Dar es Salaam. Maelezo yanayofuata yametolewa kutoka sauti kwenda kwenye maneno kutoka kwenye mahojiano maalum ambayo The Chanzo imefanya na Dk Baruani Mshale, mtaalamu wa masuala ya maliasili na mabadiliko ya tabianchi. Uhariri umefanyika kuboresha usomaji.
Kwa hapa kwetu Tanzania, na Mtanzania yoyote ninaweza kusema ambaye labda amekuwa na akili zake timamu katika miaka 10, 15, 20 iliyopita, ataweza kuthibitisha haya, [kwamba] kumekuwa na mabadiliko ambayo mimi nayaona makubwa mawili, na yote yanahusiana na mvua na kipindi cha ukame.
Mvua, katika maeneo mengi, zimekuwa zikipungua. Msimu wa mvua umepungua. Lakini pia mvua kunyesha nyingi, kwa muda mfupi, siku kadhaa, ama wiki kadhaa, matukio haya yanaongezeka. Mvua ambazo zinapelekea maafa, mafuriko, nakadhalika, zimeongezeka.
Kumekuwepo na mafuriko miaka 50 iliyopita, miaka 40 iliyopita. Lakini hata ukizungumza na wazee wetu, watakumbuka kwamba labda kulikuwa na mafuriko kipindi fulani na hata watoto waliozaliwa kipindi hicho kuna majina waliyopewa yaliyoendana na hayo mafuriko kama namna ya kukumbuka.
SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Ni Nini? Mtaalam Afafanua
Lakini wao wenyewe, wale wazee, watakwambia kwamba mafuriko ambayo yametokea ndani ya miaka 10 mpaka 20 iliyopita imekuwa ni mara kwa mara ukilinganisha na kipindi cha miaka iliyopita. Lakini vilevile jamii nyingi za Watanzania zimekuwa zikijikuta mvua zinanyesha katika kipindi ambacho sicho walichozoea.Wametayarisha mashamba, wamepanda, mvua hazikunyesha, baada ya siku kadhaa, mvua zinaanza kunyesha na zinanyesha nyingi katika muda mchache, zinaharibu mazao mashambani.
Haya matukio ya namna hii yamekuwa yakiongezeka na ndiyo maana kumekuwa na upungufu wa chakula, ama baa la njaa, katika maeneo mengi ya nchi, katika miaka hii 10, 15, 20 iliyopita, ukilinganisha na kabla ya hapo.
Lakini vilevile, suala la ukame. Ukame ulikuwepo iwe ni mwaka 1900, mwaka 1930, au mwaka 1950. Kuna nyakati ambazo kulikuwa na ukame. Na ukiangalia katika historia yetu, ukizungumza na wazee, wataeleza nyakati ambazo kulikuwa na ukame.
SOMA ZAIDI: Nini Hupelekea Mabadiliko ya Tabianchi?
Lakini kama ilivyo kwa mvua, matukio ya ukame yameongezeka miaka ya hivi karibuni ukilinganisha na miaka ya zamani. Kwa mfano, mwaka jana [2022], mwezi Oktoba, nilikuwa pamoja na wenzangu maeneo ya Longido, [Arusha] na wakawa [wenyeji wa huko wakawa] wanaelezea ukame ambao umekuwepo pale na wanasema ukame huo umeanza tangu mwaka 2019.
Kwa hiyo, mpaka mwaka jana 2022, wanaona kabisa kwamba ule ukame umekuwepo kwa muda mrefu. Kwanza, ndani ya mwaka mmoja, miezi ambayo inakuwa ni miezi ya ukame, imekuwa ni mingi, tofauti na kipindi cha nyuma, halafu kutokea kwa matukio ya ukame kumeongezeka.
Zamani ilikuwa kwamba ikitokea ukame wanajua kwamba itakuja miaka ya neema, kama ni mifugo yao basi itazaliana na wataweza kuendelea na maisha yao. Lakini wanasema kwamba kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kwa mfano mwaka 2006, 2007 mpaka 2009, kulikuwa na ukame.
SOMA ZAIDI: Wananchi Mkuranga Walia Na Athari Za Mabadiliko Tabia Nchi
Halafu mwaka 2014 mpaka 2016 kumekuwa na ukame, halafu mwaka 2019 mpaka 2022 kumekuwa na ukame, wakati zamani, ndani ya miaka 10 au 20, pasingetokea vipindi vya ukame uliokithiri vitatu kama ambavyo imetokezea katika ndani ya miaka hii 20.
Kwa hiyo, hicho ni kiashiria kimojawapo cha kwamba mabadiliko ya tabianchi Tanzania yameongezeka.
Mvua zinazosababisha maafa zimeongezeka pia. Mvua zinanyesha kipindi ambacho hatutarajii, yaani nje ya msimu ule wa mvua na zinanyesha kubwa zinazosababisha maafa.
Halafu vipindi vya ukame vimeongezeka, muda wa ukame umeongezeka na ule ukame wananchi wanasema ni ukame uliokithiri, unaosababisha athari kubwa sana. Haya ndiyo mabadiliko hasa ya tabianchi ambayo yanaonekana nchini mwetu.