The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Serikali Inataka Wafugaji Watumie Mfumo wa Utambuzi Mifugo wa Kieletroniki?

Serikali inasema mfumo huo unalenga kuzisaidia mamlaka husika kupangalia mipango yake na maendeleo kwa wafugaji vizuri zaidi.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Mkurugenzi Msaidizi  wa Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama kutoka Wizara  ya Mifugo na Uvuvi Dk Anneti Kitambi amesema kwamba mfumo wa utambuzi na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki unalenga kuisaidia Serikali kupangalia mipango yake na maendeleo ya wafugaji vizuri zaidi.

Dk Kitambi alitoa maelezo hayo wakati wa mahojiano maalum kwa njia ya simu na The Chanzo yaliyolenga kutaka kufahamu kutoka kwa afisa huyo ni kwa namna gani zoezi hilo linaenda kumnufaisha mfugaji wa Kitanzania.

Kauli hiyo ya Dk Kitambi inakuja huku kukiwa na mkanganyiko miongoni mwa wafugaji nchini juu ya lengo haswa la zoezi hilo, huku Katibu wa Chama cha Wafugaji mkoa wa Dodoma Reginaldo Lubeleje akiitaka Serikali kuendelea kutoa elimu ili kupunguza mikanganyiko hiyo.

“Wafugaji bado hawana elimu kabisa,” alisema Lubeleje wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo. “Kwa hiyo, tunahisi kama hatutapeleka elimu ya kutosha kwa wafugaji, [wafugaji hao] wataona kama wanaonewa. Ndiyo maana tunapiga kelele kwamba suala ni zuri ila elimu inapaswa kuendelea kutolewa.”

Akizungumzia wito huo, Dk Kitambi alisema kwamba tayari elimu imeshatolewa lakini Serikali itaendelea kuwahusisha wafugaji moja kwa moja na kupitia viongozi wao ili kulifanya zoezi kuwa rahisi katika utekelezaji.

Utambuzi utaiongezea mifugo thamani

Akielezea umuhimu wa zoezi hilo, Dk Kitambi amesema utambuzi wa mifugo unamuongezea mfugaji thamani na  kuweka taarifa zote za mfugaji pamoja na mifugo kwenye mfumo wa kieletroniki.

Dk Kitambi pia ameeleza kwamba mfumo huo utasaidia kuzuia magonjwa kusambaa na kuweza kuikinga mifugo dhidi ya magonjwa hayo.

“Kwa sababu, utaweza kujua huyu mnyama, kwa mfano, kama amesafirishwa ameenda mahali fulani, unajua kabisa huyu anaugua,” anasema Dk Kitambi. “Kwa hiyo, ukisoma tu ile namba unaweza ukajua huyu mnyama ametoka halmashauri fulani. Kwa hiyo, ni rahisi kwenda kuzuia ule ugonjwa usisambae.”

Lengo la Serikali ni kufikia asilimia 70 ya mifugo yote nchini ifikapo Septemba 2022 na kuisajili kwenye mfumo huo wa utambuzi wa hereni za kieletroniki.

Kwa mujibu wa Dk Kitambi, kwa Halmashauri za Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa jumla ya ng’ombe 2,769 na mbuzi na kondoo 687 zimesajiliwa kwenye mfumo huo.

Kwa maeneo mengi ya Kanda ya Kati,  ikiwemo wilaya ya Chamwino, mfumo huo wa utambuzi wa mifugo  unategemewa kuanza baada ya Sikukuu ya Pasaka ambapo mnamo Aprili 21, 2022 Waziri Mkuu Kasim Majaliwa anatarajiwa kuzindua mfumo huo mkoani Dodoma.

Wafugaji wanena

Yohana Muyeji ni mfugaji kutoka kijiji cha Kaza Roho, kata ya Manzase, wilayani Chamwino ambaye anasema yeye kama mfugaji ameamua kukubaliana na suala hilo.

“Kulingana na jinsi wanavyo tuelezea, wanasema kuna manufaa kwenye soko la kimtandao,” anasema Muyeji. “Wanasema wanavalisha ile hereni ng’ombe na itafika nje ya nchi inauzwa kwa bei yenye maslahi mno. Wao wakubwa wameliona hilo wametuambia na sisi tumependezwa ili na sisi litufikie.”

Mfugaji wa kijiji cha Fufu Fadhili Mwalimu amesema kwamba mifugo yao haijafikiwa na zoezi hilo, lakini ameelezwa kwamba likikamilika litasaidia kurahisisha upatikanaji wa mifugo endapo ikiibiwa kutokana na mfumo uliokuwepo.

Mwalimu anasema kwamba baada ya Serikali kuona wafugaji wengi wanaibiwa mifugo yao iliona ni bora itengeneze mfumo wa utambuzi ili kudhibiti vitendo hivyo.

“Hivyo ndivyo nadhani mimi ninavyoelewa,” anasema Mwalimu. “Taarifa kwa wafugaji wengine bado sana. Lakini sasa vyombo vya habari vinavyozidi kulitangaza jambo hili taarifa watu zitawafikia.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *