Wengi wetu tumewahi kuwatamkia watoto wetu maneneo mabaya ambayo baadaye tukifikiri hatuamini hata ilikuwaje mpaka tukafanya hivyo.
Baadhi ya wazazi wamekuwa wakienda mbali zaidi na kuwatamkia watoto wao maneno kama “wewe ni hasara tupu,” “mbwa kabisa wewe,” “huna akili hata kidogo” na maneno mengine kadha wa kadha yasiyofaa kutamkiwa kwa mtoto.
Baada ya kufanya hivi, hata hivyo, wazazi hawa wanaanza kujiuliza inakuwaje rahisi kuwanenea watoto wao maneno haya ambayo hasa hatukupenda kuyasikia kutoka kwa wazazi wetu yanatutoka kinywani kirahisi namna hii.
Wakati ni vigumu kurejesha maneno ambayo tayari yametoka mdomoni, zipo njia za kuonesha kujutia kwako kufanya hivyo. Moja kati ya njia hizo ni kuomba msamaha. Ni kweli, wazazi wengi huhisi uzito kuomba msamaha, lakini tunakusihi wewe usiwe mmoja kati yao.
Kama mzazi, unapaswa kufahamu kuwa kumuomba mwanao msamaha ni jambo la busara, hasa unapogundua umemkosea na imemuumiza.
“Nisamehe” ni neno moja rahisi sana ambalo lina mchango mkubwa na chanya katika kumjenga mtoto kifikra. Hata hivyo, imekuwa ni vigumu sana kwa wazazi wengi kutamka neno hili kwa watoto wao pale wanapowakosea.
SOMA ZAIDI: Fahamu Kwa Nini Watoto Wachanga Hucheua
Utafiti uliofanywa na Mtandao wa Malezi Afrika, au Parenting in African Network, kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la Save the Children, ulibaini kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watu waliofanyiwa mahojiano walisema ni vyema wazazi kuwaomba watoto msamaha pale wanapowakosea; japo baadhi walisema si vyema kwa mzazi kumuomba mtoto msamaha.
Wazazi walio wengi hawatambui umuhimu wa kuwaomba watoto wao msamaha kwa kuwa wengi wetu hatuna utamaduni wa kukubali kosa mbele ya mtoto katika mila zetu, hasa pale unapojiridhisha kabisa kwamba una makosa.
Ukweli ni kwamba, kumuomba msamaha mtoto wako itasaidia kuimarisha mahusiano mazuri baina yenu na kumjengea dhana ya kujiamini kuwa yuko kwenye mikono salama.
Pia, humjengea imani na tunu ya kwamba ni sawa kuwa binadamu na kukosea ni sehemu ya ubinadamu na pia kama mzazi utasimama kama mfano wa kuigwa kwa mwanao.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Siku 1,000 za Mwanzo za Mtoto Ni Muhimu?
Kuwa mzazi hakukuondolei uwanadamu ambao kukosea ni sehemu ya maisha. Ukimuomba msamaha mtoto wako, itamfunza stadi za maisha zenye umuhimu kama vile kuishi na watu vizuri.
Kukubali kosa ni jambo gumu lakini ni busara kufanya hivyo. Kila mara kumbuka kuwa kusema samahani kwa mtoto ni ishara ya utu na si mapungufu.
Karibia wazazi wote wanapenda watoto wanyenyekevu na wenye adabu, ila kupenda kuheshimiwa bila kuonesha heshima si jambo zuri. Mtoto anatakiwa kujifunza kutoka kwako.
Kukubali kosa pale unapokosea humpa mtoto ujumbe kwamba unamthamini na thamani hii itakurudia siku zote. Watoto ni viumbe wenye kusamehe. Tukizidisha heshima na upendo kwao, basi tunawapa nafasi nzuri ya kufanya hivyo kwetu kama wazazi na kuomba msamaha pale wanapokuwa wamekosea.
SOMA ZAIDI: Upi Ni Umri Sahihi Kwa Mtoto Kumiliki Simu ya Mkononi?
Hatupendekezi kwamba mzazi awe anaomba msamaha kupitiliza, ama kuongea kwa kumnyenyekea mtoto kila mara, na wala hatulengi mzazi asalimishe mamlaka yake.
Unachotakiwa kufanya ni kuwa tu jasiri na kumuomba mtoto msamaha pale unapokuwa na uhakika umekosea na mtoto ataendelea kutambua kuwa wewe ndiye mwenye mamlaka.
Je, unaweza kumuomba mwanao msamaha kirahisi, au unapata ugumu kufanya hivyo? Nini maoni yako juu ya hili? Tungependa kusikia mawazo yako.
Makala hizi za maelezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.