Mwezi huu wa Disemba, kuna mataifa kadhaa ya Afrika yalioadhimisha sherehe zao za Uhuru kutoka kwa wakoloni. Mbali na nchi tatu za Afrika Mashariki – Tanganyika, Zanzibar, iliyoungana na Tanganyika baadaye kuunda Tanzania, na Kenya – kuna Burkina Faso, kutoka Afrika Magharibi.
Kilichonivutia zaidi hadi kuandika makala haya, hata hivyo, ni maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Burkina Faso, taifa ambalo hadi kufikia mwaka 1984 likijulikana kama Upper Volta.
Wengi huiita Burkina Faso nchi ya mwanamapinduzi Thomas Sankara, muasisi wa jina hilo lenye maana ya Ardhi ya Watu Waaminifu.
Katika kuadhimisha miaka hiyo 62 ya Uhuru, kiongozi mpya wa Burikna Faso, Ibrahim Traoré, alilihutubia taifa kwa njia ya televisheni.
Traoré, afisa kijana wa kikosi cha mizinga mwenye umri wa miaka 34, (mwaka mmoja zaidi kuliko Sankara) akiwa pamoja na vijana wenzake wa vyeo vya chini, alitwaa madaraka hapo Septemba 30, 2022, na kumuondoa mwanajeshi mwengine, Paul-Henri Sandaogo Damiba.
Yalikuwa ni mapinduzi ya pili katika muda wa miezi minane baada ya mnamo mwezi Januari, Damiba kuuangusha utawala wa kiraia wa Roch Marc Christian Kaboré.
Traoré alizitaja sababu za msingi zilizowalazimisha wao kutwaa madaraka na kumuondoa Damiba, ikiwa ni pamoja na kile alichodai ni kushindwa kwa utawala wake katika vita dhidi ya ugaidi.
Sababu nyengine ni hali mbaya ya kiuchumi huku akimshutumu Damiba kujiwekea malengo ya kisiasa zaidi kuliko kutatua matatizo yanayoikabili Burkina Faso.
‘Hakuna cha kusherehekea’
Katika hotuba yake fupi kwa lugha ya Kifaransa kuadhimisha siku hiyo ya miaka 62 ya Uhuru hapo Disemba 12, 2022, Traoré, ambaye aliapishwa Oktoba kuwa Rais wa mpito, alisisitiza juu ya kitisho kinachoikabili Burkina faso:
“Ndugu wananchi wenzangu, umma wa wapiganaji wa Burkina Faso mlioko ndani na nje ya nchi, Desemba 12, 2022, ni siku ya kuadhimisha miaka 62 ya uhuru wa Burkina Faso, lakini sitatoa hotuba mwaka huu kwa sababu sikukuu hii, wakati huu, siyo ya sherehe.
“Nchi yetu haina uhuru kamili kwa kuwa inakaliwa; uchumi wetu uko katika hali mbaya na umma unateseka. Ni kwa sababu hiyo nitazungumza kwa ufupi.
“Ni wiki chache sasa, mustakbali wa taifa umebadilika tangu Septemba 30. Walisema tumeasi na leo siku ya Uhuru wa nchi yetu tungali tumeasi. Vita vya kuwania Uhuru kamili wa nchi yetu ulianza tangu muda huo. Vita hivi si vya silaha peke yake bali pia vya kulinda heshima yetu na mageuzi ya uchumi wetu.
“Mapambano dhidi ya wale wanaoikalia ardhi yetu yameanza. Vita hivi vina gharama na ndiyo maana sina budi kuvipongeza vikosi vyote vinavyohusika, vya anga na nchi kavu na wale waliojitoa muhanga kwa ajili ya taifa hili.
“Na wapongeza pia kwa umoja tuliouonesha kama taifa katika siku na miezi ya hivi karibuni kuanzia Jeshi la Ulinzi hadi umma na wale waliojitolea magari yao kwenda katika uwanja wa mapambano, kuwalinda Waburkinabe. Hatuna zaidi la kuwaomba zaidi ya mshikamano huo.
“Kwa Waburkinabe mnaoishi nje, nasema shukurani nyingi kwa msaada wenu wa hali na mali na tunatoa wito kwa wadau wote wa ndani katika jamii, ili vita hivi viwe vyetu Waburkinabe wenyewe na kuikomboa ardhi yetu. Nawashukuru wote wanaoungana nasi iwe Waburkinabe au la.
“Leo hii, kwa hiyo, hatuna la kusherehekea kwa sababu vita tulivyonavyo vitaendelea hadi ukombozi kamili wa taifa letu.
“Pia, ninatoa wito kwa Waburkinabe wote tubadili tabia, kwa sababu ushindi katika vita hivi vya kupigania uhuru kamili hautatokana tu na mapambano ya silaha lakini kama nilivyosema mwanzoni na vita vya kiuchumi.
“Vita hivi vya kiuchumi kwa upande mwengine ni mapambano dhidi ya rushwa. Mapambano haya yameanza na hayatasita hadi hatimaye wana wote wa Burkina Faso wanapata chakula na kuishi katika hali ya usalama bila hofu katika nchi yao.
“Tumejitolea na matumaini yetu ni makubwa. Endeleeni kuwa imara na wenye mshikamano, mkisimama pamoja na jeshi lenu la ulinzi na vyombo vya usalama. Sisi tumejitolea kuendelea hadi ukombozi kamili wa Burkina Faso.”
Shangwe za matumaini
Ari ya maafisa hao vijana ya kuleta mabadiliko yanaonekana kuleta mwamko mpya na kukaribishwa kwa shangwe za matumaini na raia wa nchi hiyo.
Baadhi ya wachambuzi wametafsiri kinachoendelea hivi sasa nchini Burkina Faso kama mchakato wa kuzifufua fikra za Thomas Sankara ambaye wakati wa utawala wake alitambuliwa kuwa mfano wa uongozi wa matumaini barani Afrika.
Sankara aliuwawa mwaka 1987, miaka minne baada ya yeye kutwaa madaraka katika mapinduzi ya kijeshi. Wapo wanaoamini kwamba kuuwawa kwake ilikuwa njama iliyoandaliwa na makamu wake, sahibu yake wa chanda na pete, Blaise Compaoré.
SOMA ZAIDI: Afrika Na Demokrasia Bado Mguu Ndani, Mguu Nje
Compaoré siyo tu anashutumiwa kuyasaliti mapinduzi ya Burkina Faso, lakini pia anashutumiwa kutawala kwa mkono wa chuma hadi umma ulipomgeukia mwaka 2014 kutokana na vuguvugu lililopewa jina la Balai Citoyen, yaani Fagio la Umma, na kukimbilia nchi jirani ya Cote d`Ivoire, kwa msaada wa Ufaransa.
Ufaransa ina historia ya kuwaondoa madarakani kwa njia ya mapinduzi, na hata mauaji, wale waliothubutu kwenda kinyume na maslahi yake ya kisiasa au kiuchumi.
Tukio linalofanana na kadhia ya Sankara ni kupinduliwa, na kuuwawa, kwa Rais wa Comoro, mjamaa Ali Soilih M’Tsashiwa, mnamo mwaka 1978. Utawala wa kimapinduzi wa Soilihi ulidumu kwa miaka mitatu tu.
Ukinzani dhidi ya Ufaransa
Ni kutokana na msingi huo ndiyo Ufaransa kwa sasa inakabiliwa na ukinzani mkali siyo tu nchini Burkina Faso bali pia hata nchini Mali na Guinea.
Mali na Guinea pia zinaongozwa na wanajeshi vijana waliotwaa madaraka kwa kile wanachosema ni kuyaokoa mataifa yao dhidi ya tawala za kiraia zilizoshindwa kulinda rasilimali za taifa na badala yake kutumikia masilahi ya Ufaransa.
Mapinduzi ya Burkina Faso yameleta mshikamano kati ya viongozi wa kijeshi wa nchi hizo tatu wanaokabiliana na changamoto zinazofanana, kubwa ikiwa ni hali mbaya ya uchumi na umasikini wa kupindukia wa raia wao.
zao.
Sambamba na hali hiyo, Mali na Burkina Faso zinakabiliwa na changamoto ya vita dhidi ya makundi ya kigaidi katika nchi zao.
SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?
Mali iliingia kwenye mvutano na Ufaransa baada ya Kanali Assimi Goïta kutwaa madaraka katika mapinduzi ya kijeshi mnamo Mei 2021 na kuvunja mikataba yote ya ushirikiano wa kijeshi na mkoloni wake huyo wa zamani.
Goïta ameikosoa vikali Ufaransa kuwa inaendeleza sera za kuinyonya nchi yake na hakuna tija iliyopatikana katika kuisaidia kupambana na ugaidi, akiamuru majeshi yote ya Ufaransa kuihama nchi hiyo na kuijongelea Urusi kwa msaada wa kijeshi katika vita dhidi ya ugaidi.
Baada ya mapinduzi ya Goïta nchini Mali yakafuata yale ya Kanali Mamady Doumbouya nchini Guinea mnamo Septemba mwaka huo huo wa 2021 dhidi ya Rais Alpha Condé.
Condé alikuwa tayari amekataa kuondoka madarakani baada ya muhula wake kumalizika na akaibadili Katiba kujipa muhula wa tatu.
Mshikamano
Mshikamano wa Goïta, Traoré na Doumbouya umeibua mwamko mpya na msimamo wao wa kuondokana na ushawishi wa Ufaransa unaungwa mkono na sehemu kubwa ya raia katika nchi zao.
Kinachosubiriwa kwa hamu ni endapo kama wanamapinduzi hao watafanikiwa katika vita hiyo waliyoianzisha dhidi ya ukoloni mamboleo.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba historia ya miaka mengi iliyopita inaonesha kwamba baadhi ya viongozi wa Kiafrika walitumika kuwasaliti viongozi wenzao na kuungana na njama za kikatili za Ufaransa.
Wapo pia baadhi ya wachambuzi wanaoamini kwamba kinachoendelea hivi sasa ni wimbi la mageuzi litakalochochea mabadiliko katika nchi nyengine zinazotawaliwa kwa mkono wa chuma na viongozi wao kulindwa na dola.
SOMA ZAIDI: Ni Kwa Kiwango Gani Waafrika Wanaweza Kujitatulia Matatizo Yao Wenyewe?
Katika hotuba yake ya kuadhimisha siku ya Uhuru wa Burkina Faso, Traoré alimaliza kwa kauli mbiu ile ile iliyokuwa ikitumiwa na hayati Thomas Sankara ya La Partie au la Mort nous Vaincorons, au Nchi Yetu au Kifo, Tutashinda, kwa Kiswahili.
Chimbuko la kauli hii ni waasisi wa mapinduzi ya Cuba, Fidel Castro na Ernesto che Guevara, waliokuwa wakitumia kauli mbiu ya La Partia o Muerte, Venceremos katika harakati zao za ukombozi.
Hapana shaka mshikamano wa viongozi hao wa Burkina Faso, Mali na Guinea umesimama katika msingi huo wa kufikia ushindi ili kuziokoa nchi zao na kuzipa matumaini ya kuwa na mustakbali mwema.
Swali la je, watafanikiwa au la, ni wakati tu ndiyo wenye jibu sahihi!
Mohammed AbdulRahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mammkufunzi@outlook.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.