The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Usumbufu Ni Mkubwa’: Wajasiriamali Waichambua Mikopo ya ‘Inuka na Uchumi wa Buluu’

Wajasiriamali wamelalamikia kukosa mikopo hiyo licha ya kufuatisha masharti na kukidhi vigezo vyote, huku wengine wakipewa mikopo pungufu kulinganisha na kiwango walichoomba.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Baadhi ya wajasiriamali visiwani hapa wamekuwa na uzoefu mchungu wa kusimulia kuhusiana na mikopo isiyo na riba inayotolewa na Benki ya CRDB kwa ushirikiano na Serikali ya Zanzibar chini ya kampeni ijulikanayo kama ‘Inuka na Uchumi wa Buluu.’

Mnapo Februari 12, 2022, Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi alizindua mikopo hiyo ambayo walengwa wake wakiwa ni wajasiriamali wanaojishughulisha na uvuvi, ufugaji wa samaki, na kilimo cha mwani, huku jumla ya Shilingi bilioni 60 zikitangazwa kutengwa kwa ajili ya wajasiriamali kutoka visiwa vya Unguja na Pemba.

Wajasiriamali walitegemewa kunufaika na fursa hiyo kupitia vikundi vyao vilivyosajiliwa ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuyawezesha kiuchumi makundi ya akina mama, vijana, na watu wenye ulemavu.

Hata hivyo, kutokana na tathmini iliyofanywa na The Chanzo, wajasiriamali wengi wameilalamikia mikopo hiyo, huku wengi wakiwa na wasiwasi endapo kama lengo lake la kuchochea ukuaji wa uchumi litafanikiwa.

SOMA ZAIDI: Shauku ya Kujitegemea Yawasukuma Wanawake wa Kizanzibari Masokoni

Baadhi ya malalamiko ambayo The Chanzo iliyasikia kutoka kwa wajasiriamali ni baadhi yao kukosa mikopo hiyo licha ya kufuatisha masharti na kukidhi vigezo vyote; waombaji kupewa mikopo pungufu sana kulinganisha na kiwango walichoomba; pamoja na michakato kuwa migumu, mirefu, na inayochosha ya kupata mikopo hiyo.

Maua Ali ni Mwekahazina wa kikundi cha Mungu Muweza, kikundi chenye wanachama 16, kilichopo Wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja. Kikundi hiki kilichoanza mwaka 2018 kinajishughulisha na uuzaji chumvi.

Maua aliiambia The Chanzo kwamba kikundi chake kiliomba mkopo wa Shilingi milioni  10 kwa ajili ya kuendeleza biashara yao ya ufugaji kuku na kukuza mtaji wa kuuza chumvi nje ya Zanzibar.

Walianza utaratibu wa kujaza fomu, zoezi walilolifanya zaidi ya mara tatu mpaka kulipatia kwa usahihi, lakini fomu yao ilipofika wilayani ilibadilishwa kiwango cha fedha na kupunguzwa hadi Shilingi milioni mbili na nusu, fedha ambayo ndiyo waliipata, kitu ambacho Maua anasema haikuwa lengo la kikundi hicho.

Usumbufu ni mkubwa

“Kwanza usumbufu ni mkubwa,” Maua alilama alipokuwa anaongea na The Chanzo. “Kisha, sisi uwezo wa [Shilingi] milioni mbili tunao [lakini] tukaambiwa tunapewa hizo kama majaribio ila tukishalipa watatuongeza.”

Maua na kikundi chake kwa sasa wanapambana wamalize deni lao ili waweze kupata mkopo unaoendana na mahitaji yao. Hata hivyo, itachukua muda mpaka wakamilishe deni hilo kulingana na namna benki inakata deni lao.

SOMA ZAIDI: EAC Yatakiwa Kuboresha Sera, Sheria Kusaidia Wajasiriamali Wanawake Mipakani

“Sisi tunalipa pesa nyingi ili tumalize, tupate nyingine,” alisema Maua. “Ila kule benki hata ukipeleka [pesa] nyingi wao wanakata [Shilingi] 120,000 tu, nyengine wanatuwekea. Kwa hiyo, bado tuna deni lakini tuna na akiba pia.”

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mikopo hiyo hapo Februari mwaka jana katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil, Kikwajuni, Zanzibar, Rais Mwinyi alisema mikopo hiyo itakuwa kichocheo kikubwa kwa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, akiwataka wajasiriamali kuchangamkia fursa hiyo ya kipekee.

Lakini The Chanzo ilikutana na wajasiriamali kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya kisiwa cha Unguja ambao walieleza kwamba licha ya kutekeleza ushauri huo wa Rais wao na kukidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo, maombi yao yameambulia patupu.

Umoja ni Nguvu ni kikundi kilichopo Kianga, wilaya ya Magharib A, mkoa wa Mjini Magharib, Unguja, chenye wanachama 25 na umri wa miaka mitatu. Kikundi hiki kinachojishughulisha na ushirika wa kuweka na kukopa kina makadirio yanayozidi Shilingi miliona 15 kwenye akaunti yao ya benki.

Mwenyekiti wa kikundi hiki, Haji Makame, aliiambia The Chanzo kwamba kwa siku nyingi walikuwa na mpango wa kutaka kununua gari ya abiria ili kukuza mtaji wa kikundi chao na faida kwa wanachama.

Waliamua kuitikia wito wa Rais Mwinyi wa kuchangamkia fursa ya ‘Inuka na Uchumi wa Buluu’ lakini hata hivyo hawajafanikiwa kupata mkopo huo.

Hatujapata kitu

“Tulipomsikia Rais anasema kuwa mikopo ipo, tutapewa, nasi tukaanza mchakato na nakumbuka sisi tulikuwa wa kwanza haswa, ila mpaka sasa hatujapata kitu,” Makame alisema kwa sauti iliyoashiria kukata tamaa.

SOMA ZAIDI: Ushauri Watolewa kwa Wanawake Wajasiriamali Mtandaoni

“Tungekuwa hatuna kitu wangesema sisi ni wapya, lakini sisi tuna kila kitu,” aliongeza Makame, akimaanisha usajili wa kikundi. “Sasa kutokujali ndiyo kumezidi haswa mara mwisho [benki] walisema hawatoi tena.”

Umoja ni Nguvu ni moja tu ya vikundi ambavyo The Chanzo ilikutana navyo ambavyo wanachama wake walilalamika kukosa mikopo hiyo ya ‘Inuka na Uchumi wa Buluu.’

Dk Talib Salum Zahor, Mhadhiri kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Idara ya Uchumi na Usimamizi wa Kodi, anasema hii ni lawama kwa Serikali.

Kwenye mahojiano na The Chanzo, Dk Zahor alisema kwamba kwa kiasi kikubwa malalamiko haya ya watu kukosa mikopo yanatokana na uamuzi wa Serikali kuiteua benki kuwa msimamizi wa masuala ya mikopo ya wajasiriamali wadogo wadogo, uamuzi ambao anadhani haukuwa sahihi.

“Suala la utaoji wa mikopo lilitangazwa kwa wananchi kama ni kitu ambacho kipo tu na watu watapewa bila ya wananchi kuambiwa kuwa kutakuwa na vigezo, masharti, na utaratibu maalum, ndiyo maana unaona malalamiko ni mengi,” alisema Dk Zahor kwenye mahojiano na The Chanzo.

Mtaalam huyo alisema kwamba CRDB, kama benki, haiwezi kutoa pesa kwa kikundi ambacho hakina mpango biashara utakaonesha jinsi ambavyo faida na biashara hiyo itakuwa.

SOMA ZAIDI: Kitendawili Vitambulisho vya Wajasiriamali Zanzibar

“Ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba kabla ya kuwaambia watu kuna pesa sehemu fulani mkakope, ili wasiende kule na kuumia, kwanza wapewe elimu na waambiwe kuwa pesa iliyoko kule si sadaka, kwamba watatumia kisha wakasahau,” alisema Dk Zahor.

Siyo wajasiriamali wote, hata hivyo, wana hadithi mbaya. The Chanzo ilikutana na vikundi vingine vilivyonufaika na mkopo huo na ambao vimeendelea kukuza biashara zao.

Moja kati ya vikundi hivi ni kikundi cha Sayari Yetu kilichopo Maungani, Mjini Unguja, kinachojishughulisha na uuzaji wa chakula kwa jumla.

Kikundi hicho chenye wanachama sita kiliomba mkopo wa Shilingi milioni 25 ila walipata mkopo wa milioni 12 na wanatakiwa kurudisha Shilingi laki tano kila mwezi.

Farida Ali, Mwenyekiti wa kikundi hicho, aliiambia The Chanzo kwamba mpaka kufikia kupata pesa ni uchovu mwingi umekikumba kikundi chao, akisema mchakato wa kuzipata fedha hizo uliambatana na kutaabika na kukata tamaa.

“Tumepata ila marejesho ni makubwa,” alisema Farida kwenye mahojiano na The Chanzo. “Halafu muda ni mdogo pia kupata huo mkopo ni mbinde na kuchoka.”

Ni vikundi kama hiki cha Sayari Yetu ndivyo Serikali huvitumia na kusema kwamba mpango wa ‘Inuka na Uchumi wa Buluu’ umetekelezwa kwa mafanikio visiwani Zanzibar.

Hali ni nzuri

Ndiyo vikundi vinavyomfanya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar, Juma Burhan Juma, kuhitimisha kwamba “hali ni nzuri” linapokuja suala la utekelezaji wa mpango huo.

Kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake, Juma alisema mpaka sasa jumla ya Shilingi bilioni 17 zimetumika kukopesha watu 18,524 kutoka Pemba na Unguja, wanawake wakiwa 11,439 na wanaume wakiwa 7,050, huku 35 wakiwa ni watu wenye ulemavu.

SOMA ZAIDI: ​​Mfumuko wa Bei Unavyohatarisha Biashara za Wanawake Masokoni

Juma alisema kwamba mpaka kufikia Mei 2023, jumla ya Shilingi bilioni 4.5 zimerejeshwa na watu walionufaika na mkopo huo wa Shilingi bilioni 17.9 ambao mpaka kufikia Mei 2023 Serikali ilikwisha toa kwa wajasiriamali kupitia Benki ya CRDB.

“Mahitaji ni mengi na pesa ni kidogo,” Juma alisema alipoulizwa kuhusu malalamiko ya baadhi ya wajasiriamali kukosa mikopo hiyo. “Ila tunaendelea kuwafikia japo hatuna uhakika kwamba tutaweza kuwamaliza na kutatua changamoto za kila kikundi kwenye suala hili la mikopo.”

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar.Kwa maoni unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts