Dar es Salaam. Wizara ya Katiba na Sheria haikutoa mrejesho juu ya swali la kwa nini Serikali hushindwa kutekeleza amri na maamuzi za Mahakama, kitu ambacho wadau wamebainisha kinatishia suala zima la utawala wa sheria nchini pamoja na dhana ya mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya dola.
Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na The Chanzo, Serikali mara kadhaa imekuwa ikishindwa kutekeleza maagizo yanayotolewa na Mahakama, hususan kwenye kesi ambazo yenyewe ni mshtakiwa, hali inayoibua maswali juu ya utayari wa Serikali kuheshimu taratibu zilizowekwa na Katiba ya nchi na mikataba mingine ya kimataifa kuhusiana na suala la utoaji wa haki.
Ibara 107A, ibara ndogo nambari moja, ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, inaitaja Mahakama kama “mamlaka ya utoaji haki” nchini.
Pia, tovuti rasmi ya Serikali inaielezea Mahakama na idara zake kama “jiwe la msingi la kudumishia sheria na taratibu katika jamii ya kidemokrasia na yenye uhuru” na kwamba Mahakama ni “mpango mkuu wa utawala bora na kutetea utawala wa sheria.”
Lakini matakwa haya ya kikatiba na uelewa huu wa Serikali mara nyingi vimekuwa havionekani pale Serikali inaposhindwa mahakamani kwenye kesi yenye maslahi nayo na hivyo kushindwa kutekeleza hukumu na maagizo yanayoambatana na hukumu hiyo.
“Serikali inadharau misingi ya utawala wa sheria na haioni kwamba inawajibika kufuata maamuzi ya vyombo vya kisheria,” Jenerali Ulimwengu, wakili na mwanaharakati wa siku nyingi, alisema wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Ni tabia mbaya inayojenga utamaduni wa kutokuheshimu sheria.”
SOMA ZAIDI: Je, Ni Haki kwa Serikali Kuwaweka Rumande Washtakiwa Halafu Kufuta Kesi Bila Kuwalipa Fidia?
Sheria ya ndoa
Moja kati ya uamuzi uliopokelewa kwa furaha na wadau wengi ni ule wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliosema kwamba vifungu nambari 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa, ambavyo vinaruhusu mtoto wa kike kuanzia miaka 15 kuolewa, vinavunja Katiba.
Mahakama iliitaka Serikali kubadilisha vifungu hivyo ndani ya mwaka mmoja, hatua ambayo iliifanya Serikali kukata rufaa mwaka 2017.
Mnamo Oktoba 2019, Mahakama ya Rufaa ilibakiza maamuzi ya awali ya Mahakama Kuu na kusisitiza vifungu hivyo vinavunja sheria za kimataifa juu ya haki za watoto ambazo Tanzania imeridhia.
Mahakama pia ilisema kuweka umri wa mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 15 tofauti na wa kiume siyo upendeleo chanya na inamuweka mtoto wa kike katika hatari zaidi ya matendo ya ukatili.Mpaka leo hii Serikali haijaweza kutekeleza maamuzi ya Mahakama.
Mnamo Aprili 28, 2021, aliyekua Waziri wa Katiba na Sheria Professa Palamagamba Kabudi, alilieleza Bunge kwamba Serikali imeamua kukusanya maoni ya wadau mbalimbali ili kuweza kuadili sheria hiyo ya ndoa.
Mpaka leo, hata hivyo, ikiwa ni miaka takribani sita toka Serikali ipewe maelekezo na Mahakama juu ya kubadili sheria hii ndani ya mwaka mmoja, mabadiliko hayo hayajafanyika.
SOMA ZAIDI: Ndoa za Utotoni Zinavyowanyima Fursa Mabinti Kutimiza Ndoto Zao
Mgombea binafsi
Moja kati ya uamuzi mkubwa ambao Serikali imegoma kuufanyia kazi ni ule uliotolewa mnamo Juni 14, 2013, na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu uliyoitaka Tanzania kuchukua hatua za kikatiba na kisheria kuruhusu wagombea binafsi kwenye chaguzi za urais, ubunge na udiwani.
Uamuzi huo ulifuatia kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo mnamo Juni 2011 na mwanasiasa Christopher Mtikila, akishirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ikiishtaki Serikali kuminya uhuru wa wananchi kushiriki kwenye masuala ya uongozi kwa kuzuia mgombea binafsi.
Kwenye hukumu yake iliyoitoa siku hiyo ya Juni 14, 2013, Mahakama ya Afrika iliikuta Serikali na hatia ya kukiuka ibara nambari 2, 3, 10 na 13 (1) za Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu. Ibara nambari 2 ya Mkataba huo inazuia mtu kubaguliwa kwa namna yoyote ile.
Ibara nambari 3 inahusu watu wote kuwa sawa mbele ya sheria na kwamba kila mtu anastahili ulinzi wa kisheria. Ibara ya 10 inahusu haki ya raia kujumuika huku ibara nambari 13(1) inahusu haki ya kila raia kushiriki kwenye uendeshaji wa Serikali, iwe ni moja kwa moja au kupitia kwa mwakilishi.
SOMA ZAIDI: Lini Polisi Iliahidi Hadharani Kutekeleza Ushauri Kutoka Chama cha Upinzani?
Licha ya maagizo hayo ya Mahakama ya Afrika, na licha ya ukweli kwamba Serikali haikukata rufaa, Serikali imeshindwa kuchukua hatua zilizopendekezwa ili kuruhusu wagombea binafsi kwenye chaguzi za urais, ubunge na udiwani nchini Tanzania.
Na wakati hii ni moja ya kesi kubwa mashuhuri inayoonesha kushindwa kwa Serikali kutii maagizo ya Mahakama, hii siyo kesi pekee ambayo Serikali imeshindwa na kuagizwa kufanya mabadiliko ya kisheria lakini mpaka sasa imeshindwa kufanya hivyo.
Mnamo Machi 25, 2022, kwa mfano, Mahakama ya Afrika Mashariki ilitamka kwamba vifungu nambari 3,4,5,9,15 na 29 vya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 vinakiuka ibara 6(d), 7(2) na 8(1)(c) za Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuitaka Serikali kuchukua hatua stahiki kubadilisha hali hiyo.
SOMA ZAIDI: Kuachiwa kwa Mbowe na Mapungufu ya Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania
Hata hivyo, mpaka wakati wa kuandika habari hii, Serikali haikuwa imetangaza hadharani hatua hizo zilizoamriwa kwenye kesi hiyo iliyofunguliwa na Freeman Mbowe, Zitto Kabwe, Hashimu Rungwe, Seif Sharif Hamad, Salum Mwalim na LHRC. Hii ni moja kati ya kesi nyengine nyingi tu.
Kupoteza imani ya wananchi
Dk Rugemeleza Nshala ni moja kati ya mawakili mashuhuri nchini Tanzania ambaye amewawakilisha watu wengi kwenye kesi zao dhidi ya Serikali. Wakati wa mahojiano na The Chanzo, gwiji huyo wa sheria alisema kwamba anaihurumia Serikali akiona inafanya mambo kama haya kwani inajiondoshea imani kwa wananchi.
“[Matendo haya] yanawaonesha wananchi kwamba yenyewe [Serikali] ipo juu ya sheria,” Nshala, ambaye amewahi kuhudumu kama Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema. “Sasa hapo unawaambia tena watu waiamini Serikali yao?”
Kwa Nshala, hii tabia ya Serikali kutotekeleza maagizo ya Mahakama ni sehemu tu ya tatizo kubwa linaloikabili Tanzania kwa sasa: uwajibikaji kwa wale waliopewa dhamana ya uongozi. Dk Nshala anaamini pia mfumo mzima wa utoaji haki nchini una dosari kadhaa za msingi.
“Yanatakiwa mabadiliko makubwa sana katika mfumo wa kuendesha kesi dhidi ya Serikali,” alisema Dk Nshala. “Ni lazima wote tuwe sawa mbele ya sheria.”
SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo Serikali Inavyoweza Kuuboresha Mfumo wa Haki Jinai Tanzania
Ulimwengu anadhani ipo haja kwa Serikali kujitathmini na kubadilika, akionya kwamba kama hali itaendelea kama ilivyo hivi sasa matokeo yake ni Tanzania kuendeshwa kwa sheria ya msituni, kwamba mwenye nguvu anatimiza anachokitaka bila kuwepo kwa uwajibikaji wowote.
Licha ya kufuata taratibu kama wizara husika ilivyoelekeza, The Chanzo ilishindwa kupata majibu kutoka kwa Waziri wa Katiba na Sheria Damas Ndumbaro. The Chanzo ilitaka kufahamu kwa nini Serikali mpaka sasa haijatekeleza maagizo haya ya Mahakama na endapo kama kuna mpango wowote wa kufanya hivyo.
Wizara iliomba tutume maswali kupitia kwa msemaji wake lakini licha ya kufanya hivyo na kusubiri kwa takriban wiki mbili, The Chanzo ilishindwa kupokea mrejesho wowote kutoka wizarani.
Kutokujali
Victor Kweka ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria kutoka chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo ambaye ameiambia The Chanzo kwamba sababu kubwa kwa nini Serikali haihisi kulazimika kutii maagizo ya Mahakama ni kutokujali na kudhani kwamba hakuna mtu anaweza kuwafanya kitu.
Hii, hata hivyo, haimaanishi kwamba hali hiyo haitaliathiri taifa la Tanzania kwa namna yoyote ile, ametahadharisha Kweka ambaye pia ni wakili.
“Athari ni kubwa,” alisema Kweka wakati akihojiwa na The Chanzo. “Kwa sababu kama unakuwa na mhimili ambao hautaki kuheshimu mamlaka ya mhimili mwingine hapo kunakuwa na tatizo kubwa.
Huu ni ukiukwaji wa Katiba iliyobainisha kwa ufasaha haya mambo. Kitendo hiki pia maana yake ni kwamba hata lile tamko la kwamba sisi ni nchi ya kidemokrasia, ni nchi ambayo inaongozwa katika misingi ya haki na utawala bora, linakuwa linavunjwa.”
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.