Jinsi Sakata la Viti Maalumu Linavyoiweka Chadema Katika Njia Panda

Na Mwandishi Wetu9 November 202025 min

Jumapili ya Novemba 8, 2020, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitoa taarifa kuwa vyama vyenye sifa ya kupata ubunge wa viti maalumu ni chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) na chama kikuu cha upinzani nchini Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Hii inatokana na ukweli kwamba ni vyama hivyo tu pekee nchini Tanzania ndivyo ambavyo viliweza kupata asilimia tano ya kura zote za ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Octoba 28, 2020. Jumla ya vyama vya siasa ishirini vinatajwa kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya NEC imeibua mjadala mkubwa sana miongoni mwa watu wanaofuatilia siasa za Tanzania pamoja na wafuasi na wapenzi wa vyama vya upinzani na hata chama tawala. Mjadala huu kwa kiasi kikubwa umetawala kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii mpaka sasa. Na hoja kubwa inayokinzaniwa ni kwamba je, ni sawa kwa Chadema kupeleka majina NEC kwa ajili ya uteuzi wa wabunge wa viti maalumu kwenda kwenye Bunge la 12 linalotarajiwa kuanza hivi karibuni au kufanya hivyo si sawa.

Wale wanaotaka Chadema ipeleke majina NEC kwa ajili ya uteuzi wanajenga hoja kwamba hilo ni jambo ambalo Chadema ni lazima walifanye, kwani ni takwa la Kikatiba, na wala siyo utashi binafsi wa chama fulani kwamba kinaweza kuamua kupeleka au kutopeleka wabunge wa viti maalumu Bungeni. Wengine wanadhani kwamba itakuwa ni jambo jema kwa Chadema kuwapeleka wawakilishi hawa, wakidai kwamba kuwa na wabunge ambao hawana shinikizo la kufanya kazi majimboni inaweza kuongeza ufanisi katika kuisimamia na kuiwajibisha Serikali Bungeni.

Hofu ya misimamo kinzani

Lakini wengine wanadhani kama Chadema itapeleka majina NEC kwa ajili ya uteuzi wa wabunge wa viti maalumu uamuzi huo utakinzana na msimamo wa chama hicho chenye kufuata itikadi ya mrengo wa kati-kulia (centre-right) wa kutokutambua matokea ya Uchaguzi Mkuu wa Octoba 28, 2020, hoja ambayo hata Raisi wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Fatma Karume ameiibua. Chadema, pamoja na vyama vingine vya ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), inadai kwamba uchaguzi huo ulighubikwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi pamoja na matukio mengi ya uvunjifu wa haki za binadamu.

Baadhi ya kasoro ambazo vyama hivyo vimezitaja ni pamoja na uwepo wa kura feki, kuzuiwa kwa mawakala wa vyama vyao kwenye vyumba vya kupigia kura, pamoja na ukamataji wa wadau mbalimbali wa uchaguzi toka vyama hivyo. NEC imekanusha madai yote haya, na kutaka wananchi wapuuze taarifa hizo. Vyama viwili, Chadema na ACT-Wazalendo, vilitangaza maandamano yasiyokua na kikomo kuanzia Novemba 2, 2020, kushinikiza Serikali iitishe Uchaguzi Mkuu mpya utakaosimamiwa na tume huru za uchaguzi kwa Tanzania na Zanzibar. Lakini maandamano hayo hayakufanikiwa na viongozi na wananchama wengi wanakabiliwa na kesi mbalimbali zilizotakana na ushiriki wao katika maandalizi ya maandamano hayo.

Kwa mujibu wa wadadisi wa mambo, endapo kama Chadema itapeleka wabunge wake wa viti maalumu kwenye Bunge la 12, wawakilishi hao hawatakuwa na msaada wowote kwenye kuisimamia na kuiwajibisha Serikali kwenye Bunge lililojaa wajumbe wa CCM ambao wanakisiwa kuwa ni asilimia 99 ya wajumbe wote. Kuna hofu kwamba wabunge hao wa upinzani watatumiwa tu na Serikali kuhalalisha maamuzi yatakayoamuliwa na wabunge wa CCM.

Maswali magumu kwa Chadema

Maswali yanayoikabili Chadema kwa sasa ni pamoja na je, wao kupeleka majina ya viti maalumu sio kukubali rasmi kwamba uchaguzi ulikuwa sawa na haukuwa na dosari zozote? Kama wasipopeleka majina nini itakuwa hatma ya Chadema kwa miaka mitano ijayo? Mpaka sasa inaonekana jitihada za Chadema na ACT-Wazalendo kutaka uungwaji mkono na wananchi kupitia maandamano bado hazijafanikiwa. Pia, pamoja na matamko kadhaa kutoka kwa balozi mbalimbali nchini na mashirika mengine ya haki za binadamu bado inaonekana hakuna msukumo wa ziada kutoka kwenye Jumuiya ya Kimataifa juu ya malalamiko ya dosari za uchaguzi zilizotolewa na vyama hivyo.

Idadi ya viti maalumu inayotegemewa ni viti 113. Hii ni sawa na asilimi 40 ya viti vyote vilivyopo ndani ya Bunge: viti vya majimbo 264; viti vya kuteuliwa na Raisi 10; wajumbe watano kutoka Baraza la Wawakilishi la Zanzibar; Spika wa Bunge; na Mwanasheria Mkuu. Kwa upande wa CCM, Katibu Mkuu ameshaainisha  kuwa wamepata viti 94,  hii ikimaanisha CHADEMA watapata viti 19 vilivyobakia.

Kwa mujibu wa cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343, kifungu cha 86 A, NEC ina jukumu la kutoa idadi kamili ya wabunge wa viti maalumu watakaotoka kwenye vyama husika. Vyama vitahusika kutoa majina kwa NEC katika mpangilio maalumu, yaani kuamua atakayekua wa kwanza kupewa kipaumbele mpaka wa mwisho. Baada ya hapo NEC, kwa kutumia mpangilio uliwasilishwa na vyama vya siasa, itatangaza wabunge wapi wameteuliwa na kutuma majina kwa Spika wa Bunge.

Minong’ono ndani ya chama

Tayari kumeshakuwa na minong’ono kutoka Chadema juu ya utangazwaji wa majina ya viti maalumu utakofanywa na NEC. Kufuatia taarifa zilizosambaa mitandaoni kwamba Chadema kimepeleka majina NEC kwa ajili ya kuteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum, Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika alikanusha taarifa hizo katika ukurasa wake wa Twitter, akisema: “Kamati Kuu ya Chadema haijafanya uteuzi wa wabunge wa viti maalum mpaka sasa, hivyo hakuna orodha iliyopelekwa na Katibu Mkuu kwa NEC, tumedokezwa wanataka kughushi saini na orodha, Tume  ifanye uteuzi haram na Bunge libariki.”

Hii inafanya maswali yazidi kuongezeka. Ikiwa Chadema kitaamua kuendelea na kuteua majina ya viti maalumu, je, majina wanayopendekeza ndiyo majina yatakayotangazwa ilhali chama hicho kimeonyesha kutokuwa na imani na NEC? Kwa upande wa NEC bado hawajatolea ufafanuzi zaidi mchakato utakavyokuwa.

Uwakilishi katika Bunge ni moja ya rasilimali kubwa katika ujenzi wa chama, hivyo hivyo imani katika misimamo ya chama ni rasilimali kubwa zaidi. Swali ni je, Chadema wataangalia mazingira na uhalisia wake au kusimamia misimamo ya harakati?

Na Mwandishi Wetu

2 comments

 • Rick

  9 November 2020 at 3:37 PM

  Wasidanganyike kwenda asilani,itakuwa wameukubali uchafuzi haramu🙄

  Reply

 • Abu Kauthar

  13 November 2020 at 2:13 PM

  CCM nayo imepoteza katika uchaguzi huu, mshindi JPM tu

  Uchaguzi wa 2020 Tanzania umepita. Inasemekana Watanzania wameamua kukirejesha chama tawala, CCM kwa kishindo. Kishindo kilikuwa ni kikubwa mno. Kishindi cha bomu lililoteketeza sio tu vyama vya upinzani, bali hata mmea uliobeba ua zuri liitwalo demokrasia ambalo ndio hubeba tunda tunalolijua kama ‘vyama vingi’.

  Huenda kishindo cha bomu hili la ushindi litaitekeleza hadi CCM yenyewe wakabakia wasanifu wa bomu lenyewe. Ni suala la muda tu tutajua.

  Kuna wanaoshangilia. Hawa ni wanachama, wafuasi na wapenzi wa CCM. Wapo wanaouguza majeraha ya maumivu ya kushindwa, ya moyoni na baadhi hata katika miili yao. Hawa ni wafuasi wa vyama vya upinzani ambao vyama vyao vimepata kipigo cha mbwa mwitu.

  Lakini lipo kundi la tatu la wale ambao wameweza kujitoa kifikra katika boksi dogo la ‘chama’ anachokishabikia iwe ni CCM au upinzani na kuzingatia zaidi maslahi ya taifa. Hawa wanasikisikishwa na wanaumia kutokana na yaliyotokea. Mi ni mmoja kati yao.

  Mimi ni muumini wa demokrasia. Naamini demokrasia sio siasa au nadharia timilifu lakini ni njia pekee yenye nafasi kubwa ya kufanikiwa katika jamii yenye watu mchanganyiko kama ya Tanzania kuweza kujenga na kuhakikisha ustawi wa nchi kiutulivu, mshikamano, maendeleo ya vitu na watu nk.

  Lakini demokrasia niliyoiamini imekejeliwa; imetusiwa, imebakwa katika namna ambayo sikuwahi kudhani ingeweza kutokea Tanzania. Si kupitiliza mipaka viongozi wa vyama vya upinzani walipougeuza jina uchaguzi huu na kuuita ‘uchafuzi’. Ulikuwa ni uchafuzi dhahiri kwa kigezo chochote kile.

  Nikiwa muumini wa demokrasia nikiangalia mtiririko wa matukio kuanzia 2015 pale awamu ya tano, naona wazi wazi kuwa huenda yajayo katika mustakbali wa nchi yetu yasiwe ya kufurahisha.

  Tunachokiona ni kuwa, nchi inazidi kuponyoka kutoka mikononi mwa wananchi na kuingia katika udhibiti wa wachache ambao huamua hatima ya kila mtu kutokana na wanavyojisikia moyoni.

  Ni ujinga kudhani kuwa Chama Tawala kinapata nguvu zaidi kwa hujuma iliyofanyika dhidi ya demokrasia na dhidi ya upinzani. Si kweli. Anayezidi kupata nguvu na kujilimbikizia mamlaka, madaraka ya kuamua chochote ni mtu mmoja tu: John Pombe Magufuli, aliyetangwa na tume ya uchaguzi kuwa mshindi wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  Spika wa Bunge katika hafla ya kuzinduliwa bunge amesema wao, wabunge wa CCM, wamedhaminiwa na rais kuja kwao bungeni. Na ni wazi kuwa, kwa kuwa wao ni wengi, basi kimsingi bunge la sasa linadaiwa fadhila na Rais Magufuli. Tunaona kila uchao viongozi wa mahakama nao wakitoa kauli zinazoashiria kudhalilika kwa mhimili huo mbele ya Magufuli.

  Kiujumla, ni Rais John Pombe Magufuli pekee anayeweza kuamua kwa kadri anavyojisikia moyoni, sio tu aina gani ya maendeleo yaletwe, yaende wapi, nani akose, kwa kiasi gani, na nani apate. Na hii inatishia ustawi wa nchi yetu kwa sababu yeye sio malaika; na hata katika ubinadamu wake twaona mapungufu mengi

  Mungu ibariki Tanzania

  Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved