The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Utahitaji Kibali cha TCRA Kuweza Kuishitaki TCRA Mahakamani

Ni matakwa ya sheria ya EPOCA inayolalamikiwa kwa kuminya uhuru wa habari Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Ndiyo, utahitaji kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ili kuweza kuishitaki TCRA mahakamani kwa mujibu wa kifungu namba 68, kifungu kidogo namba mbili, cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010.

Sheria hii ni moja kati ya sheria zinazolalamikiwa sana kwa kuminya uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania na kifungu hiki kinatajwa kama moja kati ya vifungu vibaya sana vya sheria hiyo kwani inavizuia vyombo vya habari kupinga maamuzi ya TCRA mahakamani.

Sheria hii ya EPOCA, pamoja na kanuni zake, inaipa mamlaka TCRA kusimamia shughuli zote za kimawasiliano ya kielektroniki nchini, jukumu linaloipa TCRA wajibu wa kudhibiti uendeshaji wa vituo vya habari vya runinga, redio na hata vile vya mtandaoni.   

Pamoja na mambo mengine, TCRA husimamia utoaji wa leseni kwa vyombo hivi vya habari pamoja na kudhibiti maudhui yanayochapishwa na vyombo hivyo. Kukiuka sheria hii, pamoja na kanuni zake, kunaweza kupelekea adhabu mbalimbali, ikiwemo kwa chombo cha habari husika kutozwa faini au kupokonywa leseni yake, kwa muda au milele.

SOMA ZAIDI: Wadau Walalamikia Muamko Mdogo wa Kuandika Habari za Haki za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza

Vyombo mbalimbali vya kielektroniki nchini Tanzania vilishawahi kukumbana na kadhia hii, hali inayoibua malalamiko lukuki kutoka kwa wadau wa uhuru wa habari kila inapojitokeza. Malalamiko yanakuwa makubwa zaidi ukizingatia ugumu uliowekwa na sheria ya EPOCA pale chombo cha habari kinapotaka kupinga hukumu iliyotolewa na TCRA mahakamani.

Kifungu hicho namba 68(2) kinasema: “Mtu atapaswa kupata kibali kutoka kwa mamlaka [ya TCRA] ili kwenda mahakamani kwa ajili ya utekelezaji wa matakwa ya kifungu hiki [cha suluhu za kutofuata matakwa ya EPOCA] labda iwe ni kwa uamuzi mdogo.”

The Chanzo ilimuuliza wakili mashuhuri nchini Tanzania ambaye amehusika sana na harakati za kupigania haki za kidigitali Benedict Ishabakaki kifungu hiki kinamaanisha nini kwa lugha rahisi ambapo alisema ni kwamba mtu hawezi kuishitaki TCRA bila kupata kibali kutoka TCRA.

“Ni kwamba bila cheti cha mamlaka husika hutaweza kutekeleza maamuzi mahakamami labda iwe ni maombi madogo,” alisema Ishabakaki. “Kuelewa hiyo ni lazima tujue muktadha, yaani kupata picha kamili ya suala unalotaka kwenda nalo mahakamani.”

Mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu Alphonce Lusako anakubaliana na tafsiri ya Ishabakaki, akienda mbele zaidi kwa kusema kwamba kifungu hicho kinakiuka matakwa ya Katiba ya nchi inayoutambua mhimili wa Mahakama kama chombo cha mwisho cha utoaji haki nchini.

“Katiba yetu ya Tanzania, Ibara ya 30(3), inaeleza kwamba mtu yeyote ambaye amevunjiwa haki ana haki ya kwenda mahakamani kupinga maamuzi yalioyotolewa awali na mamlaka fulani,” alieleza Lusako. “Kwa hiyo, kifungu hiki kinakwenda kinyume kabisa na Katiba.”

SOMA ZAIDI: Serikali, Wadau Wabainisha Changamoto Zinazoikabili Tasnia ya Habari Tanzania

The Chanzo haifahamu mtu yoyote ambaye amewahi kujaribu kutaka kupinga maamuzi ya TCRA mahakamani licha ya kuwepo kwa vyombo vingi vya habari ambavyo vimekuwa waathirika wa maamuzi ya mamlaka hiyo.

Chombo cha habari cha hivi karibuni kabisa kuathiriwa na maamuzi ya TCRA ni DarMpya Blog ambayo mnamo Julai 6, 2022, ilizuiliwa kuchapisha maudhui mtandaoni kwa madai ya kushindwa kuhuisha leseni yake ya uchapishaji. 

TCRA ilidai iligundua hilo baada ya kwenda ofisini kwa DarMPya na kufanya ukaguzi kufuatia malalamiko juu ya habari iliyochapishwa na chombo hicho kuhusu maandamano ya Wamaasai nje ya Ubalozi wa Kenya kushinikiza nchi hiyo iache kile waandamanaji walikiita kuchochea mgogoro kati ya Wamaasai na Serikali huko Ngorongoro.

Katika habari yake, DarMpya ilisema kwamba waandamanaji hao siyo wenyeji wa Ngorongoro na wamepangwa “kupotosha” ukweli juu ya kile kinachotokea huko. The Chanzo ilimuuliza Mkurugenzi Mtendaji wa DarMpya John Marwa kama waliwahi kufikiria kuyapinga maamuzi ya TCRA mahakamani  ambapo alisema hawaoni haja ya kufanya hivyo.

“Niliomba leseni lakini mpaka sasa sijapewa, tumeambiwa [na TCRA] kwamba wanafanya tathmini na hatujui itachukua muda gani,” Marwa alieleza wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Hawajaninyima leseni kiasi kwamba niende mahakamani. Nilichoambiwa ni kwamba subiri tunafanya tathmini.”

SOMA ZAIDI: Wadau Walaani Kushikiliwa Mwandishi wa Habari Zanzibar, Wataka Aachiwe Huru

Hofu ya chombo cha habari kufungiwa au kunyimwa leseni ya kuchapisha imedaiwa kuwafanya waandishi na wahariri wao kuchuja maudhui wanayozalisha, hali ambayo wadau wanasema inadhoofisha dhana nzima ya uhuru wa habari nchini Tanzania.

Deodatus Balile ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambaye shirika lake limekuwa mstari wa mbele katika kuishawishi Serikali kuzifanyia marekebisho sheria kadhaa zinazolalamikiwa na wanahabari, ikiwemo ile ya EPOCA.

Balile, ambaye ni mwandishi na mhariri wa gazeti la Jamhuri, alisema kwamba sheria inayomtaka mtu kupata kibali cha TCRA ili aweze kuishitaki TCRA mahakamani “haijakaa vizuri” na ndiyo maana wao kama wadau wamekuwa wakipigania sana sheria hii na zingine kama hizi zifanyiwe marekebisho.

“Changamoto inayojitokeza ni pale ambapo mnaahidiwa kwamba mwaka huu tutabadilisha sheria, halafu mnaona kwamba mambo yanakaribia kuiva, mnazungumza vizuri na Waziri [mwenye dhamana ya habari] lakini mnajikuta muda umefika mnaambiwa hili hapana,” alisema Balile. “Mwaka jana hatukufanya vizuri, tutaendelea mwaka huu.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *