The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hivi Ndivyo Serikali Inaweza Kulishughulikia Suala la Ngorongoro

Serikali inaweza kunufaika zaidi endapo kama itawaweka wenyeji karibu badala ya kuwaacha warubuniwe na wanasiasa na wanaharakati.

subscribe to our newsletter!

Nadhani kuna namna bora zaidi ambazo Serikali inaweza kuzitumia kushughulika na suala la Ngorongoro kwa ufanisi mkubwa na kwa manufaa ya kila upande unaohusika na suala hilo, nikimaanisha Serikali yenyewe na wenyeji wa Ngorongoro.

Moja kati ya njia hizi ni maofisa wa ngazi za chini za mamlaka ya nchi kuzungumza na wenyeji kwa lugha ambayo wanaweza kuielewa kuhusiana na suala husika. Serikali inaweza kuachana na kutumia wanasiasa ambao wao wanamakazi yao na wanajaribu kulinda maslahi yao fiche.

Kwa kweli, nadhani, kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenda kuongea na wananchi wa kawaida kabisa kule chini itashindikana kuweza kupata mitazamo ya wenyeji. Hii ni kwa sababu Waziri Mkuu ni mtu mkubwa sana. Hata Mkuu wa Mkoa ni mtu mkubwa. Watu wakisikia tu kwamba Mkuu wa Mkoa anakuja kuongea nao basi tayari wananchi wanajawa na hofu.

Nadhani kuna maofisa wa kawaida ambao wangeweza kwenda vijijini, siyo kuishia kwenye kata, siyo kuishia wilayani. Namaanisha kwenda vijijini kabisa wakakutane kabisa na wananchi na itolewe elimu.

Kwa hiyo, mimi nadhani ni bora hii kazi ya kuongea na wenyeji ingeachwa kwa maafisa wa ngazi za chini ambao kimsingi wanaweza kwanza kutoa elimu na kueleza namna sahihi siyo tu kueleza. Tusiishiye kwenye kutumia Kiswahili tu. Ikibidi tunaweza kutumia Kimaasai ili watu waelewe.

Uhamisho usiwe jumuishi

Unaweza kuitishwa mikutano ya wananchi ambapo wananchi wanaweza kuwa huru na kutoa maoni yao kuhusiana na suala husika. Hili ni suala la kwanza. Suala la pili pili ni kwamba Ngorongoro ina kitu kinachoitwa eneo la matumizi makubwa na eneo la matumizi madogo.

Kwa mfano, leo ukiangalia upande wa Ngorongoro kabisa eneo la Kreta unakuta kwamba ni eneo la matumizi makubwa sana ambalo linatumika sana kwa shughuli za kitalii.

Lakini kuna wananchi ambao bado wanakaa Kakesio mwishoni kule ambako hujawahi kumuona hata mtalii akienda. Sasa kuna sababu gani ya kuwasumbua watu wanaokaa Kakesio kule au wanaokaa maeneo mengine kama hayo wahame?

Kwa hiyo, inamaana kwamba haya maeneo ambayo yanafikiriwa kwamba labda ni maeneo ya matumizi makubwa labda ndiyo mjadala ungeanzia katika maeneo hayo.

Wamaasai ni watu ambao wanaelewa wakielezwa vizuri hasa kwa kupitia kwenda kwa wananchi wa kawaida kabisa na kwa kuwatumia wazee wa mila ambao ni Malaigwanan ambao na hao Malaigwan ni lazima kuweza kuwachagua kwa kiasi kikubwa kwa sababu kuna wengine ambao tayari wameshalishwa sumu mbaya sana na hao wanasiasa.

Kuwa makini na wanasiasa

Kuhusu wanasiasa, Serikali, kama ingewezekana, ingewatoa kabisa hawa wanasiasa kwenye hili zoezi. Kwa sababu, mwisho wa siku watawapotosha wananchi. Matatizo yakitokea hawa wanasiasa hawataweza kuwasaidia na hicho sisi ndiyo kitu ambacho tunachukia.

Kwa mfano, kwenye kutengeneza mahusiano mabaya, unamkuta mtu anatengeneza mahusiano mabaya sana na Mamlaka ya Hifadhi, kuanzia kuwashambulia viongozi wa Hifadhi ya Ngorongoro. Sasa unamshambulia mtu, huyo mtu atakusikiliza, huyo mtu utaweza kufanya naye kazi?

Ndiyo maana mimi nikasema Serikali ishuke kule chini iache kutumia hawa watu ambao mwisho wa siku wanakuwa hawaelewi; hawa siyo watu ambao wapo kule kwenye jamii yenyewe, au watu wenye maslahi mengine ambayo ni mabaya.

Na mimi nashangaa kwamba mtu mmoja ambaye ni mwanasiasa anakuwaje na nguvu ya kuweza kuzuia Serikali kukutana na wananchi wake jamani? Mimi nimekuwa nashangaa labda sielewi kama Serikali na yenyewe haina nia ya kuweza kukutana na wananchi na kuweza kuzungumza.

Kwa sababu mwisho wa siku uhamasishaji, uelewa, majadiliano, kuzungumza, kuelezana, na kueleweshana inabidi ichukue muda kwa sababu naamini pia hata huu ujenzi wa hizo nyumba haziwezi kumalizika ndani ya mwezi mmoja.

Kwa mfano, Serikali ingeonesha kila dalili ya kuwa tayari kuzungumza na wananchi kutoka kule chini toka mwanzo zoezi hili limeanza mpaka sasa hivi walau asilimia kubwa ya wananchi wangekuwa wameelewa nini kinaendelea.

Nafasi ya AZAKI, vyombo vya habari

Ni muhimu pia Serikali kutoa nafasi kwa asasi za kiraia, ambazo sisi ni mmoja wao, kushiriki kwenye mijadala ya wazi kati ya Serikali na wenyeji. Sina shida, wala sina shaka kabisa, hata kama kwenye hicho kikao cha asasi za kiraia, hata kama ingekuwa ni Mkuu wa Mkoa ndio atakaye kiwezesha, kama asasi za kiraia zitagoma kushiriki.

Naamini kwamba watu wa asasi za kiraia wanakuwa na hadhi na uelewa mkubwa kuliko wananchi wa kawaida. Kwa hiyo, mimi nadhani, kwa sababu najua sasa mkiwa kwenye meza ya majadiliano, mkizungumza huyu haelewi, tumueleweshe, au huyu anakusudia kuharibu, tumtoe. Mwisho wa siku inakuwa ni rahisi zaidi kuuelewa ukweli.

Kwa sababu mwisho wa siku mimi ninachotaka tu ni kwamba kila mtu tuwe pamoja, asasi za kiraia ziwe pamoja, wananchi wawe pamoja na vyombo vya habari viwe pamoja.

Baadhi ya watu wanasema unajua mauaji yanafanyika Ngorongoro. Uongo mtupu. Inatengenezwa sifa mbaya kuhusiana na Ngorongoro. Picha mbaya sana. Hawa watu wanajenga hofu kwa wananchi.

Nikuhakikishie tu ndugu msomaji kwamba hakuna mauaji yanayofanyika Ngorongoro. Niseme tu kuna ukamataji ukamataji kwa kiasi kidogo unaondelea unaotokana na tabia tu za watu binafsi. Lakini pia, unajua kwamba pale inapotokea suala kidogo kuna kuwa na wachache ambao hawapendi amani. Kwa hiyo, unaweza ukashangaa kuna wengine wanatokea wanafanya hivi na vile.

Lakini pia tunaona kwamba walinzi wa Hifadhi ya Ngorongoro kidogo wanakuwa wakali. Unakuta kwamba sasa watu wanakamatwa hovyo hovyo. Umeingiza ng’ombe kwenye sehemu isiyoruhusiwa, unakamatwa. Mwisho wa siku itajengwa mahusiano mabaya.

Mwisho wa siku ile picha mbaya ambayo ilijengwa na wanasiasa kwamba Serikali ina nia mbaya inaweza ikaja ikafanania pale watu wnapokuwa wanakamtwa kamatwa hovyo hovyo.

Kwa hiyo, mimi nadhani ni muhimu kurekebisha haya yote, na kuwafikia wananchi mashinani, kama kweli tumedhamiria kulitekeleza zoezi hili kwa ufanisi na kwa manufaa ya pande zote zinazohusika.

Joseph Parsambei ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Wafugaji Tanzania (TPCF). Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *