Dodoma. Mwandishi na mwanaharakati mkongwe nchini Tanzania Jenerali Ulimwengu amekituhumu Chama cha Mapinduzi (CCM) kupoteza mwelekeo, akisema chama hicho tawala nchini kimesahau kilipotoka na wala hakijui kinapokwenda, huku akibainisha kwamba chama hicho kikongwe barani Afrika kimetupilia mbali misingi ya kifalsafa iliyopelekea kuanzishwa kwake.
The Chanzo ilipomtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka kujibu tuhuma hizi simu yake ilikua inaita tu bila kupokelewa, hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakurudisha majibu. Ulimwengu alitoa tathmini hiyo ya CCM siku ya Jumatano, Oktoba 6, 2021, wakati wa Mdahalo wa Rai ya Jenerali ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini hapa.
“Nadhani [CCM] ilikuwa kimeshasahau kilipotoka na sasa hivi kimepotea nyikani, hakijui kinakwenda wapi,” alisema Ulimwengu kwenye mdahalo huo wakati wa kujadili umuhimu wa Katiba Mpya ambayo viongozi na makada kadhaa wa CCM wamekuwa wakinukuliwa wakisema Watanzania kwa sasa hawahitaji Katiba Mpya. “[Ni] kama vile [CCM] imepoteza mwelekeo. [CCM] hawakumbuki tena ni wapi walikotoka na falsafa ya kimsingi ya chama chao walishaitupilia mbali.”
Mdahalo huo ni sehemu ya midahalo inayoendelea kufanyika nchini Tanzania kujadili kitabu kipya cha Jenerali Ulimwengu kiitwacho Rai ya Jenerali ambacho kilizinduliwa mnapo Agosti 7, 2021, jijini Dar es Salaam. Kitabu hicho chenye ukubwa wa kurasa 220 ni mjumuisho wa makala kadhaa ambazo Ulimwengu alikuwa akizichapisha kwenye gazeti la Rai mnamo mwaka 1996. Hii ni juzuu ya tatu ya mjumuisho wa makala za Ulimwengu huku juzuu mbili zikiwa zimeshatoka tayari.
Miongoni mwa mambo yanayoangaziwa kwenye kwenye juzuu hiyo ya tatu ya Rai ya Jenerali ni pamoja na Uchaguzi Mkuu wa 1995 ambao ulikuwa ni uchaguzi mkuu wa kwanza tangu Tanzania irejeshe mfumo wa vyama vingi mnamo 1992 pamoja na suala zima la Katiba Mpya, huku swali la msingi likiwa ni je, Katiba iliyopo sasa ya mwaka 1977 inakidhi mahitaji ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya taifa la Tanzania?
Suala la Katiba Mpya ndilo lililotawala hoja za msingi katika mdahalo huo uliofanyika katika Hoteli ya Morena jijini hapa na kuhudhuriwa na makundi mbali mbali ya wananchi wakiwemo wanaharakati, wasomi, waandishi wa habari na wananchi wengine kwa ujumla. Mjadala huo wa Katiba Mpya ulifanyika wakati ambao Rais Samia Suluhu Hassan amewaomba wananchi wampe muda kidogo arekebishe hali ya nchi ya kiuchumi kabla hajatatua changamoto za kisiasa, ikiwemo ufufuaji wa Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
Mmoja kati ya watu waliohudhuria mdahalo huo na kupata fursa ya kuzungumza ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu Profesa Mussa Assad ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia umuhimu wa kuwa na Katiba Mpya ambayo ina uwezo wa kuwadhibiti viongozi wenye maarifa na wale wasio na maarifa.
“[Katiba] hii [ya 1977] ni nzuri lakini inamuhitaji kiongozi mwenye maarifa makubwa sana,” alisema Profesa Assad. “Atakapotokea kiongozi mweye hulka mbovu ni rahisi sana kuitumia Katiba ile na tutapata dubwana litakalo tupa shida kubwa sana. Kwa ninavyoona mimi, kwa hii miaka iliyopita tulipata shida kubwa sana ya namna hii.”
Mwanasheria kutoka LHRC Wiliam Mtwazi amesema kwamba kiu ya mabadiliko ya Katiba miongoni mwa wananchi ni kubwa sana ikidhihirika kwenye ushiriki wao kwenye midahalo ya Katiba Mpya ambayo LHRC imekuwa ikiandaa kwa siku za hivi karibuni.
“Kwenye midahalo ambayo tumekuwa tukiandaa wananchi wanakuwa na hamasa kubwa ya kutaka kujua mambo kadhaa yahusianayo na Katiba,” anasema Mtwazi. “Unakuta wananchi wanahoji masuala kama vile: Tutapata lini Katiba Mpya au Katiba inatengenezwaje? Na tumekuwa tukiwajibu kuwa ni suala la kimchakato.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumfikia kupitia jaquelinevictor88@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.
2 Responses
CCM hawataki kubadiri katiba,kwasababu wanajua ndio itakuwa mwisho wao madarakani,na wanahofu ya kushitakiwa kwa maovu waliyofanya.Lakini watatoka tuuu
*MAWAZO NA USHAURI WANGU BINAFSI KWA:* 1. *Jukwaa la vyama vya siasa. (TCD) 2. Serikali. 3. Vyombo vya habari, na 4. Watanzania wote kwa ujumla ni:. .* Moja ya mambo ya kufanya katika kutekeleza dhana ya kuendesha sisa za kiustaarabu na kukuza demokrasia, iwe ni pamoja na kuanza kujenga mazingira ya matumizi ya Neno USHINDANI kwenye siasa. Neno UPINZANI linaleta taswira (mindset) ya uadui, kutoafikiana, kutosikilizana, kulaumiana, kubishana kutotakiana mema na kutoaminiana. ” ” Adui yako mwombee njaa.” Hata akisema au kufanya jambo jema, hutauona wema huo. Adui akifanya kosa, hata kama ni dogo utalikuza ili kumchafulia. Kwenye siasa inatakiwa KUSHINDANA kwa hoja kuingia IKULU (kuingoza nchi) Wacheza mpira WANASHINDANA kuingiza mpira wavuni kwenye goli. KUSHINDANA kuna taswira ya urafiki, upendo na maelewano. Ndo maana wacheza mpira mwisho wa MASHINDANO bila kujali nani kashinda wanakumbatiana, kupeana mikono hata kubadirishana jezi. Kwenye siasa TUNAPINGANA ili tupate nini.? Kwa faida ya nani? IKO HAJA YA KUBADIRIKA. Vyama vya siasa viitane VYAMA VYA USHINDANI siyo VYAMA VYA UPINZANI. Imetugharimu, inatughatimu na tusipotambua impact ya. ” Psychology ya Subconscious mind- mindset ” na nguvu ya maneno haya, itatugharimu zaidi. Maneno YANAUMBA, ndo maana hata Mungu alitumia maneno tu kwenye uumbaji wake. Naitwa Dr. Mhoro mstaafu. 0744-460529