The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wadau Wasisitiza Utekelezaji wa Vitendo Mikakati Elimu Jumuishi

Wito huo unafuatia ripoti inayoonesha kwamba Tanzania kwa sasa haina mwongozo wowote unaoeleweka wa namna bora ya kugawa bajeti inayotengwa kwenye elimu ili ielekezwe kwa ajili ya elimu jumuishi.

subscribe to our newsletter!

Wadau wa elimu nchini wamebainisha kwamba ili Tanzania iweze kuwa na mfumo wa elimu jumuishi uliobora kunahitajika ufafanuzi wa kina wa kisera pamoja na uwepo wa mikakati madhubuti itakayotekelezwa kwa vitendo kwenye aina hiyo ya elimu inayolenga kuwaweka pamoja watoto wenye mahitaji maalumu, kama walemavu, na wale wenye uwezo wa juu kiakili katika ufundishaji na ujifunzaji.

Hayo yameelezwa siku ya Alhamisi, Aprili 29, 2021, wakati wa uzinduzi wa taarifa ya utafiti kuhusu uchambuzi wa kina wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali linalohusika na kupigania upatikanaji sawa wa haki ya elimu nchini Tanzania, HakElimu. Wadau hao wameeleza kwamba kuna changamoto kadhaa zinazowakabili watoto wenye uhitaji maalumu nchini Tanzania ambazo zinahitaji jitihada mahususi kuweza kukabiliana nazo.

Akiongea katika haflfa hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Tungi Mwanjala, Makamu Mwenyekiti wa Shrikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), alisema kwamba licha ya kuwepo kwa sera ya watu wanaoishi na ulemavu ya mwaka 2014 bado kumekuwepo na changamoto nyingi  kwenye suala la elimu jumuishi, akiongeza: “Mpaka sasa inazungumziwa tu elimu jumuishi lakini kwa vitendo haitekelezwi kwa kasi inayotakiwa. Ni muhimu tukakumbuka kwamba kuna wanafunzi wenye changamoto na wao wanahitaji kujifunza kama wengine.”

Katika uchambuzi wake wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, HakiElimu imebaini kwamba nyaraka hiyo muhimu kwenye mfumo wa elimu wa taifa haielezi kwa uwazi  kuhusu upatikanaji wa elimu kwa watu walio kwenye mazingira magumu au wenye mahitaji maalum, kama wale wenye ulemavu wa viungo, matatizo ya akili, kutokuona, kutokusikia, kutokuongea, usonji nakadhalika. Sambamba na hilo, uchambuzi huo pia umeeleza kuwa mpaka hivi sasa hakuna mwongozo wowote ule unaoeleweka wa namna bora ya kugawa bajeti inayotengwa kwenye elimu ili ielekezwe kwa ajili ya elimu maalumu.

Jambo hili pia limethibitika katika taarifa  ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2019/2020 iliyowasilishwa mwezi Machi, 2021, ambapo imebainisha kwamba moja ya changamoto inayokabili utoaji wa elimu kwa watu wenye uhitaji maalum nchini ni kukosekana kwa utaratibu endelevu wa ugharamikiaji wa elimu hiyo. CAG alitolea mfano katika mwaka wa fedha 2019/20 ambapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitumia Sh272 milioni iliyotengwa kwa ajili ya elimu ya watu wenye mahitaji maalum kwa shughuli nyingine tu kama vile kugharamia shindano la insha kwa lugha ya Kiingereza la nchi za Jumuia ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Ripoti ya HakiElimu pia imekuja huku takwimu za Serikali zikionesha kwamba nchini Tanzania kwa sasa kuna watoto zaidi ya 400,000 wenye changamoto ya ulemavu wa aina mbalimbali na wapo katika umri wa kwenda shule, kati  yao ni watoto 42,783 pekee ndio wameandikishwa katika shule za msingi.

“Tunazungumzia elimu jumuishi lakini kumekuwepo na makundi mawili yanayoishi kwenye dunia mbili tofauti,” alisema Neema Msangi, Afisa Programu Mwandamizi kutoka Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT), shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utetezi wa haki za wanawake nchini. “Tukiangalia hata humu ndani ni wachache wanaoweza kumuelewa yule dada anayetafsiri kwa lugha ya ishara pale. Sasa ili kuondoa matabaka na kuwawezesha watu wa makundi yote kuwasiliana ni vyema mfumo wetu wa elimu ukatambua kuwafundisha watu wote lugha za alama ili waweze kuwasiliana na wenzao kwenye jamii wanaotumia hiyo lugha.”

Robert Semtongo ambaye ni mtaalamu wa elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu alisema kwamba Sera ya Elimu na Mafunzo ya sasa haioneshi kwa kina mbadala wowote wa elimu jumuishi ili kuwawezesha wale watu wenye changamoto mbalimbali za ulemavu waweze kupata elimu bora. Semtongo alisisitiza kwamba sambamba na sera, pia kunahitajika mkakati kabambe wa kuwapatia mafunzo zaidi walimu wa shule zinazotoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

“Elimu jumuishi imebaki kama nadharia tu na sio vitendo,” alisema Semtongo. “Sisi wataalamu wa elimu maalumu bado hatupati kile tunachopaswa kuwapatia wanafunzi wenye uhitaji ili waende sawa na dunia ya sasa.”

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *