The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tutathmini Ufanisi wa Radio Zetu Katika Kuhabarisha, Kuelimisha Umma

Wakati redio zimeendelea kubaki kuwa njia imara zaidi za kuwapasha habari Watanzania, maudhui yanayozalishwa na baadhi ya radio zetu yanaacha maswali mengi. 

subscribe to our newsletter!

Tangu kituo cha kwanza cha radio, KDKA cha Pittsburgh, Pennsylvania huko Marekani kilipoanzishwa mwaka 1920, teknolojia hii ya upashanaji habari imeendelea kubaki kuwa muhimu, licha ya ujio wa teknolojia kadhaa mpya zikiwemo televisheni na intaneti.

Hapa Tanzania, baada ya uhuru, kipindi cha siasa za Ujamaa, radio ilitumika kama chombo muhimu cha kuelimisha wananchi. Mabadiliko ya mfumo wa kisiasa na kiuchumi kuanzia miaka ya katikati ya 1980 yaligusa pia uhuru wa vyombo vya habari ambapo kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 90, vituo binafsi vya radio na pia televisheni vilianzishwa na kuongezeka maradufu.

Hivi sasa, kuna takriban radio 200 nchi nzima, lakini ongezeko hilo linaibua mambo mengi ya kujadili kuhusu ubora wa maudhui. Makala hii inatathmini utendaji na ufanisi wa radio nchini Tanzania, ikiangazia aina mpya za watangazaji na mitindo ya utangazaji na namna inavyoathiri ubora wa maudhui.

Msingi wa maendeleo

Mnamo Machi 16, 1965, Waziri wa wakati huo wa Habari na Utalii, Idris AbdulWakil alisema wakati akilihutubia Bunge: “Radio ni msingi wa maendeleo ya nchi. Tanzania, ambako watu wengi hawajui kusoma au kuelewa yanayotokea nchini mwao, ni radio pekee ndio inaweza kuelimimisha watu wote…”

Miaka zaidi 50 baadae, sababu nyingi zinafanya teknolojia ya radio iendelee kuwa muhimu. Kwanza, kaya nyingi maskini ambao ndio Watanzania wengi, zinaweza kumudu kununua na kumiliki radio.

Radio nyingi hasa za masafa ya FM, zinapatikana hata kwenye simu za kitochi. Hii maana yake ni kuwa unaweza kwa urahisi kabisa kusikiliza ukiwa popote.

Ukifanya ulinganishi wa radio na vyombo vingine, utaona kuwa televisheni ni ghali na pia ina malipo ya kila mwezi. Kwa upande wa gazeti, kununua nakala kila siku pia unahitaji fedha. Hata mitandao nayo lazima uwe na kifaa wezeshi na ulipie vifurushi. Hoja hizi zote zinaonesha kuwa radio ni chombo mujarrabu kwa kuleta mageuzi ya kifikra katika jamii au vinginevyo.

Radio ni chombo kinachoruhusu watu kuendelea na kazi zao wakati pia wakisikiliza radio ukilinganisha na, mathalan, televisheni ambayo inahitaji sio tu usikivu wako bali pia macho kuzingatia picha. Kama televisheni, gazeti pia linahitaji uweke akili yote katika kusoma, kama ilivyo pia kwa mitandao ya kijamii.

Waandaaji wa vipindi na watangazaji wa radio pia wameweza kuchukua maudhui ya vyombo vingine  kama televisheni, mitandao ya kijamii na magazeti na kuyawasilisha kwa wasikilizaji waliobanwa na shughuli wanaotaka taarifa ya kusimuliwa kwa ufupi na haraka au wale ambao hawana uwezo wa kumudu hivyo vyombo vingine.

Ushawishi wa watangazaji

Sababu hizo zote zinafanya vituo vya radio na watangazaji wake kuwa na ushawishi mkubwa katika jamii.

Ushawishi wa radio si nadharia tu bali unathibitika kiuhalisia. Watangazaji wa radio tatu zinazoongoza kwa kusikilizwa: Clouds FM, EFM na Wasafi FM ni miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii, hasa miongoni mwa vijana.

Lily Ommy, Geah Habibu, B12, Adam Mchomvu, Meena Ally – Hawa ni baadhi ya watangazaji waliojipatia umaarufu kutoka kwenye radio.

Radio ni biashara za watu lakini pia zina wajibu mkubwa kwa jamii katika kuchochea maendeleo na ustawi wa umma. Hii ina maana, kwa nchi maskini kama Tanzania, yenye changamoto lukuki za kisiasa, kiuchumi na kijamii, ni muhimu sana tuwe na maudhui yanayoweza kuisaidia jamii kutoka hapa tulipo.

Hata hivyo, maudhui ya baadhi ya radio zetu yanaacha maswali mengi.

Uwiano kati ya kuburudisha na kuelimisha

Kwanza, radio, kama vyombo vingine vyote vya habari, zina kazi ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii, lakini lazima kuwe na uwiano mzuri wa majukumu hayo matatu.

Tatizo ninaloliona ni kuwa radio zetu sio tu zimejikita zaidi katika kuburudisha kuliko kuhabarisha na kuelimisha lakini pia hata vile vipindi vya habari na elimu vimejaa mizaha na wakati mwingine hata upotoshaji.

Tatizo linaanza katika sera ya uajiri wa watendaji wa radio hizi. Katika soko gumu la ushindani wa kuvutia wasikilizaji, radio zinahama kwenye kuajiri waandishi weledi na kuona umuhimu wa kuwa na watangazaji ambao tayari wana majina na umaarufu mkubwa huko katika mitandao ya kijamii na ambao watavutia wasikilizaji.

Hata hivyo, aina hiyo ya watangazaji hawafahamu kanuni za  kiweledi wa fani ya habari na wala hawana ufahamu wa masuala mbalimbali ya kinchi kiuchumi, kisiasa na kijmaii.

Hii si ajabu kwa sababu hawa ni watangazaji waliopata umarufu kwenye mambo ya hovyo kama ulevi, upambe (uchawa), uropokaji, misemo ya vichekesho na kadhalika.  Matokeo yake tunaona watangazaji walioteuliwa kutokana na uwezo wao wa kufanya mizaha, kuropoka, ulevi, tabia za uchawa na kadhalika.

Ucheshi usiwe sifa pekee ya utangazaji

Ni asili ya binadamu kupenda kucheka, mizaha, utani, kwa hiyo habari au elimu iliyowasilishwa kwa ucheshi ni rahisi zaidi kuteka watu. Lakini, haipendezi ucheshi iwe ndio sifa pekee ya watangazaji wanaoajiriwa, hata kama ni wazi kuwa hawana weledi katika utangazaji na hawajui maadili ya fani hiyo.

Katika mtindo wa uwasilishaji huru kupitia mijadala, unaona kabisa majopo ya watangazaji yanapwaya mno – hawajui mambo ya msingi kabisa kuhusu siasa za nchi, uchumi na jamii.

Katika fani hizi za habari inasemwa kuwa moja kati ya sifa za waandishi bora wawe na uelewa wa kiwango cha msingi (tunaita A, B, C ) za mambo mengi.

Ni aibu kuwa na watangazaji ambao hawajui mambo ya msingi kuhusu historia ya nchi yao, mfumo wa siasa, utawala na uchumi. Kikubwa wanachojua ni miziki – na hata hiyo miziki hawaifahamu kwa upana wake.

Mtangazaji ni mwalimu mkubwa kuliko walimu wote wanaofundisha kwenye madarasa rasmi kuanzia chekechea, shule ya msingi, shule ya sekondari, vyuo na kadhalika. Yeye anasikilizwa na mamilioni ya watu.

Hivyo, taarifa zisizo sahihi zinapotosha watu hao wote wanaosikiliza, ambao nao wanaenda kuhadithia wenzao!

Ukiacha taarifa zisizo sahihi zinazopotosha ukweli uliowazi, vyombo vya habari vinatengeneza ajenda katika jamii. Nadharia ya utengenezaji ajenda inasema vyombo vya habari vinaweza visiwe na uwezo wa kumshawishi mtu afikiri vipi kuhusu jambo, lakini vinao uwezo wa kuwashawishi watu wafikiri kuhusu nini. Yale mambo yaliyopewa kipaumbele ndio yataacha athari kwa msikilizaji na kumfanya ayafikirie.

Umbea na mizaha mingi

Hamna ubishi kuwa vipindi vingi vya redio vimejikita kwenye miziki, lakini hata vile vipindi visivyokuwa vya miziki moja kwa moja, mambo makini na mazito yanajadiliwa kutoka kwenye mtazamo wa umbea, mizaha na wakati mwingine kwa kuangazia maisha binafsi ya wanaoitwa ‘mastaa.’ Watangazaji wetu ndio hao machawa wa wasanii na watu matajiri, kwa ufupi wamenunuliwa.

Ni muhimu Watanzania tujifunze kutoka jirani zetu. Uganda, kwa mfano, kupitia vipindi maarufu vya midahalo vijulikanavyo kama vibemeeza (meza ya duara) radio za huko zilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuifanya nchi izungumze na kujadili mambo muhimu ya kitaifa.

Vipindi hivi vilianza 2001 kwenye Radio One ya nchini humo kisha vikaigwa kwenye vituo vituo vingine. Katika makala iliyoandikwa na Stephen Otage katika gazeti la Serikali la New Vision,  mwandishi ananukuu wasomi mbalimbali wakikiri kuwa vipindi hivyo vilikuza uelewa na kuwajenga Waganda kuwa raia  wenye mwamko mkubwa kisiasa.

Kuna msemo wa wataalamu wa TEHAMA usemao Garbage in, garbage out. Yaani ukiingiza kwenye kikokotozi takwimu zisizo sahihi majibu pia huja siyo. Tusitegemee kuulisha umma mambo ya kipuuzi halafu tutegemee kuwa na kizazi makini, chenye ufahamu wa mambo ya siasa za nchi zao, chenye kufanya tafakuri tunduizi na kujihusisha kikamilifu katika masuala yanayoamua mustakbali wa nchi yao.

Njonjo Mfaume ni Mhadhiri wa Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *