matumaini yangu kwamba matendo yako yatarekebisha namna ulivyowavunja watu moyo kwenye hili.”
Ikiwa ni sehemu ya kuonesha kukerwa kwao na tabia hiyo ya Ahmed Asas, wakosoaji wa tabia yake hiyo walienda mbali zaidi na kuanza kupigia kampeni kampuni ya maziwa ya Tanga Fresh ambayo ni mshindani mkuu wa kibiashara na kampuni ya Asas Diaries. Miongozi mwa watu maarufu ambao hawana tabia ya kutangaza bidhaa katika mtandao wa Twitter lakini wamefanya hivyo kwa maziwa na bidhaa zingine za Tanga Fresh ni kama vile wakili na mwanaharakati Fatma Karume, mwanaharakati Maria Sarungi-Tsehai, na wengineo wengi kama inavyoonekana hapa, hapa na hapa.
Mpaka sasa, si kampuni ya Asas Diaries wala Mkurugenzi wake Ahmed Asas waliotoa tamko lolote kuhusianaa na kadhia hii ya siku mbili tatu. The Chanzo ilimtafuta msemaji wa Asas Diaries Faraj Asas kupata maoni yao ya namna walivyolipokea suala hili na kama wanadhani linaweza kuwa na athari yoyote kwenye biashara zao lakini alituma ujumbe mfupi wa simu akisema, “Asante kwa ujumbe wako sitoweza kujibu kwa sasa, lakini nitakujibu haraka iwezekanavyo, asante.” Hata hivyo, mpaka wakati wa kuandika habari hii akawa hajafanya hivyo.
Naye Clemence Mwapwele, Afisa Habari wa kampuni ya Tanga Fresh, ameiambia The Chanzo hafahamu kuhusiana na jambo hilo, kwamba ndiyo kwanza alikuwa anasikia kutoka kwa mwandishi. Alisema: “Kuhusu hizo habari za mtandaoni kwamba watu wanapigia promo maziwa ya Tanga Fresh, hatujaliona. Ila kwa kuwa umetuambia, basi tunalifatilia kwa ukaribu.”
Wakati wa mahojiano na The Chanzo, kijana Hussein Abui aliyehusika na kuibua kadhia hiyo alisema kwamba ana amini vijana wengi wanakumbana na changamoto za ajira na kuomba nafasi ya kazi sio dhambi, akibainisha kwamba majibu mabaya yanakwamisha ndoto za vijana wengi.
“Ni vyema kutoa majibu pale mtu anapokuomba msaada kwa wakati ule ule na hata kama hakuna nafasi ni vyema kumjibu vizuri,” anasema Abui, na kuongeza: “Nawashauri mabosi wenye tabia kama hizo waache lakini pia wawe na imani ya kuweza kusaidia wengine, maana leo wanacho lakini kesho hawana lakini pia kama hawezi kumsaidia mtu wawe na lugha nzuri kwa wale wanaowaomba nafasi za kazi.”
Dk Juma Makaranga ni mchambuzi na mkufunzi wa masuala ya kibiashara ambaye anawashauri wakuu wa makampuni kuwa makini na shughuli zao za mitandaoni, akisema kwamba majibizano na mabishano yasiyo ya lazima huweza kufanya watu wawe na taswira tofauti tofauti kuhusu wao binafsi na biashara wanaohusishwa nazo kitu ambacho kinaweza kuwa na athari hasi kwa biashara husika.
“Ni lazima kuheshimu nafasi yako katika jamii na hivyo ndivyo kanuni za biashara zinavyotaka,” anabainisha Dk Makaranga wakati akiongea na The Chanzo. “Vinginevyo, utajikuta unaingia gharama ambazo ingekuwa sio lazima upate.”
Aveline Kitomary ni mwandishi wa habari za kisiasa kutokea Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: avekitomary@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatilie, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, unaweza kuwasiliana na mhrariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.