The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kuondolewa Wakazi Loliondo: Kama Siyo Machozi Yao, Kipi Kitazuia Operesheni ya Serikali Dhidi ya Wakazi Hao?

Nguvu za pamoja zinahitajika kukabiliana na mitazamo ya kijamii na kiuchumi inayoilazimisha Serikali kupora ardhi za wananchi kwa jina la uwekezaji.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Septemba 30, 2022, Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) ilitupilia mbali ombi la wakazi wa Loliondo  katika kesi inayohusu mgogoro wa ardhi kati yao na Serikali ya Tanzania. Hukumu hiyo ilibaki kuwa tumaini la mwisho la jamii hiyo katika kulinda ardhi yao dhidi ya dhamiri ya Serikali ya kuitwaa.

Hatua hiyo ilikuja ikiwa miezi minne tayari imepita tangu Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuonesha dhahiri kutaka kutimiza nia yake ya kukamilisha zoezi la kuwaondoa wakazi wa vijiji 14 katika tarafa za Loliondo na Sale. 

Eneo hilo la vijiji hivi 14 vilivyopo katika kata nane na tarafa mbili za Loliondo na Sale linapatikana Wilaya ya Ngorongoro, kaskazini mwa Tanzania, na limekuwa kwenye migogoro kwa takribani nusu karne sasa. 

Kurejeshwa tena kwa operesheni za Serikali mwanzoni mwa mwezi Juni 2022, kumekatisha kipindi kifupi cha fungate tangu operesheni ya mwisho kufanywa katika eneo hilo mwaka 2017. 

SOMA ZAIDI: Kashfa ya Loliondo Inatuonyesha Kwamba Uhifadhi Tanzania Upo Kwa Malengo ya Kibiashara, Siyo Kulinda Mazingira

Mashambulio

Mnamo Juni 9 na Juni 10, 2022, tulishuhudia picha zikisambazwa katika mitandao ya kijamii zilizosemwa kuwa ni za wakazi wa Loliondo zikioneesha watu wameumizwa vibaya sana na vitu vyenye ncha kali au alama za risasi.

Pia, tuliona vipande vya video vikionesha mapigano kati ya askari polisi na wananchi jamii ya Kimaasai huku milio ya risasi na mabomu ya machozi ilikuwa ikisikika.

Kwa nyakati mbalimbali, Serikali imekuwa ikiendesha operesheni za kuwaondoa wafugaji wa jamii ya Kimaasai katika eneo la Loliondo na Sale kupisha utalii, uhifadhi na uwekezaji wa makampuni kutoka nje.

Katika operesheni zote kuanzia zile za wakati wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete hadi ile chini ya Rais John Pombe Magufuli na sasa chini ya Rais Samia maumivu na madhara makubwa yameachwa kwa wananchi wa Loliondo, ikiwemo kubolewa kwa makazi yao, kujeruhiwa, vifo, kupotezwa kwa mifugo yao na kuenea kwa vitisho.

SOMA ZAIDI: Ufafanuzi Mdogo wa Kile Kinachoendelea Ngorongoro

Machozi na damu za wananchi hao kwa nyakati zote havijaweza kuzuia mpango wa Serikali na vyombo vyake vya mabavu wa kuwaondoa wananchi hao. 

Kitu pekee kinachosikika kwa wananchi hawa wanyonge ni vurugu za milio ya risasi, mabomu ya machozi, kufunguliwa kesi, mateso na unyanyasaji dhidi yao, huku miili yao ikishambuliwa na njaa kali, ombwe za bongo za watoto wao zikizibwa na ujinga kutokana na ukosefu wa huduma ya elimu kama inavyostaili. 

Uwekezaji

Serikali kwa nyakati zote imekuwa ikisukumwa na haja ya kukidhi masharti ya kimataifa ya uhifadhi, kuvutia watalii na kukidhi mahitaji ya uwekezaji wa kigeni huku ikipuuza vilio vya wananchi.

Badala ya Serikali kusikiliza vilio vyao, imekuwa ikiwatuhumu wananchi kuwa wanaharibu mazingira na kuzuia maeneo ya mazalia ya wanyapori, kwa hiyo kuwaondosha ni jambo linalozingatia maslahi ya uhifadhi na ikolojia ya mazingira kwa ajili ya uendelevu wa maliasili. 

Wafugaji wanaopinga kuondolewa na kulinda ardhi yao dhidi ya uporaji wanaitwa wahamiaji, wachochezi na wengine wanabambikiwa kesi.

Jambo linalotia matumaini kidogo ni kuwa Wamaasai hawa hawajabaki peke yao kwenye mapambano yao dhidi ya hujuma za Serikali. 

Wapo wanaharakati walioonesha kuungana nao pamoja na wanasiasa wa vyama vya upinzani, hususan ACT-Wazalendo na CHADEMA. 

SOMA ZAIDI: Kuwaondoa Wananchi Ngorongoro ni Shambulio Dhidi ya Ufugaji wa Asili

Katika kutimiza azma yake, Serikali imekuwa ikipata nguvu kutoka chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM), Bunge, vyombo vya mabavu kuanzia Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Askari wa Uhifadhi na Jeshi la Wananchi.

Aidha, makampuni ya uwekezaji na mashirika ya kimataifa yanayotoa masharti yanayopaswa kufuatwa na Serikali yamekuwa mstari wa mbele katika kubariki zoezi hili la Serikali. 

Halikadhalika, vyombo vya itikadi kama vile vyombo vya habari na baadhi ya watu wenye ushawishi kama vile wasanii wamekuwa wakiipaka rangi operesheni na kuiuza kwa Watanzania na dunia kwa ujumla kama ni jambo jema.

Mizani ya kimapambano

Mshikamano wa wakazi wa Loliondo na baadhi ya wanaharakati na wanasiasa na vyama vyao unaweza kuchambuliwa na kuwekwa kwenye mizani ya kimapambano na kupata makundi mawili.

Kundi la kwanza ni lile linalotazama mshikamano na huo katika jicho la haki za binadamu pekee, kwamba operesheni hizi zinaendeshwa kwa mabavu ambayo yanapelekea vifo, kujeruhi, utesaji na madhila kwa watoto, wanawake na wazee. 

Kwao, wanachopinga ni matumizi ya nguvu kupita kiasi hadi kupelekea kuvunja haki za binadamu kama zilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa (UN). 

Pia, wanatazama kisa cha Loliondo kama kisa mahususi bila kufungamanisha na visa vya makundi mengine ya wazalishaji wadogo nchini. Kwa ufupi, tunaweza kusema kundi hili halitazami kiini cha tatizo.

SOMA ZAIDI: Namna Ukosefu wa Ardhi ya Kutumia Unavyogeuka Kuwa Janga Kilosa

Kundi la pili, kwa upande mwingine, linalitazama suala la Loliondo kama mwendelezo wa dola kupora haki za wananchi juu ya umiliki na utumiaji wa rasilimali zao. 

Kwao, wanapinga mtazamo wa kwamba ardhi ni bidhaa, au mtaji, unaopaswa kutazamwa katika kutengeneza faida zaidi kuliko kukidhi mahitaji ya kijamii. 

Mtazamo huu unaona uporaji hautaishia kuwaathiri wafugaji wa Loliondo pekee, bali makundi mengine pia kama tunavyoshuhudia maeneo mengi nchini tayari yameathiriwa na uporaji wa ardhi kimabavu au kisheria kwa jina la uwekezaji. 

Wanachama wa kundi hili wanaona siyo sahihi kuchukulia matumizi ya ardhi kijamii aidha kwa makazi, kujipatia kipato (kujikimu) au kiutamaduni (matambiko, ibada na dawa) kuwa ni kuzuia maendeleo.

Adha za wazalishaji wadogo

Kwangu, naunganisha kisa cha Loliondo na kile kinachoyakabili makundi mengine ya wazalishaji wadogo ya wakulima, wavuvi na wachimbaji wadogo wa madini na wafugaji.

Makundi haya yamekuwa yakikabiliwa na wimbi kubwa la uporaji wa utajiri wao wa asili tangu kuingia kwa sera za kiliberali mamboleo katika sura ya ugenishaji wa ardhi, uwekezaji, ubinafsishaji na ulegezaji wa masharti. 

Shida zao pia zinaweza kuhusishwa na matumizi ya mantiki na mitazamo ya soko (ubidhaishaji) kwenye usimamizi wa rasilimali muhimu kama vile ardhi, madini, misitu na bahari.

Mbinu mashuhuri zinazotumika kupora rasilimali hizi kutoka kwa wenyeji na wazalishaji wadogo ni sheria za uhifadhi, sera za ubidhaishaji wa ardhi na kupigia chapuo uwekezaji wa makampuni makubwa kutoka nje.

SOMA ZAIDI: Barua ya Wazi kwa Waziri Bashe Juu ya Mradi wa ‘Ujenzi wa Kesho Njema’

Nguvu za kupinga na kukataa uporaji wa ardhi Loliondo zinapaswa zielekezwe kwenye mtazamo unaoingoza Serikali na taasisi za kimataifa linapokuja suala la ardhi na rasilimali zingine kama vile bahari, misitu na madini, yaani mitazamo yote inayoishia kunyangánya rasilimali na kuwafukarisha wananchi.

Pia, mapambano ya watu wa Loliondo yasichukuliwe ni mapambano ya Wamaasai ambao wana upekee aidha kwa historia au kabila lao bali tunapaswa kuunganisha na mapambano mengine yanayofanywa na wananchi kukataa kunyang’anywa ardhi zao kwa jina la uwekezaji au kile kinachoitwa maslahi ya umma popote pale.

Mwisho, ikiwa machozi, jasho na damu hayajasikilizwa na Serikali, sasa ni wakati wa mavuguvugu ya kijamii na mashirika ya kiraia yenye mtazamo wa kimaendeleo (progressive) yanayopinga kunyang’anywa au uporaji wa ardhi ya Loliondo kuingilia kati.

Ni lazima tufungamanishe kati ya kunyang’anywa kwa wakazi wa Loliondo ardhi yao na athari pana za ubidhaishaji wa sheria za ardhi na wimbi kubwa la unyakuaji wa ardhi nchini Tanzania.

Idrisa Abdul Kweweta amejitambulisha kama mjamaa na mtafiti anayependa kuchambua mambo ya kijamii. Barua pepe yake ni idrisakweweta@yahoo.com. Yupo Twitter pia kama @idrisa_kweweta. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *