The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Miaka 45 ya CCM: Mapungufu Makuu ya Chama Hicho Tawala Tanzania

Kitendo cha CCM kukwepa kuongelea mapungufu yake limekuwa ni moja ya sababu kuu zinazosababishwa na kutokuwepo kwa jitihada za makusudi kurekebisha maeneo mbalimbali yanayolalamikiwa kuhusu chama hicho.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Februari 5, 2022, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetimiza miaka 45 tangu kianzishwe. Chama hicho kiliadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwake mkoani Mara ambako Mwenyekiti wake wa taifa, Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi.

Kwa vile takriban wiki nzima kabla ya sikukuu hiyo viongozi na wanachama wa CCM wamekuwa “wakipita huku na kule” kujigamba kuhusu mafanikio ya chama chao kwa Tanzania yetu, makala hii haitojihusisha na mafanikio hayo bali mapungufu pekee.

Kwa upande mmoja, hakuna tija katika kurudia kauli zilezile za viongozi na wanachama wa chama hicho tawala kuhusu mafaniko ya chama chao. Kwa upande mwingine, viongozi na wanachama hao wamekwepa kwa makusudi kuongelea mapungufu lukuki ya chama hicho.

Na hili la kukwepa kuongelea mapungufu ya CCM limekuwa ni moja ya sababu kuu zinazosababishwa na kutokuwepo kwa jitihada za makusudi kurekebisha maeneo mbalimbali yanayolalamikiwa kuhusu chama hicho.

Lakini hilo sio tatizo la chama hicho pekee, kwani kama nilivyoeleza kwenye makala yangu nyingine iliyochapwa kwenye safu hii hii, hata wapinzani wao, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nacho kimekumbwa na kasoro hiyo.

Kama ilivyo kwa CCM, habari pekee zinazoruhusiwa kuhusiana na chama hicho kikongwe cha upinzani ni zile “nzuri tu” au zinazoendana na matakwa ya viongozi au wanachama wa chama hicho. Kinyume na hapo, matusi ni halali kwa “wenye chama” dhidi ya mtoa hoja.

CCM na umoja na mshikamano wa Watanzania

Kuhusu mapungufu ya CCM, ni mengi kiasi kwamba hayawezi kujadiliwa yote kwenye makala kama. Yahitaji kitabu kizima. Lakini mapungufu makubwa ya chama hicho tawala katika miaka 45 yake tangu kizaliwe ni pamoja na kile ambacho chama hicho kinajivunia: umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Ni kweli CCM ina mchango mkubwa katika eneo hilo lakini pia umoja na mshikamano huo umekuwa ukitumika kwa upande mmoja kudhibiti mijadala kuhusu mambo yanayoonekana kutishia umoja na mshikamano huo.

Mara nyingi jitihada za kukemea vitu kama ukiukwaji wa haki za binadamu, rushwa, ufisadi, nakadhalika hupelekea tuhuma kutoka CCM kuwa jitihada hizo zinalenga kuhatarisha umoja na mshikamano wetu.

Wanaojaribu kuongelea kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, au kuamsha tafakuri kuhusu pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho, huishia kutuhumiwa kuwa wanataka kuhatarisha umoja na mshikamano wetu.

Kwa hiyo, licha ya umoja na mshikamano wetu kuwa moja ya mambo ambayo CCM imekuwa ikijivunia, ukweli mchungu ni kwamba sifa hiyo pia imekuwa silaha inayotumiwa na chama hicho tawala kudhibiti mijadala mbalimbali yenye maslahi kwa taifa, kwa kisingizio cha “tishio kwa umoja na mshikamano wetu.”

Mapungufu ya kurithi

Baadhi ya mapungufu ya CCM ni ya kurithi kutoka kwa watangulizi wake, TANU na ASP, vyama viwili vilivyoungana Februari 5, 1977, kuunda Chama cha Mapinduzi.

Miongoni mwa mapungufu ambayo CCM ilirithi kutoka kwa watangulizi wake hao ni pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho.

Japo CCM ilizaliwa wakati Tanzania ikiwa nchi ya kijamaa, itikadi iliyosisitiza usawa wa binadamu, ukweli mchungu ni kwamba kulikuwa na matabaka “yaliyokubalika” kwa wakati huo.

Kwa mfano, mfumo wa elimu ya kijamaa ulilenga zaidi kwenye maendeleo ya sekta ya kilimo. Lengo lilikuwa kuzalisha wataalamu mbalimbali, kama vile mabwana shamba, watakaotumia ujuzi na elimu yao katika maendeleo ya kilimo.

Japo lengo halikuwa baya, mfumo huu ulizaa angalau matabaka mawili, dogo la wasomi na kubwa la wakulima. Mfumo wa kisiasa nao ulitawaliwa na tabaka dogo la “wateule wachache” waliotoa uongozi kwa tabaka kubwa la watawaliwa.

Mahusiano yasiyo na usawa kati ya makundi hayo hapo juu, na mengineyo, yamechangia uwepo wa pengo kubwa kati ya wenye nacho na wasio nacho.

Kwa upande mmoja, mazingira yaliruhusu makundi kama ya wasomi na viongozi kuwa na kipato kulinganisha na wakulima, kwa mfano, lakini kwa upande mwingine, baadhi ya watendaji walitumia nafasi hizo kujinufaisha wenyewe.

Ni katika mazingira hayo ndiyo maana mara baada ya “Azimio la Zanzibar” – tamko lisilo rasmi, na ambalo ni vigumu kupata undani wake, linalotafsiriwa kama tangazo la kifo cha Ujamaa – kuliibuka tabaka la wenye utajiri mkubwa “usio na maelezo ya kueleweka” hasa ikizingatiwa kuwa Ujamaa haukuruhusu kulimbikiza mali.

Katika hilohilo la matabaka, CCM imezidi kuwa “chama cha wateule wachache” ambapo uongozi umekuwa kama kupokezana vijiti kati ya “koo za kiutawala.” Japo hakuna sheria inayokataza watoto wa viongozi kuwania uongozi, chama hicho tawala kinaweza kuwa na wakati mgumu kujitanabaisha kuwa kina fursa sawa za uongozi kati ya “watoto wa viongozi” na wale “wasio na ndugu au jamaa kwenye uongozi.”

CCM na makundi ya wakulima, wafanyakazi

Mapungufu mengine ya CCM ni kwamba chama hicho kinaonekana kuzidi kuwa mbali na makundi makuu mawili yaliyokuwa msingi wa chama hicho – wakulima na wafanyakazi, na badala yake kimekuwa kikiwakumbatia zaidi wafanyabiashara.

CCM kuwa kama “sumaku inavyovuta wafanyabiashara kuingia kwenye siasa” imechangiwa pia na sababu mbili hivi. Kwanza, chini ya utawala wa chama hicho tawala, siasa imegeuka kuwa chanzo cha mapato kana kwamba ni biashara flani. Kwa hiyo, mfanyabiashara anayewania uongozi katika chama hicho anakuwa kama anafanya uwekezaji wa kibiashara.

Pili, kwa mfanyabiashara kujiweka karibu na CCM, anakuwa amejitengenezea “kinga” dhidi ya “usumbufu” wowote ule, iwe wa Mamlaka ya Mapato (TRA) au askari mgambo wa jiji.

Umasikini katikati ya utajiri lukuki

Wakati chama hicho tawala kikijigamba kwa mafanikio lukuki, ya kweli na ya kufikirika, moja ya mapungufu yake makubwa ni pamoja na Tanzania kuendelea kuwa moja ya nchi masikini zaidi duniani. Na tatizo hapa sio nchi kuwa masikini, bali “nchi yenye utajiri lukuki” kuwa masikini.

Rushwa na ufisadi vimechangia sana mamilioni ya Watanzania kuendelea kuwa masikini huku viongozi wa chama hicho tawala wakijigamba na takwimu zinazopuuzia ukweli kwamba “watu sio namba.” Takwimu zinazopendeza kuhusu GDP ilhali mamilioni ya watu wapo kwenye umasikini wa kutupa, hazina maana.

CCM sio tu inakwepa kujiuliza kwa nini Tanzania na Watanzania wengi ni masikini bali pia inakwepa jukumu la kiuongozi kuikwamua nchi yetu na watu wake kutoka kwenye janga la umasikini, licha ya utajiri lukuki uliopo.

Demokrasia hati hati

Kwa upande wa demokrasia, japo chama hicho kinajitahidi kufanya chaguzi zake kwa uwazi, chaguzi hizo hutawaliwa na rushwa huku vyombo vya dola vikichelea kuchukua hatua stahili. Ni wazi viongozi wanaopatikana katika chaguzi zilizogubikwa na rushwa hawawezi kuongoza mapambano dhidi ya rushwa.

Katika eneo hilohilo la demokrasia, CCM imeendelea kuwa adui wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ambapo Serikali zake kwa kusaidiwa na vyombo vya dola zimekuwa mstari wa mbele kukandamiza vyama vya upinzani.

Miaka 30 tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi, bado vyama vya upinzani vimekuwa vikitegemea hisani kufanya shughuli zake halali za kisiasa, hususan mikutano na maandamano.

Nihitimishe makala hii kwa kurejea maelezo ya awali kuwa makala hii imejikita kwenye mapungufu tu ya CCM, kwa vile hakuna tija kurudia kutaja mafanikio ya chama hicho kwani kazi hiyo imekuwa ikifanywa na viongozi na wachama wa chama hicho katika miaka yote hii 45.

Mwisho, heri kwa CCM kwa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa!

Evarist Chahali ni mchambuzi wa siasa anayeishi nchini Scotland. Unaweza kumpata kupitia evarist@chahali.com au kupitia Twitter kama @chahali. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *