Kuna mambo, kama taifa, tunapaswa kuhoji na kuyachukulia tahadhari za mapema, hususan katika jicho la kisheria na muktadha ambao tunao ili kupima dhamira inayonenwa majukwaani na viongozi wetu kuhusu kupata Katiba Mpya siku za usoni.
Moja kati ya mambo haya ni huu mkazo wa kuboresha mfumo wa haki jinai nchini wakati ambao wananchi wanapaza sauti zao kuhusu uhuishwaji na umalizikaji wa mchakato wa Katiba Mpya.
Hatua hii inaibua maswali mengi ya kisheria, ya kimantiki na ya kimazingira kama ambavyo nitajaribu kuainisha katika andiko langu hili fupi sana.
Rais Samia Suluhu Hassan ameunda Tume ya Kutathmini Mfumo wa Haki Jinai inayoongozwa na Jaji Mkuu (Mstaafu) Mohammed Othman Chande ili kuboresha taasisi zinazohusika na utoaji haki jinai nchini kama vile Jeshi la Polisi na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS).
Taasisi nyingine zinazolengwa na tume hiyo ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Magereza na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Siyo jambo baya hata kidogo kuboresha mfumo wa utoaji haki jinai nchini ambao kwa kweli umeoza. Lakini swali la msingi linabaki kwa nini tuboreshe mfumo wa haki jinai nje kabisa ya muktadha wa mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya nchi?
Ninachokiona mimi ni juhudi za kutaka kuezeka paa la nyumba wakati hata msingi wenyewe haujajengwa!
Katika sayansi ya sheria, Katiba ya nchi ni sheria mama na wakati wa sasa kwa kuwa hatuna Katiba Mpya, Katiba ya Tanzania ya 1977 ndiyo sheria mama ambayo inapaswa kurejewa katika msingi wa maboresho ya mfumo wa haki jinai.
Mamlaka makubwa ya Rais
Lakini kimsingi Katiba hii ndiyo tatizo la msingi la utoaji haki nchini Tanzania, iwe ni haki jinai au haki nyingine yoyote ile. Hii ni kutokana na mamlaka makubwa Katiba hii inampa Rais wa nchi, hususan yale ya kiuteuzi, mamlaka yanayokwamisha utoaji wa haki vizuri.
Mfano mzuri ni mamlaka makubwa ya Rais katika kuteua Majaji na Mahakimu kama ilivyo kwenye Katiba, hali ambayo imethibitishwa mara kadhaa inavyoathiri uhuru wa Mahakama zetu katika utoaji haki.
SOMA ZAIDI: Ben Ishabakaki: Katiba Mpya Italeta Mageuzi Kwenye Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania
Pili, mamlaka ya Rais katika kumteua Mkuu wa Jeshi la Polisi kumetajwa kwa kiasi kuathiri uhuru wa jeshi hilo katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.
Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo yamechagiza mfumo mbovu wa haki jinai nchini Tanzania na ambayo yana msingi wake kwenye Katiba inayoendelea kutumika hivi sasa nchini.
Mchakato kuboresha haki jinai pia unaibua maswali na shaka juu ya dhamira ya uhuishwaji wa mchakato wa Katiba Mpya iliyodhihirishwa na Rais Samia mara kwa mara.
Mtu anaweza kujiuliza, kama nia ya kurekebisha mfumo wa utoaji haki jinai Tanzania ni ya kweli, kwa nini tusilitekeleze hilo kwenye muktadha wa utengenezaji wa Katiba Mpya ya nchi?
Katika Rasimu ya Pili ya Katiba, chini ya Jaji (Mstaafu) Joseph Sinde Warioba wananchi, kwa wingi wetu, tulipendekeza mambo tunayotaka yaweke misingi ya maboresho ya mfumo wa haki jinai.
Moja kati ya mapendekezo makubwa na ya kimageuzi ambayo wananchi tulitoa lilihusu kumuondolea Rais mamlaka makubwa ya kiuteuzi ambayo, kama nilivyoeleza hapo juu, yamekuwa yakichangia kupindisha mfumo wa utoaji haki jinani nchini.
Rasimu ya Warioba
Kwa mfano, Ibara ya 245 ya Rasimu ya Pili ya Katiba, maarufu kama Rasimu ya Warioba, inamuondolea Rais mamlaka ya moja kwa moja katika kumteua Mkuu wa Jeshi la Polisi na badala yake inamtaka Rais kushauriana na Baraza la Ulinzi na Usalama wa Taifa katika kufanya hivyo, kitu ambacho kwa sasa hakifanyiki.
Vilevile, ibara ya 249 ya Rasimu ya Warioba ilipendekeza kwamba Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.
Ikiwa ni katika nia hiyo hiyo ya kuufumua mfumo wa utoaji haki nchini Tanzania, Ibara ya 208(4) ya Rasimu ya Warioba ilipendekeza kwamba Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora watapatikana kwa kuthibitishwa na Bunge.
SOMA ZAIDI: Tito Magoti: Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Hali ya Haki Jinai Tanzania
Hii ni tofauti na utaratibu wa sasa uliobainishwa kwenye Katiba inayotumika hivi sasa ambapo unataka Rais siyo tu ateue Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo muhimu bali pia makamishna wake.
Hali hii, bila shaka, ina minya uhuru wa tume katika utekelezaji wa majukumu yake na kuathiri mfumo mzima wa utoaji haki.
Hii ni sehemu tu ya misingi iliyowekwa kwenye Rasimu hiyo inayopigiwa chapuo na wadau wa Katiba ambayo inaakisi mapinduzi kwenye mfumo mzima wa utoaji haki nchini Tanzania.
Kimsingi, maboresho ya mfumo wa haki jinai Tanzania yanagusa mihimili yote mitatu: Bunge, Mahakaka na Serikali. Kwa lugha rahisi, mihimili hii ndiyo roho ya Katiba na ndiyo msingi wa mfumo wa haki jinai.
Katiba Mpya
Kwakua mapambano ya Katiba Mpya yalianza kutokana na madhaifu ya muingiliano hasi wa Serikali dhidi ya mihimili mingine miwili na taasisi nyingi za utoaji haki, kipaumbele cha kwanza cha Rais kilipaswa kiwe Katiba Mpya ambayo kimsingi ingejibu maswali yake mengi kuhusu mfumo wa haki jinai nchini.
SOMA ZAIDI: Kuachiwa kwa Mbowe na Mapungufu ya Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania
Kuundwa kwa Tume ya Kutathmini Mfumo wa Haki Jinai kabla ya kumalizika kwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba, kwa mtazamo wangu, ni kupoteza rasilimali fedha za Watanzania na rasilimali muda kwani wananchi walishapendekeza misingi ya vyombo hivi vya haki jinai katika Rasimu ya Warioba kama nilivyoonesha, kwa ufupi, hapo juu.
Tulipaswa kuwekeza nguvu katika upatikanaji wa Katiba Mpya ambayo ndiyo ingeweka misingi na mawanda mapana ya mfumo wa haki jinai na ambayo ingechochea mapinduzi kwenye mfumo wetu wa haki jinai kwa maslahi mapana ya taifa letu!
Alphonce Lusako ni mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia alusako@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.