Dar es Salaam. Timu maalumu imependekezwa kwa ajili ya kuchunguza utata katika baadhi ya mali zilizotaifishwa katika utaratibu wa vikosi kazi na mashauri ya kukiri kosa ili kuishauri Serikali ipasavyo.
Hili ni kati ya mapendekezo ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai Tanzania iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Janauri 31, 2023, na kukabidhi ripoti yake kwa Mkuu huyo wa Nchi hapo Julai 15, 2023.
Pendekezo hilo limetokana na uwepo wa malalamiko miongoni mwa wananchi kwamba baadhi ya vikosi kazi vilivyokuwa vinaundwa na Serikali, hususan chini ya utawala uliopita, kufanyia kazi masuala kama vile ya kikodi, vilitumia vibaya mamlaka zao na kubinafsisha mali za watu ambao hawakuwa wanastahiki kufanyiwa hivyo.
Hali kama hiyo pia inatajwa kutokea kwa watu waliongia kwenye utaratibu wa kukiri makosa, au plea bargaining kwa kimombo, ambapo watu kadhaa wanadaiwa kutaifishiwa mali zao na Serikali katika mazingira yaliyojaa utata na kuacha maswali mengi.
SOMA ZAIDI: Tume Yataka Mkakati wa Kitaifa Kubaini, Kuzuia Uhalifu Tanzania
Makubaliano ya kukiri makosa ya jinai ni utaratibu wa kumaliza kesi za jinai mahakamani kwa njia ya makubaliano ambapo mshtakiwa anakubali kukiri kosa analoshtakiwa nalo au kosa dogo miongoni mwa makosa aliyoshtakiwa nayo au kwa makubaliano na mwendesha mashtaka kumshtaki kwa kosa dogo au kosa lenye adhabu ndogo.
Utaratibu wa makubalino ya kukiri kosa unafanyika katika nchi mbalimbali duniani, ikiwa ni pamoja na Marekani, Afrika Kusini, India, Ufilipino, Kenya na Zambia.
Nchini Tanzania, utaratibu wa makubaliano ya kukiri kosa unasimamiwa na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura 20; The Criminal Procedure (Plea Bargaining Agreement) Rules, G.N No. 180 of 2021; Notisi ya Ugatuzi wa Mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Mwaka 20224 na Mwongozo wa Mkurugenzi wa Mashtaka wa Makubaliano ya Kukiri Kosa wa Mwaka 2022.5
Utaratibu wa kukiri kosa unahusisha hatua kuu tatu ambazo ni kuwasilisha mahakamani taarifa ya kusudio la kuingia makubaliano ya kukiri kosa; marekebisho ya hati ya mashtaka; na kusainiwa na kuusajili mahakamani mkataba wa kukiri kosa.
SOMA ZAIDI: Wakuu wa Mikoa, Wilaya Wasiwe na Mamlaka ya Kukamata Watu, Tume Yashauri
Kesi nyingi za kukiri makosa zilijitokeza kipindi cha utawala wa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, zikiambatana na malalamiko kadhaa ya watu kuonewa kwa kulazimishwa kuingia kwenye makubaliano hayo na kesi hizo kufanyika hata kabla ya kanuni husikwa kutungwa. Kanuni hizo zilitolewa Februari 2021.
Tume imekiri kwenye muhtasari wa ripoti yake kwamba kutungwa kwa kanuni hizo, zinazojulikana kama Kanuni za Jaji Mkuu, kumesaidia kwa kiwango kikubwa kuepusha malalamiko yaliyokuwa yanatokana na utekelezaji wa utaratibu wa kukiri kosa.
Hatua nyingine iliyosaidia kupunguza malalamiko hayo ni kugatuliwa kwa mamlaka ya Mwendesha Mashitaka katika ngazi za mikoa na wilaya, uamuzi uliofanyika mwaka 2022.
Mbali na kutaka uchunguzi juu ya madai ya watu kutaifishiwa mali zao, tume pia imependekeza malalamiko ya washtakiwa kulazimishwa kuingia katika makubaliano ya kukiri kosa yashughulikiwe kwa njia ya Mahakama kwa mujibu wa sheria ili haki itendeke kwa pande zote.
SOMA ZAIDI: Tume Yataka Mamlaka Mpya Iundwe Kushughulikia Upelelezi, Uchunguzi Tanzania
Mapendekezo mengine ya tume kuboresha utaratibu wa kukiri makosa ya jinai nchini yanahusu utolewaji wa elimu zaidi kwa wananchi na wadau muhimu kuhusu utaratibu huo na umuhimu wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kutunza kumbukumbu za majadiliano ya makubaliano ya kukiri kosa.
Hii, hata hivyo, siyo mara ya kwanza kwa mapendekezo juu ya uchunguzi wa kina kufanyika juu ya malalamiko ya dhuluma yaliyohusu utekelezaji wa utaratibu wa kukiri makosa hapa nchini.
Mnamo Aprili 14, 2023, kwa mfano, Ngome ya Vijana ya chama cha upinzani ACT-Wazalendo, kwenye risala yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, iligusia pendekezo hili, ikitaka uchunguzi wa kina kufanyika juu ya madai ya washtakiwa kutishwa na kulazimishwa kukiri makosa ili kupewa uhuru wao na kile ilichokiita ukiukaji wa kanuni za mwenendo wa mashtaka ya jinai.