The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kelele au Matangazo?: Mtindo wa Wafanyabiashara Kuvutia Wateja Kupitia Vipaza Sauti

Sauti hizi hulenga kumshawishi mpita njia aende huko zinakotokea kwa lengo la kununua bidhaa au huduma zinazopatikana hapo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Hakuna sehemu utakwenda ndani ya jiji hili kuu la kibiashara usikutane na spika na vipaza sauti vingine vilivyofunguliwa kwa sauti za juu zenye lengo la kumshawishi mpita njia aende huko sauti zinakotokea kwa lengo la kununua bidhaa au huduma zinazopatikana hapo.

Sauti hizi unaweza kukutana nazo mara tu unapotoka ndani ya nyumba yako au ofisi yako. Hulazimiki kwenda masokoni, au pembezoni mwa barabara, ili uweze kuzisikia. Ukweli ni kwamba muda mwengine hukufuata hata nyumbani kwako; anaweza akawa ni mtu anasajili laini za simu au anauza sabuni za chooni.

Je, hizi ni kelele au ubunifu tu wa kimatangazo unaolenga kuwanufaisha wote, muuzaji wa bidhaa na huduma pamoja na mteja wake mtarajiwa? Kwenye tathmini yake ndogo iliyofanya katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam, The Chanzo ilishindwa kuja na jibu mahususi.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba wote, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida, wanakiri kwamba sauti hizo ni kelele lakini ni kelele ambazo wote wanaweza kuzivumilia kutokana na umuhimu wake, hususan ule wa kuwakutanisha wawili hao na kufanikisha biashara.

Athuman Bakari ni mfanyabiashara katika soko la Big Brother lililopo Manzese jijini hapa ambaye anasema kwamba sauti hizo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kuwavutia wateja kwenda kununua bidhaa kwenye kibada chake.

‘Sisi tunafanya biashara’

“Unajua kila mtu anakuwa na ufahamu wake,” Bakari, ambaye anauza mabegi ya mtumba sokoni hapo, aliiambia The Chanzo. “Kwa hiyo, maadamu yeye anaona kama ni kelele sawa, lakini sisi tunafanya biashara, siyo kwamba tunapiga kelele ilimradi tu. Hapana.”

Sauti hizi ni muhimu sana kwa wafanyabiashara kiasi ya kwamba kama ikitokea umeme unakatika, na mfanyabiashara hana njia mbadala ya kukifanya kipaza sauti chake kiendelee na kazi, hiyo inakuwa na athari ya moja kwa moja kwenye mauzo yao.

Hii ni kwa mujibu wa Juma Fadhili, mfanyabiashara mwengine sokoni hapo, anayejishughulisha na biashara ya nguo za mtumba. Fadhili, hata hivyo, hatupilii mbali madai kwamba sauti hizi zinaweza kuwa na athari kwao na wananchi wa kawaida kwa kipindi cha muda mrefu.

“Wataalamu wa afya walishatuambia kwamba hizi spika baadaye zitakuja kutuletea matatizo,” anaeleza Fadhili. “Lakini kwa sababu ndiyo utafutaji wetu, na ndiyo riziki zetu zinavyopatikana, basi hakuna jinsi. Lakini kiathari kweli zipo.”

The Chanzo ilimuuliza Stella Bakari, mkazi wa Manzese jijini hapa, ana maoni gani kuhusiana na matumizi ya spika na vipaza sauti hivyo ambaye alieleza kwamba kwake yeye matangazo hayo siyo kelele ikiwa inamsaidia kujua bei ya bidhaa husika.

“Hapana siyo kelele, yaani kwanza inakusaidia, kwa mfano, ulikuwa hujui bei ya begi ukifika pale unajua,” anasema Stella. “Ila kila mtu na anavyoona. Kuna mwingine anasema kelele. Lakini kwangu mimi siyo kelele. Zinamsaidia mtu kujua bei za bidhaa.”

Akihojiwa na The Chanzo kuhusiana na mtazamo wa mamlaka za Serikali kuhusiana na suala hili, Afisa Mazingira wa Halmashauri Jiji la Dar es Salaam Peter John alisema kwamba zipo kanuni na sheria zinazotawala matumizi ya spika na vipaza sauti ili kutunza usafi wa mazingira. Kelele ni aina moja ya uchafuzi wa mazingira.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2014, pamoja na kanuni zake za mwaka 2015, kelele ni sauti isiyokubalika na inayoudhi ambayo inamadhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

Malalamiko dhidi ya wafanyabiashara

John alisema kwamba ofisi yake ilishawahi kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Kariakoo kuhusiana na matumizi haya ya spika na vipaza sauti na wafanyabiashara, akibainisha kwamba kwa kiwango kikubwa viwango vya sauti na mitetemo vilivyowekwa na sheria na kanuni huwa vinakiukwa.

“Kwa hiyo, kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo ambayo ni ya makazi, wanatakiwa kuzingatia hiyo sheria [na] kuzingatia hiyo kanuni,” alitoa wito John. “Kwamba wahakikishe [hizo sauti] haziathiri mtu mwingine ambaye yupo katika maeneo hayo. Kelele wanazozitoa wahakikishe kwamba ziko katika viwango vinavyotakiwa.”

Dickson Kimaro ni Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu katika Jiji la Dodoma ambaye ameiambia The Chanzo kuwa hata huko kwenye makao makuu ya nchi, mamlaka zimekuwa zikipokea malalamiko kutoka kwa majirani kutokana na matangazo hayo ambapo wamekuwa wakichukua hatua kadhaa, ikiwemo kuwazuia wahusika kufanya hivyo.

Kimaro anaendelea kueleza kwamba wapo wafanyabiashara ambao hutoa matangazo yao kwa sauti ambayo siyo rahisi kuleta usumbufu kwa majirani. Lakini ipo changamoto kubwa katika maeneo ya mjini na masoko ikiwa ndiyo sehemu ambazo matangazo huweza kuzidi kiwango cha sauti kinachohitajika na kuleta usumbufu, anasema.

“Kuna zile sauti za kawaida kabisa ambazo siyo rahisi kuleta usumbufu kwa majirani wengine ambao wapo kwenye [hayo] maeneo,” alisema Kimaro wakati wa mahojiano na The Chanzo kwa njia ya simu. “Suala hili hujitokeza zaidi kwenye maeneo ya mjini na masoko. Nje ya mji huwezi kukutana na masuala kama hayo.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *