Dar es Salaam. Hatimaye marufuku ya kufanya mikutano ya hadhara iliyokuwa imewekwa dhidi ya vyama vya upinzani nchini Tanzania imeondolewa, huku CHADEMA kikiwa ni chama cha upinzani kinachoongoza kufanya mikutano mingi ya hadhara tangu zuio hilo litenguliwe hapo Januari 3, 2023.
CHADEMA kilizindua mikutano yake ya hadhara huko Mwanza hapo Januari 21, 2023, shughuli iliyoambatana na maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake. Ikafanya pia mkutano wa hadhara Musoma na Tarime mkoani Mara.
Chama hicho pia kilifanya mkutano wa hadhara Temeke, Dar es Salaam hapo Januari 25, 2023, ulioambatana na mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wake (Tanzania Bara) Tundu Lissu. Pia, mkutano wa hadhara ulifanyika Ikungi, Singida, mnamo Februari 5, 2023.
Ajenda kubwa zilizotawala mikutano hiyo ya hadhara ya CHADEMA ilikuwa ni madai ya Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi lakini pia kupanda kwa gharama za maisha, hali inayohusishwa na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma muhimu, jambo linaloendelea kulalamikiwa na wananchi walio wengi.
John Mrema, akieleza tathmini yake ya mikutano hiyo kwa The Chanzo, alisema mikutano hiyo imeonesha ni kwa namna gani Watanzania walikuwa na kiu kubwa ya haki ya kukusanyika na kutoa maoni yao.
“Waliukosa uhuru huo ambao ni haki yao,” Mrema, ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa CHADEMA, alisema. “[Watanzania] walikosa watetezi wa masuala yao kwani hawakuwa na sauti. Sasa sauti ya Watanzania imerejea.”
“Watanzania bado wapo tayari kwa mabadiliko makubwa ya kisiasa na ya kiutawala,” aliongeza Mrema kwenye mahojiano yake na The Chanzo.
Katazo la mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani lilidumu kwa kipindi cha takriban miaka sita tangu liwekwe na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli kabla ya kutengeliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mapema mwaka huu.
Samia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), chama tawala, alichukua hatua hiyo kufuatia pendekezo la kikosi kazi alichokiunda kukusanya maoni ya wadau juu ya namna bora ya kuendesha siasa za vyama vingi nchini.
Hatua hiyo pia ilikuja katika muktadha wa mazungumzo yanayoendelea kati ya Serikali, CCM na CHADEMA ya kutafuta maridhiano ya kisiasa nchini yaliyotokana na hatua ya CHADEMA kususia mchakato unaoendeshwa na Kikosi Kazi cha Rais ambacho mwenyekiti wake ni Profesa Rwekaza Mukandala.
Kukosekana kujiandaa
The Chanzo ilimuuliza Ezekiel Kamwaga, mwandishi wa habari wa siku nyingi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, ni ipi tathmini yake ya mikutano hiyo ya CHADEMA ambapo alibainisha kwamba anaona kukosekana kujiandaa kwa chama hicho cha upinzani.
Hata hivyo, Kamwaga alieleza kwamba hilo linaeleweka ukizingatia ukweli kwamba uamuzi wa kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ulikuja ghafla, hali iliyovisababishia vyama vya upinzani, ikiwemo CHADEMA, kukosa kitu cha msingi cha kuzungumza na wanachama wake.
“Sasa, kwa mfano, sasa hivi mtu akisema kwenye mikutano ambayo imeshafanyika ya CHADEMA ni kitu gani kikubwa kimezungumzwa, ni kipi ambacho labda hakikuwepo zamani utakiona kipya?” anahoji Kamwaga. “Utaona mambo ni yaleyale tu.”
SOMA ZAIDI: Ni Kwa Namna Gani CHADEMA Inaenda Kudai Katiba Mpya?
Tathmini nyingine kwa mujibu wa Kamwaga ni kukosekana kwa ajenda ambayo CHADEMA ilipanga kuiuza kwa wanachama wake na Watanzania kwa ujumla, ajenda ambayo itawafanya wananchi waende kwenye mikutano yao kwa ajili ya kuwasikiliza.
“Sasa hivi tumeruhusu mikutano, ajenda ya upinzani ni nini?” anahoji Kamwaga. “Nadhani ndicho nilichokuwa nakitafuta. Unaweza ukasema Katiba Mpya lakini pia unaona ukiingia bungeni, ukiingia barabarani unakuta watu wanazungumzia kuhusu ugumu wa maisha. Watu wanashida zao nyingi wanapitia kwenye wakati mgumu.”
Hata hivyo, Kamwaga ana imani kwamba pengine vitu vyote hivi vitakaa sawa siku zinazokuja, akitahadharisha dhidi ya kuvihukumu vyama hivyo ambavyo kwa miaka zaidi ya sita vilikosa uhuru wa kujijenga na kujiimarisha kitaasisi.
Upinzani bado upo
Kwa upande wake, Dk Aikande Kwayu, mtafiti na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, ameieleza The Chanzo kwamba tathmini yake kubwa ya mikutano hiyo ni kwamba upinzani bado upo nchini na una nguvu ya ushawishi kwa wananchi.
“Mikutano hii imezidi kuwahakikishia na kuwaonesha umma kuwa bado upinzani upo [na] bado wananchi wanafurahia na wapo tayari kwa mabadiliko au kwa kuunga mkono hoja mbadala,” alisema Dk Kwayu.
Tathmini nyengine ya mtafiti huyo ni kwamba Jeshi la Polisi limekuwa mstari wa mbele kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
“Tumeona polisi wamekuwa na ushirikiano na ninafikiri kwa ujumla hali hii na mambo yanavyozidi kuendelea yanaleta kama kujiamini kwenye nchi kuwa kila mtu anaweza akafanya siasa na akaongea mambo ambayo yanaleta hoja mbadala kwa Serikali na pia kuweza kuiwajibisha Serikali,” alibainisha Kwayu.
SOMA ZAIDI: Ilikuwa Ni Lazima CHADEMA Ipoteze, Suala Lilikua Ni Nini Wanapoteza
Akielezea tathmini yake ya mikutano hiyo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Richard Mbunda aliiambia The Chanzo kwamba anapata maswali juu ya kama CHADEMA inataka kuachana na siasa za ukosoaji – au za “harakati,” kama alivyoziita – na kuhamia kwenye siasa za “kupakana mafuta.”
“Nilikuwa naona kwanza kuna mkanganyiko kwa viongozi wa CHADEMA,” Dk Mbunda alisema. “Je, wanakubaliana na kufanya siasa hizi za kistaarabu, siasa za kupakana mafuta, siasa za kupongeza na kusifia?”
Dk Mbunda anasema kwamba kwenye mkutano wake wa hadhara kule Mwanza, Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe alijaribu kuzungumza vitu vingi bila kumshambulia Rais Samia, akitumia muda mwingi kukosoa uongozi wa mtangulizi wake na siasa za ndani za CHADEMA.
“Kwa hiyo, hii ni moja ya tathimini niliyoiona,” anasema Mbunda. “Sasa sijui ni kwa kiasi gani itabadilisha upepo wa kisiasa hapa nchini, kwa maana ya jinsi ambavyo CHADEMA watafanya siasa zao.”
Katiba Mpya
Kwenye mahojiano yake na The Chanzo, Mrema alisisitiza kwamba ajenda kuu ya CHADEMA ambayo itakuwa inaieneza kwenye mikutano yake ya hadhara ni ile ya Katiba Mpya, kitu pekee anachoamini kinaweza kuizuia Tanzania isirudi kwenye “siku za giza.”
“Watanzania watarajie ajenda ya Katiba Mpya kusukumwa kwa nguvu zaidi na tunategemea hiyo ndiyo itakuwa ajenda kuu ya taifa, mpaka Katiba Mpya itakapopatikana,” alisema Mrema.
“[Lakini pia Watanzania] wategemee kuwa tutaendelea kuwa sauti yao kwenye masuala yote muhimu kwa taifa na kwa Mtanzania mmoja mmoja kama ugumu wa maisha, ufisadi na kadhalika,” aligusia mwanasiasa huyo.
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.