Dar es Salaam. Mvutano mkali unaendelea kati ya wananchi wapatao 5,000 wanaoishi katika eneo linalojulikana kama Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo, au kwa kifupi RAZABA, mkoa wa Pwani na Serikali ya mkoa huo ambayo imedhamiria kuwahamisha wananchi hao bila ya kuwalipa fidia.
Wananchi hao walitakiwa wawe wamehama kwenye makazi yao Septemba 1, 2023, lakini zoezi hilo halikufanyika baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Pwani, kuingilia kati, kikiwataka wananchi waendelee kukaa kwenye eneo hilo huku chenyewe kikitafuta “huruma” kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hassan Juma Omari, mmoja ya wananchi waliokuwa wanapaswa kuhama eneo hilo, aliiambia The Chanzo hapo Septemba 5, 2023, kwamba hatua hiyo ilikuja baada ya wananchi wenzake kwenda kulala kwa siku nne kwenye ofisi ya CCM ya mkoa, wakitaka chama hicho tawala nchini kiingilie kati kwenye mtafaruku huo.
“Alipokuja Mwenyikiti wa CCM mkoa, akafanya kikao na kamati yake ya siasa, akiwemo Mkuu wa Mkoa [wa Pwani Aboubakar Kunenge], baada ya kumaliza kikao wakawaambia wananchi warudi kwenye makazi yao, wakiwaambia hawatasumbuliwa na TFS mpaka pale viongozi wa CCM watakapokuja kutoa neno,” alisema Omari.
TFS ni kifupi cha Tanzania Forestry Service, au Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, taasisi ya Serikali ambayo, pamoja na mambo mengine, ina jukumu la kuhakikisha usimamizi wa rasilimali za misitu nchini. Kwa mujibu wa wananchi, ni TSF ambao waliwapa notisi ya siku saba kuhama kwenye maeneo hayo.
‘Siyo wavamizi sisi’
Wananchi hao, ambao wanadai kuishi katika eneo hilo lililopo katika kata ya Makurunge tangu kwenye miaka ya 1970, mpaka sasa wamegoma kuondoka kwenye makazi yao, wakisema hawawezi kufanya hivyo bila ya Serikali kuwapa eneo mbadala la kuishi au kuwalipa fidia stahiki.
Wakizungumza na The Chanzo iliyotembelea eneo hilo mnamo Agosti 30, 2023, ambayo iliwakuta wamekaa nyumbani kwa Omari, ambaye ni Mwenyekiti mstaafu wa Kitongoji cha RAZABA, wananchi hao walisema ni vigumu kwa wao kuacha makazi yao na mazao waliyolima bila kuoneshwa mahala pa kwenda.
SOMA ZAIDI: CCM Yadaiwa Kupora Ardhi ya Wanakijiji Kilimanjaro
“Sisi tunataka tutendewe haki, yaani tujue tunaenda wapi,” alisema mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Andrew Fahamu Mbode. “Tunahitaji Serikali itutendee haki. Muda tuliokaa hapa ni zaidi ya miaka 25. Tuna sababu gani ya kuitwa wavamizi kwenye eneo hili?”
Mwananchi mwingine wa eneo hilo, Anza Ramadhani, alionesha kukerwa na hatua ya Serikali kumtaja yeye na wenzake kama “wavamizi,” akisema ni jina baya kupewa kwa wananchi halali wa nchi wanaofanya kazi kwa bidii kulitumikia taifa lao.
“Hili jina la wavamizi, hivi mvamizi anakaa Tanzania?,” alihoji mwananchi huyo. “Mvamizi nahisi ni mtu wa kuja, labda mkimbizi hivi kutoka nje [ya nchi], siyo wa humu. Sasa sisi wazaliwa wa humu, na tunaishi humu, na ni Watanzania wa humu, huu uvamizi sisi hatujaujua.”
Lakini Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, aliiambia The Chanzo hapo Septemba 5, 2023, kwamba Serikali haina mpango wa kuwalipa wananchi hao fidia, akisema kwamba eneo wanalolikalia hivi sasa walilivamia, na hivyo wanapaswa kuondoka.
“Ukweli ni kwamba ni wavamizi, sheria inasemaje kuhusu mtu anapoingia eneo la mtu? Tunasema ile ni jinai,” alisema Kunenge kwenye mahojiano hayo kwa njia ya simu. “Sasa mtu anapotaka kukutoa katika eneo lake anaweza kuamua kukulipa chochote, anaweza kuamua kukulipa fidia, au asikulipe, ni utashi wake, halazimiki.”
Serikali ilipe
Lakini je, wananchi hawa ni wavamizi au siyo wavamizi, na je, wanastahili kulipwa fidia au la? Dk Ronald Ndesanjo ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye amekuwa akifanya utafiti kuhusiana na mvutano huu kati ya wananchi wa RAZABA na Serikali kwa kipindi kirefu sasa.
Kwenye mahojiano yake na The Chanzo ya hivi karibuni, Dk Ndesanjo alisema kwamba pamoja na kwamba Serikali inataka kutwaa eneo lake, wananchi walioishi katika eneo la RAZABA wanazo haki za msingi, ikiwemo kulipwa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Hapana shaka kuwa eneo husika lilikuwa ni ardhi ya jumla, chini ya Serikali, kwa nyakati tofauti,” mtafiti huyo alieleza kwenye majibu yake marefu ya kimaandishi kuhusiana na sakata hilo kwa The Chanzo. “Hata hivyo, eneo hili limekaliwa na wananchi kwa muda mrefu tangu miaka ya mwanzo ya 1980,” hali inayowafanya wastahili fidia endapo kama watahamishwa.
SOMA ZAIDI: Wakulima Wadogo 852 Mbarali Waiburuza Serikali Mahakamani Wakitetea Ardhi Yao
Dk Ndesanjo anasema kwamba utafiti wao haujaweza kubaini kama fidia hii ilishalipwa kwa wananchi, isipokuwa kwa wale baadhi tu waliopisha uwekezaji wa kiwanda cha Bagamoyo Sugar, kinachomilikiwa na Said Salim Bakhresa, moja kati ya wafanyabiashara wakubwa nchini Tanzania.
Eneo la ufugaji, malisho
Historia inaonesha kwamba kati ya mwaka 1977 na 1978, eneo la takribani hekta 28,096 katika kijiji cha Makurunge lilikabidhiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya shughuli za ufugaji au malisho ya ngo’mbe, eneo lililokuja kujulikana kama RAZABA.
Ilipofika mwanzoni mwa miaka ya 1980, wafanyakazi wa kiume wa RAZABA walimuomba Mkurugenzi kuzileta familia zao na kuishi nazo ndani ya sehemu ya eneo hilo, ambapo walipewa eneo la Bozi, lililoko kusini kwa RAZABA, ambapo walijihusisha pia na kilimo cha mazao ya muda mfupi kujikimu kimaisha.
Wananchi hawa wanadaiwa kuendelea na shughuli hii ya kilimo mpaka kufikia mwaka 1989 ambapo eneo la Bozi lilikuwa limeendelea na waliweza kuwa na kituo cha afya na shule. Mwishoni mwa miaka ya 1980, utendaji wa ranchi ulikuwa wa kusuasua na hatimaye ranchi ilifungwa mnamo mwaka 1994.
Kwa kuwa eneo la ranchi halikuwa limebinafsishwa kama ilivyokuwa kwa mashamba mingine ya Serikali kwa wakati huo, waliokuwa wafanyakazi wa ranchi walimuomba meneja wa ranchi waendelee kubakia katika eneo hilo, ambaye aliwaruhusu kwa mdomo kwa masharti kuwa wasilime mazao ya kudumu.
SOMA ZAIDI: Apigania Haki Yake ya Ardhi Kwa Miaka 36 Bila Mafanikio
Hata hivyo, kutokana na kutoendelezwa kwa eneo hilo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wananchi wa Bozi walianza kulima mazao ya kudumu. Mnamo mwaka 1995 eneo la RAZABA lilisajiliwa kama kitongoji cha kijiji cha Makurunge na kushiriki katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, mwaka 1995.
Tangu wakati huo, eneo hili linatajwa kuendelea kukua kutokana na ujaji wa wageni ambapo baadhi yao waliomba ardhi kupitia uongozi wa kitongoji, huku wengine wakijitwalia maeneo ambayo hayakuwa yakikaliwa au kutumiwa.
Ulipaji fidia
Mnamo mwaka 2013, kampuni kutoka Sweden, SEKAB, ambayo sasa inaitwa EcoEnergy, ilimilikishwa eneo hilo kwa ajili ya kilimo cha miwa kuzalisha sukari.
Kufuatia changamoto mbalimbali ndani ya EcoEnergy, kampuni hiyo haikuwa imefanya uwekezaji wa msingi katika eneo husika hata kufikia mwaka 2016 ambapo Serikali ya awamu ya tano ilifuta umiliki wa ardhi wa EcoEnergy.
Miongoni mwa shughuli za awali ambazo EcoEnergy walikuwa wamefanya ni tathimini ya mali za wananchi waliokuwa ndani ya eneo husika kwa ajili ya kulipwa fidia. Hata hivyo, mpaka EcoEnergy wanafutiwa umiliki inadaiwa kwamba hawakuwa wamelipa fidia hiyo kwa wananchi.
Mwaka huohuo wa 2016, takribani hekta 10,000 kutoka eneo la RAZABA lilikabidhiwa kwa kampuni ya Bakhresa ili kufanya uwezekezaji wa kilimo cha miwa kuzalisha sukari.
SOMA ZAIDI: Wadau wa Ardhi Waitaka Serikali Kuheshimu Maamuzi ya Mahakama
Ilipofika mwaka 2018 baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi ndani ya hekta 10,000 za Bakhresa walilipwa fidia na kampuni hiyo ili kuondoka kupisha uwekezaji. Hata hivyo, wananchi walioko nje ya eneo la Bakhresa wameendelea kusubiri kulipwa fidia na EcoEnergy kwa mujibu wa tathimi iliyofanywa.
Kwenye maelezo yake kwa The Chanzo, Dk Ndesanjao ameshauri namna bora kwa mamlaka za nchi kuutatua mvutano huu uliopo kati yao na wananchi, akisema kwamba hakuna utata mkubwa juu ya umiliki wa ardhi husika.
“Serikali itafute namna bora zaidi ya kuhakikisha kuwa haki za wananchi wa RAZABA zinalindwa, ikiwemo kulipwa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi,” alishauri mtafiti huyo. “Kuwafukuza watu bila fidia hakuleti suluhu bali kunahamishia tatizo kutoka sehemu moja kwenda nyingine ndani ya nchi hii hii.”
Hadija Said ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anayepatikana mkoani Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia hadijasaid826@gmail.com.