The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, Dunia Inaweza Kupata Suluhu ya Kudumu ya Mgogoro wa Israel na Palestine?

Je, pendekezo la kuwa na dola huru la Palestine linaweza kuepusha watu zaidi kuuwawa kutokana na mvutano huo wa kihistoria?

subscribe to our newsletter!

Mnamo Oktoba 7, 2023, majira ya asubuhi, wanajeshi wa Hamas, ambacho ni kikundi cha kisiasa na kijeshi kinachounda Serikali katika Ukanda wa Gaza, nchini Palestine, walianza mashambulizi ya anga kuelekea Israel, wakilenga zaidi miji ya Tel Aviv na Jerusalem ya taifa hilo lililoasisiwa mnamo Mei 14, 1948.

Shambulizi hilo, ambalo wadadisi wa mambo wameliita la kihistoria, na ambalo mataifa ya Magharibi yamelielezea kama tukio la kigaidi, lilikuwa la ghafla mno na kuchochea mgogoro mpya kati ya Israel na Palestine ambao mpaka sasa unahofiwa kusababisha vifo zaidi ya 2,000 kutoka pande zote mbili za vita hiyo.

Kiongozi wa Kijeshi wa Hamas, Muhammad Deif, alizungumza Jumamosi katika ujumbe wa sauti uliorekodiwa na kusambazwa kuwa mashambulizi dhidi ya Israel ni oparesheni ya “kuwafanya maadui kufahamu muda wao wa kuikalia Palestine bila kuwajibika” umefika mwisho.

Azimio la Balfour

Ujumbe huo wa Deif unakita moja kwa moja kwenye kiini cha mgogoro huo kati ya Palestine na Israel. Unaanzia na Azimio la Balfour, la Novemba 2, 1917, wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, pale Uingereza ilipotangaza kuunga mkono Wayahudi kuanzisha taifa lao ndani ya Palestine.

Historia inaonesha kuwa wimbi la kwanza la Wayahudi kuhamia Palestine lilikuwa mwaka 1878 mpaka 1882. Uhamiaji huo unaitwa Aliyah. Tafsiri yake ni Wayahudi kutoka uhamishoni, kurejea kwenye ardhi yao ya kihistoria na kijiografia.

SOMA ZAIDI: Kwa Kuzipatanisha Saudia na Iran, China Imelamba Dume Kwenye Siasa za Kimataifa

Mwaka 1920 ilianzishwa Mamlaka ya Palestine. Uingereza ikaikalia Palestine kama koloni lake, haikufanya Wayahudi na Wapalestina waelewane. Vilevile, wimbi kubwa zaidi la uhamaji wa Wayahudi, kutoka maeneo mbalimbali ya dunia, kuingia Palestine, kufuatia Azimio la Balfour la kuwaunga mkono kuanzisha taifa lao.

Halafu ikaja Vita ya Palestine ya kati 1947 na 1949, ambayo ililigawa eneo la Mamlaka ya Palestine katika vipande vitatu. Kipande cha kwanza ndiyo Israel, cha pili ni West Bank, iliyotwaliwa na Jordan, kisha Ukanda wa Gaza, iliyomilikiwa na Misri.

Mnamo Mei 14, 1948, Wayahudi walilitangaza eneo lao kuwa dola huru ya Israel, hivyo kukoma kwa mamlaka ya kikoloni ya Uingereza. Halafu, mwaka 1967, Israel iliwashitukiza Waarabu kwa mashambulizi ya ghafla, hivyo kuchukua maeneo yote ya Palestine, Peninsula ya Sinai, Misri na Golan, Syria.

Kwa mujibu wa hukumu ya mwaka 2004 ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), Ukanda wa Gaza na West Bank, inayojumuisha Jerusalem Mashariki, ni maeneo ndani ya miliki ya Palestine. 

Tangu mwaka 1967, Jordan na Misri zilipofurushwa Palestine, Gaza na West Bank ni maeneo yaliyotambulika kuwa yanashikiliwa kijeshi na Israel mpaka mwaka 2005, Israel ilipojiondoa Gaza, lakini imeendelea kubaki West Bank.

Kwa mantiki hiyo, Deif anaposema oparesheni yao ni ukumbusho kuwa muda wa adui kuikalia Palestine umefika mwisho, ni tafsiri kuwa Israel inapaswa kuondoka West Bank pamoja na Jerusalem Mashariki.

SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?

Deif alifafanua kuwa kitendo cha Israel kuikalia West Bank, na hivi karibuni polisi wa Israel kuvamia Msikiti wa Al Aqsa, Jerusalem, vilevile Israel kuwaweka kizuizini maelfu ya Wapalestine kwenye jela za Israel, ni nyongeza ya sababu za mashambulizi ya Jumamosi.

Hamas na Fatah

Ndani ya Palestine kuna vyama vikuu viwili, Hamas na Fatah. Kwa muda mrefu, Fatah, kilichoasisiwa na shujaa wa wakati wote wa Wapalestine, Yasser Arafat, kiliongoza Mamlaka ya Palestine, au PA, yaani West Bank na Gaza, chini ya Israel.

Uchaguzi wa Bunge wa mwaka 2006 uliingiza Palestine kwenye machafuko ya wenyewe kwa wenyewe. Hamas walishinda viti 74 vya ubunge, Fatah walipata viti 45. Vyama vingine viliambulia viti 13. Wagombea huru wanne pia walishinda.

Fatah waligomea matokeo hayo. Yakaibuka mapigano baina ya Hamas na Fatah. Hamas waliunda Serikali ambayo ilisusiwa na Fatah. Serikali ya Hamas ilikumbwa na kibano kikali kutoka Israel, ikiwemo vikwazo vya kiuchumi na mawaziri wake kukamatwa na kufungwa magereza za Israel.

Athari za uchaguzi huo ziliigawa Palestine mara mbili na ndivyo inavyoongozwa mpaka sasa. West Bank ipo chini ya Fatah kwa mwavuli wa Israel, na Ukanda wa Gaza ambao unatawaliwa na Hamas.

Fatah na Hamas ni vyama vyenye itikadi na mitazamo tofauti. Hamas wanataka kusimika dola ya Kiislam Palestine, wakati Fatah mtazamo wao ni kutofungamanisha dini na dola, yaani dola la kisekula.

SOMA ZAIDI: Mnyukano wa Mafahali Wawili Unavyowatesa Raia wa Sudan

Mkakati wa Hamas katika kupigania dola huru ya Palestine ni mapambano ya kijeshi. Fatah wanaamini inawezekana kufanikisha dola huru ya Palestine kwa njia ya mazungumzo.

Kimalengo, Hamas hawaitambui kabisa Israel, ila wanakubali mipaka ya mwaka 1967, inayotambua uwepo wa Israel. Fatah, kwa upande wao, wanatambua uwepo wa Israel, na malengo yao ni kuunda dola ya Palestine kulingana na mipaka ya mwaka 1967.

Tangu mwaka 2007, ambapo Hamas waliwafukuza Fatah Gaza, ukanda huo umekuwa ukipitia vikwazo vingi vya kiuchumi. Misri ndiyo imekuwa msaada mkuu wa Gaza kwa kipindi chote hicho.

Israel imedhibiti Gaza kuingiza bidhaa za kielektroniki, zikiwemo kompyuta. Hilo limefanyika kuhakisha Hamas hawatengenezi silaha. Kingine, Israel inadhibiti watu kuondoka na kuingia Gaza.

Tangu mwaka 2005, Israel ilipojiondoa Gaza rasmi, eneo hilo limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na ndege za kivita za Israel pamoja na Fatah, kutokea West Bank. Chuki na roho ya kisasi inaishi ndani ya Wapalestine, hasa wale wa Gaza.

SOMA ZAIDI: Maji Yalivyohatarisha Vita Kati ya Iran na Afghanistan

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel, amesema Waisrael wameingia kwenye vita kamili ya kujilinda, akiagiza kukatwa kwa umeme, chakula, mafuta na huduma nyingine za kijamii kwa watu wanaoishi Gaza, wanaokisiwa kuwa milioni mbili.

Ipi suluhu ya kudumu?

Kutokuundwa kwa taifa la Palestine kunasabisha nchi hiyo iwe tegemezi wa huduma nyingi za kijamii, ikiwemo nishati ambayo West Bank inapokea kutoka Jordan na Israel, wakati Gaza wanategemea Israel na Misri. Ndiyo sababu Netanyahu amekuwa na jeuri ya kuwakatia huduma.

Mkuu wa Sera za Kimataifa wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amesema tamko la Netanyahu linakiuka sheria za kimataifa na sheria za kibinadamu, akisema: “Israel wana haki ya kujilinda, ila kuwakatia umeme watu na kuwanyima chakula ni kinyume na sheria za kimataifa.”

Matamko ya China na Urusi kuhusu dola mbili, yaani taifa la Palestina na Israel kama ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro wa Mashariki ya Kati ndiyo wito wa muda mrefu. Hata Marekani walishakuwa na sera hiyo.

SOMA ZAIDI: Miaka 20 Tangu Marekani Ivamie Iraq kwa Udanganyifu. Je, Kuna la Kujifunza?

Mwaka 2019, nchi 138 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, ziliridhia Palestine kuwa dola huru na kuunga mkono ipewe kiti UN. Amerika Kusini, Afrika, Asia na visiwa vya Caribbean, wanaunga mkono Palestine kuwa dola rasmi.

Kikwazo kikubwa kwa Palestine ni nchi za Ulaya, Australia, Canada, Mexico na Marekani yenyewe. Kadiri taifa la Palestine linavyocheleweshwa, chuki inaongezeka. Uadui unakuwa mkubwa. 

Je, mapigano haya mapya yatachochea umuhimu wa kuwepo kwa dola huru la Palestine? Tusubiri tuone!

Luqman Maloto ni mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia thisluqman@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts