The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Sakata la Ruto na Kasumba ya Kuzungumza Kiingereza Afrika Mashariki

Kwa kuamua kutumia Kiingereza badala ya Kiswahili, tena nchini Tanzania ambapo watu wake wengi ni wazungumzaji wa Kiswahili, Rais Ruto amezipa nguvu kasumba zinazohusu lugha hizo mbili.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Oktoba 9, 2022, Rais wa Kenya William Ruto alitembelea Tanzania katika ziara ya siku mbili iliyoishia Octoba 10, 2022, ikiwa ni ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu achaguliwe kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya kwenye uchaguzi uliofanyika Agosti 9, 2022. 

Tanzania ilikuwa ni kituo chake cha tatu baada ya Rais Ruto kuzizuru nchi za Uganda na Ethiopia.

Ujio wa Ruto nchini Tanzania ilikuwa ni fursa muhimu ya kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ambayo, pamoja na Uganda, ni waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), tangu ile ya awali iliyoanzishwa mwaka 1967 na hii ya sasa waliyoifufua mwaka 2000. 

Ilikuwa ni malengo ya waasisi wa EAC kuleta utengamano na mshikamano zaidi kati ya wakaazi wa nchi hizi tatu, na nyengine zilizokuja kujiunga baadaye – Rwanda, Burundi, Sudani ya Kusini, na DRC –, huku lugha ya Kiswahili ikitegemewa kutoa mchango mkubwa kwenye kufanikisha malengo hayo.

Ilitegemewa kwamba viongozi wa nchi wananchama wa EAC, hususan wale ambao mataifa yao wamekiteua Kiswahili kuwa lugha ya taifa, kama vile Tanzania, Kenya na Uganda, watumie lugha hii kwenye shughuli za kiserikali, hususan wakiwa ziarani kwenye mwanachama wa EAC.

Ni katika muktadha huu ndipo nilipoungana na wana EAC wengine kumshangaa Rais Ruto alipogoma kutumia Kiswahili alipokuwa nchini Tanzania na kuomba ruhusa ya kutumia Kiingereza.

‘Utanichanganya’

Akiwa ziarani nchini Tanzania, Ruto alimuomba ruhusa mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan kutumia Kiingereza kwenye hotuba yake, akisema: “Nimen’gan’gana sana na Kiswahili asubuhi lakini kidogo inanichanganya. Utaniruhusu niseme Kiingereza ndiyo nieleweke vizuri.”

Rais Ruto hakuishia hapo tu kwani alimnyamazisha hata mkalimani aliyekuwa akiitafsiri hotuba yake kwenda kwenye lugha ya Kiswahili, akisema: “Sidhani [kama] kuna haja ya kutafsiri. Kuna mtu haelewi Kiingereza hapa?” 

Alipoambiwa ni kwa ajili ya vyombo vya habari, Rais Ruto alimsihi mkalimani aache kutafsiri, akisema: “Haya nitarudia mimi [mwenyewe]. Wewe achana nayo. Nitarudia baadaye. Wewe utanichangaya zaidi wewe. Pole.”

Nilipomsikiliza Rais Ruto, binafsi nilishangaa na kuzongwa na maswali kadhaa kichwani mwangu. Miongoni mwayo ni, mbona maneno machache aliyoyazungumza yalikuwa ya Kiswahili kinachoeleweka?

Mbona nyumbani Kenya mara nyingi tu Mheshimiwa Ruto amezungumza  kwa Kiswahili na hata wakati wa kampeni alitumia sana Kiswahili kufikisha ujumbe na sera zake kwa wapiga kura na kueleweka hadi wakamchagua?

SOMA ZAIDI: Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili

Kilichonishangaza zaidi ni kuwa hakuwa akizungumza kwengineko bali Tanzania, ambako wananchi wake na wale wa Kenya huwasiliana zaidi kwa Kiswahili  na kuelewana kwani, kama nilivyosema, ni lugha rasmi na ya taifa ya nchi zao hizo.

Nakumbuka hotuba ya Rais Samia aliyoitoa kwa lugha ya Kiswahili katika hafla ya kuapishwa kwa Rais Ruto, huku Rais huyo wa Kenya akisema: “Karibu sana Mheshimiwa Rais, tunakuenzi [na] tunakuheshimu.” 

Unaweza kudhani huyu ni mtu asiyeweza kuwasilisha hotuba yake kwa Kiswahili?

Ukuaji wa Kiswahili

Tanzania na nchi nyengine wanachama wa EAC zimekuwa zikichukua juhudi za makusudi ili lugha ya Kiswahili itambulike kimataifa. 

Jitihada hizi ndizo zilizopelekea mnamo Februari 2022, kwa mfano, Umoja wa Afrika (AU), wenye nchi wanachama 55, kukiainisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kikazi katika shughuli za umoja huo. 

Leo hii, zaidi ya watu milioni 100 barani Afrika na zaidi ya milioni 200 duniani  wanazungumza Kiswahili na hivyo kuwa lugha yenye kuzungumzwa  na watu wengi zaidi barani humo, kwa mujibu wa Shirika la Elimu, Sayansi ana Utamaduni  la Umoja wa mataifa (UNESCO).

SOMA ZAIDI: Sifa Kedekede Zamwagwa Dunia Ikiadhimisha Siku ya Kiswahili

Haishangazi basi kuona UNESCO ikipitisha azimio katika kikao chake mjini Paris, Ufaransa la kuifanya Juali 7 ya kila mwaka iwe ni Siku ya ya Kiswahili Duniani

Matumizi ya Kiswahili yamevuka mipaka ya Afrika na kubisha hodi hadi eneo la Ghuba, ikuzungumzwa katika nchi kama vile Oman na Yemen. 

Pia, Kiswahili kinafundishwa katika vyuo vikuu kadhaa barani Afrika na duniani kwa jumla.

Huu, kama nilivyosema, kwa namna yoyote ile siyo ushindi wa Tanzania pekee bali ukanda nzima wa Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla.

Kasumba dhidi ya Kiswahili

Hakuna namna nyengine naweza kuelezea uamuzi wa Rais Ruto kuacha kutumia Kiswahili na badala yake akatumia Kiingereza mbali na kasumba zilizopo nchini Tanzania na ukanda nzima wa Afrika Mashariki kuhusu uzungumzaji wa Kiswahili na Kiingereza. 

Miongoni mwa watu wetu wengi, kuzungumza Kiingereza ni ishara ya ustaarabu na humpatia mzungumzaji hadhi maalum kwenye macho ya wasikilizaji wake. 

Kwa kuamua kutumia Kiingereza badala ya Kiswahili, tena nchini Tanzania ambapo watu wake wengi ni wazungumzaji wa Kiswahili, Rais Ruto amezipa nguvu maradufu kasumba hizi. 

SOMA ZAIDI: Kutweza Kiswahili ni Ishara ya Kujidharau, Kutojiamini

Lakini hata kabla ya uamuzi huo wa Rais Ruto, tayari kasumba hizi zimekita mizizi nchini Tanzania ambapo athari zake zimeonekana kujitokeza hata bungeni ambapo umezuka mtindo wa baadhi  ya wabunge kuchangia kwenye midahalo kwa Kiingereza badala ya Kiswahili.

Huenda wawakilishi hao wa wananchi hufanya hivyo ili kuonesha wapiga kura wao kwamba wao ni msomi. 

Hata hivyo, wanasahau kwamba mpiga kura aliyemtuma bungeni anataka kumsikiliza kwa lugha ya kitaifa kuhusu yale aliyokusudia kuyafanya katika kumtumikia!

Wakati tunakipuuza … 

Kilipofika Kiswahili kimataifa ni heshima kubwa, tusitowe mwanya wa heshima hii kuchukuliwa na wengine. 

Vinginevyo, yatatokea yale niliyowahi kuonya kwenye gazeti la RaiaMwema kuhusu Kiswahili iliyokuwa na kichwa kisemacho Wakati Tunakipuuza, Wengine Wanakitukuza.

Viongozi wa Afrika Mashariki wana jukumu kubwa la kusaidia kuienzi, kuipanua na kuiendeleza lugha hii adhimu ya Kiswahili. 

SOMA ZAIDI: Hatua Zilizobaki Ili Kiswahili Kiwe Lugha ya Kufundishia Tanzania

Mheshimiwa Ruto angeweza kujiandaa tokea awali. Kama ni wasiwasi nina imani kuna maafisa wake wasaidizi waliobobea katika lugha ya Kiswahili wangeweza kumuandikia hotuba yake. 

Ni nadra kumuona kiiongozi wa Urusi, China au Japan akizungumza kwa lugha ya kigeni. Kwa nini wakwetu wasiweze? 

Ni matumaini yangu kwamba safari nyengine Rais Ruto atakapoitembelea Tanzania  atazungumza kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili kama alivyozoea kufanya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta!

Mohammed AbdulRahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mammkufunzi@outlook.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts