Hizi Hapa Faida za Anwani za Makazi

Pamoja na faida nyengine, mfumo huo unategemewa kurahisisha utambuzi wa wakazi na makazi katika ili kurahisisha mchakato wa kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Dodoma. Mratibu wa Mfumo wa Anwani  za Makazi Jampyon Mbugi ameeleza kwamba ili Tanzania iwe katika nafasi nzuri ya kufaidi mapinduzi ya kidijitali yanayoendelea kutokea ulimwenguni kote ni muhimu kwa taifa hilo la Afrika Mashariki kuwa na mifumo mizuri ya utambuzi, zoezi ambalo kwa sasa linafanyika kwa kuhakikisha wananchi wanakuwa na anwani rasmi za makazi

Picha na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Mbugi, ambaye yupo katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tekinolojia ya Habari, alieleza hayo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyolenga kufahamu ni kwa namna gani zoezi hili linaloendelea litawanufaisha wananchi na Tanzania kwa ujumla.

Picha na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Mahojiano hayo na Mbugi, ambaye kitaaluma ni mhandisi, yanakuja takriban miezi miwili tangu Serikali izindue mfumo huo unaolenga kurahisisha utambuzi wa wakazi na makazi katika kuleta maendeleo endelevu nchini.

Picha na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

“Uchumi wa kidigitali unategemea  sana uwepo wa miundombinu ya utambuzi,” anaeleza Mbugi kwenye mahojiano hayo. “Huwezi ukazungumza uchumi wa kidigitali bila kuwepo na miundombinu imara wa  utambuzi. Sasa miundombinu wa  utambuzi ndio hii tunaita Mfumo wa Anwani za Makazi.”

Picha na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

“Mfumo huu [pia] utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama,” aliendelea kueleza Mbugi. “Ulinzi na usalama kwa maana ya kwamba watu wote  watatambulika. Na ukizingatia kwamba huu mfumo  utaenda kutumika kama daftari la kazi. Kwa maana mtu yeyote pale anapoishi, anapotoka, anapohamia [ni] lazima atatambulika  kwamba ni mtu fulani na leo pale kuna mtu fulani kahamia.”

Picha na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Mbugi ansema matarajo ya Serikali ni kwamba ifikapo Mei 2022 mfumo huo uwe umekamilika, kitu ambacho amebainisha kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo kufanikisha hilo.Zoezi hilo kwa mkoa wa Dodoma linalenga kata 41 na mitaa yake 222 kwa mujibu wa mratibu wa zoezi hilo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Nkuba. Nkuba anaeleza kwamba zoezi hilo linalenga kumuwezesha mtu kujua taarifa za mtu binafsi, kampuni na taasisi ikiwa ni taarifa zinazohusu sehemu anayoishi pamoja na shughuli anayofanya.

Picha na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

“Dodoma tumeanza Machi 15, [2022]. Hatukufanya kwa mfululizo tulianza tarehe 15 lakini kati kati tulisimama kulikuwa na tatizo la mtandao kidogo kwa hiyo tumefanya ndani ya siku tano tu,” Nkuba alieleza kwenye mahojiano na The Chanzo.

Picha na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Nkuba alibainisha kwamba zoezi hilo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma litafanyika kwa siku 30. Hadi akiongea na The Chanzo mnamo Machi 26, 2022, Nkuba alisema walikuwa wameingiza taarifa 30,000 kati ya taarifa 200,000 ambazo wanatarajia kuzipata.

Picha na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Kwa mujibu wa Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kati Boniface Shoo mchakato wa Postikodi ulianza tangu mwaka 2007 na TCRA ilianza kwa kutengeneza kanzi data ya Postikodi ya kata zote nchini kisha kuendelea kujaribu kutekeleza mpango wa kuweka postikodi na anwani za makazi katika baadhi ya miji.

Picha na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Shoo anaamini anwani za makazi itarahisisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu wa 2022. Anaeleza: “Kwa sababu, ukishajua watu wako mahali walipo hata kuwa hesabu ni rahisi na pia kuwafikishia zile huduma za msingi.”

Picha na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Wakati akiendesha Kikao Kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma kilichofanyika Februari 8, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alisema kwamba lengo la mfumo huo ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa na Anwani ya Makazi katika eneo lake analoishi, kaya, ofisi ama eneo la biashara ili kuweza kuhudumiwa kwa ufanisi.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutokea Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Jackline Kuwanda

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved