Mbivu, Mbichi Bajeti ya Tanzania 2022/2023

Je, tunapaswa kufanya kitu gani kama taifa kuweza kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi nchini pasipo kuleta athari za kijinsia kwa makundi mbalimbali, wakiwemo wanawake na watoto?
Deus Kibamba21 June 20227 min

Nimeipitia kwa umakini hotuba ya Bajeti ya Taifa kama ilivyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba mnamo Juni 14, 2022. Kiukweli, nitakuwa mzandiki nikisema kuwa ilikuwa rahisi kuichambua bajeti hii. Ni bajeti iliyosheheni takwimu, hoja, utafiti na vibwagizo lukuki.

Kwa maoni yangu, hotuba ya Waziri wa Fedha pekee inaweza kuchambuliwa kwa zaidi ya miezi miwili. Aidha, juzuu zake zilizo katika vitabu vinne pamoja na viambata vyake, yakiwemo majedwali mbalimbali, vinafanya bajeti hii kuwa yenye kina cha kutosha.

Nachukua wasaa huu kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango na wataalamu wote wa wizara waliofanikisha kuandaliwa hadi kukamilika kwa bajeti aliyoisoma bungeni na Serikali kwa mapana yake kupitia Baraza la Mawaziri chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan ambao ndio wamebariki bajeti hii iweze kuwasilishwa bungeni.

Kwa maoni yangu, bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23 ina mazuri mengi na mapungufu kadhaa. Ukiisoma, kuichambua na kuitafakari, unapata hisia mchanganyiko. Kwa mfano, kimuundo, bajeti nzima imebeba makadirio ya mapato na matumizi kwa nchi nzima ikihusisha wizara, idara zinazojitegemea na wakala wa Serikali.

Aidha, bajeti pia inahusisha makadirio ya matumizi kwa sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa. Bajeti inajumuisha makadirio ya matumizi ya maendeleo yale ya kawaida kwa ofisi zote za umma nchini. Baada ya kujadiliwa na kupitishwa bungeni, Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 na Sheria ya Matumizi ya Mwaka 2022 zitakuwa ndiyo mwongozo wa mgawo wa fedha zote nchini katika kipindi cha Mwaka wa Fedha ambao unaazia Julai 1, 2022 hadi kufikia Juni 30, 2023.

Kwa ujumla, hakuna matumizi ya fedha yanaweza kufanyika nje ya mpango huu wa bajeti katika kipindi cha miezi 12 ijayo isipokuwa katika mazingira fulani tu ya udharura ambapo napo italazimu Serikali kwenda kuomba idhini ya Bunge kwa matumizi yaliyofanyika nje ya mpango huu wa Bajeti ya Taifa kama ilivyowasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa Bungeni.

Bajeti ya Mwaka 2022/23 inafikia kiasi cha Shilingi trilioni 41.48, ikitarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo mbalimbali vya kodi, tozo, mikopo na misaada toka ndani na nje ya Tanzania. Katika hizo, makadirio kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yamekadiriwa kufikia Shilingi trilioni 23.65. Makusanyo yasiyotokana na kodi kutoka wizara na idara mbalimbali yatafikia Shilingi trilioni 3.35 na ushuru na makusanyo mengine kutoka halmashauri mbalimbali nchini vinakadiriwa kuwa vitafikisha Shilingi trilioni 1.01.

Kwa upande mwingine, mapato ya Tanzania yatategemea misaada na mikopo isiyo ya Kibiashara ambavyo kwa pamoja vinakadiriwa kuingiza nchini Shilingi trilioni 4.64 huku mikopo yenye riba kutoka ndani na nje ya nchi inakadiriwa kuwa itafikia jumla ya Shilingi trilioni 8.81 katika kipindi cha mwaka mmoja ujao ikiwa ni pungufu kidogo tu ya ile iliyokopwa Mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30, 2022.

Kwa upande wa matumizi, maeneo mawili makuu yatakula pesa kwa mwaka wa fedha 2022/23. Kwanza, inajatarajiwa kuwa matumizi ya kawaida kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali yatafikia Shilingi trilioni 26.47 ambapo kati ya hizo mishahara pekee itagharimu kiasi cha Shilingi trilioni 9.83 na matumizi mengineyo yatafikia Shilingi trilioni 5.33.

Kwa upande wa miradi ya maendeleo, mpango wa bajeti unaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 15, ikijumuisha gharama za Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao umepangiwa kiasi cha Shilingi trilioni 1.11; Mradi wa Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (Shilingi trilioni 1.43) na miradi mingine ambayo itagharimu jumla ya shilingi Trilioni 9.13.

Ukosefu wa urari mzuri

Kitaalamu, bajeti ya Tanzania bado inakosa urari mzuri ambao hupaswa kuwa na bajeti ya maendeleo katika kiwango cha japo mara mbili ya bajeti ya matumizi ya kawaida tofauti na mfumo wa Tanzania ambapo bajeti ya matumizi ya kawaida ni zaidi ya mara moja na nusu ya ile ya maendeleo. Hii inamaanisha kuwa nchi yetu ina kibarua kigumu cha kufikiria zaidi namna ya kupanua wigo wa ukusanyaji mapato ili pesa inayoelekea kwenye ‘kula’ iwe ni pungufu ya ile inayoenda ‘kujenga.’

Ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana, bajeti ya mwaka huu imeongezeka kwa takribani Shilingi trilioni 4. Ingawa hili si jambo baya, kuna wasiwasi juu ya endapo kweli tutaweza kutimiza malengo ya makusanyo yaliyokisiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao. Uzoefu unaonesha kuwa kwa miaka kadhaa mfululizo, uwezo wa kukusanya mapato kwa kiwango cha makisio ya bajeti umekuwa ni mdogo.

Kwa mfano, utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/22 ulikuwa ni mdogo kwa kiasi kikubwa. Kati ya mapato yanayofikia Shilingi trilioni 37.99 yaliyokadiriwa mwezi Juni 2021, ni Shilingi trilioni 29.84 pekee ndizo zilizopatikana kama kodi, ushuru, tozo, misaada na mikopo. Hii inaonesha upungufu wa makadirio dhidi ya makusanyo unaofikia Shilingi trilioni 8.15.

Upungufu huo unakaribia kufikia kiwango chote cha mishahara kilichokadiriwa kuwa kitalipwa kwa mwaka wa fedha 2022/23. Hali hii inakinzana na dhana ya upangaji bora wa bajeti ambapo tofauti ya makadirio na mapato halisi hupaswa kutozidi asilimia 10. Je, Shilingi trilioni 8.15 ni asilimia ngapi ya makadirio yote ya 2021/22 ambayo yalikuwa ni kukusanya Shilingi trilioni 37.99?

Ukitazama bajeti inayoishia Juni 30, 2022, kumekuwa na shida ya matumizi pia. Mathalani, kati ya Shilingi trilioni 29.84 zilizokusanywa, hotuba ya bajeti inabainisha kuwa kiasi cha Shilingi trilioni 18.79 zilitumika kwa matumizi ya kawaida. Kati ya hizo, kiasi cha Shilingi trilioni 6.73 zililipa mishahara huku jumla ya Shilingi trilioni 7.27 zilitumika kugharamia deni la taifa.

Pamoja na juhudi hizo za kulipia deni la taifa, deni hilo halijapungua bali limeongezeka kutoka Shilingi trilioni 60.72 mwezi Aprili 2022 hadi kufikia Shilingi trilioni 69.44. Ongezeko hili ni zaidi ya kiasi ambacho Tanzania ilitumia kuhudumia deni la taifa kwa mwaka 2021/22. Kwa mwendo huu, itakuwa vigumu sana kuweza kufikia wakati ambapo kiwango cha deni la taifa kinashuka.

Nionavyo mimi, kupania kupunguza kiwango tunachokopa kama taifa ni hatua muhimu zaidi katika kukabiliana na madeni kuliko kulipa na kukopa kwa vile riba ya mikopo ya kibiashara inapaisha deni kwa viwango vya kibeberu mno.

Heri tukawa na makadirio ya bajeti yaliyo chini kuliko kuweka makisio ya juu na kushindwa kufikia makusanyo na tunakopa kwa urari usio sawia. Haya ni maoni yangu binafsi, nikiwa mmoja wa Watanzania wachache waliosomea Siasa-Uchumi darasani!

Mambo kadhaa mazuri

Ukiacha machungu haya machache, bajeti iliyosomwa na waziri ina mambo kadhaa mazuri. Kwa mfano, bajeti ya kilimo itaongezeka kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 954 kwa mwaka wa fedha unaoanza wiki mbili zijazo. Nimechambua kuona fedha hizi zitaelekezwa katika maeneo gani ya kilimo na kubaini kuwa, kwa mara ya kwanza, kilimo cha kisasa kinachohusisha umwagiliaji kitakumbukwa.

Waziri anabainisha kuwa Serikali imepania kuongeza idadi ya maeneo ya kilimo yenye miundombinu ya uhakika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kufanya eneo la umwagiliaji nchini kufikia hekta milioni 8.5.

Ikiwa kutakuwa na umakini wa kupanga mipango ili maeneo hayo yatumiwe na wananchi wa kawaida, wakiwemo wanawake na vijana, Tanzania inaweza kumaliza uhaba wa chakula, umasikini wa kipato na kunyanyua nguvu ya manunuzi ambayo kwa lugha ya kimombo huitwa purchasing power. Hilo limenifurahisha sana!

Ifahamike pia kuwa Serikali imeendeleza nia ya kuboresha mazingira ya kusomea nchini. Huku juhudi za ujenzi wa miundombinu shuleni zikiendelea, na baada ya kufutwa kwa ada katika shule za msingi na sekondari nchini, Bajeti ya 2022/23 imeongeza wigo wa elimu bila ada kufikia kidato cha tano na sita. Jambo hili linafanya elimu bila ada sasa kuwa ni kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.

Aidha, bajeti pia imepanga kuwekeza katika kuimarisha elimu ya ufundi stadi nchini. Katika hotuba yake, Waziri wa Fedha ametangaza kuwa fedha zaidi zitapelekwa kwenye kujenga vyuo vya ufundi stadi ambavyo kwa sasa viko chini ya NACTVet ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama NACTE.

Kuanzia mwaka ujao wa fedha, mkoa wa Songwe, ambao kwa sasa hauna chuo hata kimoja cha ufundi stadi, utapatiwa chuo sambamba na wilaya 36 kote nchini ambazo hazina vyuo hivyo.

La kufurahisha zaidi, Serikali imekerwa na tatizo la utoro shuleni na kutenga bajeti inayofikia Shilingi bilioni 8 kwa kuanzia, kuanzisha dirisha maalum kupitia TASAF kusaidia watoto wa familia masikini kumudu mahitaji ya lazima ya kielimu.

Naungana na Waziri Mwigulu katika kusema kuwa hatua hii itasaidia kupunguza utoro, mimba na ndoa za utotoni miongoni mwa wanafunzi wa kike nchini. Kwa hili, urari wa elimu na usawa wa kijinsia unaweza kupatikana!

Mambo mengine mazuri ni pamoja na kufutwa kwa kodi ya ongezeko la thamani kwenye mafuta ya kula yanayozalishwa hapa nchini, hatua ambayo ni chanya katika kuongeza uzalishaji wa mazao ghafi ya mafuta hayo nchini na pia kupunguza bei ya bidhaa hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa kupanda bei kila uchao. Hatua hiyo pia itapunguza utegemezi wa Tanzania kwa mafuta ya kula ya kuagiza kutoka nje ya nchi na hivyo kulinda akiba ya pesa za kigeni tulizonazo.

Jingine kubwa ni kuwa wazee wastaafu nao wamekumbukwa. Kuanzia Julai 2022, kiwango cha malipo ya mkupuo kwa wazee wastaafu kimepandishwa hadi kufikia asilimia 33 (theluthi moja) kutoka asilimia 25 (robo) ya jumla ya stahiki ya mafao ya mstaafu iliyoamuliwa na Serikali mwaka 2018.

Kwa hatua hii, malalamiko ya wastaafu kuhusu kulipwa mafao ya mkupuo kiduchu watokapo kazini yatapungua kwa kiasi fulani. Sambamba na hilo, kima cha chini cha mshahara wa mtumishi wa umma kimepandishwa kwa asilimia 23.3, ongezeko ambalo ni zaidi ya nyongeza iliyoongezwa katika nchi yoyote ya ukanda wa SADC, EAC au COMESA.

Aidha, posho za safari kwa wafanyakazi nazo zimeongezwa kutoka kiwango cha Shilingi 120,000 hadi Shilingi 250,000 kutegemeana na ngazi ya utumishi. Pia, tozo katika miamala ya fedha zimeshushwa kutoka Shilingi 7,000 kama kiwango cha juu hadi Shilingi 4,000. Mambo hayo yote yanafanya maisha ya mfanyakazi wa Tanzania kuwa bora zaidi kuanzia mwaka wa fedha 2022/23.

Mambo yanayoleta shida

Pamoja na mazuri hayo yote, bajeti pia ina mambo ambayo kwa jicho langu naona kuwa yanaleta shida. Mambo hayo yenye mapungufu ni pamoja na kuanzishwa kwa ada mpya ya ving’amuzi ambayo itakuwa ni kati ya Shilingi 1,000 na Shilingi 3,000 kutegemeana na viwango matumizi kwa mwezi.

Jambo hili litaathiri vibaya hali ya upashanaji habari katika nchi ambayo ufahamu miongoni mwa wananchi tayari uko kwa kiwango duni sana. Pia, bidhaa nyingi watumiazo wanawake na watoto zimeongezewa viwango vya kodi.

Kwa mfano, nywele za bandia za wanawake zimeongezewa ushuru wa forodha kwa asilimia 10, kutoka asilimia 25 mpaka asilimia 35. Hii itaathiri bei ya bidhaa hiyo na kupandisha gharama ya kuzinunua madukani. Mbaya zaidi, taulo za watoto, yaani baby diapers, zinazoagizwa kutoka nje nazo zimepandishiwa ushuru wa forodha kwa kiwango cha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35.

Ingawa hatua hii inaweza kuwa imefanywa kwa nia nzuri ya kulinda viwanda vya taulo za watoto na nywele bandia za akina mama, ni bahati mbaya kuwa utafiti unaonesha kuwa hakuna uzalishaji wa kutosha kwa bidhaa hizo hapa nchini. Aidha,  ubora wa baadhi ya taulo za watoto zizalishwazo nchini ni duni sana kiasi cha kuathiri watoto.

Mwisho, nimeshangazwa kuwa ingawa Waziri Mwigulu amewamwagia sifa wanawake kama ni warejeshaji wazuri wa mikopo, bajeti yake inapunguza kiwango cha mikopo kwa wanawake kupitia halmashauri kutoka asilimia nne hadi asilimia mbili. Jambo hili linafanya wanawake wa Tanzania wawe kwenye maandalizi ya kilio kwa bajeti ya 2022/23 inayoanza kufanya kazi Julai 1, 2022.

Je, tunapaswa kufanya kitu gani kama taifa kuweza kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi nchini pasipo kuleta athari za kijinsia kwa makundi mbalimbali, wakiwemo wanawake na watoto?

Deus Kibamba ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya siasa Tanzania anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Deus Kibamba

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved