The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tunapimaje Maoni ya Umma?

Na kwa nini tunahitaji kupima maoni ya umma?

subscribe to our newsletter!

Moja kati ya masuala tata katika siasa zetu ni maoni ya umma (public opinion). Ni nini maoni ya umma? Maoni ni imani, au fikra, aliyonayo mtu kuhusu jambo fulani, haijalishi kama mtazamo huo umejengwa juu ya msingi wa hoja au umetokana ana mapenzi, hisia na imani ya kidini ya mtu. Ama kuhusu neno la pili, umma, linamaanisha ‘watu wengi’ katika jamii.

Kwa hiyo, kama ambavyo kuna vitu vingi vinaweza kuitwa vya umma, tuna pia maoni ya umma, ikimaanisha matakwa au mitazamo inayokubalika na wengi katika jamii husika.

Katika siasa, maoni yana jukumu kubwa katika kujenga muelekeo wa siasa. Kwa kawaida, maamuzi mbalimbali ya Serikali yanaongozwa na maoni ya umma. Hili liko wazi ukirejea maamuzi ya karibuni ya Serikali kuchukua hatua za kuratibu bei ya mafuta, ambapo inajulikana Serikali haikuweza tena kupuuza vilio vya watu.

Viongozi wa kisiasa, hasa wale wapenda mabadiliko, hujenga hoja kwa kudai ni maoni ya umma. Kwa hili, rejea hoja za madai ya Katiba Mpya yanayoendelea sasa hivi.

Kwa sababu ya kujua umuhimu wa maoni ya umma, viongozi wa siasa wamekuwa wakipambana juu chini kushawishi maoni yaendane na misimamo yao au ya vyama vyao.

Katika hili zipo nadharia kadhaa katika sayansi ya mawasiliano zinazojadili namna ya kushawishi maoni. Moja ya nadharia hizo ni ile ya kutaja jambo mara kwa mara ili kuwafanya wananchi waone ni suala muhimu na hivyo kuanza kulijadili, hii inaitwa agenda setting kwa kimombo.

Ipo nadharia inayozungumzia kulipa kipaumbele jambo kwa kulipa nafasi kubwa katika uwasilishaji, hii huitwa priming. Ipo nadharia nyingine inayozungumzia kuliwasilisha jambo kwa namna fulani ili kushawishi watu wawe na mtazamo kama wako katika jambo hilo ambayo huitwa framing. Katika makala hii sikusudii kujadili namna ya kushawishi maoni ya umma bali lengo ni ugumu wa upimaji wa maoni ya umma katika siasa za Tanzania.

Kwa nini tunahitaji kupima maoni?

Ni muhimu kujua maoni kwa sababu ambazo baadhi nishazitaja. Moja, ni kusaidia kufanya uamuzi wa suala fulani. Kwa mfano, hakuna chama makini kitaandaa ilani yake kwa ajili ya kuiuza kabla ya kufanya utafiti wa maoni ya umma.

Baadhi ya maswali muhimu katika utafiti wa namna hiyo ni pamoja na kujua ni yepi masuala muhimu yanayopewa kipaumbele na wapiga kura? Swali jingine muhimu ni je, wanafikiri nini kuhusu swala hilo (mtazamo)? Mathalan, swala la kipaumbele ni elimu, swali la pili wanataka nini kwenye elimu, elimu bure, maboresho ya mitaala, Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia?

Serikali inatumia maoni ya umma inayoyakusanya kwa njia zake inazozijua kufanya maamuzi mbalimbali kila siku, kama nilivyotoa mfano wa bei ya mafuta, ingawa pia hutokea bei za bidhaa mbalimbali nyingine zikipanda au likitokea suala la usalama wa raia kama vile Panya Road.

Umuhimu mwingine wa kujua maoni ya umma ni katika kujenga hoja za kutaka mabadiliko. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameweza sana kutumia kisingizio cha matakwa ya umma kudai mambo mbalimbali, ikiwemo Katiba Mpya, maridhiano na kadhalika.

Tunapimaje maoni ya umma?

Kwanza, ijulikane kuwa maoni ya umma yanapimika, bila wasiwasi. Njia za kupima maoni ya umma ni nyingi lakini pia zina changamoto zake.

Moja ya njia kuu za kupima maoni ya umma ni uchaguzi huru na wa haki. Tumekuwa na chaguzi nne tangu turudi katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 lakini nani anaweza kusema zilikuwa huru na haki? Kwa uzoefu wa uchaguzi uliopita, ni wazi kuwa dola ikiamua inaweza hata kumpa mwenye asilimia 70 ya ushindi 30 na yule wa 30 akapewa 70.

