The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Magereza Walivyomuachia Majonzi Mteja Wangu ‘Rasta’ kwa Kumnyoa Nywele Zake

Watu wa imani ya Rastafarai kunyolewa nywele zao kwa nguvu na pasipo ridhaa yao, kabla hata ya kukutwa na hatia, ni jambo la kikatili na la kinyanyasaji linalopaswa kulaaniwa na kukemewa.

subscribe to our newsletter!

Ilikuwa ni siku ya neema na baraka kubwa kwangu na kwa mteja wangu baada ya Jamhuri kuamua kuiondoa/kuifuta kesi iliyokuwa ikimkabili. Kama wakili, hususani wa jinai, hamna jambo linalofurahisha kama kushuhudia haki ikitendeka na mteja wangu kuachiwa, au kutamkwa kuwa, “huru.”

Hata hivyo, furaha yangu haikuizidi ile ya mteja wangu kwani baada ya kumpatia taarifa hizo, alisimama, akakaa, akasimama tena, kisha akakaa, akatoa gwala (tano) la kwanza, kisha la pili, la tatu, huku akisema, “Amani na upendo, kaka. Irie, kaka.” Kama nisingeuweka mkono wangu mfukoni, basi naye angeendelea kugonga mpaka mwisho!

Hakika nililiona tabasamu lisiloelezeka usoni mwake, mdomo wake ulichanua na meno yake yalicheza cheza kwa heko. Alisema: “Asante sana mani. Ninashukuru sana. Niko huru. Nina furaha!”

Ndugu yangu huyu hakuacha kushukuru kwa kushikamana naye kwa kipindi chote cha kesi hiyo ambayo ilimkabili kwa takribani muda wa miezi 17, ambayo ni dhahiri, pasi na shaka, ilikuwa miezi 17 mirefu kuliko yote maishani mwake.

Safari yake ya miezi 17 ilianza na usiku mmoja ulioelezwa kuwa alikutwa na “puli moja” ya bangi, iliyoelezwa kuwa ya gramu 34.50 na hapo hapo ndipo maisha yake yakakumbwa na mkwamo mmoja usiomithilika.

Msoto wake ulianza katika Kituo cha Polisi ambako kitendo cha yeye kuwa mtu wa imani ya Rastafari – mtu wa amani, kama anavyosema – hakikuwa na msaada sana kwani alizongwa zaidi kwa hali yake hiyo ya kuwa na nywele za rasta kichwani mwake.

Hali na mambo ilizidi kumuendea kombo pale ambapo alipelekwa katika Gereza la Segerea. Ni huko ndipo alipoiona chungu kamili ya kuwa kwake mwana Rastafari na kuwa na rasta kichwani mwake.

Wakati awali akiwa Kituo cha Polisi alitishwa kunyolewa nywele na baadhi ya maofisa polisi, huko katika Gereza la Segerea wao hawakuwa na muda wa kumtisha kwani wao ni watu wa kazi kweli kweli na hivyo wakamnyoa nywele zake – vishungi (maarufu kama rasta/ dredi).

Walininyoa

“Walininyoa mani,” alinieleza ndugu yangu huyu katika awamu ya kwanza kabisa nilipokutana naye na kunieleza kisa chake. “Yaani hamna siku nimewahi kujihisi mnyonge na kupokwa utu kama hiyo siku.”

SOMA ZAIDI: Rastafari Tunaonekana Kama Raia Daraja la Pili Tanzania 

Unyonge aliokuwa nao na mapenzi yangu binafsi na muziki wa Reggae, ambao ni muziki mkuu wa jamii ya watu Rastafari na mapenzi yangu binafsi na imani na misingi ya kimaisha ya jamii ya Rastafari, ilinifanya nikubali kushikamana na huyo ndugu katika kesi yake hiyo ya mchongo.

Katika kipindi cha mwaka mzima nimekuwa nikishikamana na ndugu yangu huyu na kufika mahakamani katika nyakati tofauti mpaka dakika ya mwisho ambapo baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuwasilisha ushahidi wowote ule Mahakama ikaifuta kesi hiyo.

Lakini hata baada ya kesi hiyo kufutwa, ndugu yangu huyu tayari alishajiona kama mkosefu, mwenye dhambi, mhalifu na mwenye hatia.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba afisa mmoja katika Gereza la Segerea alishamuhukumu kwa kumnyoa nywele zake. Maelezo na hisia zake zilinisisimua sana.

“Nywele kwa mtu Rasta ni sehemu ya mwili, asili na ni ibada kwake,” alinieleza mteja wangu huyo. “Na mwili kwake ni hekalu, ambalo halina budi kutunzwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa.”

Kwa maelezo yake, maumivu aliyoyasikia aliyafananisha na maumivu ambayo angeyasikia endapo ingeamuliwa akatwe mkono.

Kitendo hicho kilimpoka haki zake zote za msingi za kuabudu, kuishi kwa staha na uhuru wake binafsi na hata haki ya usawa chini ya sheria. Nywele kwake ni imani na ibada na nywele kwake ni tafsiri ya uhuru na utu wake.

Wakati hii kesi ikiwa inaendelea, naye kaka mkubwa Innocent Richard Nganyagwa alipata kupitia shuruba za aina hii hii akiwa mikononi mwa polisi huko mkoani Iringa ambapo alikamatwa na kushutumiwa kwa mambo mbalimbali ya uhalifu.

SOMA ZAIDI: Ras Inno: Hatutungi Nyimbo Tukaziimbe Rumande

Pamoja na shutuma hizo, naye alitishiwa kunyolewa nywele zake – vishungi (rasta) – na askari polisi, kitendo ambacho kinaingiliana na haki zake kama mtu.

Jambo la kikatili

Jambo hili la watu wa imani ya Rastafari kutishiwa kunyolewa, na hata kunyolewa kwa nguvu na pasipo ridhaa yao, kabla hata ya kukutwa na hatia, ni jambo la kikatili, la kinyanyasaji na linapaswa kukemewa.

Ni muhimu sana kwa vyombo vya dola kama Mahakama, Jeshi la Polisi pamoja na Magereza kujitathmini na kuona kama kweli uwepo wao unapaswa kuwa chanzo cha unyanyasaji huu kwa raia wa Tanzania.

Hoja mufilisi na zisizokuwa na misingi yeyote ile ya kisheria na zisizo na utashi wowote ule wa kifikra zinapaswa kukemewa vikali, ili kuhakikisha jamii ya watu Rastafari nao wanaweza kufurahia haki zao za kisheria na kiasili.

Lugha hizi ni kama zile alizoelezwa “mteja” wangu kuwa, “Mtu Rasta ukibaki na nywele unaweza kujinyonga nazo,” au kwamba, “Watu Rasta wanakuwa wabishi au wanajawa na ubishi.”

Mteja wangu huyu ameachiwa huru kwa kesi yake kufutwa. Hata hivyo, ameondoka pia mahakamani akiwa na kumbukumbu, jeraha, kovu na doa kubwa lililouchafua moyo wake – si lingine bali ni lile la kupokwa utu wake!

Jasper “Kido” Sabuni ni mchambuzi wa masuala ya kijamii. Anuwani yake ya barua pepe ni kidojasper@gmail.com. Anapatikana pia Twitter kama JasperKido. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *