Songwe. Baadhi ya wakulima wa kahawa kutoka wilayani Mbozi mkoani hapa wamegoma kuuza zao lao hilo la biashara wakisema kwamba bei wanayotakiwa wauze ni ndogo sana ambayo haitaweza kurejesha gharama walizotumia kwa ajili ya kilimo na kupata faida.
Wakulima hao wanaolima kahawa aina ya arabika wamegoma kuuza kahawa hiyo kwa bei ya kati ya Sh4,600 na Sh5,100 kwa kilo wakitaka wauze kwa bei ya kati ya Sh7,100 na Sh7,500, kwa kilo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo The Chanzo imezipata, wakulima kutoka jumla ya vyama 19 vya ushirika kwenye zao la kahawa wilayani Mbozi hawajaweza kuuza zao hilo licha ya kulipeleka ghalani wakisubiri kutengamaa kwa bei.
The Chanzo imetaarifiwa kwamba wakulima hao wamekuwa wakisubiri bei hiyo kutengemaa tangu Julai 2022 bila kuweza kuuza kahawa yao, hali inayotegemewa kuwaathiri wakati ambao wanatakiwa wajiandae na msimu mpya wa kilimo.
Chama cha Ushirika cha Mbulu ni moja kati ya vyama hivyo 19 ambavyo wanachama wake wameiangukia Serikali, wakiiomba iingilie kati ili waweze kuuza kahawa yao kwa bei yenye maslahi kwao.
SOMA ZAIDI: ‘Sitegemei Kuvuna Kitu’:Wakulima Mtwara Walia na Ukosefu wa Mvua
Kati ya wanachama 65 wa chama hicho, wanachama 40 walipeleka kahawa katika ghala kama ambavyo mfumo wa vyama vya ushirika unaelekeza kwa ajili ya kusubiri bei nzuri ambayo inakuwa shindani kulingana na uhitaji wa siku hiyo.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho wameiambia The Chanzo kwamba wanapata shida kuendesha shughuli zao za kilimo katika msimu huu mpya wa kilimo kwani bado hawajapata fedha za msimu uliopita kutokana na bei sokoni kuwa changamoto.
Moja kati ya wanachama hawa ni Emanuel Fredy Dagasi ambaye ameeleza kwamba kwa miaka mingi wamekuwa wakiuza kahawa bila shida lakini mwaka huu hali imekuwa tofauti ambapo mpaka msimu mwingine wa mavuno unakaribia kufika bado kahawa yao haijauzwa.
“Miaka ya nyuma sisi kama wakulima tulilipwa hela zetu kwa wakati na ndiyo maana tuliendesha kilimo chetu kwa mafanikio,” Dagasi, 53, aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano yaliyofanyika kwa njia ya simu.
“Lakini mwaka huu tunashangaa ni kwa nini hii Mbozi tumekusanya kahawa yetu kwenye vyama vya ushirika tangu Julai [2022] mpaka leo hii tunaelekea msimu wa mwaka mwingine hatujapata fedha,” aliongeza. “Tunaomba ambaye anaweza kutusaidia, atusaidie.”
SOMA ZAIDI: Wakulima Walalamikia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Serikali Yafafanua
Mkulima mwengine wa kahawa, Ramsoni Mwaweza, alisema kwamba kushindwa kuuza kahawa yake kwa wakati kumeathiri shughuli za kilimo kwa mwaka huu ambapo analazimika kubadilisha mtindo wa kilimo ilimradi kutosalia nyumbani wakati wakazi wengine wa Mbulu wanaendelea na shughuli za uzalishaji.
“Tunashindwa kuendesha hata kilimo,” Mwaweza, 43, alisema. “Pili, ada, tumeshindwa kupeleka karo za watoto shuleni. Tumeshindwa kuwahudumia kwa hali hiyo. Ndiyo maana nasema tumeathirika. Hata mbolea yenyewe tumeshindwa [kununua]. Hata mahindi yenyewe tuliyolima siyo ya kuridhisha.”
Lukasi Mwakalinga, 37, aliiambia The Chanzo kuwa alipeleka kahawa ghalani ili aweze kurejesha fedha ambazo alikopa kwenye taasisi za kifedha na fedha zilizobaki aweze kuendeleza shughuli za kiuchumi.
“Kwa kweli hatujapokea pesa yoyote,” Mwakalinga alisema akiwa pembeni mwa shamba lake lenye ukubwa wa hekari moja. “Halafu isitoshe, pesa yenyewe hakuna. Tulitegemea tupeleke kahawa kwenye kikundi tukipata pesa tulipe deni halafu pesa inayosalia tuendeshe kilimo.”
Akiongea na The Chanzo kuhusu kadhia hiyo, Meneja wa Vyama vya Ushirika Wilayani Mbozi Mon Mwampamba alisema kwamba mpaka sasa tayari asilimia kubwa ya vyama vya ushirika wilayani Mbozi vimelipwa fedha zao na vikundi vichache vimesalia kulipwa.
Kuhusu vile vichache ambavyo havijalipwa, Mwampamba ameeleza kuwa bado havijalipwa kutokana na ukweli kwamba majadiliano ya muda mrefu kuhusu bei ya kuuzia yameshindwa kuzaa matunda.
SOMA ZAIDI: Wakulima Wadogo 852 Mbarali Waiburuza Serikali Mahakamani Wakitetea Ardhi Yao
“Baadhi ya vyama kukaa na kujadili kwenye vyama vyao kutofanya mauzo mpaka hali itakapotengamaa lakini imekuwa tofauti na matarajio yao hali iliyowalazimu wauze kwa kuchelewa mpaka sasa, alisema Mwampamba.
Afisa Kilimo Wilaya ya Mbozi John Peter ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano kwamba baadhi ya vikundi ambavyo havijauza ni kushindwa kufika muafaka wa kuuza kahawa yao.
Alisema bei ya zao hilo imeporomoka na hivyo wakaamua kusubiri mpaka bei ya kahawa ipande, hali ambayo imekuwa tofauti kwani bei ya kahawa imeendelea kuwa chini hadi baadhi ya siku kuuzwa kwa Sh4,800 kwa kilo moja.
“Tulikuwa na vyama karibu 25 havijauza,” alisema Peter. “Hivi karibuni vimeuza vyama sita na tayari wameshalipwa na vyama 19 havijauza bado kutokana na bei ya soko la dunia kuwa mbaya.”
Vyama vingine ambavyo bado havijauza kahawa yao mpaka sasa ni pamoja na Mahenje kilichopo kijiji cha Mahenje, Igamba, Iganda na Imasha, vyote vikiwa vipo katika wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.
Asifiwe Mbembela ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Anapatikana kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com.