Nyomi, neno maarufu, linalomaanisha wingi wa watu katika mikutano lilitumika pia kuashiria, kwa namna fulani, maoni ya umma juu ya mgombea. Hata hivyo, ukiacha ugumu wa kukadiria wingi wa watu, tunajuaje waliokuja ni wafuasi au raia tu wanaotaka kusikiliza sera au wamevutiwa na burudani?

Wapo wafuasi ambao hutembea na mgombea katika mji popote aendapo, hivyo basi unakuta robo ya hadhira ya mkutano wa Temeke ndio haohao waliopo Mbagala, Magomeni, Kawe nakadhalika. Baadhi ya vyama husafirisha kabisa wafuasi mji hadi mji.

Ukiacha changamoto hiyo, kwa kawaida baada ya uchaguzi maoni ya umma huendelea kubadilika kutokana na ufanisi wa Serikali iliyopo madarakani na harakati za upinzani. Hivyo, ipo haja ya kuendelea kufuatilia maoni ya umma kadri muda unavyosonga.

Njia nyingine ya kujua maoni ya watu ni kupitia vyombo vya habari vikuu na mitandao ya kijamii. Hata hivyo, katika mazingira ambayo vyombo vyenyewe vimechagua upande kisiasa na kushindwa kutofautisha habari na maoni, hapo unakuta maudhui yao pia hayawezi kusaidia sana kujua maoni ya umma hasa ni yepi kwenye jambo linalobishaniwa.

Mitandao ya kijamii imekuwa iitumika sana kuhalalisha mitazamo fulani kuwa ni maoni ya umma, lakini hili nalo lina changamoto nyingi. Kwanza, kiasi gani cha Watanzania wanatumia intaneti na mitandao ya kijamii? Kati yao, wangapi wanatumia kufutilia na kutoa maoni ya kisiasa?

Katika hao wanaotumia kufuatilia siasa, kwa kiasi gani wanawakilisha jamii pana ya Watanzania: Watu wa vijijini ukilinganisha na wa mijini, vijana ukilinganisha na wazee, wanaume ukilinganisha na wanawake, wenye elimu ya juu ukilinganisha na wenye elimu ya chini, Waislamu ukilinganisha na Wakristo na hata ukilinganisha uwakilishi wa kanda, wafuasi wa chama tawala ukinganisha na wapinzani?

Bahati mbaya katika mitandao ya kijamii ambayo inavutia mijadala ya kisiasa na hivyo kutumika zaidi kujadili mambo ya nchi, Twitter inaongoza. Hata hivyo, Twitter ni mtandao mdogo ukilinganisha na Facebook na Instagram kiufuasi. Hivyo, kuna watu wengi mitandaoni huenda hata hawana habari na siasa.

Ikumbukwe pia kuwa kipindi cha awamu ya tano wakati Serikali ilipovibana vyombo vya habari hadi vikalazimika kuacha kuchapisha au kutangaza habari za wapizani, wafuasi wengi wa vyama hivyo wakahamia mitandaoni. Kwa hiyo, kuna uwezekano mkubwa Twitter kuwa na wapinzani wengi, kutokana na uhitaji wa uhuru wa kufanya siasa na msukumo wa kutaka kuhubiri mabadiliko.

Kura za maoni

Moja ya njia bora kabisa za kujua maoni ya umma kuhusu jambo fulani ni kufanya tafiti za kura ya maoni. Hii ni njia ya kisayansi zaidi inayotumika katika nchi mbalimbali kujua umma unawaza nini, fikra gani zinaungwa mkono zaidi na kwa kiasi gani. Kuna taasisi ambazo zinafanya tafiti na kuuza. Taasisi za kitafiti pia zinaweza kuajiriwa na watu fulani kuwafanyia utafiti.

Kwa hapa Tanzania, tunajua kuwa vyama vya siasa hufanya tafiti zao lakini ni wazi kuwa matokeo yake hayaweza kukubalika kote kwa sababu ya hisia kuwa takwimu imechezewa. Wanasema anayemlipa mpuliza zumari ndio achaguaye wimbo.

Zipo taasisi za kielimu ambazo zimekuwa zikifanya tafiti za kura za maoni lakini nazo haziaminiki kwa sababu wahusika wengi wamekuwa na mafungamano na vyama, hasa chama tawala.

Taasisi za kiraia zikifanya tafiti nazo zinaonekana kama zinaelemea upande wa upinzani. Sheria nazo zimekuwa kikwazo cha ufanyikaji wa tafiti kwa sababu vibali wakati ni ngumu kupatikana.

Kwa ujumla kura za maoni, kama njia ya kujua maoni ya umma nayo ina changamoto zake.

Njonjo Mfaume ni Mhadhiri wa Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *