Wasoshalisti nchini Bolivia na wajamaa sehemu nyengine Amerika Kusini na Kati wamesherehekea ushindi unaotajwa kuwa wakihistoria baada ya uchaguzi wa Rais Jumapili iliopita, Octoba 18, 2020. Ni ushindi wa mgombea wao Luis Arce, sahibu wa chanda na pete wa Rais wa zamani wa Bolivia Eva Morales na wa Chama cha Kisoshalisti cha Movement for Socialism (MAS), au Vuguvugu kwa Ajili ya Ujamaa MAS.
Morales alikuwa Rais wa kwanza wa Bolivia kutoka jamii ya wakaazi asilia wa nchi hiyo aliyechaguliwa mwaka 2006. Morales aliyekuwa kiongozi wa chama cha wafanyakazi kabla ya kujibwaga kwenye siasa, alipata umaarufu mkubwa hasusani miongoni mwa wakaazi asilia (indigeneous people) kutoka maeneo ya vijini ya nchi hiyo ya Amerika ya Kusini.
Baada ya kuitumikia Bolivia kwa miaka 14 kama kiongozi wake mkuu, Morales aliyapa kisogo matokeo ya kura ya maoni ya 2016 yaliounga mkono hoja ya kuwepo kwa ukomo wa mihula ya uraisi nchini humo. Mwaka jana, 2019, Morales akagombea kipindi cha nne. Tume ya Uchaguzi ilipomtangaza tena kuwa mshindi dhidi ya mpinzani wake Morales akapata upinzani mkubwa kutoka kwa wahafidhina na shinikizo kutoka nchi ya Marekani pamoja na viongozi wa kihafidhina kutoka Jumuiya ya Mataifa ya Amerika, OAS.
Evo Morales aliendelea kusakamwa pia na vyombo vya ulinzi vya Bolivia, ikiwemo polisi. Baadhi ya vigogo jeshini nao walijiunga na wimbi hilo. Akiwa amebanwa kila kona, Morales akalazimika kujiuzulu na kwenda uhamishoni kwanza nchini Mexico na baadae Argentina.
Wahafidhina waunda Serikali
Spika wa Bunge Jeanine Anez akakimbilia kuchukua madaraka kwa mujibu wa Katiba. Bibi huyu mhafidhina aliyeiongoza serikali ya mpito, aliingia kwa mbwembwe na kutangaza hatua kadhaa za kuachana na sera za kijamaa zilizoasisiwa na Morales na chama chake cha MAS.
Katika uchaguzi huo ulioitishwa Jumapili, Oktoba 18, Anez alijitangaza mgombea lakini baada ya kuona dalili za kushindwa alijiengua akisema ni hatua ya kuzuia kuzigawa kura za wahafidhina na hivyo kumuachia uwanja mhafidhina mwenye msimamo wa wastani Carlos Mesa.
Mesa alikuwa na nafasi zaidi kuliko Anez. Ilitumainiwa kuwa pindi uchaguzi ukiingia duru ya pili watakuwa na nafasi ya kumshinda Luis Arce, mrithi wa Morales kutoka chama cha MAS. Hata hivyo, mambo hayakuwa kama walivyotarajia kwani matokeo yalimpa Arce ushindi wa moja kwa moja.
Ushindi wa Arce unaweza kuwa na maana nyingi. Moja inaonekana kwamba raia wengi wa Bolivia, wakiwemo wajamaa, huenda walimkataa Morales asijiongezee muhula mwengine lakini hawakuzikataa sera za chama chake cha kisoshalisti.
Hilo wamelidhihirisha bayana katika uchaguzi wa Oktoba 18 kwa kumpa ushindi mnono mgombea wao Arce ambaye wapinzani wake wamedai aliteuliwa na swahiba yake Morales.
Fundisho kwa nchi za kijamaa
Wabolivia wamezingatia matunda waliyovuna tangu Morales alipoingia madarakani. Hawakusahau madhila ya miongo mingi chini ya tawala za kijeshi, kidikteta na kihafidhina ambazo zilikandamiza haki za binadamu na kutojali maisha ya walio wengi katika taifa hilo masikini.
Bolivia imetoa fundisho la kuwa sera za kijamaa zinatekelezeka, ikiwa viongozi watakuwa waadilifu na kipimo ni mafanikio yaliyopatikana. Ndio maana mgombea wa Chama cha Kisoshalisti Arce akachaguliwa na kukirejesha chama hicho madarakani.
Na amini kwamba hili pia litakuwa funzo kwa watawala na vyama vyengine vya mrengo wa kushoto katika Amerika Kusini na Kati ambavyo vishindwa kujenga mustakbali mwema na raia wa nchi hizo na kutumbukia katika dimbwi la ubadhirifu wa mali za umma na kujitajirisha, kinyume na walichokuwa wakikipigania kabla ya kuingia madarakani.
Mfano mmoja ni nchi ya Nicaragu, nchi ya Amerika ya Kati, na kiongozi wake Daniel Ortega, aliyegeuka mtawala wa kimabavu na aliyelewa madaraka. Viroja vya Ortega ni pamoja na kumteuwa mkewe kuwa makamu wake wa Rais. Miongoni mwa waliompinga alikuwa mtu niliyemhusudu binafsi Comrade Ernesto Cardenal aliyewahi kuwa waziri wa utamaduni, mwanazuoni wa kikatoliki aliyehasimiana wakati mmoja na Kanisa alipolishitumu lilikuwa likiyafumbia macho maovu ya watawala wa kidikteta katika Amerika Kusini. Cardenal aliyendelea kumkosoa Ortega kwa kwenda kinyume na malengo ya mapinduzi alifariki mwaka jana, 2019.
Ushindi wa Arce utakuwa umepokelewa kwa furaha na serikali za mrengo wa kushoto katika kanda hiyo, kama Mexico, Argentina, Venezuela na Cuba ambazo zilikiunga mkono chama cha MAS. Wote watakuwa wanayaangalia matokeo kuwa ni kurejea kwa Ujamaa katika eneo hilo.
Ushindi huu ni pigo kubwa kwa wahafidhina nchini Bolivia, lakini pia ni pigo kwa utawala wa Raisi wa Marekani Donald Trump na washirika wake katika kanda ya Amerika kama Brazil na Chile walioshadidia na kushinikiza Morales aondoke madarakani. Trump na Rais wa Brazil Jair Bolsonaro, mfuasi wa siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia aliyepewa jina la Trump wa Amerika Latino, walishangiria alipojiuzulu Evo Morales mwaka 2019.
Mohamed Abdulrahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Alishawahi kuwa Naibu Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, DW, katika idhaa yake ya Kiswahili. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mamohamed55@hotmail.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.