The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Maajabu ya Maalim Seif Akiwa Hai Yanaendelea Mpaka Akiwa Kaburini? 

Kwamba ACT-Wazalendo wameamua kufuata ushauri wa hayati Maalim Seif Sharif Hamad wa nani awe mrithi wake kwa nafasi ya Makamo wa Kwanza wa Rais inaonesha ni kwa kiasi gani kiongozi huyo alikuwa na ushawishi usiokifani kuweza kuamua mambo kutokea kaburini.

subscribe to our newsletter!

“Kila tukikuunga mkono, tunaona wewe mwenzetu Uislamu umekujaa. Kwa hiyo mwenzetu, ikiwa Uislamu umekujaa, nafasi achia wenzio. Ukae nyuma, uwe mshauri kama ulivyo mshauri. Nafasi ya kugombea urais kwa chama cha ACT-Wazalendo ukae nyuma, wapo kina … siwataji. Kwa sababu wewe kila tukija juu, [unatuambia] ‘tulieni, tulieni, tulieni.’ Hatutaki tena. Hatuna muda wa kufanya kazi wala wa kulea watoto wetu kwa weye. Si mwingine, kwa weye. Ikiwa nafasi imekushinda, [mwaka] 2020 ukae benchi, uwe mshauri.”

Haya ni maneno ya Fatma Omar, mwanachama wa ACT-Wazalendo huko Chokocho, Mkoa wa Kusini, Pemba.  Fatma alikua akimpa ‘makavu’ Maalim Seif Sharif Hamad, kwenye kikao hicho kati ya viongozi wa chama na wanachama ikiwa ni moja kati ya mikutano ya ujenzi wa chama hicho. Hapa ilikuwa ni siku chache baada ya Maalim Seif na wenzake kuhamia ACT-Wazalendo kutokea CUF wakifuatwa na maelfu ya wafuasi wao. Fatma alikuwa anawasilisha maoni ya walio wengi kisiwani Pemba waliokuwa wakiamini kwamba Maalim Seif, licha ya kuwa dhamira yake ya kuwakomboa kisiasa watu wake ilikuwa wazi, alichangia kwa namna fulani watu hao kutokupata haki zao.

“Vurugu haina macho, au siyo?” Maalim Seif alimjibu Fatma baada ya mwanachama huyo kumaliza kuongea. Kwenye jibu lake, Maalim Seif alionesha kwamba analaumiwa kwa kutokuchochea au kuhamasisha matumizi ya vurugu katika harakati zake za kudai haki, akionya kwamba vurugu si nzuri kwani haichagu nani wakamzuru. “[Ikianza] hujui nani ataumia,” Maalim Seif aliendelea na jibu lake kwa upole na umahiri wa mwanasiasa aliyena uzoefu wa kuongea na wananchi. “Tena na mimi nakiri [kwamba] mimi ni Muislamu sana. Na sioni aibu kusema mimi ni Muislamu. Tena ni Muislamu sana.”

Maajabu ya Maalim Seif 

Hili ni moja tu kati ya maajabu mengi aliyokuwa nayo muasisi huyo wa vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa nchini Tanzania aliyefarika Februari 17, 2021, akiwa na umri wa miaka 77. Huyu ni mwanasiasa ambaye amegombea nafasi ya uraisi wa visiwa vya Zanzibar kwa vipindi sita mfululizo bila kutangazwa mshindi lakini akaendelea kuamini kwamba ipo siku atatangazwa mshindi na kuiongoza nchi hiyo.  Ni mwanasiasa ambaye ripoti zinaonesha kwamba alikuwa akigawa kiasi fulani cha fedha kutoka kwenye mshahara wake kila mwezi kwa wajane na watoto wa marafiki zake waliotangulia mbele ya haki. Alikuwa na nyumba moja tu tena aliyojengewa na wafuasi wake huko Jadida, Wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba, licha ya kukaa kwenye nafasi za juu za kisiasa karibu miaka 40. Maalim Seif alifungwa na kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu lakini aliporejea uraiani akaendelea kutaka maridhiano na mahasimu wake wa kisiasa.

“Wakati anatukanwa sana kwenye majukwaa ya kisiasa, nilimuuliza babu vipi? Una moyo gani?” mjumbe mmoja wa Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo alinijibu baada ya kumuuliza atamkumba Maalim Seif kwa lipi akieleza kushangazwa kwake na uvumilivu aliokuwa nao Makamo huyo wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyezikwa Februari 18, 2021, kijijini kwake Mtambwe, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba. “[Maalim Seif] akajibu: nina moyo, naumia. Lakini nikija kufa watanisema kwa mema tu, hawatasema baya langu japokuwa wakati wa uhai walinikejeli.”

Nilimuuliza Katibu wa Idara ya Bunge, Wawakilishi na Serikali za Mitaa wa ACT-Wazalendo Hamad Yusuf ni nini kilikua kikimfanya Maalim Seif awe mwepesi wa kuhimiza maridhiano kila mara na hiki ndicho alichosema: “Kwangu mimi Maalim Seif kiuongozi ni kama bahari. Unaweza kumuona dakika moja amekasirika na dakika ya pili inayofuata tayari amesamehe.”

Ismail Jussa Ladhu, mwanasiasa mashuhuri Zanzibar ambaye pia ni mmoja katika ya vijana waliolelewa na Maalim Seif kisiasa nilisikia jambo lingine, alikuwa na haya ya kusema kuhusiana na Maalim Seif: “Pamoja na uzee wake lakini [Maalim Seif] alikua akinitembelea hospitali kila siku asubuhi na jioni wakati nimelazwa hospitalini baada ya kupigwa kwenye harakati za kupinga matokeo ya urais, ikabidi nimkataze. Alikua anasema inabidi awamu hii apumzike kwenye nafasi ya umakamu wa rais na tupendekeze mtu mwingine ila tukamkatalia.”

Ushawishi kutokea kaburini

Simulizi nyingi kuhusu Maalim zinastaajabisha. Lakini mimi Charles William nimestaajabu zaidi baada ya kusikia kwamba Maalim Seif akiendelea kufanya maajabu mpaka akiwa kaburini. Ndiyo, kaburini! Kamati ya Uongozi ya ACT-Wazalendo ambayo imejaa watu wenye sifa za kurithi wadhifa wake, wa Umakamu wa Kwanza wa Uraisi wa Zanzibar imekubali kufuata maagizo ya Maalim Seif ambaye leo ni siku ya 10 yupo ndani ya shimo la futi sita kwenda chini.

Akitangaza hatua ya chama hicho kuwasilisha jina la mrithi wa Maalim Seif, Kiongozi wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe alisema: “Tumeshapendekeza kwa Raisi Hussein Mwinyi jina la mtu wa kurithi majukumu ambayo Maalim Seif alikua akiyafanya. Maalim aliacha maelekezo ya nini kitokee iwapo atatangulia mbele ya haki. Viongozi wa Chama wamefuata maelekezo yake na sasa umebaki wajibu wa Rais wa Zanzibar wa kuyatekeleza hayo.”

Kwa lugha rahisi ni kwamba ACT-Wazalendo wamempendekeza mtu wa kuchukua nafasi ya Makamu wa Mwanza wa Raisi kuwa ni yule ambaye Maalim Seif enzi za uhai wake aliagiza kuwa akifa, mtu huyo ndiye achukue mikoba yake. Ni nani huyo aliyeukonga moyo wa Maalim Seif hata gwiji hilo la siasa za Tanzania likaona aache wosia kuwa akifa mtu huyo ndiyo awe mrithi wake? Nina shauku sana ya kumjua. Nimesikia anatajwatajwa ila bado siamini kama ndiye. (Wakati makala hii inawasilishwa kwa mhariri, jina la mrithi wa Maalim Seif lilikuwa halijajulikana. Hata hivyo, mnamo Machi 1, 2021, Raisi Mwinyi alimteua Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar Othman Masoud Othman Sharif kuwa mrithi wa nafasi hiyo.)

Sijui Maalim Seif alimuachia nani ujumbe kuhusu mrithi wa nafasi aliyokua akiitumikia. Sijui aliacha ujumbe wa maandishi, wa sauti au wa video lakini bado naona ni muendelezo wa maajabu yake. Vikao vya chama chake vinamtii ingawa yu kaburini kwa sasa. Hasikii, hasemi wala haoni. Viongozi wa ACT-Wazalendo waliopo Kamati ya Uongozi iliyopendekeza jina wamekubalina na maagizo ya Maalim. Hata wale wenye sifa za kuchukua nafasi yake na ambao wangeweza kushawishi wajumbe wawapendekeze lakini wamekubali achukue nafasi yule aliyetajwa na Maalim Seif tu.

Maajabu ya Maalim Seif yanaenda mbali zaidi ya matendo yake, yakianzia kwenye majina ya mwanasiasa huyo ambaye msiba wake unaendelea kuombolezwa. Majina yake yote yamebeba maana nzito. Maalim ina maana yake, Seif ina maana yake, Sharif ina maana yake na Hamad ina maana yake. Nini maana gani majina haya? Tafiti mwenyewe. Ila nimalizie safu hii kwa kukujuza tu ya kwamba majina haya yote yanabeba maana zinazoshabihiana na matendo ya ajabu yanayosimuliwa kuhusu mwanasiasa huyu.

 

Charles William ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni charleswilly93@gmail.com au Twitter kupitia @2charlesWilliam. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unaweza kuchapisha kwenye safu hii kwa kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *