The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Fatma Karume: Hakuna Mtoto Wangu Anayefikiria Kufuata Nyayo Zangu

Mwanaharakati huyo mashuhuri anaieleza The Chanzo kwenye mahojiano maalumu kwamba watoto wake wanamshangaa kwa nini anajisumbua kupigania utawala wa sheria nchini Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mnamo Agosti 11, 2021, Mahakama Kuu kanda ya Zanzibar ilimkuta na hatia mtu anayejitambulisha kama ‘mwanaharakati huru’ Cyprian Musiba ya kumdhalilisha na kumvunjia heshima mwanasheria na Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Fatma Karume na kumuamrisha amlipe fidia ya shilingi bilioni saba kutokana na usumbufu huo. Musiba, kupitia gazeti lake la Tanzanite, alimshutumu Fatma, pamoja na mambo mengine, kutoa mimba aliyodai amepewa na muuza madawa ya kulevya. 

Hatua hii ilikuja wiki kadhaa baada ya Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, mnapo Juni 22, 2021, kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Mawakili wa kumfutia Fatma Karume leseni yake ya kufanya kazi za uwakili nchini. The Chanzo imefanya mahojiano maalumu na Fatma Karume kufahamu hatua ambazo michakato hii imefikia mpaka sasa pamoja na masuala mengine kadhaa yanayohusiana na kazi na maisha yake. Endelea …

The Chanzo: Kuna mambo mengi hapa yametokezea kuhusiana na kesi uliyokuwa nayo wewe na mwanaharakati huru Cyprian Musiba, mpaka Mahakama Kuu kanda ya Zanzibar ikatoa maamuzi. Kuna masuala ya wewe na suala lako la kufanya kazi kama mwanasheria kutolewa uamuzi na Mahakama Kuu kama nakumbuka vizuri. Nilikuwa nataka kufahamu tu, umekuwa ukifanya nini ndani ya miezi hii kadhaa labda?  

Fatma Karume: Kuna rafiki yangu mmoja ananiita Fatma K, ananiambia: “Unajua nini Fatma K? Wewe tangu Januari [2021] mpaka sasa hivi umefanya mambo mengi sana. Tatizo lako ni kwamba hujitambui kwamba unafanya mambo mengi.” Kwa hiyo nimekuwa nafanya nini? 

Kitu muhimu kabisa ambacho nimefanya nimekuwa nalea watoto wangu kwa sababu mimi ni mfanyakazi, tangu nimetoka chuo kikuu nimekuwa nafanya kazi. Sijawahi kupumzika, nimekuwa nafanya kazi tu. Kwa hiyo, imekuwa kitu kizuri kumpeleka mwanangu shule, kurudi nae, kumuuliza anataka kula nini, kuwepo tu kwa ajili ya mtoto wangu wa kike na wa kiume. Hicho kimekuwa kitu chema.

Kitu cha pili nimefanya, niko na vimradi vyangu vidogo vidogo naendelea navyo. Bado naombwa kutoa ushauri wa kisheria. Kwa hiyo, nimekuwa natoa ushauri. Naandika maoni ya kisheria kwa watu wanaotaka maoni ya kitaalamu [kutoka kwangu].  

Na kitu kingine muhimu sana ambacho nimekuwa nafanya, naendelea na harakati zangu za kuhakikisha kwamba Tanzania tunaheshimu sheria, na kwa kweli kuwasema watu waliopo madarakani wakifanya vitu vilivyo nje ya sheria, na kuhakikisha kuwa tunafuata sheria na tunafuata Katiba [ya nchi].

Japo tuna Katiba hii tunayosema ni dhaifu lakini bado ni Katiba na tujaribu kujenga utamaduni wa kufuata Katiba yetu. Na ingelikuwa tunaifuata hii Katiba kwa asilimia 50 tu basi Tanzania kungekuwa mahali pema zaidi kuishi kuliko hivi sasa. Kwa hiyo, najaribu bado kufanya harakati za kuhakikisha kwamba kuwasema, unajua, watu waliopo madarakani [pale ambapo] hawafuati Katiba na sheria. 

The Chanzo: Umegusia kuchukua muda kutoka kwenye kazi na kujihusisha na malezi ya watoto wako. Hivi watoto wako wanafahamu harakati zako? Wanaelewa unachokifanya kwenye eneo hilo ulilotoka kugusia sasa hivi la kuhakikisha kwamba Katiba inaheshimiwa na kunakuwepo na utawala wa sheria [nchini]? Wanafahamu kwamba una nafasi kubwa ya kitaifa ya kupigania masuala ya haki, utawala wa sheria, [na] demokrasia?

Fatma Karume: Nafikiri wanaelewa. Hawaelewi nafasi yangu kitaifa kwa sababu sidhani [kwamba] mtoto yoyote hamtazami mzazi wake hivyo. Lakini nadhani wanaelewa umuhimu wa kuwa na taifa linaloendeshwa kwa mujibu wa sheria.

Na kusema la haki, nikiongea nao, wanakuwa wanavunjika moyo sana na Tanzania na namna inavyoendeshwa. Na ni vijana na unaona huzuni yao, na kuvunjika kwa moyo na wasiwasi wao, na hawaelewi hii nchi kweli tutafika. Au nafasi yao kwenye hatima ya nchi hii wakati kuna mambo ya kijinga yanatokea. Mambo [kama] watu hawafuati utamaduni wa sheria.

Kwa hiyo, nikiongea nao naona kuvunjika moyo kwao kuhusu nchi yao na mustakabali wa nchi na uelekeo wa nchi na hatma yao kwenye hii nchi. Kwa hiyo, nahuzunika kwa sababu naona kwamba wana wasiwasi na wamevunjika moyo. 

The Chanzo: Labda pengine wana umri wa miaka mingapi, labda? 

Fatma Karume: Kumi na sita na kumi na tisa.

The Chanzo: Pengine unapoongea nao, na unapojadiliana nao na unapowatazama, unadhani kuna yoyote anayeeonesha dalili ya kuja kuchukua mikoba yako? 

Fatma Karume: Hapana, hakuna hata mmoja kwa sababu nadhani kwenye wasiwasi wao, wanasema, nikizungumza nao, wanasema: “Kwa nini unajisumbua, mama, kwa nini unajisumbua? Huwezi kubadilisha [kitu].”

The Chanzo: Na hiyo inakufanya ujisikiaje?

Fatma Karume: Huzuni. Kwamba mtoto wa miaka 16 na kijana wa miaka 19 anatazama watu waliopo kwenye madaraka na anaona kwamba hawana matumaini. Hakuna matumaini kwa ajili yao. [Kwamba watu waliopo madarakani] hawawezi kubadilika na hawaelewi vipi kuendesha nchi kwa misingi ya kisheria.

Na sehemu inayohuzunisha zaidi ni kwamba [hawa watoto] wameshawakatia tamaa hawa [viongozi wao waliopo madarakani]. Watoto wangu wa miaka 16 [na] miaka 19 wamewakatia tamaa hawa watu. 

Kwa hiyo, kitu pekee ninachoweza kusema ni [kwamba] kama watoto wangu wamekata tamaa, watoto wa wenzangu je? Hawa watoto wa umri wa miaka 16, 17, 18, 22. Vipi kuhusu wao? Je, na wao wamekata tamaa? Na kama wamekata tamaa, ni aina gani ya maisha ya baadae wanayategemea? Tumewaangusha. Tumewaangusha na hiyo inahuzunisha.     

The Chanzo: Tunafahamu kwamba kwenye kesi yako na Bwana Cyprian Musiba, ulikuwa una kesi naye Zanzibar kule, kwenye Mahakama Kuu kanda ya Zanzibar, na tunafahamu kwamba Mahakama ilitoa uamuzi wa kukupendelea na kumtaka [Musiba] akulipe bilioni saba hivi fedha za Kitanzania. Nilikuwa nataka kufahamu labda hii kesi, au huu mchakato umefikia wapi, sasa hivi, shilingi ngapi tayari [Musiba] ameshakulipa?

Fatma Karume: Hajanilipa hata shilingi moja. [Anacheka]. Lakini nasubiri hukumu ichapwe kwa sababu nimeelezwa na mwanasheria wangu [kwamba] hukumu bado haijachapwa na pia kuna amri ya mahakama lazima itoke [inayomtaka Musiba kulipa]. Kwa hiyo, na hiyo amri bado haijachapwa. Kwa hiyo, nasubiri hukumu ichapwe na amri ichapwe ili nianze mchakato wa utekelezaji, [yaani] kukaza hukumu. Sijuwi hiyo itachukua siku ngapi, lakini nasubiri.

The Chanzo: Musiba pengine amekutafuta kuyazungumza kifaragha labda [na] kukubaliana?

Fatma Karume: Hapana. Hapana. Hapana. Hajanitafuta wala hajazungumza na mimi kifaragha [na kuingia] makubaliano yoyote.

The Chanzo: Hii kesi na huu uamuzi uliutarajia? Ulitarajia kwamba Mahakama Kuu kanda ya Zanzibar ingetoa uamuzi kama huu? 

Fatma Karume: Angalia, bila ya shaka kwa sababu maneno aliyoyasema ni ya uongo na yameniharibia heshima yangu, yamenivunjia heshima yangu. Na nisinge-, nilikuwa na hakika kwamba kama kutakuwa na uwanja sawa wa kuchezea, nitashinda. Kwa nini nisishinde wakati mtu kasema uongo [kwa] kutumia magazeti yake kunichafua na kusema uongo? 

The Chanzo: Na labda kwa niaba ya watu ambao pengine hawakufuatilia kwa karibu, aliandika nini haswa?

Fatma Karume: Alisema kwamba mimi nina mwanamme, [yaani] boyfriend, [ambaye] ni muuza unga [wa madawa ya kulevya], [yaani] drugdealer, na kanitia mimba na nikatoa mimba. Sasa, kwa nini, haya maneno yalikuwa yanaudhi na kukera? 

Kwa sababu, tuelewane kitu kimoja, kwanza kutoa mimba Tanzania ni kinyume na sheria. Ukitoa mimba, unavunja sheria. Isipokuwa tu pale, tuseme, inatolewa [mwenye mimba] anaumwa au kitu kama hicho. Kwa hiyo, kwanza ameniambia mimi nimevunja sheria. Pili, ananihusisha mimi na muuza madawa ya kulevya.

Kwa hiyo, nilijua kwamba washapanga, kwamba, wakishanihusisha mimi na muuza madawa ya kulevya, wanataka kunipa kesi ya madawa ya kulevya ili [nikishtakiwa] nisipate dhamana. Unajua hawa watu ni waovu tu. Hawa ni watu waovu. Kwa hiyo, unaona wanapanga nini. Na mimi nina watoto. Nina familia. Ilibidi mimi nijitetee kwa sababu siyo haki. 

Nina watoto, siyo haki kwa watoto wangu, kwamba, mama yao anaambiwa maneno haya na [mtu] kama Musiba. Kwa sababu huyu mtu ni muovu. Ni mtu muovu na ilinibidi niende mahakamani.

The Chanzo: Na kwa nini ulichukua uamuzi wa kwenda kufungua shauri lako Mahakama Kuu kanda ya Zanzibar, na si hapa Tanzania Bara?

Fatma Karume: Kwa sababu watu wengi walijaribu kumpeleka Musiba Mahakama Kuu ya Tanzania Bara, hakuna hata mmoja wao [ambaye] kesi yake imesikilizwa ikafika mwisho. Hata mmoja wao. Mpaka sasa hivi, kesi ya [Waziri mstaafu wa Mambo ya Nje] Bernard Membe — Bernard Membe alianzisha kesi yake kabla yangu mimi — iko wapi? [Mwanaharakati] Maria Sarungi, alianzisha kesi yake kabla yangu mimi, dhidi ya Musiba, iko wapi? Umenielewa? 

Kwa hiyo, nilijua nikiipeleka kesi [Tanzania] Bara, kesi yangu haitofika popote. Kwa sababu walikuwa wameshaonesha hiyo dalili. Wameonesha [hizo dalili kwenye kesi ya] Membe, iko wapi kesi ya Membe mpaka leo? Unajua kaanza kesi yake pengine mwaka mmoja kabla yangu mimi? Kwa hiyo, nilijua.

The Chanzo: Sasa kitu ambacho mtu anaweza akajiuliza, hiyo inakwambia nini kuhusiana na suala zima la utoaji haki, linapokuja suala la Tanzania Bara na Zanzibar, kwamba, kwa nini iwe hivyo kwa Mahakama za Tanzania Bara na kwa nini iwe tofauti kwa Mahakama Kuu kanda ya Zanzibar kwa mfano? Kuna chochote ambacho unadhani kinaweza kikawa kimechochea hali hiyo?

Fatma Karume: Hilo ni swali la kumuuliza Jaji Mkuu, siyo mimi. Kwa sababu, swali la kumuuliza Jaji Mkuu [ni] ilikuwaje mtu anaweza kuanza kesi Zanzibar dhidi ya Musiba, miaka miwili au mwaka mmoja baada ya kesi iliyoanzishwa na Bernard Membe [Tanzania] Bara, kesi yake [aliyefungua Zanzibar] ikasikilizwa, tena imechukua muda, ikasikilizwa, ikamalizika, ikatolewa hukumu, huku Bara nyinyi mpaka sasa hivi hamjafika popote? 

Inaacha maswali mengi sana bila majibu. Unanielewa, enh? Na mimi niliamua kwenda Zanzibar kwa sababu Zanzibar ina jurisdiction. [Gazeti la Tanzanite analomiliki Musiba] likichapishwa linauzwa Zanzibar. Siyo kwamba inauzwa huku [Tanzania Bara] tu. Linauzwa Zanzibar na, kwa hiyo, [Musiba] akichapisha anachapisha na Zanzibar pia. Nikaamua niende kule kwa sababu nilikuwa nahisi hapa [Tanzania Bara] nitahangaishwa tu. Nitahangaishwa tu.

The Chanzo: Lakini, ukiachana na hiyo pesa ambayo Musiba atapaswa kukulipa, unadhani hii hukumu inatuma ujumbe gani kwa watu kama Musiba, au watu ambao pengine wanapanga kufanya kitu kama hicho alichokifanya kwa watu wengine pengine? Unadhani ni mafunzo gani makubwa ambayo tunaweza tukayapata kutoka kwenye uamuzi wako wa kumpeleka Musiba mahakamani na mpaka Mahakama ikatoa uamuzi wa aina hii?

Fatma Karume: Nimefurahi sana kwamba [tumepata] mafunzo gani. Pesa siyo kila kitu na Mahakama ikitoa hukumu, zile pesa wanazoamua kukupa inaonesha fikra za Mahakama kwa uzito wa lile jambo alilolifanya yule mtu, alivyokuchafua. Kwa hiyo, mtu akikuchafua -, angenichafua kidogo ningepata pesa kidogo [anacheka]. 

Lakini, zile pesa nyingi, ina maana kwamba Mahakama imekubaliana na mimi kwamba kakuchafua vibaya sana kama mwanamke mwenye staha, mwenye familia yako, kakuchafua vibaya, sawa? Hususani kama mwanamke. Sasa zile pesa umuhimu wake siyo kwamba nitazipata, umenielewa? Umuhimu wake upo [kwenye] kuonesha ubaya wa kile kitendo.

Mimi sifikiri kwamba Musiba anazo-, tena siyo [shilingi] bilioni saba, ni bilioni 11 kwa sababu kulikuwa na gharama nyingine pia, kwa hivyo sidhani kama anazo bilioni 11, bilioni 12, samahani. Lakini, mimi nitaendelea kukaza hukumu. Siyo kwa sababu nataka bilioni 11 au 12 kutoka kwa Musiba. Ni kwa sababu nina amini ninamdai Musiba hizo pesa. [Anacheka]. Umenielewa? Ninamdai hizo pesa. 

Na nimeapa, hata nikipata Sh5 kutoka kwa Musiba, nitazitoa kama zaka. Na nikipata zaidi ya Sh5, nikipata shilingi milioni moja, nitahakikisha nitamsomesha mtoto wa kike aliyeshika mimba [akiendelea na masomo ili] amalize elimu yake. Siwezi kuzitumia pesa za Musiba mimi mwenyewe. Lazima nizisafishe maana ni chafu. Na nitazisafisha kwa kuhakikisha kwamba nitawasomesha watoto wa kike, hasusan watoto walioshika mimba [wakiwa masomoni] na waliofukuzwa [shuleni] kwa sababu ya sera mbovu ya [Rais mstaafu hayati John] Magufuli. 

Nikipata bilioni 13 kutoka kwa Musiba, sijuwi bilioni 12, nitafungua shule. Nikizipata bilioni 12, nitafungua shule kusomesha watoto wa kike, watoto wa kike tu, walioshika mimba. [Hawa watoto] wameharibiwa kabisa kabisa na Serikali hii. Kama sipati bilioni 12-, nikipata milioni moja, nitajaribu, nitatumia hizo hizo, kumpeleka shule mtoto mmoja. Nikipata milioni 10, nitapeleka shule watoto 10, watoto wakike walioshika mimba.

The Chanzo: Na vipi kuhusiana na mchakato wa kurejeshewa leseni yako ya kufanya kazi kama mwanasheria au kama wakili Tanzania? Pengine unaweza kutuambia kwa ufupi labda, [huu mchakato] umefikia wapi? Maana nakumbuka mara ya mwisho Mahakama ilitoa uamuzi, kama nakumbuka vizuri, kwamba kuna dosari zilijitokeza kwenye mchakato mzima wa kukutoa wewe kwenye orodha ya mawakili. Labda unaweza kutuambia kwa sasa kuna nini kinaendelea labda ili wewe kupata haki yako ya kufanya kazi yako kama mwanasheria. 

Fatma Karume: Tazama, kwa sasa, wame-, nasikia, Mwanasheria Mkuu kakata rufaa, anaipeleka kesi Mahakama ya Rufaa. Vyovyote vile iwavyo, hilo ni tatizo lake. Ni maamuzi yake. Mwanasheria wangu kaiandikia Mahakama, akawaomba Mahakama, wanirejeshee leseni yangu kwa sababu Mahakama Kuu ilibatilisha ule mchakato mzima. Mahakama, [kupitia] Msajili [wa Mahakama] alijibu akisema kwamba lazima niombe chini ya kifungu fulani cha sheria kwa sababu nilikuwa nimefutwa, kwa hiyo lazima niombe, mpaka sasa hivi, kanijibu hivyo.

Mpaka sasa hivi mimi kusema la haki sijafuatilia lakini nadhani hapo kati kabla ya mwisho wa mwaka nitawaandikia nione watafanya nini. Swali la msingi kwangu mimi kwa kweli ni, “Nataka kuendelea kufanya [uwakili] kwenye hizi mahakama [za Tanzania]?” 

The Chanzo: Unadhani hautaki tena?

Fatma Karume: Hapana, sina haja tena. Sina haja tena. Nimesoma ruling ya [Jaji Elineza] Luvanda ya juzi na kusema, “Mungu wangu, sawa!”  

The Chanzo: Kwa hiyo-, kwa kusema kwamba hautotaka tena kufanya kazi kama wakili, utabaki kulea tu watoto au na kufanya kazi zingine? 

Fatma Karume: Nitafanya mambo mengine. Unajua maisha-, nafikiri-, kitu ninachotaka kusema ni kwamba ukiendelea kugonga ukuta kwa kichwa, utaumwa na kichwa. [Anacheka]. Sasa unakwenda mahakamani, unajua, unachoka [wakati] kuna mambo mengi ya kufanya. Unajua kwa sasa nna umri wa miaka 52, mahakimu wengi sasa hivi ni wadogo kuliko mimi. Majaji wengi wa Mahakama Kuu ni wadogo kuliko mimi, wachache sana wana umri sawa na mimi. 

Sitaki ifike umri wa miaka 60 niende mbele ya watu wenye umri wa miaka 35. Unaelewa, enh? Sina haja tena [kwenda mbele ya] watu wenye umri wa miaka 40. Unapambana na mtu, unajaribu kumweleza, hapana, sina haja tena. Ni muda muafaka wa mimi kuendelea kufanya mambo mengine.

The Chanzo: Kwa hiyo, inawezekana kabisa hautoshinikiza, [au] kufuatilia kivile kurejeshewa ile leseni?

Fatma Karume: Hapana, nafikiri ni suala la misingi. Kuna misingi, umenielewa enh? Na nimepata msaada mkubwa sana kutoka Chama cha Wanasheria [Tanganyika – TLS], na Chama cha Wanasheria wanataka kuhakikisha kwamba misingi inabaki vile na inaheshimiwa na Mahakama. Kwa hiyo, nitaendelea kushinikiza kwa sababu hii misingi ni muhimu. Ni muhimu kwa sababu ya wanasheria wengine, mawakili wengine wanaotaka kuendelea.

Lakini kwangu binafsi, kamwe sitojitokeza tena mahakamani, sina haja tena. Siyo kwenye mahakama za Tanzania. Kamwe! Sina haja tena. Hata hivyo, kuna majaji watanikumbuka sana. [Anacheka]. Lakini nawaambia kwa heri. Kimsingi, kuna ambao walinisaidia kwa kiwango fulani, lakini inabidi niende.

The Chanzo: Umesema watakukumbuka, labda watakukumbuka kwa nini?

Fatma Karume: Kwa sababu mimi niko vizuri kwenye vitu ninavyofanya na baadhi ya majaji walinipenda, nikijitokeza [mbele yao] wanajua [kwamba] nitawasaidia kufanya kazi zao kadiri ya uwezo wao. Kwa sababu hiyo ndiyo kazi ya wakili, na baadhi ya majaji walikuwa wanapenda hivyo, nikijitokeza [mbele yao] tu unaona wanatabasamu. 

The Chanzo: Nilikuwa nasema, watu wengi sana, tunakufahamu yaani mtu anaposikia jina Fatma Karume huwa kitu kinachomjia akilini mwake moja kwa moja ni harakati zake. Harakati ambazo Fatma Karume amekuwa akizifanya, hususani kwenye eneo la utawala wa sheria, demokrasia, na kwa sababu kule mwanzo tulianza na suala zima la wewe kuchukua muda na kukaa na familia yako na kushughulika na malezi. Nilikuwa nataka kufahamu [iwapo] kuna namna nyingine yoyote ambayo ungependa watu wamfahamu Fatma Karume labda ukiachana na masuala ya harakati, kuna vitu vingine unajihusisha navyo, au vitu vingine unavipenda, na vitu ambavyo pengine ungependa watu wakisikia jina la Fatma Karume, viweze kumjia akilini mwake labda?  

Fatma Karume: Hakuna, mimi ni mtu wa faragha sana. [Anacheka]. Unaweza kuona hata kwenye [ukurasa wangu wa] Twitter, watu wengi hawajui kama nna watoto. Watu hawajui kama nna watoto, hawajuwi kitu nnachokipenda mimi, mimi ni mtu wa faragha sana. Sipendi kabisa, na ukiona kwenye Twitter yangu, mara chache sana ntaweka picha yangu, mara chache sana, umenielewa enh? Kwa sababu mimi ni mtu wa faragha sana.

The Chanzo: Labda na hiyo inatokana na nini, ni uzoefu ambao pengine umewahi kukutana nao kutokana na kazi zako au ni kitu ambacho ni kibinafsi tu kwamba uko hivyo kimaumbile?

Fatma Karume: Kwa sababu niko hivyo kimaumbile lakini pia naelewa kitu muhimu kwamba suala siyo mimi. Suala ni misingi, umenielewa? Suala ni misingi, siyo mimi. Nikigombania utawala wa sheria, siyo mimi [bali] misingi ya utawala wa sheria. Nikigombania demokrasia, siyo mimi, ni misingi ya demokrasia. 

Hiki ndicho nnachojaribu kuuza kwa watu wa Tanzania. Hiki ndicho nnacho jaribu kuwaelimisha watu wa Tanzania. Haihusiani kabisa na mimi. Ni misingi. Ni dhana, umenielewa? Kitu ninachojaribu kufanya ni kuuza dhana na siyo mimi. Mimi sina umuhimu wowote. Naweza kufa leo. Lakini matumaini yangu ni kwamba nikiondoka naacha watu nyuma ambao watakipokea kijiti na kuendelea kupigania hizi dhana. 

Mimi sina umuhimu huo, umenielewa? [Anacheka]. Kilicho cha muhimu, Khalifa [Said, mwandishi] ni hizi dhana, kwani hutengeneza jamii iliyo bora. Kamwe huwezi kuniona mimi nikiweka mbele mambo yangu binafsi, sina haja [ya kufanya hivyo]. [Anacheka]. Niko wazi sana kati ya Fatma Karume na dhana ambazo napenda kuzipigania. Mimi napenda kupigania dhana.

The Chanzo: Shangazi mimi nakushukuru sana kwa muda wako. Kusema kweli, siku zote ni faraja sana kuzungumza na wewe [kwani] kuna busara na taaluma nyingi najipatia. Nakushukuru sana kwa muda wako na nakutakia kila la kheri kwenye maisha yako na harakati zako.

Fatma Karume: Nashukuru, lakini usifikiri yameisha. [Anacheka]. Kwa sababu nitaendelea kupigania ukatiba [na kupigania] utawala wa sheria. Hata hii Katiba tuliyonayo sasa hivi lazima tuiheshimu.

The Chanzo: Nakubali, asante sana, Shangazi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 Responses

  1. Nakupongeza mwandishi kwa weledi wako ulokuwezesha kumuuliza mwanaharakati, Fatama Karume, ambaye kimaumbile ni mtu wa “faragha”, kutulia nakufungua kidogo pazia ya maisha yake. Wakati wote alikukuwa anajua anazungumza nini. A smart lawyer and well aware of her role in a country, where the Constitution is not taken seriously. Inshallah Mungu ataendelea kumlinda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *