Zuhura Yunus: Nafahamu Hisia Zitakazoibuliwa na Kitabu Changu

Ni kitabu chake cha Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi kilichochapishwa mwaka huu na kuzinduliwa Novemba 13, 2021, jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu14 November 202125 min

Dar es Salaam. Mnamo Novemba 9, 2021, mwandishi wa habari wa siku nyingi nchini Tanzania na mtangazaji mashuhuri wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Zuhura Yunus alizindua kitabu chake kiitwacho Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi.

Kitabu hicho kinachohusu maisha na mchango wa mwanamama wa Kizanzibari Biubwa Amour Zahor katika Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, pia kilizinduliwa Dar es Salaam, mnamo Novemba 13. 2021, katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi pamoja na wanazuoni, waandishi wa vitabu, wanaharakati, waandishi wa habari na wananchi wengine kwa ujumla.

Kufuatia hatua hiyo ya kuandika kitabu kuhusu maisha ya mmoja kati ya wananwake wengi walioshiriki kikamilifu katika Mapinduzi ya Zanzibar, The Chanzo imefanya mahojiano maalum na Zuhura Yunus ili kujadili baadhi ya mambo yanayopatikana kwenye kitabu hicho ambacho tayari kinapatikana sokoni. Endelea …

The Chanzo: Karibu sana The Chanzo.

Zuhura Yunus: Asante sana Khalifa [Said, mwandishi]. Shukran!

The Chanzo: Siku nyingi tulikuwa tunatafuta hii fursa hatimaye tumefanikiwa.

Zuhura Yunus: Hatimaye!

The Chanzo: Unaweza ukawa mwandishi wa habari wa siku nyingi, watu wamekuona kwenye runinga na ushawahi kuandika pia, lakini unajisikiaje kuweza kufanikisha kuandika hiki kitabu? 

Zuhura Yunus: Najisikia raha kwa sababu mara ya kwanza nilivyo kipata hata sijui nilikuwa najisikia vipi, kama ni raha au huzuni. Yaani,  nilikuwa na hisia mchanganyiko. Na nilivyo kipata hata kukifungua nilikuwa ninaogopa. Nasema sijui kizuri, sijui kimekaa vipi, unajua ile? Lakini baadae nikatulia. Nadhani nilikipata asubuhi vile wakati nipo kule Uingereza. Nakala ya kwanza kabisa. Kumbe nakala ya kwanza anapewa mwandishi aliyeandika. 

Kwa hiyo, nilikaa nacho mpaka jioni. Nimekaa nikatulia ndio nikafungua kuangalia. Kwa hiyo, nilifurahi maana safari ilikuwa ndefu sana. Hatimaye unakishika mkononi unasema eeh hiki kitabu nimeandika mie? Kwa hiyo, kulikuwa na raha fulani.

The Chanzo: Safari ilikuwa ndefu, nilisikia wakati upo Zanzibar kwamba ilianza 2017, si ndio?

Zuhura Yunus: Naam!

The Chanzo: Hongera sana.

Zuhura Yunus: Asante!

The Chanzo: Najisikia faraja sana kuona mwanamke mwandishi anaandika kitabu kuhusu mwanamke ambaye pia ni Mtanzania. Na hili lilizungumzwa katika uzinduzi wenu kule Zanzibar kwamba si kitu maarufu kusema ukweli, mara nyingi tumeona Wazungu wakija wakifanya tafiti na kuandika. Sitaki kukuuliza kwa nini ulifikiria kuandika hiki kitabu kwa sababu hili swali lilishajibiwa  tayari huko, lakini mtu akitaka kufahamu inabidi asome kitabu [kicheko] akitaka kufahamu kwa nini Zuhura Yunus ameandika hiki kitabu. Lakini mimi nataka kukuuliza kwa mtu ambaye hajapata fursa kabisa ya kukisoma hiki kitabu au kusoma chochote kuhusiana na hiki kitabu, unadhani kwa nini asome hiki kitabu?

Zuhura Yunus: Asome hiko kitabu kwa sababu nadhani ni nadra sana kusikia wanawake wa Kizanzibari wameshiriki kwenye Mapinduzi [ya] Zanzibar. Sijui kama kuna kitabu chochote, siwezi kusema kwamba nimefanya utafiti wa kutosha. Hilo peke yake lina mvuto wa aina yake, sio kwamba hawapo, lakini hawatajwi. Ndiyo kama hiyo ipo picha maarufu kwenye hicho kitabu na hata kama uki-google hiyo picha maarufu unaiona wako wanaume wote lakini mwanamke mmoja tu. 

Lakini nadhani hatudadisi sana. Hatuulizi huyu mwanamke ni nani? Na  unawakuta watu maarufu kina Abeid Amani Karume, kina Abdulrahman Babu, kina [Kassim] Hanga. Wote wamo  humo na kuna mwanamke mmoja tu kakaa kwa nyuma hivi ambaye ndio yeye Biubwa [Amour Zahor]. Kwa hiyo, hilo nadhani peke yake linakufanya mtu useme hebu ngoja nisome. 

Vile vile utata, [Biubwa] ni mtata. Kwa kifupi unaweza kusema hivyo. Kwa sababu ukimtaja Unguja, mimi nimeshasikia miaka mingi kuna mambo fulani ambayo alihusishwa nayo. Kama unavyojua, mapinduzi yalikuwa na pande mbili, kuna wanayo yafurahia na ambao hawa yafurahii. Kwa hiyo, hizo pande mbili zinaleta chachu ya kufikiria huyu mtu ana umuhimu wa kuzungumziwa. 

Na ukikisoma [hiki kitabu] kuna mambo ya udhalilishaji wa wanawake ambayo ukiangalia mpaka sasa tunapigizana nayo kelele. Unaona hapa juzi Hollywood, Marekani wakaanzisha ile hashtag  ya #Metoo kila mmoja anataja. Kwa hiyo, ni vitu vilivyokuwepo tangu zamani ni basi tu havifanywi kama inavyofanywa sasa lakini masuala ya kudhalilishana yapo sana. Kujua kwamba mwanamke kama huyu kapewa kazi maalum na Rais wa wakati huo eeh, wangapi wanajua kuwa wanawake walikuwa wanapewa kazi muhimu sana katika masuala ya harakati za mapinduzi?

The Chanzo: Na kazi yenyewe maalum ndugu wafuatiliaji wa The Chanzo, nitawaibia kwa sababu nimesoma kitabu. Hizo kazi maalumu ni kwamba Rais wa kwanza wa Zanzibar Abeid Amani Karume alikuwa akimtuma Biubwa Amour Zahor nchini Uganda, nchini Kenya kwenye kazi maalum. Sasa kazi maalum gani inabidi usome kitabu. 

Zuhura Yunus: Na vile vile kuna utata sana. Kama unavyojua, wakati wa mapinduzi kuna watu waliuawa. Tunajua Zanzibar ni mchanganyiko wa watu mbalimbali lakini kwa bahati mbaya wakati ule Waarabu ndio waliathirika zaidi wanasema. Lakini yeye [Biubwa], kwa asili, baba yake na mama yake ni Waarabu, na baba yake aliuawa wakati ule. 

Kwa hiyo, kumekuwa na maneno mengi sana yanasemwa dhidi ya Biubwa mwenyewe na mauaji ya baba yake. Kwa hiyo, tutaishia hapo kama ulivyosema [ili msomaji akasome kitabu]. Lakini, hiyo naona watu wengi sana wakijadili wanaijadili sehemu hiyo ya mauaji ya baba yake. Kwa hiyo, nadhani vitu hivyo vitatu, vinne vinavuta mtu kuvisoma bila shaka.

The Chanzo: Umegusia hapo masuala ya udhalilishaji wa wanawake au wa kijinsia. Nimesoma kitabu ni mambo ambayo ni ya miaka hamsini, sitini iliyopita. Lakini ukiangalia haya mambo yanaendelea kutokea leo. Kwa hiyo, kitu kimoja kinakufunua kichwa ni, kumbe mambo yaliyokuwepo leo hata zamani yalikuwepo japo kuna mabadiliko chanya na hasi tangu miaka ya 1950s bado kuna mambo yapo vile vile. Lakini vipi kuhusu mrejesho tangu kitabu hiki ukizindue na kianze kupatikana sokoni, una tathmini vipi mrejesho ulioupata kutoka kwa jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla?

Zuhura Yunus: Nadhani mrejesho, mimi nitasema ni mzuri kwa asilimia kubwa sana hata kama wapo wanakosoa, huo nao ni mrejesho mzuri tu kwa sababu kama wote tutakuwa tunakubaliana ina maana sijafanya kazi inayostaili. Kwa bahati mbaya au nzuri ilianza kujadiliwa mapema sana hata kabla kitabu hakijatoka, lakini ile tu walivyoanza kujua kinaitwa nini na kinamuhusu nani tayari kuna watu wakaanza kuandika mambo chungu nzima, hawajakisoma, lakini wa kuhukumu wamehukumu. 

Lakini vile vile, kuna wengine wakaanza kuzungumzia mapinduzi, wanakumbushana mapinduzi yalikuwa vipi. Ndio kama hivyo nilivyosema kulikuwa na pande mbili. Lakini baada ya baadhi ya watu kusoma wamenipigia simu na wamekifurahia, kwa kweli kwa asilimia kubwa nimepata mrejesho ambao ni mzuri. Hata kama anakosoa hapa kidogo lakini kwa ujumla wake wamependa nimetumia reference eeh, hadidu rejea nadhani, sijui kama nimepatia [kwa Kiswahili] eeh za kutosha.

Halafu, nimeweza kuzungumza na watu mbalimbali pamoja na kwamba ni wasifu wa Biubwa lakini nilijitahidi kushirikisha na watu wengine pia. Kwa sababu, unajua masuala ya historia anavyokumbuka huyu sio sawa na anavyokumbuka yule. Halafu mwingine akanambia, “Zuhura naona kama kuna vitu ambavyo umevificha ficha hivi.” Nikamwambia kama umegundua vimejificha basi lengo ni sawa, ina maana unatakiwa vitu vingine nawewe utumie akili lakini sio kila kitu. 

Mwingine, kwa majina nawahifadhi, akanambia nimependa mtiririko ambao umekwenda nao, yaani mtu unamsimulia kama yupo pale na vitu kama hivyo. Na mimi ndio ilikuwa inanitia hofu sana. Nikasema aah huu mtiririko wangu! Unajua wakati unajaribu kuandika, sababu mimi sijawahi kuandika kitabu, unajaribu kumuiga huyu, unamuiga huyu, unajua? Mwisho nikasema siwezi, acha niandike ninavyojihisi mimi mwenyewe. 

Nikatafuta ule mtiririko ambao nauhisi mimi mwenyewe nikaenda nao. Kwa hiyo, ninapopata huu mrejesho  unanipa moyo, na ni watu ambao wanasoma sana vitabu. Kwa hiyo, wanaponipa mrejesho, na kwenye makosa wananiambia hapa mbona uliisema ikaeleweka vizuri kidogo umeificha. Na ni kweli wanavyosema nakubali kweli nilikususida. Kwa ambao walikuwa [kwenye uzinduzi] Unguja, kuna sehemu ndogo, [unajua kwenye uhariri] unarudia na kurudia lakini kuna sehemu ndogo nilikosea kuandika eneo. Ilikuwa  niandike Dunga, nikaandika Donge. 

Kwa hiyo, mpaka sasa hivi inaniuma lakini inatokea. Kwa ujumla, naweza kusema  mrejesho umekuwa mzuri na mjadala [kuhusu kitabu] unaendelea. Nadhani kikubwa ni kwamba kuna mjadala kila sehemu. Mara Clubhouse, mara Twitter, mara WhatsApp. Mjadala umekuwepo, na ndio lengo. Watu wajadili na hasa katika maudhui ya mwanamke, umeelewa eeh? Sasa hii taarifa imejadiliwa na mwanamke. Na nimehoji na wengine. Kwa mfano Bi Ashura Babu nimemtumia kwa kiasi kikubwa kusikia na yeye anakumbuka vipi mapinduzi na mambo kama hayo. 

The Chanzo: Bi Ashura Babu ni mke wa aliyekuwa mwanamapinduzi Abdulrahman Babu.

Zuhura Yunus:  Naam!

The Chanzo: Mimi pia nimekisoma.

Zuhura Yunus: Nakujua wewe tena, najua una tathmini yako [Kicheko].

The Chanzo: Ndugu mfuatiliaji wa The Chanzo, hiki kitabu kinapatikana katika aina mbili, wenyewe wanaita hardcover, yaani nakala gumu ambayo wanauza kwa Sh45,000. Hlafu kuna hiki cha jalada laini, au softcover ni kwa watu kama sisi, kinauzwa Sh30,000. Kwa kweli, mimi nilikitafuta hiki nikakisoma, kusema ukweli mimi nimekipenda. 

Kwanza nilipenda vile ulivyoanza, umeanza na sasa halafu  ukarudi  zamani. Umeanza na vita vya Juni 1961. Nilivyoanza kukisoma kitabu hiki, kina kurasa kama 220, na nilipoanza kukisoma sikukiacha, wenyewe wanasema ni unputdownable, yaani huwezi kukiweka chini. Na pengine kwa sababu mimi ni Mzanzibari na unajua Wanzanzibari wafuatiliaji sana kwenye mambo yanayohusu nchi yao, kwa hiyo nilikuwa nakisoma kwa shauku kubwa. Sasa ningependa kufahamu kwenye upande wa soko, kitabu kinafanyaje sokoni? Watu wananunua?

Zuhura Yunus: Siwezi kusema kabisa kabisa lakini kwa mfano Zanzibar, mashallah, watu walinunua zaidi ya nakala 100, ambayo naambiwa aghalabu watu kidogo wanajivuta [kununua vitabu huko]. Halafu, baada ya hapo nimekuwa nikipigiwa simu sana kutoka ndani na nje ya nchi, maana yake wananiambia sasa tunakipataje, tunafanya vipi. Kwa hiyo, na mpaka jana wangine wameniagiza uende ukatuchukulie, niende dukani nikawanunulie. 

Kwa hiyo, nadhani kwa ujumla wake sijui kama nitafanya vizuri lakini au sijui wengine wanauza vipi lakini kiujumla inaonesha watu wengi wanatamani kukisoma. Kwa mfano, [nchi za] nje hasa, Omani, Canada, Uingereza, Marekani. Kwa hiyo, sasa wanajitahidi angalau kitoke pia Amazon, kwa ambao wako nje wanaweza tu kununua kwenye mtandao. Kwa sababu hapa inakuwa ngumu kidogo maana mtu anasema aah kuna ndugu yangu anasafiri naomba umpe ndugu yangu akija aniletee, na vitu kama hivyo. Kwa hiyo, kama watafanikiwa kukiweka Amazon itakuwa vizuri.  

The Chanzo: Naamini kinafanya vizuri, kwa sababu mimi nilikuwa nahitaji kitabu cha nakala ngumu lakini nilipofika nikaambiwa ushachelewa, kwa hiyo wakasema inabidi nichukue hicho kilichobaki, cha nakala laini. Mimi nikasema sina shida nitasoma hicho hicho.

Hapo mwanzo uligusia jinsi historia ya mapinduzi inavyoangaliwa kwa macho tofauti, na huo ni ukweli. Ukiangalia kwenye maandiko, historia ya Zanzibar ni kama Wazanzibari wamegawanyika, kuna watu wanakubali kilichofanyika 1964 na kuna watu wanaona kilichofanyika sio sahihi. Na wewe ukamuua kuandika kitabu kinachozunguka hapo kwa kutumia mtu mmoja anayeitwa Biubwa Amour Zahor. 

Nataka kufahamu, haukuwa na hofu labda? Nakuuliza hivyo sababu mimi kama mwandishi, japo sio mwandishi wa vitabu lakini kwenye kazi zangu za uandishi, muda mwingine unapotaka kuandika habari fulani unakuwa na hofu fulani ambayo inaweza ikakurudisha nyuma kidogo. Mapinduzi yanawagawa watu, watu mpaka wanafikia kugombana au kuhasimiana, lakini wewe ukaamua kuendelea nayo. Nataka kufahamu ilitokezea ukawa na wasiwasi kidogo, ukawa na hofu, ukawa unajiuliza kama unachofanya ni sahihi?

Zuhura Yunus: Tangu mwanzo nilijua nagusa mapinduzi kutakuwa na mtihani, hilo la kwanza. La pili, ni mtu mwenyewe, na hasa baada ya kuzungumza naye nikasema ooh! hapa habari nzito. Lakini nikasema tuna haki ya kujua na sote tukiogopa [kaundika] nani atafanya, ushaona eeh?

Kwa hiyo, mimi nikasema hii hofu naweza tu kupambana nayo nikifanya haki [kwenye kusimuliza maisha ya Biubwa Amour Zahor]. Nihakikishe nafanya utafiti wa kutosha, hata kama itanibidi niulize watu 1,000 ili mradi nitakapoandika niwe nimejiridhisha kweli kweli. Kwa hiyo, hata mtu akishambulia, nimuambie aaah nimeuliza huyu mtu alikuwepo. Nadhani ndio maana ilinichukua muda mrefu sana maana kutoka 2017 mpaka sasa hivi [2021] , watu wanaandika vitabu kwa mwaka, umeelewa eeh?

The Chanzo: Na ukilinganisha na ukubwa wake!

Zuhura Yunus: Wala sio kikubwa, labda [useme kina] kurasa mia tano, ushafahamu eeh? Sababu iliyonichukua muda mrefu ni hiyo [ya kuhakikisha natenda haki katika kusimuliza kwangu]. Unakuta wakati mwingine kuna jambo moja lakini nachukua miezi mitatu, kwa sababu naongea na huyu nahisi, mmh, sijaridhika nampigia mwingine, na-google, nasoma vitabu. Kwa hiyo, kitu kimoja kinanichukua muda mrefu sana, nikasema nihakikishe sikosei na namtendea kila mmoja haki na ukweli usemwe. 

Kwa sababu tukisema tunaogopa ni ukweli, mapinduzi yalifanyika,  na wanawake walikuwepo au hawakuwepo? Biubwa si alikuwepo na, alhamdulillah, yupo mpaka leo, si asikilizwe na yeye? Kama mtu anaona bado [kitabu changu hakitoi majibu yote], basi bado tuna nafasi. Kesho Khalifa utakuja [kuandika]. Kuna angles [pembe]  chungu nzima za kuandika kuhusu mapinduzi, lakini nikasema huyu mwanamke jamani  lazima asikike, na nadhani ile kujua yupo hai ndio ilinipa chachu nikasema bora sasa hivi. Kwa hiyo, kama mtu ana lake bora aseme. 

Ndio kama nilivyosema awali nimejitahidi kuzungumza na watu tofauti na kusoma vitabu mbalimbali mpaka nijiridhishe. Kuna kitu kingine ninachoona sijaridhishwa nacho sikiandiki sababu najua hata mimi nikihojiwa baadae nitashindwa kukitetea.  Kwa hiyo, lazima nijiridhishe sababu najua hata kama huyu akinipiga hapa  najua kujitetea kuwa kadha wa kadha wa kadha, watu watatu hapa wamezungumza, sasa kama hamuwezi kuamini watu watatu sasa basi tena. 

Kwa hiyo, nikasema mi nijitahidi nifanye wajibu wangu na hasa sasa kilipokuwa tayari nikasema, bismillah, sasa hapa nijiandae. Na ni kweli tulipoanza matangazo tu kidogo watu wakaanza, lakini nilikuwa nimejiandaa kisaikolojia. 

The Chanzo: Upo uwezekano kwamba watu wako wa karibu ambao walikushauri usiendelee? Kuna uwezekano ilitokea kwa watu wako wa karibu, si kwa sababu hawaoni umuhimu wa unachotaka kukifanya, lakini kwa sababu ya huo mgongano wa kimawazo uliopo kuhusu mapinduzi, wakakwambia Zuhura usifanye, upo huo uwezekano?

Zuhura Yunus: Kwanza, [watu wangu] wengi niliwaficha kwa sababu unajua mimi pia nimetoka Zanzibar, kwa hiyo nilikuwa sina uhakika wataichukulia vipi. Kwa hiyo, wengi walikuwa hawajui kama nilikuwa naandika. Baadhi niliwaambia na sikutaka mjadala kwamba naandika kuhusu Biubwa Amour Zahor. Mtu wa kwanza kumwambia ni mama yangu, Mungu amrehemu. Nilivyo mwambia tu aliniunga mkono moja kwa moja. Yeye ndio kwanza alinambia zungumza na fulani, zungumza na fulani.

The Chanzo: Yeye anafahamu eeh?

Zuhura Yunus: Yeye anafahamu. Kwa hiyo, hakunibishia kabisa. 

The Chanzo: Samahani ndugu mfuatiliaji wa The Chanzo, yawezekana tunachanganya [lahaja za] Kiunguja na Kipemba. Kufahamu tunamaanisha kuelewa. [Kicheko].

Zuhura Yunus: Kwa hiyo, [mama yangu] hakuwa na tabu.  Sasa na mimi ushajua nikishapata radhi ya mzazi wangu basi, mwingine hata akiwa na wasiwasi hainishghulishi. Nakumbuka mmoja tu kwenye familia, najua hakumbuki, lakini nilivyo mwambia akanambia aah unataka kumwandika Biubwa? Kama hivyo. 

Nikamwambia nataka kuandika, akanambia unajua Biubwa alifanya nini wewe? Nikamwambia ndio tutajua sasa ukweli huu ndio wakati. Mmoja tu ndio alibisha lakini kwa ujumla wake na hata baada ya uzinduzi, [huko] Unguja nusu ya familia yangu ilikuwepo kwenye shughuli [ya uzinduzi]. Kwa hiyo, wameridhia. Hawana tabu. 

The Chanzo: Uligusia utata wa muhusika mkuu wa hiki kitabu Biubwa Amour Zahor, labda kwa kumuibia tu mfuatiliaji wa The Chanzo ni kwamba Biubwa alihusishwa na mauaji ya baba yake, kitu ambacho yeye anakanusha. Na kuna watu umezungumza nao kwenye kitabu chako wamethibitisha hilo jambo hakulifanya yeye. Sasa nataka kufahamu hiki kitabu kimeandikwa kumfutia Biubwa hatia au lawama au ni kitabu kilichoandikwa kusimulia tu kuhusu Biubwa ambapo mpaka kinachapwa hiki kitabu wengi tulikuwa hatujui [upande wake wa hadithi]?

Zuhura Yunus: Lengo hasa ni kusimulia. Kwa sababu, mimi nilipoanza kuzungumza naye, mimi sio wa rika lake, ni mtu mzima, kwa hiyo kuna mambo mengi nilikuwa siyajui. Lakini hiko kipande kwamba alihusika na kumuua baba yake, wewe mwenyewe unajua mwandishi wa habari kuna vitu ukivisikia masikio yako yanasema eeh huyu? Kwa hiyo, nikasema huyu atakuwa na historia nzuri. 

Hapo mimi sijui kama ni kweli au la! Lakini mimi nimesikia kama watu walivyokuwa wanazungumza. Kwa hiyo, hata mimi pale nilivyokuwa naenda nikasema ala! Kumbe huyu kahusika [katika mauaji ya baba yake]? Kama kahusika kweli, kwa nini na ilikuaje, ushafahamu eeh? Kwa hiyo, mimi nimekwenda pale sijui kama atasema kweli au si kweli. Unaweza ukaona jinsi gani nilivyokuwa nababaika kuuliza hilo jambo, maana sio jambo rahisi kumuua mzazi wako. 

Kwa hiyo, nataka kuuliza nababaika babaika lakini mwisho tukafika. Kwa hiyo, mimi haikuwa kazi yangu kumsafisha mtu, unapoandika historia unaandika ule ukweli. Na ndio maana ningetaka kusafisha ningetumia kauli yake tu, nikasema nimeamini alichokisema basi. Lakini pamoja nikasema nimezungumza naye kwa nini watu wengi wanahisi hivyo, nikasema hebu niwasikilize na wengine wanasemaje.

Wao wana ushahidi gani? Kwa sababu  unaweza kukuta mtu aliyekuwepo wakati huo akatoa kauli tofauti, akasema si kweli kwamba  huyu mtu  [Biubwa] alikuwa hayupo akasema alikuwepo, lakini kila niliyezungumza naye anashindwa kusema alikuwepo wapi hasa siku ya mapinduzi. Mmoja, kama ulisoma [kitabu] kwa makini, anasema alikuja baada ya siku tatu,  siku tatu baada ya mapinduzi. 

Kwa hiyo, utaona kabisa nimetumia watu watatu au wanne, halafu mwenyewe msomaji ataangalia lipi la kuamini na lipi sio la kuamini. Lakini mimi nikasema kama mwandishi nijitahidi nizungumze na watu mbalimbali. Kwa hiyo, haikuwa kumsafisha mtu ila tu kusema ukweli.

The Chanzo: Sawa, kwa hiyo lengo la kitabu sio kumaliza mjadala unaoendelea kama Biubwa alimuua baba yake au la? 

Zuhura Yunus: Hapana.

The Chanzo: Kwenye kile kitabu, nadhani ukurasa wa 33, kuna picha umeweka pale ambayo unamuonesha Biubwa pamoja na Fatma Karume ambaye alikuwa mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume. Ukiangalia ile picha takribani wote ukiangalia walikuwa hawajavaa Hijab, hawakujifunika.  

Mbele pia kwenye kitabu chako pia, nadhani kwenye ukurasa wa 63, umegusia kuwa Zanzibar ya wakati huo watu walikuwa wanavaa mpaka vimini, kitu ambacho unakiri siyo sana siku hizi. Kwa sababu wewe umefanya tafiti, umejisomea wakati wa kuandika hiki kitabu, na pengine nilikuwa nawaza  kama unaweza kutueleza haya mabadiliko yamechochewa na nini? 

Na hili watu wengi wanajiuliza, ukiangalia picha za watu za zamani Zanzibar walikuwa hawavai Hijab hata ukiangalia picha za Biubwa mwenyewe, kama kwenye ile picha maarufu, kama vile hajavaa hijab na hiyo ni miaka ya 1970, 1960. Nini kilitokea hapa katikati katika kujisomea kwako umeona?

Zuhura Yunus: Hilo nadhani inaweza kuwa hadithi nyingine tofauti na inahitaji utafiti wa kutosha. Lakini nadhani watu wakisikia Zanzibar na kwa sababu ina Waislamu wengi hata familia zetu ambazo wametoka kwenye Usheikh hawakuwa wanalazimisha mtoto wa kike kuvaa [hijab], lakini wanaelimisha umuhimu wake. 

Nadhani walikuwa na uhuru wa kuchagua kuvaa au kutovaa. Sina uhakika kitu gani kimetokea badae lakini Unguja nadhani ilitokea badae shuleni lazima wavae kama hivyo. Kama unavyosema zamani wazee wetu, picha kama unavyoziona, wanajirusha. Ukiwauliza wakati mwingine wanakwambia wanaume wa zamani sio kama wa sasa, kwamba walikuwa salama wanaume wa zamani. Lakini nasema, mmh, walikuwa na tofauti gani [Kicheko]. Hawana tofauti yoyote. 

The Chanzo: Ni kitu ambacho nataka sana kufahamu, nini kilitokea?

Zuhura Yunus: Ni kweli, maana picha nyingi kabla na hata baada ya mapinduzi. Lakini hata kabla ya mapinduzi utaona wamevaa picha ya mabaibui ya kizee.

The Chanzo: Mabaibui ya kizee yapo, watu walikuwa wakivaa. 

Zuhura Yunus: Lakini nadhani walikuwa na uhuru. Ambaye anataka kuvaa baibui la kizee anavaa, asiyetakai havai. Kwa hiyo, kama unavyosema baadae kitu kilitokea kila mmoja alitaka ajifunike. Nadhani dini iliingia ikaweka msisitizo, na hakuna ubaya kuvaa hijab.

The Chanzo: Ooh hapana, simaanishi ni vibaya kuvaa hijab, usije niletea matatizo [Kicheko].

Zuhura Yunus: Lakini uhuru upo, sio kwamba huwezi kuingia Zanzibar bila ya kuvaa baibui. 

The Chanzo: Kitu kingine, ni katika kujiuliza maswali, na wakati nasoma kitabu chako nilikutana nacho. Kwa mfano, baba yake Biubwa, Amour Zahor, alikuwa mwarabu, wazungu wanasema pure [halisi] Maana kuna Waarabu wengine.. [Kicheko].

Zuhura Yunus: Kama sisi wa kuapa [kicheko]. Utani tu!

The Chanzo: Kwa hiyo, alikuwa mwarabu haswa [Amour Zahor] lakini alifikia mpaka hadhi ya kuwa Inspekta wa Polisi, lakini hicho kitu kwa sahizi ni nadra kukiona kwa Tanzania yetu na Zanzibar. Achilia mbali Inspekta, hata askari tu wa kawaida kumuona ambaye ni mwarabu kwa mfano, au muhindi, hiyo unaizungumziaje?

Zuhura Yunus: Nadhani wewe umelifikiria lakini mimi hata sikuliwaza. Kwa sababu, ukiangalia Zanzibar ya zamani ilikuwa ni mchanganyiko sana, kwa hiyo hata hiyo tunavyoambiwa Waarabu ndio walikuwa wanatawala sio Waarabu wote walikuwa na damu ya Kisultani, na sio Waarabu wote walikuwa wanaishi kwenye maeneo ya hadhi ya juu.

Kwa hiyo, wapo Waarabu waliokuwa wanaishi maeneo ya kawaida, wana hali za kawaida unajua eeh? Kwa hiyo, wamejichanganya sana. Kwa hiyo, nadhani ilikuwa ni kawaida, kwa hisia zangu, na kwa huo utafiti mdogo ambao nimeufanya kuona na wao wapo katika kazi tofauti. Labda sio wengi ambao walikuwa wanapenda kuingia kwenye masuala hayo ya upolisi lakini baadhi, na unajua wengi walikuwa wanapenda biashara zaidi, na hata Wahindi unakuta wao nadhani wanapenda biashara zaidi. 

The Chanzo: Kwa hiyo, hudhani kwamba kuna sera mahususi ya kuzuia watu hao wasiingie [kwenye polisi]?

Zuhura Yunus: Mbona sasa Amour Zahor alikuwepo?

The Chanzo: Namaanisha kwa sasa au baada ya mapinduzi, sera mahsusi kwa upande wa mamlaka yenyewe au jamii yenyewe ya Waarabu na Wahindi kujitenga?

Zuhura Yunus: Labda kwa sababu baada ya mapinduzi wengi wanasema kama hivyo [Waarabu] waliuawa, wengi walikimbia.  Labda vizazi vyao havikuwa na hamu ya kuingia katika masuala kama hayo ya upolisi na kadhalika. Labda hiyo inaweza kuwa sababu, sababu wengi walikimbia, walikimbilia Omani na vitu kama hivyo. Wachache waliobaki hawakuwa na hamu tena na baada ya mapinduzi ili waathiri watu fulani zaidi. 

The Chanzo: Mimi binafsi nitaendelea kutafiti nini kilitokea sababu hata hapa Tanzania Bara, hapo zamani kulikuwa mpaka na Makamanda wa Jeshi wenye asili ya Asia lakini hiyo baadae ikatoweka.

Kule mwanzo [wa mahojiano] uligusia masuala ya kwa nini mtu asome hiki kitabu, moja ya kitu ulichogusia kwa nini mtu asome kitabu uligusia masuala ya udhalilishaji wa kijinsia. Kuna kitu kimoja mimi naona kinaendana na mazingira yetu hapa, kwamba Biubwa licha ya kwamba alibeba ujauzito, aliolewa kabisa lakini hiyo haikumfanya asiendelee na masomo, na hiki wewe umekizungumza kwenye kitabu chako kwamba hilo lilikuwa linawezekana zamani lakini kwenye Tanzania yetu ya sasa hilo ni jambo ambalo linaonekana kama ni la ajabu, ni kitu ambacho hakiwezekani. Hayo mabadiliko yana kushangaza kama mwanamke au kama mtu unayefuatilia mambo?

Zuhura Yunus: Ni kweli kama unavyosema, kwa sababu wakati nafanya utafiti nilikuwa sijui kwamba zamani ulikuwa unaweza kuolewa na unaendelea na skuli [shule], kwa sheria ya Zanzibar ilikuwa unaolewa, unaweza kuwa kidato cha pili umeolewa na skuli unaendelea. Kwa hiyo, nikasema mi nilikuwa sijui hilo suala ndio maana nikalibebea bango hilo. Nikasema hili muhimu sababu kama mimi nimeshangaa  basi watu wengi watakuwa wameshangaa. Ndio nikajiuliza kama iliwezekana zamani, kwa nini isiwezekane hadi sasa? Mashallah, kuna watu wanavichwa,  anaweza kuolewa na kuendelea na masomo!

The Chanzo: Kama Biubwa!

Zuhura Yunus: Kama Biubwa, si unaona? Amepata ujauzito, ameolewa na akaendelea na masomo yake kama kawaida. Kwa hiyo nikajiuliza … 

The Chanzo: Na huko mbele Biubwa mwenye akaamua kuacha shule si kwa sababu ya kufeli bali kwa sababu ya utata wake.

Zuhura Yunus: Aliendelea mpaka alimaliza kidato cha nne. Ujue zamani [Zanzibar] kulikuwa hakuna kidato cha tano na sita. Alimaliza kabisa, na ujauzito wake akajifungua, akamaliza na akafaulu. Sasa sijui kitu gani na sheria gani badae zikaja, na sijui nani akaja wakabadilisha wakazuia na mpaka unaona siku hizi mtu akipata ujauzito inakuwa ni mtihani, lakini inawezekana labda hizo sera tu wabadilishe. 

The Chanzo: Labda pia watunga sera wanahitaji kusoma hiki kitabu [kicheko].

Zuhura Yunus: Labda watajua zamani kwani ilikuaje. Nadhani muhimu kama mumeo anakupa rukhsa, najua sio wote wanaweza kuunga mkono akuoe halafu ukasome.

The Chanzo:  Lakini kwenye kitabu chako imeandikwa unasainishwa, Serikali inakusainisha mume mkataba kwamba huyu mwanamke anatakiwa kuendelea kusoma.

Zuhura Yunus: Na hiyo kama sikosei  ilikuwa ni baada ya mapinduzi. Walisema  kama una mruhusu unasainishwa [makataba] kabisa. Kwa hiyo, kuna mambo mazuri, kulikuwa na sera nzuri zamani. 

The Chanzo: Sasa huo si ndio USONGA [falsafa ya Afrika songambele]  wenyewe?

Zuhura Yunus: Aaah USONGA wenyewe [kicheko]. Sasa sijui nani kabadilisha, sijui kabisa!

The Chanzo: Unajua mimi picha ninayoipata, miaka sitini [baada ya mapinduzi] ni kama tumerudi nyuma fulani kwenye baadhi ya mambo. Mfano, kama  vyombo vyetu au serikali kuwa mchanganyiko, kuna hili suala pia la watoto wanaosoma shule kulazimishwa kuacha shule kuendelea na masomo kwenye mfumo rasmi kwa sababu amepata ujauzito, ni kama vile tumerudi nyuma kidogo, unakubaliana na mimi?

Zuhura Yunus: Nakubali ndio. Kwa sababu, kama iliwahi kufanyika na watu wakaendelea kabisa, na mfano ni Biubwa  ameolewa kidato cha pili kama sikosei, akajifungua na akaendelea na shule mpaka akamaliza. Kwa hiyo, unaweza kukuta watoto wakike wangapi wanakosa hiyo fursa? Na kama imefanyika humu humu nchini Tanzania, visiwani Zanzibar sheria hiyo hiyo ni kitu gani kinachotushinda tusiweze kukaa chini na tukasema jamani  miaka ya sitini mbona watu wengi waliolewa, walijifungua, wakaweza kusoma, kitu gani kinatuzuia kwa sasa, na ukiangalia watu wa zamani, mashallah, elimu yao nzuri sana. 

Ukiwatizama wazee wa zamani wana elimu nzuri sana, wanawake na wanaume tofauti na sisi. Hata lugha, wakizungumza Kiswahili au Kiingereza, kina hadhi fulani unadhani labda huyu mtu ana shahada mbili au hata tatu. Lakini hapana, kasoma zake mpaka kidato cha nne tu, [lakini walikuwa na] walimu wazuri na elimu nzuri. Na inavyoonekana walimu walikuwa wana waunga mkono watoto. Yaani walikuwa wanataka mtoto asome mpaka afaulu, tofauti na ukisikia taarifa zingine za wanafunzi siku hizi, na hata sisi wengine tumepita vyuo na nini unakuta mwalimu anakazana lazima mtoto ufeli. Lakini ukiangalia zamani unahisi mtoto anasaidiwa mpaka afaulu. Kwa hiyo, nadhani ni kitu muhimu sana.

The Chanzo: Sidhani kama watu wengi wanafahamu, Zanzibar hilo wamefanikiwa labda kwa sababu waliwahi kutekeleza hilo zamani. Walibadilisha hiyo sera  mtoto akipata ujauzito haruhusiwi, kwa hiyo kwa Zanzibar mtoto akipata ujauzito atajifungua halafu atarudi shule.

Zuhura Yunus: Zanzibar wao pia hata mtihani wa kidato cha pili [mtihani wa upimaji] hata kama umeanguka unaambiwa uendelee, unasogea  hadi kidato cha nne, kuna sera kwamba kila mtoto hadi afike kidato cha nne, ushafahamu? Kwa hiyo, kuna tofauti kidogo.

The Chanzo: Asante sana, tukirudi kwenye kitabu, kwa Kiswahili sijui nasemaje dramatic.

Zuhura Yunus: Kizaazaa, kashikashi, kitahanani  eeh [kicheko].

The Chanzo: Nitaenda na kitahanani [kicheko]. Na nimeona huku mbele ya kitabu chako umetafsiri neno kitahanani.

Zuhura Yunus: Eeh, maana nilijua watu wanaweza wasifahamu.

The Chanzo: Sasa moja ya kitahanani kikubwa au kizuri kinachoonekana kwenye hiki kitabu ni hatua ya familia ya Biubwa kumtenga kwa sababu ya uamuzi wake binafsi wa kuolewa na mtu Mweusi, bwana Hassani Kingwaba.

Zuhura Yunus: Dk Kingwaba.

The Chanzo: Ndio, Dk Kingwaba, hili labda Zanzibar limebadilika kwa kiasi gani?

Zuhura Yunus: Eeeh? Unanikwaza [kicheko]. Limebadilika kiasi fulani. Lakini unajua bado huo mtihani upo, ukisikia mtu kaolewa utasikia kaolewa na [mtu] wa [Tanzania] Bara huko. Kwa hiyo, bado ipo lakini mimi nadhani imebalika kwa kiwango kikubwa sana kwa sababu kuna ndoa nyingi sasa unaona za mchanganyiko wa bara na visiwani. 

Japo nadhani kwa wakati ule lilikuwa jambo zito, kusema ukweli lilionekana ni jambo la ajabu lilikuwa halijazoeleka. Lakini kadiri miaka inavyokwenda utaona  kwamba watoto wengi, vizazi vyetu sisi wapo wengi waliozaliwa na wazazi mchanganyiko Zanzibar. Bado ipo kidogo, bado haijazoeleka kuna utata kidogo. Nadhani mtu anakuwa anapendelea aolewe na Mzanzibari mwenzie lakini ikitokea sio wagumu kama ilivyokuwa zamani. Kwa sababu ukisikia stori za zamani nyingi inakuwa mtihani sana kuolewa [na mtu kutoka Bara].

The Chanzo: Wanaita intermarriage, yaani watu Weusi na Waarabu kuoana.

Zuhura Yunus: Kidogo ilikuwa mtihani sana, lakini nadhani siku hizi sio kama zamani.

The Chanzo: Ni kweli ni tofauti, mimi natoka Zanzibar pia.

Zuhura Yunus: Unajua, ikitokea unasikia [wanasema] kaleta mbara tena. 

The Chanzo: Lakini baada ya muda inaanza kuondoka. 

Zuhura Yunus: Lakini sio vibaya muda mwingine wazazi wanakuwa na wasiwasi kwa sababu kuna mila fulani za Kizanzibari mzazi anasema huyu ataweza kweli kwa sababu hajui huku bara, na unajua mwingine  hawajafika bara hata siku moja anahisi eeh Mtume bara kuna mambo gani tena. Lakini mambo yamebadilika sana.

The Chanzo: Ukisoma hiki kitabu chako inaonekana unatumia sana lahaja ya [Kiswahili cha] Kizanzibari. Kwa mfano, kuna matumizi makubwa ya neno skuli badala ya shule. Kuna maneno mengi, maneno kama muhali. Huu ulikuwa uamuzi makusudi wa kutaka kuandika kitabu chako kwa Kiswahili kinacho zungumzwa Zanzibar?

Zuhura Yunus: Kuna mawili. Moja nimeandika kama mimi ninavyo zungumza. Kwa mfano, neno muhali, mimi ninalitumia kwa sababu ya jinsi nilivyo lelewa na nilivyo kuzwa. Kwa hiyo, nimekuzwa katika maneno hayo.

The Chanzo: Kwa hiyo muhali ina maana yake huku inabidi nimsomee mfuatiliaji wa mahojiano haya. Kuna kitahanani, kuna aila, na muhali ikamaanisha kuona tabu. 

Zuhura Yunus: Mara nyingi sana linatumika na watu wa Pwani [maana ndiyo watu wenye] muhali sana. Mtu anashindwa kumkatalia mtu kitu, hebu nibebe huo mzigo sasa unashindwa kukataa [unasema] naona muhali, acha tu nimbebee. Kwa hiyo, kuna maneno mengi ambayo mimi katika maisha yangu ya kila siku natumia. 

Lakini yapo mawili matatu, kweli, kwa mfano, mimi natumia shule lakini watu niliokuwa nazungumza nao walikuwa wanapendelea zaidi kutumia skuli na inaeleweka. Kwa hiyo, nikatumia skuli. Lakini machache sana nimeyaweka tu kwa sababu naandika historia ya Zanzibar, lakini mengi kusema kweli mfano kuna neno kama kufurutu ada. Sisi kwetu tunasema [mtu  anayefanya jambo kuliko kawaida] kafurutu ada. Nilikuwa najiuliza hili nikilitumia kwa [wasomi] wa Bara [wataelewa] sasa? 

Na hata kutafsiri ilinichukua muda kueleza kufurutu ada ni kitu gani [kwenye Kiswahili fasaha]. Lakini ni kitu cha kawaida ndio maana kuna watu wengine wananiambia jinsi ulivyoandika ni kama nakuona unavyo zungumza. Kwa hiyo, hivyo ndivyo ninavyo zungumza mimi. Nikasema watajua huko huko, ndio watajifunza!

The Chanzo: Zuhura mimi nakushukuru sana, unajua nina maswali mengi. 

Zuhura Yunus: Nakuona [kicheko].

The Chanzo: Nina maswali mengi dada yangu lakini mimi sitaki kukuchosa ili siku nyingine unikatalie. 

Zuhura Yunus: Siwezi.

The Chanzo: Kwa hiyo, mimi nakushukuru sana kwa kutenga muda na kuweza kuzungumza na sisi kuhusu kitabu chako ulichokiandika. Ndugu mfuatiliaji wa The Chanzo, kama tulivyosema hapo mwanzo hiki kitabu kinapatikana Dar es Salaam na maeneo mengine. Labda pia katika kutumia fursa hii mwandishi atueleze tukitaka kupata kitabu hiki tunakipataje?

Zuhura Yunus: Kwa hapa Dar [es Salaam], ujue tuna orodha ya wauzaji ambayo tunairusha kwenye mitandao ya kijamii, kuna TPH, vipo Dodoma, Mwanza, vipo Unguja na sikumbuki mkoa gani lakini kuna namba za simu kwenye hilo tangazo la mitandao ya kijamii. Vile vile kitakuwepo pia Amazon kwa wale waliopo ughaibuni. 

The Chanzo: Au pia unaweza ukatuandikia sisi The Chanzo kupitia editor@thechanzo.com, sisi tutakusaidia, tutaongea na Zuhura tuone kwa namna gani anaweza kukusaidia kupata hiki kitabu.  Labda unafikiria kuandika kitabu kingine? Maana kuna kunogewa?

Zuhura Yunus: Khalifa niko hoi bin taabani [kicheko], sahizi mtu akinambia kuandika kitabu kingine kichwa kinawaka moto. Lakini nadhani kuna umuhimu, ngoja nikusanye nguvu tena maana kuna wanawake chungu nzima ambao hawajaandikwa, na labda kwa sababu sahizi nimepata uzoefu kidogo labda hicho hakitanichukua muda mrefu sana kama cha mwanzo. Lakini muda mwingine kama mtu hana shauku kinaweza kikamchukua muda mrefu zaidi kuliko mtu ambaye ana shauku. 

Kwa hiyo, sijui lakini kwa sasa nimesema hebu nipumue kidogo lakini baadae inshallah. Umuhimu upo na nimekuwa nikiwaambia wenzangu nyie na wazee waliokuwepo kwenye maeneo mbalimbali, kila mzazi ni muhimu ila sio kila mzazi anaweza kuandikwa historia yake, lakini kama una wazee unawajua waulize tu unaandika pembeni kisha hifadhi. 

Tunaweza tukakusanyika baadae wenyewe tukaandika hadithi na vitabu chungu nzima za wazee wetu. Hawa wazee wana habari na wala tusidharau. Hawa wanawake wana mambo mengi ambayo hatuyajui na hata hao waume zao hawayakumbuki. Kwa hiyo, mimi nawaambia andika tu pembeni hata mimi nilikuwa sijui kuandika kitabu lakini kidogo kidogo mpaka nimeandika. Hata wewe Khalifa, kwanza we mzuri kwenye kuandika hautapata tabu kama mimi. 

The Chanzo: Inshallah! Mungu ataleta wepesi.

Zuhura Yunus: Amina!

Na Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved