Dar es Salaam. Katika kipindi cha mwaka huu wa 2022, Tanzania imeshuhudia mkanganyiko mkubwa ukitokea kwenye maamuzi ya Serikali ambapo ilikuwa ni kitu cha kawaida kusikia uamuzi fulani umesitishwa siku chache tu baada ya kutangazwa.
Ni mikanganyiko ambayo imewapa picha baadhi ya wafuatiliaji wa mambo kwamba hakuna uratibu ndani ya Serikali na kwamba kwa kiasi kikubwa maamuzi mengi hufanywa bila ya uwepo wa ushiriki mpana wa watu ambao wanaenda kuathiriwa na maamuzi hayo.
Maamuzi hayo ambayo hutolewa na idara za chini za Serikali hutenguliwa na zile za juu, hususan kutokana na ukinzani mkali unaotokea dhidi yao kutoka kwa wananchi mbalimbali, wengi wao wakiwa ni wale wanaopaza sauti kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mfano, uamuzi wa hivi karibuni kabisa kusitishwa siku chache tu baada ya kutangazwa ni ule wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) uliowataka wafanyabiashara wadogo wote wanaofanya kazi Kariakoo, Dar es Salaam, wajisajili kwenye mfumo wa kutumia Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD).
Akitangaza uamuzi hapo Disemba 12, 2022, Meneja wa TRA wa mkoa wa kikodi wa Kariakoo Alex Katundu alisema kwamba mwisho wa zoezi hilo la usajili itakuwa ni Machi 30, 2023, huku wamachinga takribani 8,900 wakitegemewa kujisajili kwenye mfumo huo.
Uamuzi huo, hata hivyo, ulisitishwa siku moja tu baada ya kutangazwa, Disemba 13, 2022, huku Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba akisema kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uamuzi huo, huku akiwataka wamachinga wasipate taharuki.
Uamuzi wa kufuta uamuzi huo ulitokana na malalamiko kutoka kwa wamachinga kwamba hawakushirikishwa kwenye mchakato huo.
“[Hili suala] tayari limeshamfikia Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu na ameshaagiza kusitishwa kwa zoezi lote hadi pale utaratibu rasmi utapowekwa,” Dk Nchemba aliiambia Clouds TV kwenye mahojiano naye. “Nitoe rai kwa machinga wasipate taharuki.
NHIF na bima ya afya
Mnamo Agosti 1, 2022, pia, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulitangaza utaratibu ambao ungemzuia mteja aliyezoea kutibiwa kwenye hospitali moja kwenda kutibiwa kwenye hospitali nyingine mpaka atakapo pata rufaa au baada ya kupita kwa siku 30.
NHIF ilibainisha kwamba lengo la kuanzishwa kwa utaratibu huo ni kupunguza gharama zisizokuwa za lazima. Mnamo Agosti 3, 2022, hata hivyo, siku tatu tangu kuanza kutekelezwa kwa utaratibu huo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliibuka na kuufuta.
Mwalimu alisema kwamba wakati anakubaliana na mkakati wa NHIF wa kupunguza gharama zisizokuwa za lazima, kabla ya utekelezaji wake kuanza inahitajika NHIF ikae na wadau wake ili kujadili utaratibu mzuri wa utekelezaji wa mpango huo.
“NHIF wanayo hoja ya kutaka kudhibiti gharama zisizo za lazima za matibabu,” alisema Mwalimu ambaye pia ni Mbunge wa Tanga Mjini (Chama cha Mapinduzi – CCM). “Lakini nilichowaelekeza, nimeitaka NHIF kusimamisha utaratibu waliouanza leo mara moja.”
TAWA na usafirishaji wanyama
Na hapo Juni 2, 2022, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilitangaza kuruhusu usafirishwaji wa wanyamapori waliokuwa wamesalia kwenye mazizi na mashamba ya ufugaji kwenda nchi za nje, utaratibu ambao ulikuwa umesitishwa tangu mwaka 2016.
Katika taarifa yake, TAWA ilitoa ruhusa hiyo ya usafirishaji kwa kipindi cha miezi sita mfululizo kuanzia Juni 6, 2022, hadi Disemba 5, 2022.
Lakini siku nne baada ya uamuzi huo kutangazwa, mnamo Juni 6, 2022, Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Pindi Chana aliibuka na kusitisha mpango huo wa TAWA kwa kile alichoeleza kuwa ni mpaka Serikali itakapopata taarifa rasmi kutoka katika taasisi husika.
“Kama Waziri mwenye dhamana wa masuala yote ya maliasili na utalii, nachukua nafasi hii kusitisha mara moja usafirishwaji wa wanyama pori hao mpaka hapo Serikali itakapopata taarifa rasmi kutoka katika taasisi husika,” alisema Dk Chana.
TANESCO na LUKU
Mnamo Agosti 17, 2022, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) nalo liliwataka wateja wake wanunue umeme wa kutosha kwa sababu lilitarajia kuuzima mfumo wa ununuaji wa umeme kwa njia ya LUKU kuanzia Agosti 22, 2022, hadi Agosti 25, 2022, kwa ajili ya kufanya matengenezo ya maboresho ya mfumo huo.
Meneja wa TEHAMA wa TANESCO Cliff Maregeli aliwaambia waandishi wa habari kwamba wateja wangeikosa huduma ya LUKU kuanzia saa nne usiku hadi saa moja asubuhi kutokana na matengenezo hayo ambayo lengo lake ilikuwa ni kuongeza ufanisi katika mfumo wa LUKU.
Saa chache baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo, hata hivyo, TANESCO ilitoa taarifa nyingine iliyoeleza kuusitisha mpango huo ambao ungewafanya wateja wake kushindwa kupata huduma ya LUKU kwa siku nne.
“Tutawajulisha pale tutakapokuwa tayari kuendelea na zoezi hilo,” TANSECO ilisema kwenye taarifa yake. “Shirika linaomba radhi kwa usumbufu wowote unaojitokeza.”
Mnamo Agosti 5, 2022, The Chanzo ilichapisha habari iliyouliza, Mkanganyiko wa Maagizo Kati ya Wizara, Idara za Serikali: Tatizo ni Nini? ambapo iliwauliza wadau mbalimbali ni sababu gani wanadhani zinapelekea hali hiyo.
Ushirikishwaji hafifu
Moja kati ya wadau waliohojiwa kwenye habari hiyo ni Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya utawala ambaye alisema kwamba kusitishwa kwa maamuzi hayo siku chache baada ya kutangazwa inasababishwa na ukosefu wa uratibu Serikalini pamoja na maamuzi ya ghafla.
“Changamoto ni kwamba wanaoathirika hawakupewa taarifa,” alisema Eyakuze wakati wa mahojiano na The Chanzo.
“Na kama kuna tatizo, basi je, kuna uwezekano wa kuzungumza jinsi ya kulitatua hilo tatizo lisiwe endelevu na siyo kufanya uamuzi ambao ni ghafla, unaumiza, halafu watu hawana sauti yoyote ile ya kujaribu kuchangia suluhisho mbadala,” aliongeza Eyakuze.
Kwa upande wake, Deus Kibamba, mchambuzi wa masuala ya kiutawala, aliiambia The Chanzo tatizo analoliona yeye ni kukosekana kwa kitu kinachoitwa “utaasisi” ndani ya Serikali na kupelekea aina hii ya mikanganyiko.
“Ninachokiona mimi ni kwamba tuna tatizo la kukosekana kwa utaasisi,” alisema Kibamba wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Serikali inatakiwa ifanye kazi kama taasisi, yaani maamuzi hayawezi kutokana na mtu mmoja.”
Je, tutarajie ushirikishwaji zaidi wa watu wanaoenda kuathiriwa na maamuzi mbalimbali ya Serikali mwaka 2023?
Na je, hilo peke yake likifanyika bila ya uwepo wa “utaasisi” serikalini kutapunguza maamuzi kusitishwa siku chache baada ya kutangazwa?
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.
One Response
Aisee nafurahia upangiliaji wa Habali zenu. Hongera sana The Chanzo