Bunge la 12 limeanza rasmi wiki hii, kwa wabunge kumpata kiongozi wao ambapo Job Yustino Ndugai, Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Dodoma kupitia tiketi ya chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM), akichaguliwa tena kwa mara ya pili kuwa Spika wa Bunge kwa kura 344 kati ya 345 zilizopigwa. Kura moja pekee ndiyo imemkataa kitu ambacho kilimfanya Ndugai aibuke mshindi kwa asilimia 99.7.
Spika Ndugai ana uzoefu mkubwa wa uendeshaji wa shughuli za Bunge. Kwanza, amekua Mbunge kwa miaka 20 sasa na katika kipindi hicho amekua kiongozi bungeni akianzia na Uenyekiti wa Kamati ya Bunge 2005-2010, Naibu Spika 2010-2015 na kisha Spika wa Bunge 2015-2020, nafasi ambayo anatarajiwa kuitumikia tena mpaka mwaka 2025.
Tofauti ya mabunge yote aliyokuwemo Spika Ndugai kwa miaka 20 na hili la sasa ni kubwa. Hili ni Bunge ambalo baadhi wanaliita la ‘kijani’ – yani limesheheni zaidi wabunge wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa jumla, kati ya wabunge wa majimbo 264, ni wabunge 8 tu ndiyo hawatoki CCM, hata hivyo wabunge wanne wa chama cha ACT-Wazalendo, wanaotoka Zanzibar, bado hawajaripoti bungeni ikiwa ni kutii agizo ya chama chao kilichowataka kutoenda bungeni.
Hii ina maana kuwa asilimia 98 ya wabunge wa kuchaguliwa na wananchi wanatoka katika chama tawala. Kwa upande wa wabunge wa Viti Maalum, ambao ni 113, vyama vyenye sifa ya kupata nafasi hizo kutokana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni CCM na Chama cha Deomkrasia na Maendeleo (Chadema). Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) tayari imefanya uteuzi wa wabunge 94 wa viti maalum kupitia CCM, na wote wamesharipoti bungeni na kuapishwa.
Lakini NEC imeshindwa kufanya uteuzi wa wabunge 19 wa Viti Maalum kupitia Chadema kwasababu chama hicho kimesusia kupeleka orodha ya wabunge wake, kwa hoja kwamba hakitambui matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kutokana na kuwepo kwa dosari nyingi zilizoathiri matokeo, hivyo hakipo tayari kunufaika na faida yoyote itokanayo na uchaguzi huo. (Unaweza kusoma uchambuzi wetu hapa wa jinsi suala hilo linavyoiweka Chadema katika njia panda).
Bunge bila Kambi Rasmi ya Upinzani
Hii ndiyo sura ya Bunge la 12. Bunge ambalo halitakua na Kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni kama ilivyozoeleka miaka mingine kwa sababu hakuna wabunge wa upinzani wanaotosheleza kuunda kambi hiyo. Hivyo Bunge hili pia halitakua na Baraza Kivuli la Mawaziri kwani wabunge wa upinzani hawafiki hata nusu ya idadi ya wizara za Serikali.
Jambo hili ni jipya kwenye siasa za nchi hii tangu ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1995. Katika mahojiano yangu na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, na mwandishi wa kitabu cha Why is Tanzania poor?, au Kwa Nini Tanzania ni Masikini, Dk Marcosy Albanie anasema hana matumaini kama Bunge la 12 litafanya kazi ya kuwakilisha kwa usahihi wananchi wa Tanzania.
“Mikutano ya Bunge hili itakua tu ikitekeleza matakwa na mipango ya CCM, sidhani kama kuna hoja yoyote ya msingi ambayo tunaweza kuitarajia sisi tuliokua tunapigania haki za binadamu, kujenga demokrasia na kuimarisha mifumo ya kikatiba ili wananchi wapate maendeleo,” amesema Dk Albanie.
Nilipomuliza, mbona wapo wabunge wengine wa CCM waliokua wakiikosoa na kuibana serikali katika mabunge yaliyopita, kwanini haoni kama wanaweza kuendelea na kazi hiyo? Dk Albanie alisema: “Wabunge wa upinzani ndiyo waliokua wanawasaidia wabunge wa CCM kuamka na kujikuta wakitekeleza wajibu kama wabunge waliochaguliwa na wananchi na ilifika mahala hata wabunge wa CCM wakataka Katiba Mpya kama walivyokua wakitaka wapinzani, kwa sasa jambo hili haliwezi kutokea.”
Hofu ya Bunge la chama kimoja
Katika hotuba yake baada ya kuapishwa kuwa Spika wa Bunge la 12, Job Ndugai alionekana kufahamu hofu ya watu kuhusu Bunge la 2020-2025. Na alianza kwa kusema: “Bunge letu linapaswa kuwa la matokeo chanya kwa maendeleo ya Watanzania, mipango ya nchi itapita hapa, bajeti itapita hapa na sheria zitapita hapa. Chombo hiki ndiyo mshauri mkuu wa Serikali kwa mambo yote, Serikali itakuja hapa kujibu maswali ambayo wabunge mtauliza kwa niaba ya wananchi. Ni kweli kabisa kwamba wabunge wengi wa Bunge la 12 wanatoka Chama Cha Mapinduzi [CCM] lakini hiyo haimaanishi kwamba litakua Bunge la ndiyo, ndiyo, ndiyo…wala haimaanishi litakua la hapana, hapana, hapana. Ni Bunge ambalo naamini litatimiza wajibu wake.”
Ndugai aliwataka wabunge wa CCM wawe huru kuwasilisha hoja zote za msingi kwa manufaa ya wananchi badala ya kusifia tu au kukaa kimya. Hata hivyo Prof Abdallah Safari, wakili wa Mahakama Kuu mwenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania akiwa amewahi kushika nafasi za juu katika Chama cha Wananchi (CUF) na Chadema katika nyakati tofauti kabla ya kuachana na shughuli za kisiasa, anasema kauli ya Spika Ndugai haiwezi kusaidia lolote.
“Huna haja ya kuuliza swali hapo. Hilo ni Bunge la chama kimoja, jicho haliwezi kujiona. Hayo ni maneno tu ya kutaka kujifariji. Hakuna kitu chochote chanya ambacho wananchi wanaweza kutarajia kutoka katika bunge hili. Hakuna kitu. Ni mufilisi,” alisema mwandishi huyo wa riwaya mashuhuri ya Joka la Mdimu katika mahojiano nami niliyofanya naye kwa njia ya simu.
Wabunge wa CCM kuwa huru?
Mjadala kuhusu matarajio katika Bunge la 12, ni mpana na mkali. Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania Pius Msekwa, ambaye aliwahi kuongoza Bunge katika kipindi cha chama kimoja 1990-1995, na kisha baadaye akaliongoza bunge la vyama vingi kutoka 1995 mpaka 2005, haamini kwamba bunge la sasa litashindwa kukata kiu ya wananchi na kuisimamia serikali.
“Wenye mawazo kwamba hili litakua bunge la kusema ndiyo kwenye kila kitu hawajafanya uchambuzi wa kutosha. Kwanza, wanapokuwepo wabunge wengi wa upinzani basi wabunge wa CCM huwa wanaogopa kuungana nao ili wasije wakawasaidia wapinzani kushinda hoja wakati wa kupiga kura lakini sasa hivi kwa kuwa ni wao peke yao basi mjue kuwa watakua huru zaidi kutoa ya moyoni,” amesema Mzee Msekwa.
Msekwa anafafanua zaidi kwa kusema kwamba wakati wa Bunge la chama kimoja tu Serikali ilikua inapata shida kupitisha hoja mbalimbali kutokana na upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa chama tawala na kusema ana uhakika hali hiyo itarudi. Kuhusu hofu kwamba wabunge watakaokua wakiikisoa sana Serikali wanaweza wasipitishwe tena na chama chao katika Uchaguzi Mkuu ujao, Mzee Msekwa amesema hofu hiyo haina mashiko.
Anasema: “Ni hofu isiyokuwa na msingi. Zipo kanuni za wabunge wa CCM ambazo mimi nilisaidia kuzitunga, zinaeleza wabunge hao wanatakiwa wafanye nini ndani ya bunge na zinawapa uhuru wa kusema yaliyo moyoni kwa uhuru kabisa. Mawaziri nao wanategemea kuchaguliwa uchaguzi ujao kwahiyo hawawezi kupeleka mambo ya hovyo ndani ya Bunge kwasababu itawagharimu kwa wananchi.”
Dk Azaveli Lwaitama ambaye ni Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini anapingana na hoja za Msekwa akisema: “Bunge la chama kimoja wakati wa uhai wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni tofauti na hili la sasa. Mimi sitarajii Bunge lililotokana na uchaguzi wa ajabu kama wa mwaka huu linaweza likafanya hayo anayosema Ndugai na Msekwa.
“Wabunge wengi wamepita bila kupingwa. Hata huyo Spika Ndugai amepita bila kupingwa, wataikosoaje Serikali? Huwezi kuniambia hili ni bunge lililotokana na wananchi na litasimimia hoja za wananchi ipasavyo. Hata kama kuna wabunge wa CCM watakua wakikosoa Serikali basi watakua wakipangwa tu wakosoe na ionekane kama serikali ilipata wakati mgumu bungeni kisha baadaye ikajieleza na kukubaliwa na wabunge,” Dk Lwaitama alisema kwa msisitizo.
Utashi binafsi wa Wabunge wenyewe
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye ana uzoefu wa kuwepo bungeni wakati wa chama kimoja na kisha baadaye kuwa kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni wakati wa vyama vingi wakati wabunge wa upinzani wakiingia kwa wingi bunge kwa mara ya kwanza, amesema matarajio ya watu kwa bunge hili yatategemea na utashi binafsi wa wabunge wenyewe.
“Kama wabunge watafanya kazi yao kama wabunge basi hawana sababu ya kushindwa kuisimamia na kuishauri serikali. Kama wabunge watakua hawana utashi wa kutekeleza wajibu wao, hata kama kungekua na wabunge wengi wa upinzani, bado lingekua bunge lisilotekeleza wajibu wake. Itategemea sana na wabunge hao wanayaelewaje majukumu yao,” amefafanua Sumaye.
Sumaye ambaye aliwahi kuwepo kwenye baraza la mawaziri chini ya Rais wa awamu ya pili, Alli Hassan Mwinyi kabla ya kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya awamu ya tatu chini ya Hayati Benjamin Mkapa aliongeza: “Nakumbuka wakati tulipokua bungeni sisi tulipewa semina nyingi sana kuhusu wajibu wa mbunge kwa wananchi wake na kwa chama chake. Mbunge akishaelewa mambo haya atatekeleza majukumu yake na kukidhi matarajio ya wananchi bila kujali chama chake.”
Charles William ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni charleswilly93@gmail.com au Twitter kupitia @2charlesWilliam.
2 responses
It is a beautiful, unforgettable and very interesting analysis worthy of the award
Interesting writeup…very detailed and very robust
Not one sided, different views explained. Its upon a reader to assess.