Nilimfahamu Bernard Membe miaka ya 2000, na hususani miaka michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2015. Kabla ya hapo nilikuwa ninamsikia tu kwa kuwa alikuwa moja ya mawaziri waliokuwa wanajulikana sana.
Hivyo, katika hali ya kawaida, sina sifa stahiki kuweza kuandika wasifu wake baada ya kufariki. Kawaida wasifu wa maerehemu huandikwa na watu waliokuwa karibu naye wakati wa uhai wake.
Hata hivyo, nimepata msukumo wa kuandika wasifu huu baada ya kurejea makala nilizowahi kuandika huko nyuma kuhusu wasifu wake kama moja ya wagombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2015. Katika makala hizi niliweza kuandika kwa kina kidogo kuhusu wasifu wa wagombea urais baada ya kufanya utafiti wa maisha ya wahusika.
Ilipofika zamu ya Membe, niliandika kwa kina jinsi alivyozaliwa na kukulia kijijini, nikirejea baadhi ya madhila ambayo baba yake aliyapata katika kumkuza. Membe aliposoma makala hiyo alinitafuta na tukapanga kukutana naye katika hoteli moja jijini Dar es Salaam.
Kawaida katika kuandika makala hizi nilikuwa sijawahi kukutana na walengwa. Nilikuwa nafanya utafiti wangu na kukusanya taarifa za mhusika bila kumhusisha yeye.
Kwa hiyo, nilipata taabu kidogo aliponitafuta, ukizingatia wakati huo alikuwa ni mgombea mwenye jina kubwa sambamba na Edward Lowasa, na akiwa bado ni waziri maarufu sana wa Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki.
Mtu mcheshi sana
Nilipokutana naye, Membe alijitokeza kama mtu mcheshi sana. Akanieleza kwa bashasha jinsi ambavyo alikuwa amefurahia sana makala yangu na kwamba aliniita ili anipe taarifa zake zaidi kwa ajili ya sehemu ya pili ya makala yangu. Moja ya taarifa aliyonipa ni taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika jimbo lake la Mtama.
Katika makala hii ninarejea baadhi ya wasifu wa Bernard Membe kama nilivyouchapisha katika makala iliyokuwa na sehemu mbili ndani ya gazeti la Raia Mwema.
Makala hii inaonesha kuwa, pamoja na kwamba Membe alizaliwa na kukulia katika familia ya kawaida sana ya kijiji cha kawaida cha Kitanzania, bidii yake katika masomo na baadaye katika kazi ilimbeba kwa kiwango ambacho alifikia kuwa miongoni mwa watu wawili tu ambao wangeweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi wa Mwaka 2015.
Akiwa amezaliwa Novemba 9, 1953, huko kijijini Rondo-Chiponda katika Wilaya ya Lindi Vijijini, Ndugu Bernard Kamillius Membe (maarufu kama BKM) alikulia katika hali ya maisha ya Mtanzania wa kawaida aliyezaliwa kijijini.
Ndugu Membe aliingia shule akiwa na umri mkubwa wa miaka 10. Hii nayo ni hali ya kawaida kwa Watanzania walio wengi tuliozaliwa vijijini. Shule ya sekondari alisomea katika seminari ya Namupa (1969-1972), na baadaye akajiunga na Itaga Seminari Tabora kwa kidato cha tano na sita (1973-1974).
Pengine jambo moja ambalo wengi hatukulijua kabla ni kwamba Ndugu Membe alipata kusomea upadri kwa miezi kadhaa kabla ya kujiunga na Itaga Seminari.
Kwa mujibu wa Ndugu Paul Maokola, rafikiye Membe wa siku nyingi, Bernard Membe alikuwa miongoni mwa vijana 11 waliopata wito wa kusomea upadri na hivyo walichaguliwa kujiunga na Seminari Kuu ya Peramiho, Songea.
Hata hivyo, baada ya matokeo ya Kidato cha Nne kutoka Membe alikuwa ni miongoni mwa vijana watatu waliofaulu vizuri sana. Kwa sababu hii aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Mtwara wakati huo Marehemu Maurus Libaba aliamua kuwahamishia Itaga Seminari, ambayo ilikuwa ni seminari pekee ya kikatoliki iliyokuwa na masomo ya Kidato cha Tano na Sita.
Baada ya kumaliza Kidato cha Sita mwaka 1974 na kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, Membe hakujiunga moja kwa moja na Chuo Kikuu. Badala yake, Membe alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1981/82, akisomea shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa umma.
Hakufaulu vizuri
Sababu kubwa ambayo ilimfanya Membe achelewe kujiunga na chuo kikuu ni ukweli kwamba alikuwa hajafaulu vizuri sana katika mitihani yake ya Kidato cha Sita. Hali hii ilimlazimu kufanya mitihani iliyoitwa ‘Mature Age Entry Examinations.’
Kwa taratibu za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mtihani huu hufanywa na watu ambao hawakupata alama za kuingia Chuo Kikuu moja kwa moja kupitia matokeo ya Kidato cha Sita.
Baada ya kuhitimu masomo yake ya shahada ya kwanza Ndugu Membe alirudi kazini kwake. Pamoja na kwamba alifaulu vizuri sana katika masomo yake ya chuo kikuu kiasi cha kupewa kazi ya kuwa mhadhiri msaidizi, Membe alilazimika kurudi kazini kwake baada ya mwajiri kukataa ombi lake la kubaki chuo kikuu.
Akiwa ameanzia kazi katika Ofisi ya Rais, Membe alipanda ngazi kadhaa na hadi kuwa msaidizi wa waliopata kuwa wakurugenzi wakuu wa Idarai ya Usalama wa Taifa, Ndugu Hassy Kitine na Apson Mwang’onda.
Baada ya kumaliza masomo ya Shahada ya Umahiri katika Chuo Kikuu cha John Hopkins nchini Marekani, Membe hakurudi tena kufanya kazi Ikulu bali alipelekwa ubalozi wa Tanzania nchini Canada kama Mwambata wa Ubalozi (Minister Plenipotentiary), akichukua nafasi ya Hayati Dk Augustine Mahiga akiyekuwa amehamishiwa Umoja wa Mataifa.
Alidumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 2000 alipoamua kugombea ubunge, ambapo alishinda na kuwa Mbunge wa pili wa Jimbo jipya la Mtama akimrithi Masoud Ally Chitende.
Katika kampeni za urais za mwaka 2005 ndani na nje ya CCM Membe alifanya kazi kwa karibu na akina Lowasa na Apson katika kuhakikisha kwamba Rais Kikwete anapitishwa kuwa mgombea na hatimaye kushinda katika uchaguzi wa urais.
Inafurahisha na hata kushangaza kwamba baadae wawili hawa wakawa ni mahasimu wakubwa kisiasa, wote wakiwania nafasi ya kumrithi Kikwete. Sote tunakumbuka ushindani mkali ndani ya CCM kati yao, ambao walikua wanaonekana kuwa na nguvu, fursa, vikwazo, na udhaifu katika maeneo tofautitofauti.
Baada ya Rais Kikwete kushinda uchaguzi wa mwaka 2005 alimteua Membe kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, nafasi aliyoshikilia kati ya Oktoba 2006 na Januari 2007, na baadaye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kati ya Januari 2006 na Oktoba 2006, na baadaye kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Waziri wa muda mrefu
Katika mawaziri 14 wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Membe ndiye waziri wa pili kwa kushikilia nafasi hiyo kwa muda mrefu zaidi, akizidiwa tu na Rais Kikwete aliyedumu katika nafasi hiyo katika kipindi chote cha urais wa Benjamin Mkapa.
Pamoja na mambo mengine, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Membe atakumbukwa kuhusu misimamo yake kadhaa, ikiwemo mgogoro wa kisiasa uliokuwepo kati ya Tanzania na Rwanda na suala la uraia pacha. Waziri Membe alikuwa na msimamo wa waziwazi wa kuunga mkono uraia pacha, tofauti na viongozi wengi katika Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Msimamo wake mkali dhidi ya mambo kadhaa kimataifa, na kukulia kwake katika kazi ya ukachero, yaliwafanya baadhi ya watu kufananisha haiba ya Membe na ile ya Rais Vladimir Putin wa Russia aliyekulia Kremlin. Ni katika msingi huu Membe alijulikana pia kwa wapenzi wake wa kisiasa kama ‘Putin.’
Pamoja na utumishi wake katika nyanja mbalimbali nchini, Ndugu Membe alikumbana na misukosuko kadhaa nje na ndani ya chama chake. Mnamo Februari 28, 2020, Katibu Uenezi wa CCM wa wakati huo na sasa Balozi Humphrey Polepole alitangaza uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM wa kumvua uanachama ‘Putin.’
Katika hali iliyowashtua wengi, siku chache baada ya kufukuzwa uanachama wa CCM, BKM alihamia chama kichanga cha siasa cha ACT Wazalendo na kisha kupitishwa kuwa Mgombea wa Urais kwa tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Membe aliendesha kampeni zake katika hali ya kufurahisha na kushangaza kidogo mithili ya nahodha anayetoka kwenye chombo wakati wa dhoruba, akionekana uarabuni katikati ya kampeni, akisema ameenda kuhudhuria kikao muhimu cha bodi.
Waingereza wanasema, the rest is history. Membe hakufanikiwa kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Wahenga walisema mwenda tezi na omo marejeo ngamani.
Mnamo Mei 29, 2022, Bernard Kamilius Membe alirudi nyumbani, CCM, akiwa ametoa somo kubwa kuhusu demokrasia na ustahimilivu kwamba bila kujali yanayokusibu maisha lazima yasonge mbele na kamwe usisaliti msimamo wako.
Historia ya Membe inatufundisha mambo mawili makubwa. Mosi, huyu ni mtu aliyekulia maisha ya kawaida katika mazingira ya Mtanzania wa kawaida kijijini. Kwa maana nyingine, Membe alizaliwa na kukulia katika mazingira ya kinyonge. Kwa hiyo, alifika hapo alipo kwa kupambana na kwa kupenya.
Pili, mazingira ya kinyonge aliyokulia Membe hayakuwa kikwazo lakini yakawa kichocheo cha kupambana hadi kumfikisha kuwa mbabe katika karibu kila nyanya ya maisha, katika utumishi wa umma na siasa, na hata katika kuondokana na umaskini.
Kwa hiyo, historia ya Membe iwe fundisho kwa vijana wa kizazi cha leo kuwa mazingira yako duni ya sasa usiyaruhusu yawe kikwazo katika kupambana kufikia ndoto yako katika maisha. Hakuna limit katika uwezo wa binadamu wa kupambana.
Buriani Mbobezi, Putin wa Tanzania, BKM!
Kitila Mkumbo ni Mbunge wa Ubungo (Chama cha Mapinduzi – CCM). Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia kitilam@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.