Mbeya. Wanakijiji wa Syukula siyo wageni wa shida na usumbufu unaohusiana na upatikanaji wa huduma bora na za haraka za afya ambazo zinawakumba Watanzania walio wengi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Ikiwa ni moja kati ya vijiji vitano vinavyounda kata ya Kimo, wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, Syukula haina hospitali, kituo cha afya wala zahanati.
Wanakijiji hapa hulazimika kufuata huduma za matibabu Kimo, ambapo kituo cha afya kilichojengwa mwaka 2021 kinahudumia watu takriban 18,676 kutoka Syukula na vijiji vingine vinne vya Kyimo, Katabe, Ilenge na Kibisi.
Kikiwa na wakazi wanaokadiriwa kuwa 1,200, Syukula, kwa vigezo vyote, ilikuwa ni kijiji sahihi kwa Dharura Fasta kupanua huduma yake ya usafiri wakati wa dharura za kiafya.
“Sitaki kuwaza nini kingetokea kusingekuwa na hii huduma kijijini kwetu,” Petrah Kajula, 25, alimwambia mwandishi wa habari hii aliyetembelea kijijini hapo mapema mwezi huu wa Agosti.
“Hapa [kijijini] hakuna huduma yoyote ya afya,” aliongeza Petrah. “Na ukitaka kuzifata hizo huduma nje ya kijiji, gharama hua ni kubwa sana. Wengi wetu huwa hatuzimudu.”
Maoni ya Petrah, mama wa mtoto mmoja, yalikuwa yanalingana na maoni ya wanakijiji takriban wote ambao The Chanzo iliongea nao ilipotembelea Syukula.
SOMA ZAIDI: Tutafakari Namna Bora ya Kuhakikisha Afya za Watu Wetu
Dharura Fasta
Kwa mujibu wa Shirika la Menejimenti ya Huduma za Bima na Afya (HIMSO), shirika lisilo la Kiserikali lenye makao yake makuu jijini Mbeya, kuna mambo makubwa manne ambayo huwacheleweshea watu kupata huduma za afya kwa haraka.
Mambo haya ni pamoja ufanyaji wa maamuzi, kwamba watu wengi huchelewa kufanya maamuzi ya kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pamoja kupanga taratibu za usafiri.
Mengine ni kukosekana kwa nyenzo za usafiri hata pale mwananchi anapokuwa amefanya maamuzi ili aende kupata huduma husika pamoja na upatikanaji wa huduma zenyewe pindi mtu anapofika katika kituo cha kutolea huduma.
Huu ndiyo msingi wa kuanzishwa kwa huduma ya Dharura Fasta ambayo hutoa huduma ya usafiri kwa mwanachama wakati wa dharura za kiafya.
Kupitia Dharura Fasta, mwanachama husafirishwa kutoka nyumbani kwake mpaka kwenye kituo cha afya, pale ambapo gari za kubebea wagonjwa za Serikali zinapokosekana.
SOMA ZAIDI: Afya ya Akili: Ushuhuda wa Mhanga na Mapambano ya Kupata Matibabu
Huduma hii kwa sasa inapatikana kwenye mkoa wa Songwe (Halmashauri ya Wilaya ya Ileje) na Mbeya (Halmashauri ya wilaya ya Rungwe), kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HIMSO Fadhili Mtanga.
Kwa mujibu wa Mtanga, ambaye pia ni mwandishi wa kazi za fasihi, huduma hiyo ambayo ilianza rasmi mwaka 2017, mpaka sasa inahudumia wanachama wapatao 30,000 kutoka kwenye mikoa hiyo miwili.
“Mtu huwa mwanachama baada ya kuchangia Shilingi 1,000, kwa wilaya kama Rungwe au Shilingi 2,500 kwa baadhi ya Halmashauri ambazo zina jografia ngumu kama wilaya ya Chunya,” Mtanga aliiambia The Chanzo.
Kijiji pia kinaweza kujiunga na huduma hiyo kwa kuchangia Shilingi 180,000 kwa Halmashauri ya Mbozi na Rungwe na Shilingi 200,000 kwa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali.
Kijiji kikiwa kimejiunga na huduma hii kinakuwa kwenye nafasi ya kunufaika kwa namna tatu, alisema Mtanga. Moja, mjamzito wakati wote atapelekwa hospitalini pale ambapo anahitajika kwenda huko.
“Watoto wote waliochini ya miaka mitano watakimbizwa kupata huduma za afya wakiwa kwenye dharura ya kiafya,” alibainisha Mtanga.
“Pia, endapo itatokea mtu yeyote katika kijiji husika atafariki akiwa ndani ya halmashauri husika akipatiwa matibabu atasafirishwa na huduma kwenye kijiji hicho,” aliongeza kwa kusema.
SOMA ZAIDI: Tusiruhusu Binadamu Atenganishwe Na Afya Yake
Uokoaji wa maisha
Julieth Kilala ni Mratibu wa Huduma ya Afya ya Mama na Watoto kutoka wilaya ya Rungwe ambaye ameihusisha huduma ya Dharura Fasta na uokoaji wa maisha ya akina mama na watoto wilayani humo.
Akiongea na The Chanzo wakati wa mahojiano maalum, Kilala alikiri pia namna bima hiyo ilivyopunguza tabia ya baadhi ya akina mama kujifungulia nyumbani wilayani humo.
“Akina mama wanawahishwa kufika kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za kiafya tofauti na ilivyokuwa mwanzoni,” Kilala alisema akiwa ofisini kwake katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe. “Wengi walikuwa wakikosa huduma kwa kukosa usafiri.”
Doset Melele ni Mwenyekiti wa kijiji cha Mbeya 1, Kata ya Isongole, wilayani Rungwe.
Melele aliiambia The Chanzo kwamba hadhani kwamba wananchi wake wangeweza kupata huduma stahiki za afya bila uwepo wa huduma ya Dharura Fasta, akitaja hali ngumu ya maisha kama sababu.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ukatili Baina ya Wapendanao Siyo Jambo la Kifamilia
“Hapa kijijini kwetu hatuna hospitali sisi,” alisema Melele. “Na changamoto ya usafiri ilitusumbua sana huko nyuma. Hali za maisha za wananchi wetu haziridhishi. Angalau hii huduma inatusaidia tunapata huduma kwa haraka.”
The Chanzo ilimuuliza Petrah anadhani ni mchango gani huduma ya Dharura Fasta inatoa kwenye kuimarisha ustawi wake na wanawake wenzake kwenye kijiji chao cha Syukula ambapo alisema inatoa mchango “mkubwa sana.”
“Ada ya Shilingi 1,000 tu ya uanachama ilinisaidia mimi binafsi kuwahishwa hospitali, sikutoa pesa nyengine yoyote ya usafiri,” alieleza Petrah. “Kwa watu kama sisi tuliokuwa tumezoea shida za usafiri, hilo ni jambo kubwa sana.”
Lakini Mtanga ameieleza The Chanzo kwamba licha ya huduma hii kuwasaidia wananchi wa hali ya chini, kumekuwa na mwamko mdogo sana miongoni mwa wananchi kujiunga na huduma hiyo.
“Viko vijiji ambavyo viongozi wanachelewa sana kufanya maamuzi ya kujiunga na vijiji vyao,” alisema Mtanga wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Tunaendelea kuwashajihisha wajiunge kwa kuwashirikisha kwenye ngazi mbalimbali za uongozi ili waeleze kwa nini ni muhimu wajiunge na hii huduma. Tunaamini wakishajua hilo itakuwa ni rahisi kwao kujiunga.”
Mbembela Asifiwe ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mikoa ya kanda za juu kusini. Anapatikana kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com.