The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hili Linakuhusu Kama Unategemea Kusafiri Nje ya Tanzania Kikazi

Watanzania wametakiwa kufuata utaratibu rasmi pale wanapotaka kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kufanya kazi kwani hiyo inawarahishia kupata msaada stahiki pale wanapopatwa na tatizo linalohusiana na kazi kwenye nchi waliyofikia.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Kufuatia hatua ya Serikali kufanya kikao na ujumbe kutoka nchi ya Qatar mnamo Februari 18, 2022, ambapo wizara za kazi za nchi hizo mbili zilijadiliana namna ya kurahisisha usafirishwaji wa wafanyakazi kutoka Tanzania kwenda Qatar, The Chanzo imezungumza na Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA) Joseph Nganga ili kufahamu ni nini kilijiri kwenye kikao hicho.

Na hapa Nganga anaanza kwa kuelezea msingi wa kufanyika kwa kikao hicho na ni nini haswa Serikali hizo mbili za Tanzania na Qatar zilikubaliana juu ya suala zima la usafirishaji wa wafanyakazi. Endelea …

Joseph Nganga: Baada ya [Tanzania] kuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia mwaka 2014 na nchi ya Qatar, tulisaini mkataba ambao unawezesha Watanzania kufanya kazi nchini Qatar kwa kufuata misingi na taratibu ambazo zimewekwa kwenye mkataba huo.

Kwa hiyo, juzi tarehe 18, Februari 2022, ugeni wa Wizara ya Kazi, tulikuwa na Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Kazi kutoka kule Qatar akiambatana na maafisa wengine waandamizi wa Serikali ya Qatar, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uhamiaji na maafisa wengine waandamizi.

Walikuja hapa nchini kwa kikao cha pamoja na ujumbe wa Tanzania kuona namna ya kuendelea kushirikiana, hasa katika maeneo ambayo yanafungua milango kwa Watanzania kwenda kufanya kazi nchini Qatar.

Nchi ya Qatar ni nchi ambayo tuna mahusiano nayo mazuri ya kibalozi. Tuna ubalozi kule Qatar lakini pia nchi ya Qatar ina ubalozi hapa na moja wapo ya mambo yanayozungumzwa ni haya kuwa na mahusiano ya kiuwekezaji lakini watu kwenda kufanya kazi.

Kwa hiyo, katika kikao hicho moja [ya ajenda] ilikuwa ni kuangalia muktadha mzima wa sisi [Tanzania] tunavyohusika na ile nchi katika masuala mbalimbali lakini tukijikita zaidi namna Watanzania wanavyoweza kunufaika na fursa za kazi nchini Qatar.

The Chanzo: Labda mmekubaliana nini haswa kupitia hicho kikao kilichofanyika?

Joseph Nganga: Kikao kile kimehimiza na kusisitiza ule ushirikiano wetu na hiyo nchi uendelee kwa kasi kubwa sana hasa katika kipindi hiki. Na sio tu uhusiano kwa ujumla [bali ni] uhusiano kwa maana ya kwamba nchi ya Qatar kuendelea kutoa fursa za kazi kwa Watanzania.

Na kama tunavyojua nchi ya Qatar kwa mwaka huu inaandaa Kombe la Dunia. Kwa hiyo, kuna fursa kadhaa za kazi ambazo zimefunguliwa kwa ajili yetu kama Watanzania na hivyo sasa ujumbe ule ulikuwa ni mahususi kuweka misingi ya namna gani Watanzania wanaweza kunufaika na hizo kazi.

Tumekubaliana kwamba ili kazi hizi zipatikane kwa uzuri kabisa Serikali lazima ziendelee kuratibu, yaani uendaji wa Watanzania Qatar kufanya kazi uendelee kuratibiwa na Serikali. Tukisema unaratibiwa na Serikali kwa upande wetu lakini na kwa upande wa wenzetu. Hatuna maana kwamba sasa sekta binafsi tunaiondoa, hapana.

Wenzetu wa sekta binafsi wanashiriki hasa kama unavyojua tunao mawakala wa huduma binafsi za ajira ambao wanaajiri watu na kuwapeleka nje ya nchi kwenye nchi mbalimbali.

Kwa hiyo, kwa upande wa Qatar wale mawakala binafsi wa huduma za ajira wataunganishwa kwa maana ya kuingia mikataba na mawakala wa kule Qatar ambao wanatambulika na Serikali ya kule na wamesajiliwa na Serikali na Wizara ya Kazi ya kule [Qatar] wanawatambua na ubalozi wetu wa Tanzania kule unawatambua.

Na jambo lingine ambalo tumekubaliana [ni] kwamba lazima vile viwango vya kazi vinazingatiwa. Viwango vya kazi vimewekwa na Shirika la Kazi Duniani kwamba ili kazi iwe ya staha iwe na mambo kadhaa.

Kwa mfano, masaa ya kufanya kazi yasizidi 48 kwa wiki. Mapumziko yamebainishwa pale. Muda wa likizo umebainishwa pale. Stahiki za mfanyakazi, kwa maana ya ujira, zimebainishwa kwa kila fani. Stahiki nyingine [kama] makazi, malazi [na] matibabu [zimeainishwa]. Na Mtanzania akipata changamoto labda hawaelewani na mwajiri wake akatoe taarifa [wapi], nani atatue mgogoro ule.

Na tumekubaliana pia kila mfanyakazi anaeondoka kwenda kufanya kazi nchini Qatar lazima mikataba, acha huu mkataba wa sisi na nchi, mkataba wa huyu anayekwenda kufanya kazi na mwajiri atakaye mwajiri kule tuuone, tuuchambue na tujue kwamba unazingatia hivi viwango vya kazi na mtu wetu anayekwenda kufanya kazi kwa mustakabali mzuri.

Tumekubaliana kwamba sasa tunaanza kupeleka Watanzania kwenda kufanya kazi mapema iwezekanavyo. Watanzania wa aina gani? Wenye ujuzi. Hatutapeleka watu ambao hawana ujuzi kwa sababu mtu ambaye hana ujuzi kwanza hata namna ya kukubaliana, namna ya kutambua haki zake ni ngumu.

Kwetu sisi hii tunaiona kama ni fursa. Hivyo, tunafanya kazi ya kuwaandaa Watanzania waende kufanya kazi za staha. Tunataka Watanzania watoke hapa kwa utaratibu rasmi, sio utaratibu ambao hauko rasmi.

Utaratibu rasmi upo hivi: fursa za kazi zinapopatikana, tunaziweka wazi kwamba kuna kazi moja, mbili, tatu. Na hii sasa ni kwa ujumla wake kwenye kazi kwenye mataifa yote. Kwamba kuna kazi nchi fulani na ina masharti moja, mbili, tatu. Inahitaji ujuzi huu. Mtanzania unayedhani kwamba anasifa aombe kwenda kufanya kazi hiyo kupitia kitengo cha huduma za ajira TaESA.

Ukishafanya hivyo michakato yote itafanyika kwa maana kwamba sisi tutawasiliana na nchi husika kupitia ubalozi wetu, kupitia wizara inayohusika na kuyaweka mazingira ya kazi kwenye mustakabali unaoeleweka.

The Chanzo: Serikali inachukua juhudi zipi kusimamia utaratibu wa Watanzania kwenda kufanya kazi nje ya nchi wakiwa salama lakini pia kuwalinda?

Joseph Nganga: Kwa Watanzania, vijana ambao wanania, wanasifa, na wanashauku ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi wala wasiogope. Upo utaratibu rasmi [na] mzuri ambao Serikali imeuandaa na inauratibu na inausimamia wa kwenda kufanya kazi nje ya nchi vizuri.

Wasiondoke bila kufuata utaratibu ambao ni rahisi. Hata kama mtu amepata kazi yeye binafsi, ameingia kwenye mitandao akaona kuna kazi mahali fulani, akaomba, akafanyiwa kama ni usaili kwa njia ya mtandao. Anapotaka kwenda aje hapa [TaESA]. Akienda kwa utaratibu wa hivyo atakwenda kufanya kazi vizuri na hakutakuwa na tatizo lolote.

Kwa vijana wa Kitanzania kwanza wajitokeze kuendelea kujiandikisha kwenye kitengo cha huduma za ajira na wanapojiandikisha na sisi tunawapatia mafunzo maalumu. Tunawapatia ushauri maalumu. Tunawaonesha namna kazi zinavyoweza kufanyika.

Lakini pia kwa wadau wa sekta binafsi, hasa mawakala wa huduma binafsi za ajira. Sasa utaratibu ni huo na wao waendelee kutafuta fursa za ajira na wakishapata sisi tupo hapa. Balozi zetu kwenye nchi mbalimbali zipo.

Tutawasaidia [na] watawaunganisha Watanzania kwa misingi inayohitajika na kwa kufanya hivyo tutakuwa tunalisaidia taifa na Watanzania wenyewe kufanya kazi vizuri. Lakini pia kukuza uchumi wa taifa letu na kuondoa umaskini.

The Chanzo: Ni nchi gani ambazo Watanzania wengi wanakwenda kufanya kazi lakini pia kama mna takwimu zinazonesha idadi ya Watanzania waliokwenda kufanya kazi huko?

Joseph Nganga: Zipo fursa nyingi duniani na kwa kweli kwa sababu ni jambo ambalo sasa ndiyo tunaanza kuliratibu lakini kwa takwimu za sasa Watanzania wengi wanakwenda Marekani. Wanakwenda kwenye baadhi ya nchi za Uarabuni. Lakini wanakwenda kwenye nchi za Asia kufanya kazi. Yaani tuseme tu kwamba ni mataifa yote.

Lakini tunaandaa sasa takwimu nzuri ambazo zitakuwa zinaonesha kila fani tumepeleka watu wangapi. Lakini niseme tu kwamba Watanzania wengi wapo kwenye mataifa yote wanafanya kazi. Lakini bado nadhani hatufanyi vizuri na ndio maana tunataka turatibu vizuri ili Watanzania wengi waende kwenye hizo nchi.

The Chanzo: Ni changamoto gani kubwa ambazo hivi sasa mnakumbana nazo kwa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Joseph Nganga: Changamoto kubwa nadhani ni uelewa. Tunadhani bado kuna watu wengi hawana ufahamu wa namna ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi. Taratibu gani azipitie.

Hilo sisi tunaona bado ni changamoto kubwa na ndiyo maana sasa tunajiingiza kwenye kampeni, kwenye vyombo vya habari, ili kuwaelemisha Watanzania na vijana kwamba unapotaka kwenda kufanya kazi nje ya nchi utaratibu wa kufuata ni moja, mbili, tatu.

Hiyo ndio nadhani ni changamoto pekee. Lakini changamoto nyingine ni baadhi ya mawakala pengine nao hawana uelewa. Kwamba unapotaka kumuunganisha mtu kwenda kufanya kazi nje ya nchi utaratibu uwe moja, mbili, tatu. Sasa hayo ndio tunayo pambana nayo kwa sasa. Kwamba Watanzania wote wapite kwenye mfumo rasmi wa kwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Hivyo, nitoe wito kwa Watanzania kufuata utaratibu huu kwa sababu wasipofuata inakuwa ni changamoto kwetu kwanza kufahamu uko wapi. Maana tu mtu umeenda hatujui hata ukipata changamoto inakuwa ni ngumu kukusaidia.

Lakini ukifuata utaratibu huu inakuwa ni rahisi sana na sisi kama nchi tunakuwa tunakutambua na nchi uliko inakutambua na ubalozi uliko inakutambua. Kwa hiyo, hilo ndiyo eneo ambalo nilidhani niweke msisitizo kwa Watanzania.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *